3 Jun 2011

Mwana blogger wa wiki hii ni Evarist Chahali wa Kulikoni Ughaibuni

Leo tumepata bahati ya kufanya mahojiano na Evarist Chahali waKulikoni Ughaibuni na kwenye Twitter anapatikana kwa jina la Chahali. Toka nimefahamu hii blog mimi personal nimekua nikiifuatilia na nilipokea email kutoka kwa wasomaji wake wapenzi wanaoifuatilia na kupendekeza kama tutaweza kufanya mahojiano naye lakini hata mimi nilikua nina mpango wa kumwandikia ili tufanye mahojiano naye. Nilikua natamani sana mahojiano haya ili watu ambao hawajawahi kuiona hii blog yake wapate kuifahamu. Ni blog yenye mambo mengi sana na anajadili mambo yake vizuri sana, kwa upana na kama inavyotakiwa (Tell it like it is). Kama hujawahi kuisoma blog yake basi usiache kuingia na kuisoma. Asante sana Evarist kwa kukubali kufanya mahjiano na sisi unaweza kutuambia kidogo kuhusu blog yako?
Jina la blogu yangu la Kulikoni Ughaibuni lilitokana na swali la msingi nililokuwa nikijiuliza mara kwa mara nilipofika hapa Uingereza kwa mara ya kwanza. Kwamba “kulikoni wenzetu wanaweza hili lakini sie tushindwe?” Yaani kwa mfano, kulikoni ninapokwenda tawi la benki hapa ninyenyekewe kama mfalme lakini kwetu iwe kama manyanyaso japo ni fedha zangu na za wateja wengine ndizo zinaipa uhai benki husika?Au, kulikoni Waingereza, kwa mfano, waweke mbele zaidi maslahi ya nchi yao kuliko maslahi ya kisiasa au kibinafsi? Kwahiyo, kimsingi hiyo ndio maana halisi ya jina la blogu yangu. Blogu hii ina-focus zaidi kwenye masuala ya siasa (hususan za Tanzania) pamoja na social justice. Mimi ni mwanaharakati wa mtandaoni (e-Activist) na Kuliko Ughaibuni ndio kama “ofisi” yangu. Malengo ya blogu ni kuhabarisha, kufundisha, kukosoa na kuburudisha jamii. Natumia Kiswahili japo nyakati nyingine huwa naweka posts kwa lugha ya Kiingereza japo ni nadra.
Je, wewe kazi yako ni kublog tu au hii ni kama kazi ya muda tu au hobby?
Hapana. Mimi nina shughuli nyingine zinazoniwezesha kumudu maisha. Moja ya shughuli hizo ni uanafunzi wa shahada ya uzamifu katika stadi za siasa (PhD in Political Studies). Kwangu, kublogu ni zaidi ya hobby kwani ninaamini sana katika kupashana habari, kuelimishana, kukosoa na kuburudisha pia. Ila napenda kukiri kuwa nina hobby ya kuandika, na siwezi kupitisha siku pasipo kuandika kitu fulani, iwe ni mtandaoni au kwenye makabrasha yangu.
Jinsi gani unaanza kublog na kwa nini?
Nilianzisha blogu yangu mwezi April mwaka 2006.Wakati huo nilikuwa naandika makala kwenye magazeti ya Mtanzania na Kulikoni. Kwahiyo lengo la awali la blogu yangu lilikuwa kuifanya iwe mahala pa kuwawezesha wasomaji kusoma makala hizo, hasa kwa vile magazeti hayo yalikuwa hayapatikani mtandaoni. Lakini kwa vile makala hizo zilikuwa zinatoka mara moja tu kwa wiki, ilinilazimu niwe naandika habari nyingine pia katika blogu zaidi ya makala hizo.
Nini changamoto unazozipata kwa kuwa na blog?
Kwa uapnde mmoja blogu hii imeniwezesha kutengeneza marafiki mbalimbali, lakini pia imenitengenezea maadui, hususan kutokana na msimamo wangu mkali kuhusu suala la ufisadi. Suala la uandishi limenigharimu sana kimaisha kwani nilishawahi kupoteza ajira sehemu flani baada ya wenye mamlaka kutopendezwa na maandiko yangu. Changamoto nyingine ni ukweli kwamba Watanzania wengi wanapenda zaidi picha kuliko habari au uchambuzi. Pengine hili linaeleza kwanini licha ya blogu yangu kuanzishwa mwaka 2006 bado imetembelewa na chini ya watu laki tano. Wakati najibu maswali haya idadi ya waliotembelea ni watu 406660 tu. Hata hivyo, cha muhimu kwangu sio mamilioni ya wasomaji bali hata wasomaji wachache ambao wanaweza kufanyia kazi ninachojaribu kuishawishi jamii yetu hususan katika vita dhidi ya ufisadi
Unafanya nini wakati ukiwa hushughulikii hii blog yako?
Again, kama nilivyojitambulisha hapo awali,kwa upande mmoja mimi ni mwanafunzi (kwa sasa ninasoma part-time) na pia ninafanya shughuli nyingine za kimaisha ambazo nisingependa kuziweka hadharani japo ni shughuli halali (sio ufisadi,lol!).
Ni mara ngapi unafikiri juu ya blog yako wakati uko mbali na kompyuta?
Kwa kweli ni vigumu kusema ni mara ngapi lakini blogu yangu ni sehemu muhimu ya maisha yangu na ninajitahidi kuipa attention mara kadhaa kwa siku
Ni nani wasomaji wa blog yako?
Kwa hakika ni vigumu kujibu swali hili lakini nadhani wasomaji wakuu wa blogu hii ni pamoja na wasomaji wa safu yangu katika jarida la Raia Mwema (safu yangu inafahamika kama “Raia Mwema Ughaibuni”). Pengine wasomaji wengine wakuu ni watu wanaofahamu msimamo wangu katika vita dhidi ya ufisadi.Na labda wasomaji wengine ni kila anayependa kusoma uchambuzi wa habari na matukio kuliko kuangalia tu picha.
Je ni mitandao gani mingine ambayo unatumia ili iweze kukusaidia kuitangaza blog yako ili iwafikie wasomaji walengwa wa blog yako? Mfano Twitter au Facebook
Posts zangu zinachapishwa pia huko Facebook, Twitter na LinkedIn. Kadhalika, kuna nyakati huwa nasambaza baadhi ya posts kwa bloga wenzangu, sambamba na kutuma kwenye kumbi za mtandaoni kama Jamii Forums
Nini hasa ni changamoto kubwa wakati unatengeneza post ya kuweka kwenye blog yako na kwanini?
Changamoto yangu kubwa ni kuwa sahihi katika kila ninachoposti kwenye blogu yangu. Kwa uzoefu wa hapa Uingereza na nchi nyingine za Magharibi, kuandika kitu mtandaoni pasipo kuwa na uhakika nacho kunaweza kusababisha matatizo makubwa kisheria. Lakini changamoto nyingine ni lugha. Watu wengi ninaofahamiana nao tangu nifikie hapa Uingereza takriban miaka 10 iliyopita hawafahamu kiswahili. Sasa inawawia vigumu kwao kuelewa ninachoandika japokuwa nimeweka Google Translator kwenye blogu yangu. Miongoni mwa malengo yangu ya baadaye ni kuanzisha version ya kiingereza ya blogu hiyo ili kukidhi matakwa ya wasomaji waiofahamu Kiswahili
Unafanya nini iwapo kuna wakati huna la kuandika kwenye blog yako?
Huwezi kuamini lakini haijawahi kunitokea hata mara moja kukosa cha kuandika. Nilibainisha hapo mwanzo kuwa nina hobby ya kuandika. Hobby yangu nyingine ni kusoma. Hakuna siku ninayopitisha bila kusoma, iwe riwaya, blogu, habari mtandaoni au chochote kile. Hobby nyingine ni habari kwa maana ya zinazotangazwa radioni au kwenye runinga au mtandaoni. Kwahiyo hivyo ni vyanzo vyangu muhimu vya kupata vitu vya kuandika kwenye blogu yangu. Kingine kinachonisaidia sana kupata habari ni maongezi na watu wa kada tofauti za maisha.
Je ni nini mkakati wako na blog yako kwa ujumla?
Lengo la muda mfupi ni kuwa na tovuti kamili. Lengo la muda mrefu ni kuwa na taasisi ya habari, uchambuzi na utafiti. Baadhi ya rafiki zangu huwa wananiona kituko ninapowaambia kuwa malengo yangu ya baadaye sana ni kuanzisha “think tank” au policy institute (yaani taasisi ya sera).Actually, mmoja wa rafiki zangu hao alinipachika jina la one-man think tank, na nimelitundika jina hilo kwenye profile yangu ya Twitter.
Je ni bora kupata ukweli au uchunguzi wa jambo unalotaka kuliandika kwenye blog yako wewe mwenyewe au kupitia mtu mwingine?
Ni vigumu kwa mimi au blogger mwingine kuwa ndio chanzo pekee cha habari. Kwangu, cha muhimu sio kuwa chanzo cha habari bali usahihi na umuhimu wa habari husika.
Ni jambo gani bora blogger anaweza kutoa kwa wasomaji wake?
Kufundisha,kuhabarisha,kukosoa na/au kuburudisha. Hayo ndio malengo yangu makuu ya blogu yangu,na ninaamini yanaendana na dhima ya vyombo mbalimbali vya habari.
Ni jinsi gani (mtu) anaweza kuelezea style ya yako unavyo blog?
Disgustingly critical.Uandishi wangu unaweza kumkera msomaji anayeangalia tu “upinzani” au “ukosoaji” wangu..Kama mwanastadi wa taaluma ya siasa,msimamo wangu kitaaluma umeelemea zaidi kwenye critical thinking,wanachoita thinking about thinking.
Ni nini imekuwa mkakati wako kwa ajili ya kujenga kujulikana kwa mwenyewe na blog yako?
Binafsi sipendi kujulikana. Mimi ni mtu down-to-earth sana. Ningependa zaidi maandiko yangu yaeleweke na pengine kufanyiwa kazi kuliko mimi binafsi au blogu yangu kujulikana. Na kama kujulikana,basi makala zangu magazetini zingeweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi,lakini hiyo sio priority yangu kabisa.
Kila mtu ana post anayoipenda au anayoichukia. Je wewe ni post ipi unaipenda sana na kwanini? Na ni post ipi unaichukia sana na kwanini?
Binafsi naamini katika kupenda kila ninachokifanya. Napenda kazi zangu. Maana kama mie mhusika nisipopenda ninachofanya nitarajie nini kutoka kwa jamii? Lakini kwa minajili ya kujibu swlai lako,post iliyogusa hisia za wengi ni hii http://www.chahali.com/2010/09/chaguo-la-mungu-mafanikio-ya-kikwete.html Niliandika post hii wakati wa kampeni za Uchaguzi,na moja ya mambo ya kupigiwa mstari ni kwamba ilinukuliwa na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Dokta Willibroad Slaa katika ukurasa wake wa Facebook.Sijawahi kuchukia post yoyote niliyoandika kwa vile siamini kwamba kuchukia kitu ni njia bora ya kukirekebisha.Badala ya kuandika kiitu kisha nikakichukia,mie nakwepa kabisa kuandika kitu cha aina hiyo.
Je ni bloggers wapi ambao wewe unawaangalia na kufuata nyayo zao? Na kwanini?
Kuna bloga gwiji anaitwa Ndesanjo Macha. Huyu ndiye aliyenifundisha kublogu japo si kama tuliwasiliana. Nilitembelea blogu yake, nikafuata maelekezo yake ya namna ya kuanzisha blogu, na hatimaye Kulikoni ughaibuni ikazaliwa. Blogger mwingine ni mwanaharakati mwenzangu, Mwalimu Nkwazi Mhango wa Canada (ambaye pia huandika makala magazetini kwa jina la Mpayukaji Msemaovyo). Kufuata nyayo, well, mie sio mfuasi. Si kwamba ni mbishi kufuata walionitangulia bali naamini katika kufuata njia sahihi. Kwahiyo labda niseme nafuata nyayo za uandishi wa blogu katika namna inavyostahili badala ya kufata nyayo za mtu.You never know, unaweza kufuata nyayo zikakupeleka porini (I’m just kidding). Huwezi amini, lakini kila siku ninajitahidi kupitia takriban kila blogu ya Watanzania wenzangu kupitia Google Reader kwenye kompyuta au kwenye simu yangu. Nathamini kila kazi ya bloga wenzangu japo nitakuwa sitendi haki nisipowataja watu kama Michuzi “Mkubwa naMdogo”,Subi, Maprofesa Mbele na Masangu, Haki Ngowi, Abdallah Mrisho,Mubelwa, Jestina George, Dinahicious na wadogo zangu DjChoka, Sarah (Angalia Bongo) na Faith Charles Hillary (Candy1) na wengineo (kutowataja haimaanishi kuwa siwathamini). Pia nathamini sana kazi iliyotukuka ya Maxence Melo wa Jamii Forums.
Hebu tuambie ni watu gani umewahi kukutana nao wakati ukisughulikia post za kuweka kwenye blog yako?
Kukutana na watu physically hapana. Hilo halijatokea bado. Kukutana na watu through mtandao, hao ni wengi. Kama nilivyobainisha awali, moja ya faida ya kublogu ni kufahamiana na watu mbalimbali. Nimetengeneza marafiki kadhaa (na maadui pia) kupitia fani ya kublogu.
Je unafikiria kuwa unadaiwa na mtu akiyeacha comment/s kwenye blog yako?
Deni kubwa ni pale mtu anapoacha ushauri, ambapo nalazimika kuufanyia kazi. Deni jinginie ni uvumilivu pale mtu anapoamua kuacha comment kwa lugha ya matusi. Inataka moyo kumezea kashfa au matusi lakini I’m not just a grown up kid but thick-skinned too.
Je kunadhamani kujibu comment iliyoachwa kwenye blog yako wakati ukijua kuwa huyo aliyeiandika labda hatarudi kusoma jibu lake tena?
Huwezi jua,labda atarudi.Wanasema bora uamini Mungu yupo ili ukifa na kukuta hayupo you’ll have nothing to lose.Imagine unakufa wakati hukuamini existence ya Mungu, then unafika huko waendapo wafu na kukutana naye mlangoni...Ni salama kuamini kuwa anayeacha comment atarejea,na inapendeza kwa msomaji kuona umethamini comment yake na kuijibu (kama inastahili kujibiwa).
Je, umewahi kufikiria kuacha kupost comment ambayo iko negative kwako na ukijua hamna mtu atakayejua?
Hilo hutokea mara kadhaa.Kuna waungwana flani tulipishana lugha siku za nyuma wanapenda kunitumia comments zisizostahili kuchapishwa bloguni. Hey,my blog is like my home,and I reserve the right to welcome or deny someone kuingia humo. Lugha chafu haina nafasi kabisa katika blogu yangu.
Je unazitreat tofauti au unafikiri watu wanaoacha comment kwenye blog yako na kuacha majina yao yaonekane wazi wanastaili comments zao kujibiwa au hata kuacknowledge kuwa umeona maoni yao?
Mie ni muumini mkubwa wa uhuru.Msomaji ana uhuru wa kuandika jina lake anapoacha comment au kubaki anonymous.Cha muhimu kwangu sio jina la mtoa comment bali umuhimu wa comment yake.Mara nyingi napenda kutoingilia uhuru wa wasomaji kuacha comments zao bloguni kwangu.Kwahiyo napendelea zaidi kutochangia comments unless kuwe na umuhimu wa kufanya hivyo.
Je, unafikiria ni makosa kucomment kwenye blog yako kwa kutumia jina lingine?
Kama una jina lako halisi, na comment unayotoa ni yako binafsi, sioni umuhimu wa kutumia jina la mtu mwingine. Hilo ni kosa kisheria.I think the word for that is identity fraud. Lakini si kosa kutumia nickname au kutotumia jina kabisa kwa maana ya kubaki anonymous.
Je unazichukulia comments zote sawa unazotumiwa kwenye blog yako bila kujali maoni uliachwa?
Kwa hakika ninaheshimu comments zote,except zinazochafua hewa ie za matusi, kashfa, nk.Kwa vile uandishi wangu umetawaliwa zaidi na kukosoa, kamwe sichukizwi na mie mwenyewe kukosolewa. Naamini kujifunza kutokana na constructive criticism.
Je, unaamini comments kwenye blog yako zilizoandikwa kwa urefu sana zinahitaji kuzawadiwa zaidi kuliko zile zilizoandikwa kwa ufupi tu?
Inategemea kama urefu huo wa comment unaendana na uzito wa kilichomo. Comment ya mstari mmoja iliyojaa mantiki ni muhimu zaidi kuliko comment ya nusu ukurasa au ukurasa mzima iliyosheheni “hewa tupu”.Lakini kimsingi, ninazi-treat comment zote kwa uzito unaostahili.
Je wewe ni mtu ambaye uko rahisi kukata tamaa?
Hapana. Kukata tamaa is only for losers.Maisha ni mapambano.Vikwazo katika maisha ni sehemu muhimu ya maisha, na wakati mwingine vinatusaidia kujipanga upya. Hakuna mahala katika cheti cha kuzaliwa cha mwanadamu palipoandikwa kuwa life will treat you fairly. By the way, kukata tamaa hakujawi kumsaidia mwanadamu yeyote kufikia malengo yake. Kuna tofauti kati ya kukata tamaa na kuachana na jambo. Kama mtu anaona hawezi kitu flani basi ni vema akaachana nacho kuliko kupoteza muda kisha kukata tamaa na kuishia kuachana nacho mbeleni. Kila sekunde ni sawa na muujiza usiojirudia maishani. So it’s now or never.
Je unaedit picha zako ili ziwavutie sana wasomaji?
Kama ku-edit kwa minajili ya zionekane kwa ufasaha, jibu ni yes. Lakini kama editing kwa minajili ya kupachika kichwa cha mwarabu kwenye mwili wa mswahili, hapana. Mie nina allergy na photoshopping hususan kwenye uwasilishaji habari kwa umma.
Je unaepuka kuweka post ambazo ziko very controversy kwasababu ya kuogopa watu hawatakubaliana na wewe au huna hizo post?
Bahati nzuri mimi sio mwoga. Nilisoma Tabora Boys High School, enzi hizo ikiwa ni mchepuo wa kieshi, nilipomaliza nikaenda jeshini mwaka mzima kwa mujibu wa sheria. Na baadaye nikapita maeneo flani ya “nusu-jeshi” (paramilitary). Uzoefu huo umeondoa kabisa kitu kinachoitwa uoga. Kwa upande mwingine, kama mwanafunzi wa zamani wa sosholojia, natambua kuwa hakuna kitu kinachoweza kuafikiwa na wote. Kadhalika, natambua umuhimu na uwepo wa mitizamo tofauti. Kwahiyo kabla ya kuandika chochote kile bloguni kwangu huwa natafakari kwa makini kwa kutumia mizani hizo, sambamba na uzoefu wangu binafsi
Je unajisikia vizuri zaidi ukiweka post kwenye blog yako na ukapata maoni ya watu zaidi ya 20 au ukipata maoni ya mtu mmoja mashuhuri tu.
Kwangu,one useful comment is more important than 100 worthless comments. Of course, inapendeza kuona watu wakichangia topic flani lakini what if michango yenyewe ni kwa minajili ya kuandika tu? Nina tabia ya ku-track wanaotembelea blogu yangu kwa kutumia njia mbalimbali zinazopatikana kwa bloggers. Na mara kadhaa ninaona watu wanaotumia muda mwingi tu kwenye blogu yangu lakini hawaachi comment. Hilo sio tatizo kwani angalau kuna mtu amesoma na huenda akafanyia kazi alichokisoma.
Je unasema blog yako kuwa inamafanikio iwapo unapata watu wengi wa kusoma au unapata watu wengi wakuacha comment kwenye blog yako?
Kwangu, mafanikio ya blogu sio idadi ya watu wanaoacha comment au kuitembelea.Mafanikio ni pale ninachoandika kinapochangia jambo flani kwenye jamii. Kama mtu mmoja atatembelea blogu na kuona kitu cha maana, kisha kafanyia kazi kwa manufaa ya jamii, hayo ni mafanikio makubwa kuliko kutembelewa na watu milioni moja wanaopita bloguni “kuosha macho”.
Je blog yako unatumia jina lako kamili au unablog kwa kutumia kivuli kingine na watu wanasoma na kuenjoy blog yako lakini hawajui wewe ni nani?
Ninatumia jina langu kamili la Evarist Chahali. Tatizo ni kwamba nina majina mawili, moja “la kiofisi” (official) na jingine “la mtaani”. Unajua katika baadhi ya mila unapozaliwa unapewa jina la kuzaliwa na kisha unabatizwa (kwa sie Wakristo). Sasa kwa niliokutana nao masomoni au kazini wananifahamu zaidi kwa jina la Evarist, lakini kwa marafiki wa mtaani wananifahamu zaidi kwa jina la Jimmy. Sasa inatokea baadhi ya hao marafiki zangu wa mtaani kuhangaika kufahamu kuwa Evarist wa Kulikoni Ughaibuni ndiye huyohuyo Jimmy wa mtaani. Anyway, sichoki kuwaelimisha na taratibu tatizo hilo linazidi kupungua. Zamani hizo, niliwahi kuandika makala kwenye magazeti “ya udaku” ya Sanifu, Kasheshe na Komesha. Huko nilianzisha safu ya nyota (unajimu “wa kizushi”) na nilikuwa natumia jina bandia la “Ustaadh Bonge”. Mpaka leo baadhi ya marafiki zangu wachache wanaendelea kutumia jina hilo la utani. Lakini kwa sasa natumia jina langu kamili na halisi katika maandiko yangu yote.
Ni nini baadhi ya malengo yako ya mwaka huu kwa ajili ya blogu yako au unaonaje mwenyeew kwa kipindi cha mwaka mmoja ua mitano toka sasa hivi blog ya itakuaje?
Kama nilivyojibu hapo awali, malengo ya muda mfupi ni kuwa na tovuti kamili ya habari, na malengo ya muda mrefu ni kuwa na taasisi kamili ya habari,sambamba na uanzishwaji wa think tank. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, ninataraji blogu yangu itakuwa tovuti kamili.
Je upi ujumbe wako kwa wale watu wanaotaka kuanza kublog?
Ujumbe wangu ni mwepesi tu. Kama Michuzi aliweza, na mimi nimejaribu, kwanini isiwe wewe? Kuanzisha blogu ni kitu rahisi tu palipo na nia. Na kama kuna yeyote anayetaka kuanzisha blogu lakini anakwama kwa namna moja au nyingine, basi namkaribisha kwa mikono miwili kumsaidia katika hilo na hata kumfanyia promosheni ya blogu yake kwenye blogu yangu.
Je kwa maoni yako ni lengo gani kubwa kwa mwanablogger?
Kama nilivyojibu hapo awali,lengo ni kuhabarisha, kufundisha, kukosoa na kuburudisha. Haya ni malengo yangu makuu japo ninatambua kuna wanaoanzisha blogu kwa minajili ya kuweka maisha yao hadharani. Hilo sio kosa lakini ukifungua mlango unapaswa kutambua sio hewa safi tu itakayoingia bali pia hewa chafu, nzi, hata nyoka, nk. Lakini, hey, kila mtu ana uhuru wa kufanya apendacho...kula ile kitu roho inapenda.
Watu wengi wanafikiria kublog kwa ajili ya kupata hela. Je ni nini baadhi ya vidokezo kwa watu wanaofikiria kufanya hivyo? Je, ni ukweli upi wa baadhi ya matarajio yanayohusina na nini kinaweza kufanywa na nini hakiwezi kufanywa wakati wa kublog?
Ni kweli kuna wenye mawazo hayo.Kwa mtizamo wangu, money isn’t everything. Naomba nifafanue: kichaa anaweza kuokota tiketi ya bahati nasibu akawa milionea. Pengine anaweza kutumia utajiri wake kutibu ukichaa wake lakini label ya ukichaa haitamwondoka licha ya fedha zake. Jambazi anaweza kupora fedha na akapata utajiri wa ghafla. Lakini label ya ujambazi itaendela kuwepo, kama si akilini basi mioyoni mwa watu. Na kuna wanaopata fedha kwa kuuza utu wao. Na wote hao wanaweza kupoteza fedha na utajiri wao kama mzaha vile.Kwa huyo kichaa anaweza kuzimalizia kwenye matumizi ya kiendawazimu. Kwa jambazi anaweza pia kuzitapanya kwa vile hakuzitolea jasho kihivyo. Kwa upande mwingine, vitu kama elimu vinaendelea kubaki milele maishani unless mwenye elimu akatwe kichwa, which means death. Nikilipwa mamilioni kwa kublogu ilhali mamilioni ya Watanzania wenzangu wakitarajia nitumie elimu yangu kusaidiana nao kuitengeneza Tanzania bora, nitabaki kuwa msaliti. Sintokuwa tofauti na huyo kichaa au jambazi aliyefuma utajiri.Ndio,fedha ni muhimu kwa minajili ya kumudu maisha lakini kuna tuzo kubwa maishani zaidi ya fedha. Na kama bloga,tuzo kubwa kwangu sio udhamini mnono wa blogu yangu bali michango wake katika jamii yetu.
Asanteni kwa mahojiano haya.
Tunashukuru sana hapa Tanzania Blog Award kwa kufanya mahojiano na sisi na tunakutakia mafanikio mengi katika blog yako.
If you or someone you know would be great for our Weekly Blogger Interview, please [email protected] and tell us!

4 comments:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube