6 Nov 2011

CCM dhaifu mtaji imara wa urais CHADEMA, CUF

Uskochi
NIANZE makala hii kwa kutoa salamu za pongezi kwa jarida hili la Raia Mwemaambalo limetimiza miaka minne tangu kuanzishwa Oktoba 30, 2007. Binafsi, jarida hili limekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu tangu nilipopewa fursa ya kuandika safu hii.
Lakini kubwa zaidi ni jinsi jarida hili lilivyosimama imara na kuwa sauti ya wasio na sauti (wanyonge), likifukua ufisadi na kuhabarisha umma pasipo upendeleo.
Pasi na shaka yoyote, Raia Mwema linastahili kuitwa gazeti la rekodi, yaani unaloweza kulitumia kunukuu chochote kile bila hofu kuwa huenda kimekosewa au kimeandikwa kwa unazi. Sitoi sifa hizi kwa vile ni mwandishi wa makala gazetini humu lakini ninaamini kila anayependa kuhabarishwa kwa ufasaha na umakini ataafikiana nami kuwa Raia Mwema limeonyesha njia sahihi ya uandishi wa habari na makala.
Baada ya pongezi hizo za dhati nielekee kwenye mada ya wiki hii. Mada hii ni mwendelezo wa ile ya wiki iliyopita ambayo iliangalia mazingira yanayotarajiwa ya chama tawala katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao hapo mwaka 2015.
Wiki hii ninajaribu kuangalia hali ilivyo katika vyama viwili, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF), ambavyo kwa sasa vinastahili kuitwa vyama vikuu vya upinzani.
Urais ndani ya CUF
Kuna msemo mmoja wa Kiingereza ambao katika tafsiri yake ya Kiswahili ni kama hivi: “Jambo zuri si lazima liwe jambo sahihi.” Kwa mfano, kumpatia chakula kingi mtu mwenye njaa kali kunaweza kusababisha kumuua mtu huyo bila kukusudia.
Mantiki ya usemi huo ni kwamba kuna nyakati tunafanya mambo kwa kuamini ni vizuri kufanya hivyo, lakini matokeo yake yanaweza kuwa mabaya kuliko matarajio. Kwa kurejea msemo huo wa Kiingereza, sote tunafahamu kuwa mtu mwenye njaa kali anahitaji chakula.
Lakini kabla ya kumpatia chakula ni vema kumpatia kinywaji cha moto kama vile chai au uji (kama wanavyofanya watu waliofunga). Kumpatia mtu huyo ugali mwingi kunaweza kusababisha akavimbiwa na pengine kuishiwa pumzi au hata kumpotezea uhai.
Chama cha CUF kililazimika kukaa meza moja na wapinzani wao wa CCM huko Zanzibar na hatimaye kufikia mwafaka na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hilo lilikuwa jambo zuri (kama kumpatia chakula mtu mwenye njaa kali).
Lakini matokeo ya uamuzi huo wa busara yameiacha CUF huku Bara (na pengine hata huko Zanzibar) ikiwa haina mwelekeo. Kimsingi, chama hicho ni nusu ya serikali inayotawala kwa vile kimetoa Makamu wa Kwanza wa Rais kuongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Na katika kutekeleza kanuni ya uwajibikaji wa pamoja, CUF hawawezi kuinyooshea kidole CCM huko Zanzibar pindi mambo yakienda kombo.
Naomba ieleweke kuwa si kama ninailaumu CUF kwa kukubali mwafaka na CCM bali ninachoonyesha hapa ni madhara yasiyokusudiwa ya uamuzi huo. Ni vigumu kubashiri chama hicho kitaendeshaje kampeni “za maana” mwaka 2015.
Katika mazingira ya siasa za Zanzibar ni dhahiri kuwa kutakuwa na umuhimu wa kuendelea na serikali ya umoja wa kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Lakini ili hilo liwezekane itabidi kampeni katika uchaguzi huo ziwe za “kistaarabu” (ambalo ni jambo zuri isipokuwa tu linaweza kupunguza hamasa ya kisiasa kwa baadhi ya wapigakura).
Hoja hapa ni kwamba kama CCM itashinda na kisha kuunda serikali ya pamoja na CUF kuna haja gani basi ya kufanya kampeni za nguvu ambazo hazitabadili picha ya matokeo ya uchaguzi huo?
Na hata kama CUF wataamua waendeshe kampeni za nguvu ili kupata ushindi mkubwa, watawezaje kuonyesha kuwa CCM haistahili ushindi ilhali vyama vyote viwili vilikuwa madarakani (na hivyo kustahili sifa kwa mema au lawama kwa mabaya waliyofanya katika muhula wa 2010-2015)?
Kwa nini mazingira ya Zanzibar ni muhimu kwa hatima ya CUF kwa nchi nzima? Kwa sababu kila anayefahamu siasa za nchi yetu anatambua kuwa nguvu kubwa ya chama hicho ipo huko Visiwani. Lolote linalotokea huko linakigusa chama hicho kwa upande wa Bara na Muungano kwa ujumla.
Urais ndani ya CHADEMA
Sote tunakumbuka yaliyoikumba NCCR-Mageuzi baada ya mgombea wake Augustine Mrema kubwagwa na mgombea wa CCM, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, katika uchaguzi wa mwaka 1995.
Licha ya kushindwa katika chaguzi mbili mfululizo (mwaka 2005 na mwaka jana), CHADEMA imeendelea kuwa imara huku mgombea wake katika uchaguzi uliopita Dk. Willibrod Slaa akiendelea kuwa na hadhi ileile aliyokuwa nayo kama mgombea urais.
Kulikuwa na hofu kuwa laiti Dk. Slaa angeshindwa kwenye uchaguzi uliopita basi angepotea kabisa kwenye ulingo wa siasa za nchi yetu lakini hali imekuwa tofauti kabisa. Licha ya kubaki Katibu Mkuu tu wa CHADEMA (wadhifa aliokuwa nao kabla ya kugombea urais na kushindwa), mwanasiasa huyo ameendelea kuwa na mvuto mkubwa huku mikutano anayohutubia ikiendelea kupata wasilikizaji.
Lakini si Dk. Slaa pekee ambaye ameendelea kuwa na umaarufu na mvuto bali hata chama chake kimemudu kubaki tishio kwa chama tawala CCM.
Ukifuatilia kwa karibu malumbano ya kisiasa yanayoendelea nchini, unaweza kudhani kuwa bado tupo kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita au uchaguzi mwingine utafanyika hivi karibuni tu.
Moja ya mitaji mikubwa ya CHADEMA ni msimamo wake kuhusu mustakabali wa taifa. Chama hicho kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujitambulisha na kukubalika kama kitovu cha harakati za mapambano dhidi ya ufisadi.
Bahati nzuri kwa CHADEMA ni namna CCM inavyoshindwa kujiondoa kwenye utando wa ufisadi, ambapo pamoja na mambo mengine suala la kujivua magamba ni kama kuafikiana na CHADEMA kuwa CCM ni kichaka cha mafisadi na hivyo chama hicho kikongwe hakina budi kujisafisha.
Mtaji mwingine wa CHADEMA ni mshikamano miongoni mwa viongozi wake wakuu na wa kada ya kati. Sina hakika sana hali ipo vipi katika ngazi za chini lakini kwa kiasi kikubwa CHADEMA inainyima usingizi CCM.
Kama mazingira yatabaki jinsi yalivyo sasa, kuna uwezekano wa CHADEMA kumteua tena Dk. Slaa kuwa mgombea wake hapo 2015. Mwanasiasa pekee anayeweza kubadili hali hiyo ni Naibu Katibu mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto, ambaye aliwahi kunukuliwa akisema kuwa angegombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mtaji mwingine mkubwa kwa CHADEMA ni hali ya mambo ndani ya CCM na mazingira yanavyotarajiwa kuwa katika mchakato wa chama hicho tawala kupata mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu ujao (ambayo niliyaelezea kwa kirefu katika makala iliyopita).
Kama kuna nafasi yoyote kwa CHADEMA au chama kingine cha upinzani kuindoa CCM madarakani ni mwaka 2015 kwani kuna kila dalili kuwa sokomoko linaloendelea ndani ya chama hicho tawala litadumu hadi kitakapofanikiwa kupata mgombea wake. Laiti CHADEMA wakiafikiana mapema kuhusu mgombea wao katika uchaguzi huo basi watakuwa na muda wa kutosha kuandaa mazingira ya ushindi huku CCM wakiendelea kupigana vikumbo.
Lakini kuna busara moja ya kuzingatia katika msemo ufuatao: “Siasa si kama fumbo la hesabu ambapo siku zote 2 kujumlisha 2 jibu ni 4. Katika siasa jibu linaweza kuwa 100 au kwa kukatisha tamaa zaidi jibu likawa 0.” Licha ya kuwa siasa ni mchezo mchafu, kipindi cha miaka minne kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao ni kirefu sana katika siasa na lolote linaweza kutokea kinyume kabisa cha uchambuzi huu.
Katika moja ya makala zijazo nitaingia kwa undani kujadili mambo yanayoweza kuikwamisha CHADEMA (au chama kingine cha upinzani) kuing’oa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa leo tuishie hapa

0 comments:

Post a comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2020

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube