26 May 2011

Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda na wakuu wa vyombo vya dola.Wa kwanza kushoto ni CDF (Mkuu wa Majeshi) Davis Mwamunyange,akifuatiwa na IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) Mwema na DGIS (Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa) Othman Rashid


Sio siri kwamba Jeshi la Polisi Tanzania lina sifa chafu na yayumkinika kuamini kuwa ni taasisi inayochukiwa sana na walalahoi.Sifa kuu mbili za jeshi hili linaloongozwa na IGP Saidi Mwema ni RUSHWA ILIYOKUBUHU na UBABE WA KUPINDUKIA.

Sifa hizo zinahusiana kwa karibu.Rushwa ya polisi inachangiwa zaidi na kipato duni kisichoendana na wajibu wao (ambao kwa asilimia kubwa hawautekelezi).Kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili,ambao tegemeo kubwa la kuutatua ni kwa kulazimisha rushwa (wakinyimwa hawakawii kumbambikia mtu kesi),askari wa jeshi la polisi wanakuwa na hasira muda wote.Lakini badala ya kuelekeza hasira hizo kwa mwajiri wao-yaani serikali-wao wanaelekeza hasira hizo kwa wananchi wanyonge wasio na watetezi (sambamba na wanasiasa wa vyama vya upinzani hususan Chadema).

Kingine kinacholifanya jeshi la polisi lifanane na Nazi Police wa Hitler ni uhaba wa elimu.Polisi limekuwa kimbilio la vilaza (watu wenye uwezo duni kimasomo) na kwa upande mwingine jeshi hilo limegeuzwa mahala pa vigogo kupeleka watoto wao watukutu.Kimsingi,jeshi hili halina nidhamu isipokuwa kwa vigogo na mafisadi wanaowatunza.

Inafahamika kuwa Rais Jakaya Kikwete na IGP Said Mwema wana mahusiano ya kibinafsi zaid ya hayo ya kiserikali.Na hili ndio tatizo la kuendesha nchi kiushkaji.Kinachompa jeuri kubwa IGP Mwema ni ukweli kwamba moja ya sababu zilizopelekea kupewa wadhifa huo ni ukaribu wake na Kikwete.Kwa maana hiyo anajua wazi kuwa Kikwete hawezi kumtosa hasa kwa vile uteuzi huo ni wa misingi ya nilinde nikulinde.

Lakini Kikwete akae akitambua kuwa moja ya sababu zilizopeleka dikteta Hosni Mubarak kung'olewa madarakani huko Misri ni unyama wa jeshi lake la polisi.Jeshi hilo ndilo lililopelekea vifo vingi wakati wa maandamano ya kudai mageuzi nchini humo.Kama wenzao wa Tanzania,polisi wa Mubarak walikuwa wanafahamu lugha moja tu:UBABE.

Kikwete atambue kuwa kuwaachia wahuni waliovaa yunifomu za polisi wanyanyase wananchi wapendavyo,waue wanachi kila wanapojiskia na waendelee kuwabambikia kesi walalahoi,siku ya siku wananchi hao wataamua liwalo na liwe.Ubabe sio ufumbuzi wa kila kitu.Kulikuwa na tawala ngapi za kibabe zilizoishia kuwa historia?

Kikwete na serikali yake ya CCM hawawezi kukemea uhuni na ukatili wa polisi kwa vile jeshi hilo,kama zilivyo taasisi nyingine za dola,limeendelea kuwa tawi lislo rasmi la chama tawala.Laiti Kikwete angekuwa anathamini haki za binadamu asingeruhusu jeshi hilo litangulize nguvu hata pale panapohitaji diplomasia.Kwanini awakemee ilhali wanawakomoa Chadema na walalahoi wengine?Unadhani Kikwete asingechukua hatua laiti polisi wangelalamikiwa na mafisadi?

Enewei,soma habari zifuatazo zinazohusu jeshi hilo la polisi

Polisi wapambana na raia Dar
Wednesday, 25 May 2011 21:56

Felix Mwagara na Ellen Manyangu
VURUGU kubwa zilizuka usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, baada ya maofisa wa Manispaa ya Temeke kuendesha operesheni ya kubomoa vibanda vya wafanyabiashara wadogo kwenye hifadhi ya barabara.

Ilibidi polisi kuingilia kati kuwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa na hasira, wakipinga uharibifu wa mali zao wakidai kuwa mkakati huo umetekelezwa bila wahusika kupewa taarifa.Zaidi ya mabanda 50 ya wafanyabiashara hao yalibololewa katika agizo hilo kwenye eneo lililopo karibu na Feri, ambalo mji wa Kigamboni unakua kwa kasi.

Baadhi ya walioshuhudia vurugu ambazo ziliandamana na vitendo vya uporaji wa mali na fedha, walisema wafanyabiashara wapatao 50, walikamatwa. Hadi jana mchana, kulikuwa na idadi kubwa ya polisi kwenye eneo hilo wakiwazuia wafanyabiashara hao wasifanye fujo huku maofisa wa manispaa wakibeba bidhaa mbalimbali zilizozagaa hapo.

Wafanyabiashara hao walisema kwamba walilazimika kupambana na askari hao ili kunusuru mali zao katika mpango huo uliotekelezwa bila notisi.

"Ilitulazimu kupambana ili kuokoa japo mali kidogo kwani ubomoaji huo umefanyika usiku wa manane pasipo taarifa yoyote. Hatujapewa notisi yoyote ya kuhama katika eneo hili," alisema Rajabu Mohamed.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Omary Mkwesu alisema tukio hilo ni la kusikitisha kwa sababu wamepoteza mali nyingi.

Alihoji kuwa kama ubomoaji huo ulikua wa haki kwa nini wasingewapa notisi ili walau watoe mali zao katika mabanda hayo?

Alidai kwamba hatua hiyo ni njama za diwani wa eneo hilo: "Zoezi hili limesimamiwa na diwani wetu ambaye amekuwa akitutishia kwa muda mrefu kuwa ipo siku atatubomolea na kwa kuthibitisha hilo, tumemuona akisimamia zoezi hili la ibomoaji hovyo saa nane usiku."

Hata hivyo, Diwani wa eneo hilo, Dotto Msama alikanusha kuhusika na tukio hilo akisema Manispaa ya Temeke ilishatoa notisi zaidi ya sita kuwataka wafanyabiashara hao waondoke katika eneo hilo.

"Jambo hili limenisikitisha hata mimi na sasa hivi naelekea manispaa kuongea na uongozi wake juu ya tukio hili. Ni kweli sikuwa na taarifa za zoezi hili kufanywa leo, tena usiku wa manane, ila notisi zilishatolewa na nakala yake iko kwa mtendaji na mwanasheria wa manispaa.

Polisi kwa upande wake, wamekanusha kuwanyanyasa wananchi hao na kusema walikuwepo kwa ajili ya kulinda usalama hasa baada ya wananchi hao kufunga barabara.

CHANZO: Mwananchi

Na habari ifuatayo ni kuhusu moja ya SIFA KUU MBILI za Jeshi la Polisi,yani RUSHWA (nyingine ni UKATILI)
Polisi, mahakama zazidi kutajwa kwa rushwa 
Wednesday, 25 May 2011 21:54

Minael Msuya

IDARA za POLISI na Mahakama zimetajwa tena kuwa ni taasisi sugu zinazoongoza kwa kudai rushwa nchini.Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHCR) katika taarifa yake imezitaja idara hizo kwamba ndizo kinara kwa kudai rushwa.
Hivi karibuni, Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa Takukuru) nayo ilizitaja idara hizo kwamba ndizo zilizo mstari wa mbele kudai rushwa nchini.

Ripoti ya mwaka 2010 ya LHCR iliyofanywa katika mikoa 26 nchini na kuhoji watu zaidi ya 5,000, ilibainisha kuwa polisi inaongoza kwa asilimia 65.1 huku Mahakama ikifuatia ikiwa na asilimia 56.4. Akisoma ripoti hiyo, Mwanasheria wa LHCR, Pasience Mlowe alisema polisi na mahakama zinaongoza kwa rushwa na matumizi mabaya ya ofisi na kwamba zinashika nafasi ya 10 kwa Afrika Mashariki.

“Utafiti wa LHCR ulibaini kuwa polisi na mahakama ni taasisi sugu zinazoongoza kwa rushwa na zinashika nafasi ya 10 kwa Afrika Mashariki,” alisema Mlowe.

Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nayo inafuatia kwa asilimia 37.8 na kwamba inaendelea kushuka kiwango kila siku ikilinganishwa na 2009 ambapo ilikuwa katika nafasi ya tano. “Hali hii inayonyesha ni jinsi gani baadhi ya watu walivyozitelekeza sheria na haki za binadamu, wananchi wengi wanataabika usiku na mchana, lakini hawapati haki zao stahiki, tunaomba marekebisho ya vifungu vya sheria yafanyiwe kazi ili haki ya binadamu iweze kupatikana,”alisema.

Mlowe alisema, matatizo hayo ya taasisi hizo nyeti za serikali yanachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha uchumi wa nchi na kwamba serikali inatakiwa kusimamia sheria muhimu. Kwa upande wake ,Mtafiti na Mwanasheria wa LHCR, Onesmo Olengurumwa alieleza kuwa, utafiti huo ulibaini kuwa mauaji ya raia wengi yanasababishwa na vyombo vya dola kutokana na wao kujichukulia sheria mikononi.

“Vifo vya watu 52 vilivyotokea mwaka 2010 vilisababishwa na walinzi wa kampuni mbalimbali na polisi kwa kujichukulia sheria mikononi badala ya kutumia sheria inayowaongoza,”alisema Olengurumwa na kuongeza: ”Mfano mzuri ni wananchi wanaoishi kando ya Mgodi wa North Mara kule Tarime wanauawa bila sababu na ukichunguza utakuta sheria za mgodi, walinzi wa kampuni ndio wanaopaswa kulinda eneo lote sasa serikali inaingiliaje huko,”alisema.

Alisema mauaji ya watu yaliyotokana na mgodi huo, serikali haiwezi kujitetea kwa lolote na kwamba utetezi wake ni wakisiasa. Alisema serikali ikisimamia tume ya sheria na haki za binadamu nchi itaweza kuondokana na changamoto za ukiukwaji wa haki hizo zinazoikabili.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube