27 Apr 2011


Ukisikia kimbembe cha zule ndio hiki kinachoikabili CCM kwa sasa.Japo chama hiki tawala ni mahiri sana kwa usanii,lakini ni dhahiri kuwa yanayoendelea sasa ndani ya chama hicho yanaweza kabisa kuwa dalili za mwanzo wa mwisho.Hebu jionee vimbwanga hivi katika stori zifuatazo:


Barua za kuwang’oa kina Lowassa zakamilika
• Yadaiwa ziko mezani kwa Msekwa

na Mwandishi wetu

Barua za makada watatu wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rostam Azizi, Edward Lowassa, na Andrew Chenge, za kuwataka wajiondoe katika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, ziko tayari.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umethibitisha kwamba makada hao, waasisi wa mtandao uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2005, wanaweza kupokea barua zao wakati wowote kuanzia leo Jumatano.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, barua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliyomaliza kikao chake hivi karibuni mjini Dodoma.

Inadaiwa makada hao maarufu na wenye ushawishi mkubwa ndani ya nje ya chama hicho tawala, walipewa siku 90 tangu siku ya kikao, wapime wenyewe uzito wa kashfa zinazowakabili na wajiengue kwenye nafasi za uongozi, vinginevyo chama kitawaengua katika kikao kijacho cha NEC.

“Barua za Lowassa, Chenge na Rostam ziko tayari, na suala lao liko mikononi mwa Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chama. Wiki hii watakabidhiwa,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya CCM.

Pamoja na mambo mengine, barua hizo zimeorodhesha tuhuma zao na kurejea maazimio ya NEC yanayowahusu.

Alipohojiwa na Tanzania Daima Jumatano juu ya barua hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alithibitisha kwamba tayari barua hizo zimeshaandaliwa. Naye alisema watakabidhiwa barua hizo wakati wowote kuanzia leo Jumatano.

“Kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa maazimio ya NEC, si jambo geni. Ninachojua, tulikuwa tunasubiri mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka yapite, kila mtu ale Pasaka yake,” alisema Nape.

Wakati barua hizo zikisubiriwa kwa hamu, baadhi ya makada wajumbe wa NEC wamekaririwa na vyombo kadhaa vya habari na katika mazungumzo yasiyo rasmi wakisema hakukuwa na azimio lolote lililopitishwa la kuwataka makada hao wapewe siku 90 za kujiengua. Vilevile, wamekanusha kuwapo kwa azimio lolote la kuwaandikia barua.

Hata hivyo, Nape amekuwa akisema kwa waandishi na katika mikutano ya hadhara kwamba NEC ilitoa azimio hilo. Baadhi ya makada wasiokubaliana na kauli za Nape, katika hali ya kuwaonea huruma au kuwatetea watuhumiwa, wamekuwa wakidai kwamba kauli za Nape zimetoka nje, si ndani ya kikao cha NEC.

Lakini baadhi yao wamekuwa wakidokeza kuwa si rahisi Nape kujitungia maneno makali ya aina hii, huku wengine wakisema anatumwa na wakubwa “kuwashughulikia” kina Rostam.

Katika kujaribu kuthibitisha kwamba Nape anazungumza jambo lisilotokana na maazimio ya NEC, baadhi ya makada wanakumbushia kauli za hivi karibuni za mtangulizi wake, John Chiligati, ambaye amepata kutaja mara kadhaa taarifa zisizosahihi za maazimio ya vikao vya Kamati Kuu na NEC, tofauti na kilichojadiliwa ndani ya vikao hivyo.

Wanasema, kwa mfano, Chiligati alipata kulalamikiwa kwa kutoa taarifa potofu kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu kuhusu uamuzi wa ama kuilipa au kutoilipa fidia kampuni ya uzalishaji umeme ya Dowans ambayo inaidai TANESCO shilingi bilioni 94.

Vilevile, wanasema Chiligati aliwahi kutoa maazimio ya kupotosha aliposoma maazimio ya NEC kuhusu utata ulioibuka baada ya kukatwa kwa jina la Hussein Bashe katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM kwa jimbo la Nzega katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Hata hivyo, Nape anasisitiza kuwa kauli yake ni ya chama na inatokana na maazimio ya NEC. Katika mikutano ya hadhara inayodaiwa ni ya kujitambulisha, amekuwa akisisitiza kwamba Lowassa, Rostam na Chenge wametakiwa kujiondoa kwenye ujumbe wa NEC ndani ya siku 90, vinginevyo watang’olewa kwa nguvu.

Ndiye pia aliyesema kwamba wataandikiwa barua za kuwaorodheshea tuhuma zao na kuwataka waondoke kwenye uongozi wa chama. Hata hivyo, hakuna kiongozi hata mmoja aliyesema kama makada hao watavuliwa pia ubunge.

Lowassa ni Mbunge wa Monduli, Chenge anawakilisha jimbo la Bariadi Magharibi, na Rostam Azizi ni mwakilishi wa Igunga.

Wadadisi wa mambo ya siasa wanasema kilichotokea mjini Dodoma ni muendelezo wa minyukano ndani ya CCM na kwamba hoja kuu inayosababisha haya si ufisadi, bali urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, hasa kwa kuwa baadhi yao wanasemekana wanatamani kugombea au kuunga mkono baadhi ya wagombea.

Nguvu yao ya kifedha na ushawishi wao ndani ya chama ni baadhi ya mambo yanayoogopwa na washindani wao ndani ya chama tawala. Ingawa wote watatu wamekuwa watu wa karibu sana na Rais Kikwete, habari zinasema kumekuwapo na taarifa za kuchongeana miongoni mwao, zikichochewa na makachero wanaomwaminisha Rais Kikwete kwamba sifa yake iliyopotea mbele ya jamii inaweza kurudi iwapo ataondokana na watatu hao.

Rais Kikwete naye anatumia ushauri huo kama fursa ya kurejesha matumaini ya wananchi kwake na CCM, akitumia kaulimbiu ya kujivua gamba.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wakosoaji wa Rais Kikwete wamesema kujivua gamba kunakofanywa naye ni unafiki mtupu, kwani kama lengo ni kupiga vita ufisadi, naye yu miongoni mwa waliotajwa kwa ufisadi pamoja na Chenge, Rostam na Lowassa.

Baadhi ya makada wamesema kwamba kama CCm inaazimia kuondoa mafisadi, basi kiwaondoe viongozi wote waliopatikana kwa pesa za kifisadi za EPA.

Katika orodha ya viongozi waliofaidika na ufisadi wa EPA, anatajwa pia Rais Kikwete, kwa maelezo kwamba pesa hizo zilitumika kununua kura ili ashinde.

Wanasema hata kuvunja Kamati Kuu na kuingiza wajumbe wengine hakukusaidia kuisafisha, kwani walioingia ni wachafu kama waliotoka, maana historia zao na wasifu wao vinafahamika.

Wengine wanakwenda mbali na kusema kwamba iwapo Rais Kikwete atatekeleza azima yake hii, atakuwa anaandaa anguko lake lisilotarajiwa, maana atakuwa anaongeza idadi ya maadui miongoni mwa watu wanaomjua vema, waliomjenga na kumsaidia hadi hapo alipo


Mafisadi CCM waandaa mamilioni kujisafisha
*Wadaiwa kuandaa vijana kupinga hatua dhidi yao

Na John Daniel

KUNDI la mafisadi wanaokabiliwa na hatihati ya kuvuliwa uongozi na pengine uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamebuni mbinu mpya
kujihami kwa kutumia haramu kwa kuandaa vijana kufanya maandamano kumpinga Rais Jakaya Kikwete na chama chake.

Kundi hilo linapinga vikali uamuzi wa CCM kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kuwapa muda wa kujiengua wenyewe kabla ya kufukuzwa baada ya siku 90.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu vimeeleza kuwa kundi hilo limepitisha bajeti ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwandaa vijana kufanya maandamano kupinga uamuzi wa kuondolewa NEC na hata CCM kwa ujumla, mara tu baada ya kukabidhiwa barua muda wowote kuanzia wiki hii.

"Tayari wameapa kuwa wakiondolewa ni lazima Rais Kikwete naye aondoke kwa kuwa ndiye aliyepitisha maamuzi ya kuwafukuza, wanapanga vijana kwa kuwarubuni kwa fedha haramu ili waandamane mara tu watakapopewa barua.

"Wiki iliyopita walikutana wakapitisha zaidi ya milioni 500 kumshughulikia Bwana mkubwa (Rais Kikwete), wanataka kumchafua ili kummaliza nguvu kuwashughulikia," kilisema chanzo kingine.

Habari hizo zilieleza kuwa mbali na Rais Kikwete anayeelezwa na kundi hilo kukabiliwa na tuhuma na ufisadi, akiwa miongoni mwa watu 11 waliotangazwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, na familia yake, akiwamo mwanawe Ridhiwan anayedaiwa kuwa mali kuliko kipato chake, pia kundi hilo linasaka kwa udi na uvumba majalada ya mawaziri wanne wa sasa kwa lengo la kuwaunganisha katika tuhuma za ufisadi, kwa kinachoelezwa kuwa ni kampeni ya 'tuchafuke wote'.

"Kati ya fedha hizo sh. milioni 18 zitatumwa katika mikoa 20 kugawiwa vijana ili wafanye maandamano ya kupinga kuondolewa na kuwapakazia wengine wanaotaka waondoke nao kama njia ya kujitakasa.

"Fedha zinazobaki zinatumika kununua mafaili ya watu wengine kutafuta makosa yao ya aina yoyote akiwamo Waziri wa Afrika Mashariki, Bw. Sitta (Samwel) Prof. Mwandosya, (Mark), Dkt. Mwakyembe (Harrison) na Membe au Magufuli," kilisema chanzo chetu.

Ilielezwa kuwa kundi hilo limekuwa likifanya vikao katika maeneo maeneo mbalimbali kwa lengo la kutaka kujisafisha na ufisadi, au kupunguza makali kwa kutaja wengine.

"Mmoja wao amejiandaa kuzungumza na waandishi wa habari kuwapa nyaraka za uongo ili kuwachafua watu wengine, walengwa wakuu ni Rais na familia yake, mawaziri wanne na wengine wadogo," kilisema chanzo kingine.

"Usifikiri hatujui hayo, mbinu zote wanazofanya tunazijua, hatuwezi kupambana na wajinga, tunasubiri tuone mwisho wao, lakini hata ninyi waandishi lazima mjue kuwa Watanzania wanaosoma vitu mnavyoandika wanajua yote," alisema kigogo mmoja wa serikali bila kutoa ufafanuzi.

Mbinu nyingine iliyotajwa mara baada ya uamuzi wa NEC Dodoma ni kuwatumia viongozi wa vyama vya siasa kutoa tuhuma mpya ili ionekane kwamba wameonewa na kupoteza lengo la kuwaondoa.

Pamoja na kwamba hakutaja jina, Chama cha demokrasia na Maendeleo ndicho kimetaja watuhumiwa wapya wa ufisadi, huku Katibu Mkuu wake, Dkt. Slaa akipinga madai ya kutumiwa kufanya hivyo kwa nia ya kuwachafua.

Katika tuhuma hizo, alizungumzia uuzaji wa nyumba za serikali bila kufuata utaratibu zilizoelekezwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na aliyekuwa waziri wake wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli; Kuhusu fedha za EPA na mahali zilipo zile zilizorejeshwa akielekeza tuhuma hizo kwa Rais Kikwete na John Malecela na Philip Mangula waliodaiwa kuhusika katika wizi wa fedha za EPA, hasa zile zilizoingia katika kampeni ya CCM mwaka 2005.

Katika hatua nyingine kundi hilo la mafisadi wa linadaiwa kuwalenga baadhi ya viongozi wa dini kuwasafisha kwa kutangaza msimamo kuwa wameonewa na hakuna mtakatifu au wao wametolewa kafara.

Majira ilipomtafuta Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye kujua kama wana taarifa hizo alikiri na kuongeza kuwa haziwasumbui kwa kuwa mfa maji hakosi kutapatapa.

"Kwanza nilishasema nilipokuwa uwanja wa Manzese, niliwaambia wananchi kuwa mafisadi wamejipanga kumchafua Mwenyekiti wetu na familia yake"

CHANZO: Majira

Diwani matatani kwa kumwita Chiligati fisadi

na Francis Godwin, Iringa

DIWANI wa kata ya Mgama, wilayani Iringa Vijijini, Denis Lupala (CCM), yuko matatani baada ya kumwita Naibu Katibu Mkuu CCM, Tanzania Bara, Kapteni John Chiligati, kuwa ni fisadi na anapaswa kuvuliwa gamba kama Katibu Mkuu aliyepita Luteni Yusuf Makamba na wenzake.

Diwani huyo anadaiwa kutoa kauli hiyo hivi karibuni mkoani Iringa wakati Chiligati na viongozi wengine wapya wa sekretarieti ya CCM taifa alipofanya ziara mkoani humo kwa ajili ya kujitambulisha.

Diwani hayu ambaye tayari ameitwa na sekretarieti ya wilaya na Kamati ya Maadili kujadiliwa kwa utovu kwa Chiligati na viongozi wengine waandamizi wa CCM ambao alipendekeza watimuliwe.

Akithibitisha kuitwa kwenye vikao hivyo, Lupala alisema alipewa barua ya kuitwa kuhusu tuhuma hizo, lakini hakuhojiwa.

‘Kweli waliniita na mwanzoni niliambiwa kikao kitanijadili kwa utovu wa nidhamu niliouonyesha badala yake tulijadili tukio la jukwaa kuanguka wakati Chiligati akihutubia,” alisema diwani huyo.

Hata hivyo alijigamba kuwa alikuwa amejiandaa kupangua hoja zao kwani hadi sasa binafsi hataki Chiligati abaki kwenye nafasi hiyo kwa madai kuwa anapaswa kuvuliwa gamba kama viongozi wenzake aliokuwa nao kwenye sekretarieti iliyopita.

“Nilijipanga vizuri kuwajibu viongozi wa wilaya iwapo wangejaribu kutaka kuniadhibu kwa kumwita Chiligati fisadi. Ni ukweli usiopingika kuwa kati ya watu wanaovuruga CCM Chiligati ni mmojawapo na hana sifa ya kuwa kiongozi ndani ya CC na nasema kuwa niko tayari kuwajibika kwa kusema ukweli dhidi ya Chiligati,” alisema diwani huyo.

Hata hivyo habari zaidi zinasema kuwa diwani huyo anatarajiwa kuitwa wakati wowote kuanzia sasa kujibu tuhuma alizozielekeza kwa Chiligati.

Wakati wa mkutano wa hadhara, diwani huyo wa CCM alipata nafasi ya kuuliza swali na kuanza kumrushia madongo Chiligati kwamba ni fisadi na ajiuzulu nafasi yake.

Pia alitaka Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Andrew Chenge (Bariadi Mashariki) na Rostam Aziz (Igunga) na wengine kufilisiwa mali zao na kunyang’anywa kadi za uanachama.

Hata hivyo alishindwa kuendelea na hoja yake baada ya baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM kuingilia kati na kusitisha swali lake kwa Chiligati.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube