29 Jul 2011

Raia Mwema Ughaibuni
Ya Rupert Murdoch na somo kwa wabunge wetu
Evarist Chahali
Uskochi
27 Jul 2011
Toleo na 196
Rupert Murdoch
MOJA ya matukio yatakayobaki kama historia, kwa mwaka huu, hapa Uingereza, ni lile lililojiri wiki iliyopita ambapo tajiri mkubwa wa vyombo vya habari duniani, Rupert Murdoch, alihojiwa na kamati moja ya Bunge dogo(House of Commons) kuhusu tuhuma za udukuzi wa simu (phone hacking simu).
Murdoch, Mmarekani mwenye asili ya Australia, pamoja na mwanaye James, walihojiwa na Kamati ya Bunge ya Utamaduni, Vyombo vya Habari na Michezo kuhusiana na kashfa ambayo tayari imesababisha tajiri huyo kufunga lililokuwa gazeti lake maarufu duniani la News of the World. Gazeti hilo linatuhumiwa kuwa kwa miaka kadhaa limekuwa likifanya udukuzi wa simu za watu mbalimbali kwa minajili ya kupata siri zao.
Lengo la makala hii sio kueleza kwa undani kuhusu kashfa hiyo; bali kuonyesha namna wenzetu hawa wanajivyojitahidi kadri wawezavyo kuweka kando kujuana pale inapohitajika kusaka ukweli kuhusu masuala yenye umuhimu kwa jamii.
Murdoch amekuwa na mahusiano ya karibu na wanasiasa mbalimbali hapa Uingereza na huko Marekani huku akitumia vyombo vyake vya habari kuwasapoti wanasiasa anaotaka washinde kwenye chaguzi kwa matarajio ya kudumisha himaya yake ya kibiashara ambayo imesambaa nchi kadhaa duniani.
Lakini ukaribu wake huo na wanasiasa haukuweza kumwepusha kuwekwa kitimoto na kamati hiyo ya bunge ambapo alibanwa vilivyo na wabunge.
Awali, tajiri huyo na mwanaye walionyesha kutotaka kuitikia mwito wa kamati hiyo kuhudhuria mahojiano hayo, lakini tishio kwamba hatua za kisheria zingechukuliwa hatua zao liliwafanya wabadilishe mawazo.
Siku moja baadaye, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alilazimika kukatisha ziara yake barani Afrika ili kuhudhuria kikao cha dharura cha Bunge na kutoa tamko rasmi kuhusiana na suala hilo la hacking.
Cameron anaguswa na kashfa hiyo kwa vile aliyekuwa Mkurugenzi wake wa Habari, Andy Coulson (aliyelazimika kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kashfa hiyo) alikuwa mhariri wa gazeti la News of the World huko nyuma.
Laiti wabunge wetu Tanzania wangepata fursa ya kuona jinsi Waziri Mkuu huyo alivyobanwa na maswali ya wabunge mbalimbali kuhusiana na uamuzi wake wa kumwajiri Coulson, ninaamini wangeweza kubaini kwa kiasi kikubwa mapungufu yao katika kuibana serikali yetu iwapatie majibu ya maana kwa maswali mbalimbali yanazowasilishwa bungeni.
Lakini kama hiyo haitoshi, kashfa hiyo tayari imesababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa afisa wa juu kabisa wa polisi wa hapa, Sir Paul Stephenson, pamoja na aliyekuwa msaidizi wake, John Yates. Wawili hao pamoja na maafisa wengine wa Scotland Yard wanatuhumiwa kuwa na ushirika usiofaa na vyombo vya habari vya Murdoch, sambamba na tuhuma za kupokea rushwa.
Hadi hapa unaweza kujiuliza: Kwa nini hadi sasa hakuna mtendaji yeyote wa chombo cha dola huko Tanzania aliyewajibishwa katika kashfa ya wizi wa fedha za EPA; japo ni ukweli usiopingika kuwa kufanikiwa tu kwa wizi huo ni mapungufu ya wazi ya viongozi hao na taasisi wanazoziongoza.
Kwa bahati nzuri au mbaya, wakati matukio hayo yakijiri hapa Uingereza, huko nyumbani nako kulitokea matukio mawili makubwa. La kwanza ni kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga kwa tiketi ya CCM, Rostam Aziz na jingine ni sakata la tuhuma za rushwa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.
Kama alivyobainisha mwenyewe kwenye hotuba yake ya kujiuzulu, uamuzi wa Rostam unatafsiriwa na wengi kama kuepukana na tuhuma zilizokuwa zikimwandama kwa muda mrefu kuhusu ufisadi. Wakati uamuzi huo unaweza kustahili pongezi kwa vile kujiuzulu si utamaduni uliozoeleka katika Tanzania yetu, baadhi yetu tunaendelea kutarajia kuwa vyombo vya dola vitatekeleza wajibu wake na kumchunguza mfanyabiashara huyo.
Ikumbukwe kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete, alimpigia kampeni Rostam na “kumsafisha” kwa utetezi kuwa hajawahi kushtakiwa kwa kosa lolote lile.
Kila anayafahamu mwenendo wa nchi yetu anafahamu bayana kuwa kati ya muda huo hadi Rostam anajiuzulu, hakujawahi kutokea tukio lolote lile la kuashiria kinyume na utetezi wa Kikwete kwa mfanyabiashara huyo.
Haihitaji japo kozi ya muda mfupi ya uchambuzi wa siasa kubashiri kuwa kilichosababisha Rostam ajiuzulu sio “kelele za akina Nape na Chiligati” pekee; bali ukweli kuwa “kelele” hizo zilikuwa na Baraka za Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho; yaani Rais Kikwete.
Swali linalohitaji majibu ni ni hili: Kwa nini Rais Kikwete alim-kapenia Rostam na “kumsafisha”; ilhali wakati huo alikuwa na tuhuma ambazo hatimaye ziliibua dhana ya “uvuaji gamba” ya CCM na kuanzisha “kelele za kina Nape” ambazo mwishowe zilimfanya Rostam “kukubali yaishe”?
Hapa, simaanishi kuwa kila mwanasiasa anayejiuzulu wadhifa wake anastahili kuchunguzwa; bali ninaamini takriban kila Mtanzania anafahamu kuwa tuhuma za ufisadi dhidi ya Rostam hazikuanza jana na haziwezi kumalizwa kwa uamuzi wake wa kujiuzulu.
Kama Rostam amejiuzulu kwa vile yeye alikuwa miongoni mwa “magamba” yaliyopaswa kuvuliwa, na magamba hayo yanamaanisha tuhuma za ufisadi, basi lazima vyombo vya dola vianze uchunguzi dhidi yake haraka.
Kuhusu Jairo, tukiweka kando kichekesho cha kumsimamisha kazi kwa siku 10 “ili ajibu tuhuma zinazomkabili” (sijui kuna mahabusu wangapi huko mahabusu walipewa japo siku 1 ya kujitetea kabla ya kutupwa selo), na tukiweka pembeni kusuasua kwa Waziri Mkuu Pinda kuchukua hatua dhidi ya mtendaji huyo (huku akimtupia mpira bosi wake Kikwete), kisichoingia akilini ni kwa nini Katibu Mkuu wa wizara ahangaike kuhonga wabunge ili bajeti ya wizara ipite!
Sote tunafahamu anayewasilisha bajeti ni waziri wa wizara husika. Kama kuna mtu “anayeumbuka” pindi bajeti ya wizara ikikwamishwa, ni waziri na si katibu mkuu wa wizara husika. Kwa nini basi Jairo abebeshwe mwenyewe lawama. Vipi bosi wake (waziri)? Vipi wakuu wa idara? Vipi asasi za wizara zilizotoa fedha hizo za rushwa kinyume cha taratibu?
Kwa nini tusihisi kuwa mtendaji huyo alikuwa akitekeleza maagizo aliyopewa na mabosi wake? Swali la msingi zaidi ni je mabosi hao wanaishia ngazi ya wizara tu au ni zaidi ya hapo?
Lakini suala hili la Jairo linaweza kutupa mwamko wa namna fulani kuhusu muundo wa sasa wa serikali ambapo licha ya waziri mkuu kuwa mkuu wa shughuli za serikali bungeni, mkuu halisi wa serikali ni Rais. Katika mazingira ya siasa za kibabaishaji, ni rahisi sana kwa waziri mkuu kukwepa majukumu muhimu kwa kisingizio cha “mwenye uamuzi wa mwisho ni Rais”.
Kwa bahati mbaya, hakuna mahala ambapo wananchi au wawakilishi wao (wabunge) wanapata fursa ya kumbana Rais (isipokuwa wakati wa Uchaguzi ambapo kwa wakati huo maji yanaweza kuwa yameshamwagika na hayazoleki).
Hivi katika umasikini huu mkubwa tulionao kuna umuhimu kweli wa kuwa na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ambao kimsingi mmoja tu kati yao angeweza kutekeleza majukumu ya vyeo vyote hivyo vitatu?
Na kama inafika mahala Waziri Mkuu anakuwa kama Naibu Waziri (kwa maana ya Naibu kusema “mwenye kuweza kujibu swali hili ni Waziri” na Waziri Mkuu kusema “mwenye uwezo wa kutoa maamuzi haya ni Rais), basi, pengine ni muhimu kwa mabadiliko tarajiwa ya Katiba yakaangalia uwezekano wa kuunganisha nyadhifa hizi mbili (urais na uwaziri mkuu).
Kuna wanaolalamika kuwa ziara za Rais Kikwete nje ya nchi zinaelekea kuvunja rekodi. Lakini pengine kama Rais ndio angekuwa “bize” kwa kukabiliwa na majukumu ya uendeshaji wa serikali kila siku (kwa kuunganisha wajibu wa Rais na Waziri Mkuu), basi, huenda hata huo muda wa ziara mfululizo za nje ya nchi zingepungua.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube