13 Oct 2011


Kama nilivyobashiri kwenye MAKALA HII,Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Benno Malisa ameundiwa zengwe zito kufuatia kauli zake jijini Arusha ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka viongozi wenzie wa CCM kuacha kuiandama Chadema.

Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa kwenye jarida la Raia Mwema,Malisa anadaiwa kuwa amekuwa akiandaa mazingira mazuri kwa ajili ya Edward Lowassa endapo harakati za kuvuana magamba ndani ya chama hicho zitamkumba.

Japo tuhuma dhidi ya Malisa zinahusishwa zaidi na kitendo cha yeye kufungua mashina ya UVCCM (ambapo anadaiwa kufanya hivyo pasipo kushirikisha uongozi wa umoja huo ngazi ya mkoa) yayumkinika kuamini kuwa kilichomponza kiongozi huyo wa UVCCM Taifa ni kauli zake za kutaka demokrasia ya kiutu-uzima,sambamba na kuikumbusha CCM wajibu wake kuwatumikia Watanzania.

Na hili ndilo tatizo litakalopelekea mauti ya chama hicho kingongwe.Kiongozi au mwanachama yeyote yule atakayeamua kuongea ukweli ataanza kusakamwa na si ajabu akajikuta anavuliwa madaraka,CCM imekuwa ikiongoza nchi kwa namna ya uchawi wa kuwafumba macho Watanzania.Licha ya vyama vya upinzani (hususan Chadema) kuwaamsha Watanzania kuwa chama hicho tawala kinaendesha nchi kwa siasa za kimafia,CCM imekuwa ikijitetea kwa kuwaita wapinzani wachochezi na watu wa majungu,huku ikitumia taasisi za dola kupandikiza migogoro kwenye vyama hivyo.

Sasa anapotokea kiongozi au mwanachama wa kawaida wa chama hicho kuakisi yale yanayosemwa na wapinzani (aambayo kimsingi ni mtizamo wa Watanzania wengi) basi ataandamwa huyo hadi aonekane kama mhaini flani.

Wanachojisahau CCM ni ukweli kwamba kuficha ugonjwa hakuwezi kuwa sehemu ya tiba ya ugonjwa husika.Hata akina Malisa wakikaa kimya na kufuata porojo za "mshikamano wa chama" au "umoja wa kitaifa" ukweli unabaki kuwa ipo siku umma utaamka na kuking'oa chama hicho kwa nguvu kwani wanaweza kudanganya umma wote kwa muda fulani lakini hawawezi kuudanganya milele.

Anyway,soma habari husika hapa chini


Wakati huo huo, hali ya kisiasa ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) ni tete ikibainika kuwa Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Benno Malisa, ameanza kucheza hadharani siasa uasi zinazoendeshwa na kambi inayotajwa kuwa ni ya kigogo mmoja wa CCM mkoani humo. 
Malisa sasa anahusishwa na tukio la hivi karibuni linalohusisha na ufunguzi wa mashina ya chama hicho Arusha mjini, unaotajwa kuratibiwa kinyemela bila viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa kutoa kufahamishwa na kwamba, sehemu ya waratibu wa tukio hilo ni vijana waliosafirishwa kutoka wilayani Monduli. 
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa tukio hilo halikushirikisha viongozi wa UVCCM mjini Arusha na viongozi wengine wa chama hicho. 
“Mipango yote kwa kiasi kikubwa imeratibiwa na watu wa kutoka wilayani Monduli. Inasemekana kuwa hii ni sehemu ya mkakati wa maandalizi ya watu hao kumhami Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa endapo atabanwa kwenye mkakati wa kujivua gamba wa CCM, basi wajifanye kushusha bendera za CCM kwenye mashina hayo ili kuuonyesha umma kuwa anakubalika sana ndani ya chama,” anasema mmoja wa watoa taarifa wetu ambao ni vijana waliohusika kuratibu mpango huo. 
Hali kama hiyo ya kujiandaa kwa ajili ya mchakato wa kujivua gamba ilijitokeza wakati aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz pale alipotangaza kujiuzulu baadhi ya vijana waliandaa mabango yenye ujumbe unaomtaka ajisiuluzu na wengine wakihoji hatua hiyo huku taarifa zikisema mabango hayo yaliandaliwa muda gani wakati alikuwa bado kutangaza kujiuzulu. 
Kiongozi mmoja wa UVCCM Arusha anaeleza; “UVCCM Arusha mjini walikataa utekelezaji wa mkakati huo haramu kupitia kikao chake cha Kamati ya Utekelezaji kilichoketi Oktoba 7, mwaka huu, kwa kumwandikia barua Katibu wa Vijana CCM mkoani Arusha.” 
Inaelezwa kuwa barua hiyo ilimjulisha kiongozi huyo kuwa wao kama wilaya hawajapata taarifa rasmi za uzinduzi wa mashina hayo ya wakereketwa na hivyo kwa muda uliobaki wasingeweza kufanya maandalizi mazuri ikizingatiwa wao ndio wenye jukumu la kuandaa mashina hayo na si Wilaya ya Monduli. 
“CCM Mkoa baada ya kupata nakala ya barua hiyo waliamua kuitisha kikao cha sekretariati ya mkoa pamoja na kamati ya utekelezaji ya vijana Mkoa wa Arusha na Wilaya Arusha mjini, Oktoba 8, 2011. 
“Katika kikao hicho maazimio yalikuwa ni kusitisha zoezi hilo hadi hapo taratibu za chama zitakapofuatwa. Chama Mkoa walimwandikia barua hiyo Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha ili aweze kuwataarifu na viongozi wengine pamoja na wanachama wa umoja wa vijana wa CCM. 
“Baada ya kupata barua hiyo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya, alifanya kikao cha faragha na Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na Benno Malisa. Baada ya kikao chao hicho, waliamua kufanya shughuli hiyo iendelee kama walivyokusudia pamoja na chama kukataza. 
“Jumatatu, Oktoba 10, 2011 walianza kushughulikia kibali cha maandamo na uzinduaji mashina hayo. Hadi saa nne asubuhi polisi waliwanyima kibali cha kazi hiyo,” alisema mtoa habari wetu mwingine ambaye naye amekataa kutajwa jina lake gazetini. 
Inaelezwa kuwa mkutano huo wa kufungua mashina uliofanyika 10/10/2011, ulihudhuriwa na vijana kutoka Monduli na vijana wengine wa vyama mbalimbali vya siasa. 
Katika shughuli hiyo, Benno Malisa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alishambulia wazi wazi chama chake akitetea Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema) chini ya mwavuli wa demokrasia na utawala bora. 
Katika hotuba yake hiyo, Benno Malisa amekejeli hata kauli ya viongozi wenzake wa CCM wanaoonyesha kwamba CCM ni chama tawala na kuonya dola kuingilia mambo ya siasa, hali inayozidi kuashiria mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho tawala.

CHANZO: Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.