20 May 2011


CCM Arusha kwachafuka

Thursday, 19 May 2011 22:42

CHATANDA ATAKIWA KUNG'OKA, GARI LAKE NUSURA LICHOMWE MOTO NA UVCCM
Moses Mashalla, Arusha
HALI si shwari chama tawala mkoani Arusha mara baada ya gari la Katibu wa CCM hapa, Mary Chatanda kunusurika kuchomwa moto na baadhi ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa chama hicho(UVCCM).Wanachama wa umoja huo kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha waliandamana katika Jengo la Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Arusha, wakishinikiza Chatanda pamoja na Mjumbe wa Baraza la Vijana mkoani Arusha, Mrisho Gambo "wajivue gamba".

Hali hiyo ilijitokeza jana katika jengo la makao makuu ya chama hicho wakati Kikao cha Kamati ya Siasa Mkoa kikiendelea ambapo, hali iliyosababisha dereva wa gari la katibu huyo wa CCM kulitoa nje ya jengo hilo na kisha kulikimbiza mahali kusikojulikana.

Vijana hao walikuwa wameshika mabango yenye ujumbe mbalimbali huku wakipaza sauti zilizokuwa zikimtaka Chatanda kuondoka katika nafasi yake ya uongozi kwa madai kwamba amekuwa akikivuruga CCM mkoani Arusha.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wanachama hao kutoka wilaya za Monduli, Longido, Arusha, Arumeru, Karatu na Ngorongoro walisema pamoja na wao kutoa malalamiko mbalimbali juu ya Chatanda na Gambo, lakini uongozi wa CCM taifa umekuwa ukiwakumbatia viongozi hao na kudai sasa wamechoka.

Walisema malaliko yao kuwa Chatanda amekuwa akikivuruga chama chao ikiwa ni pamoja na kusababisha kukosa ushindi wa Jimbo la Arusha Mjini lililoenda kwa Chadema huku wakisema kwamba ikiwa atakataa kung'oka watajua cha kufanya.

“Hatumtaki Chatanda na hatumtaki Mrisho Gambo hawa watu kwanza ni wasaliti, lakini pia wamechangia sisi kushindwa kuchukua jimbo hili kwani walikuwa wanaiunga mkono Chadema tunataka waondoke mara moja hadi kieleweke,” ilisikika sauti ya mmoja wa vijana hao.

Miongoni mwa jumbe ambazo zilikuwa zimeandikwa kwenye mambango hayo ni "Chatanda umehujumu uchaguzi kwa siasa zako za makundi zilizojaa chuki, ubinafsi na ubabe usio na manufaa kwa Chama Cha Mapinduzi", "Chatanda kwa siasa zako za ubabe umetuchonganisha na viongozi wa dini”, na nyingine kadha wa kadha.

Hali hiyo ilisababisha Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, James Ole Millya aliyekuwa kwenye kikao cha kamati ya siasa kutoka nje na kwenda ukumbini kuwatuliza wanachama hao, lakini juhudi zake ziligonga mwamba.

Akizungumza na wanachama hao, Milya aliwataka wapunguze jazba na kusema kuwa yeye ni mjumbe ametumwa kusikiliza madai yao hivyo wampatie na kisha taufikisha ujumbe huo.

“Jamani ninawaomba mtulie sidhani kama mtafanya fujo ninaomba mnipatie ujumbe mnitume niufikishe jamani nami nitaufikisha tulieni jamani,” alisema Milya

Hata hivyo, ushawishi wa Milya haukuzaa matunda na kuamua kurudi kikaoni kwani wanachama hao waliendelea kupaza sauti zao kwa wakidai kuwa wanamtaka katibu huyo aondolewe mkoani Arusha kwa kuwa amekuwa akiingilia uamuzi wa umoja wao na kuendelea kumkubatia Gambo.

“Mheshimiwa tunakipenda sana chama chetu na tunakuheshimu sana, tunaomba Chatanda aondoke la sivyo tutachoma gari lake, tukikutana nalo tutamondoa kwa nguvu,” alisema kwa jazba mmoja wa vijana hao.

Vijana wavamia kikao cha kamati ya siasa
Wakati hayo yakiendelea wanachama hao walikosa uvumilivu na kisha kuvamia ofisi ambapo Kikao cha Kamati ya Siasa mkoa kilipokuwa kikifanyika huku wakitishia kubomoa mlango kitendo kilichosababisha viongozi mbalimbali wa CCM mkoani hapa kuhaha kutuliza tafrani hiyo.

Maafisa usalama wakiwemo askari kanzu walikuwa wametanda katika maeneo ya jengo hilo huku wengine wakionekana wakizungumza na viongozi wa UVCCM kujua chanzo cha vurugu hizo.

Chatanda ajifungia ukumbini
Hadi tunakwenda mitamboni, Chatanda alikuwa bado amejifungia ndani ya ukumbi wa mkutano na hakuna taarifa yoyote ya CCM Mkoa aliyotolewa kuhusiana na tukio hilo.

Tuhuma dhidi ya Chatanda kutoka ndani ya chama chake zimekuja siku chache tangu ashutumiwe kuwa mmoja wa waliosababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa mkoani Arusha baina ya vyama vya CCM na Chadema.

Mgogoro huo unafuatia Chadema kupinga katibu huyo wa CCM wa Mkoa wa Arusha kushiriki katika vikao vya Baraza la Madiwani na kupiga kura ya kumchagua meya wa Jiji la Arusha, hali Iliyosababisha maandamano makubwa ambayo yalisababisha vifo vya watu watatu.

Wakati CCM wakidai kuwa Chatanda ni mjumbe halali wa vikao vya baraza hilo, Chadema wamekuwa wakipinga kwa maeleo kwamba mwanamama huyo ni mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Tanga hivyo hana sifa ya kushiriki vikao vya Arusha.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.