20 May 2011



Mauaji Tarime yalikoroga taifa
• Mbunge Lema apambana na kamishna wa polisi

na Mwandishi wetu

MAUAJI ya watu watano waliouawa na polisi, Tarime mkoani Mara kwa madai walikuwa ni wahalifu waliotaka kuvamia mgodi wa North Mara Barrick sasa ni dhahiri yameikoroga serikali na taifa kwa ujumla.

Jana Jeshi la Polisi pamoja na kutuma timu ya maofisa waandamizi kutoka makao Makuu ya Jeshi hilo, lilishindwa kuwashawishi ndugu wa marehemu hao ambao walikataa kusitisha mgomo kususia miili hiyo hadi serikali itoe tamko la kukomeshwa mauaji hayo na wahusika kuchukuliwa hatua.

Timu ya maofisa waandamizi kutoka makao makuu ya jeshi hilo ikiongozwa na Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja walilazimika kuondoka pasipo kufikia muafaka katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya baada ya mamia ya waombolezaji waliopiga kambi tangu Jumatatu kukataa mapendekezo yao.

Awali Kamishna Chagonja aliwahutubia wananchi hao akiwataka waridhie miili hiyo ifanyiwe uchunguzi na kuchukuliwa kwa ajili ya mazishi yatakayogharamiwa na serikali lakini juhudi zake ziligonga mwamba baada ya ndugu wa marehemu kukataa mapendekezo hayo, kwanza wakitaka taarifa ya serikali kulaani mauaji hayo.

“Sisi tumekuja hapa kushirikiana nanyi kwa lengo la kutafuta ufumbuzi sasa tunawaomba mridhie kufanyika uchunguzi halafu taratibu nyingine za mazishi zifuatwe ambapo pia tumejitolea kama jeshi la polisi kushiriki kwa kutoa msaada wa hali na mali ili tufanikishe zoezi hili, tunaomba mkubali kufanyika uchunguzi na tume huru itaundwa kuchunguza tukio hilo,” alisema Changonja.

Kauli yake hiyo ilipingwa vikali na waombolezaji hao ambao walishikilia kuwa kwa vyovyote vile ilivyotokea hakukuwa na sababu ya kuhalalisha vifo hivyo kwa sababu polisi ndio wahusika na walitumia nguvu nyingi kupita kiasi kukabiliana na raia wasiokuwa na silaha za moto.

Wakiongozwa na mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema (CHADEMA) aliyepiga kambi katika eneo hilo, wana ndugu hao walidai ingawa hawakupinga kuendelea na zoezi la mazishi lakini wasiwasi wao ulitokana na uharaka wa jeshi hilo kutaka kupoteza ushahidi kwa kulazimisha kufanyika mazishi.

Lema apambana na kamishna wa polisi

Katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti, mbunge wa Arusha mjini, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Lema alilazimika kumhoji Kamishna Changoja kwa maswali mazito akitaka kujua uharaka wa Jeshi la Polisi kufanya maziko tena ya watu waliowaita kuwa ni wahalifu.

“Kwa nini mnaharakisha maziko bila kuwepo kwa mtu anayewafanyia postmotem? Wewe unasema umetumwa na serikali umetoka makao makuu kuja kuiwakilisha serikali ni serikali ipi unayoiwakilisha?

“Asubuhi Waziri Kagasheki amesema waliouawa ni wahalifu… umekuja hapa huna mkuu wa mkoa, wilaya wala mbunge unamwakilisha nani kwenye serikali iliyokutuma? Ninatilia mashaka uharaka wa serikali kuwazika watu hawa. Ina maana serikali inazika majambazi? Umeanza lini utaratibu huu?” alihoji Lema.

Alisema polisi na serikali yao kuamua kutoa sh milioni tatu kwa kila marehemu kwa ajili ya maziko haijawahi kutokea.

Akizungumza na gazeti hili Lema alisema; “Wakati namuuliza chagonja anasema nisilete siasa kwenye jambo hilo hivi nani sio mwanasiasa? Huyo waziri aliyesema waliokufa ni wavamizi naye mwanasiasa.

“Kwa niaba ya chama changu tumefanikiwa kushwawishi ndugu wote wa marehemu na wameshawishika tukaondoka kwa pamoja pale chumba cha kuhifadhi maiti tukamuacha Chagonja na polisi wenzake, tumemwambia tunaahirisha maziko haya hadi postmotem itakayosema marehemu waliuawa kwa kupigwa risasi wapi kama ni mguuni au kichwani tujue,” alisema Lema.

Kauli nyingine ya Kagasheki

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamis Kagasheki, amemtuhumu mbunge mmojawapo wa chama fulani cha siasa (hakukitaja) kuhusika katika tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwile (CCM), aliyedai kufika katika eneo la Nyamongo kwa ajili ya kuwafariji ndugu wa marehemu waliouawa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa sera ya ukimwi eneo la kazi kwa jeshi la polisi nchini, Waziri Kagasheki alisema mbunge wa chama hicho cha siasa alitoka jimboni kwake na kufika kwenye jimbo lingine kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kufanya fujo.

“Suala la Nyamongo sitaki kulizungumzia kwa kina, ila niseme kwamba kuna mbunge mmoja wa chama fulani cha siasa, alisafiri kutoka jimboni kwake na kwenda jimbo hilo kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kufanya fujo….

“Kitendo kama hicho na vingine vinavyowiana kamwe haviwezi kuvumiliwa ndani ya nchi…,” alisema Waziri Kagasheki.

Alipoulizwa ni hatua gani serikali itazichukuliwa dhidi ya mbunge huyo, Waziri alishindwa kuweka wazi.

“Nimeshasema sitaki kulizungumzia kwa kina suala hilo, na kuliweka wazi mbele ya umma….” alimaliza na kuondoka.

Ngeleja naye azungumza

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ameeleza kusikitishwa na vurugu zilizotokea katika mgodi wa dhahabu wa North Mara. Ngeleja alieleza hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua tamko la wizara yake kuhusu vurugu hizo mgodini.

“Tumesikitishwa na taarifa hizo pamoja na vifo vilivyotokea tunatoa salamu za pole kwa wafiwa, kwa sasa vyombo vya usalama vinashughulikia hali hiyo,” alisema Waziri Ngeleja baada ya kuzindua bodi ya wakala wa ukaguzi wa madini.

Alisema pamoja na mambo mengine, serikali kupitia wizara yake imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha katika eneo hilo kunakuwa na mahusiano mazuri kati ya wawekezaji na wananchi wa eneo hilo.

Alieleza pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo katika eneo hilo tayari serikali na wawekezaji wamebuni mradi wa uchimbaji mdogo wa madini ambao utaanza baadaye mwaka huu ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 23 wameuawa kwa vipindi tofauti kwenye mgodi huo. Hata Barrick wenyewe wanasema nia yao si kuua raia hivyo hawakubaliani na kitendo kilichofanywa na polisi.

CHANZO: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.