13 Jan 2012


Waziri Magufuli ashughulikiwe

Kejeli ya kupiga mbizi
BAADA ya makala yangu katika toleo lililopita la gazeti hili ambapo nilijaribu kutabiri kuhusu masuala mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa mwaka huu 2012, nimepokea maoni kadhaa, hususan kuhusu utabiri huo kugusia masuala machache tu.
Kama nilivyobainisha katika makala hiyo, kugusia kila nyanja ya maisha kungehitaji makala zaidi ya moja. Na kutokana na ufinyu wa muda na nafasi, nilidhani ni vema kugusia maeneo machache tu ya muhimu.
Lengo la makala hii si kuendeleza utabiri huo bali ni mwendelezo wa mjadala kuhusu masuala muhimu kwa ustawi wa taifa letu.
Miongoni mwa matukio yanayoweza kutafsiriwa kama mwanzo mbaya wa mwaka huu ni sakata lililotokana na tangazo la Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuhusu nyongeza ya nauli katika kivuko cha Kigamboni.
Kilichozua sokomoko kubwa si ongezeko hilo bali kauli ya kihuni ya Waziri Magufuli kwamba “wasiomudu ongezeko la nauli hiyo wapige mbizi.”
Inasikitisha kuona mmoja wa watendaji wachache kabisa wa Serikali ambao wanaonekana kujali maslahi ya umma na taifa kwa ujumla, anaingia kwenye kundi la watendaji wengi ambao kauli zao zinaweza kabisa kutuaminisha kuwa ushirikiano kati ya ubongo wao na midomo yao ni haba kama sio sifuri kabisa.
Hivi Magufuli angepungukiwa na nini kama angetumia kauli za kistaarabu tu kwamba japo anasikia vilio vya watumiaji wa kivuko hicho kuhusu ongezeko hilo la nauli, kuna kila sababu ya uamuzi huo kubaki kama ulivyo.
Hakukuwa na haja ya kutumia lugha ya kebehi na dharau. Lakini kama lugha hiyo ya kihuni haitoshi, Waziri huyo msomi ameendeleza ubabe wake sio tu kwa kueleza kuwa hatojiuzulu wala kuomba msamaha, bali pia kuwashushia lawama nzito wabunge wa majimbo ya Jiji la Dar es Salaam.
Pengine ni muhimu kujiuliza Waziri Magufuli amepata wapi jeuri hii. Jibu rahisi ni kwamba huhitaji kuwa mchambuzi wa siasa za nchi yetu kubaini kuwa chanzo kikubwa cha jeuri na utendaji mbovu wa watendaji wengi wa serikali yetu ni kiongozi aliyewateua. Hapa ninamaanisha Rais Jakaya Kikwete.
Mwanzoni mwa mwaka 2006, muda mfupi baada ya kuingia madarakani kwa mara ya kwanza, Rais Kikwete alitoa hadhari kwamba tabasamu lake lisitafsiriwe vibaya.
Huku akiweka wazi kuwa anawafahamu wala rushwa kwa majina, Kikwete alitoadeadline kwa wala rushwa hao kujirekebisha vinginevyo wangemtaka ubaya. Kadhalika aliwaonya watendaji wanaozembea majukumu yao akisisitiza kuwa asingekuwa na huruma nao.
Miaka sita baadaye ni wazi kuwa ‘mkwara’ huo wa Kikwete ulikuwa ni kama sehemu ya kutimiza majukumu yake ya kusema chochote. Sio tu kwamba hakuna mla rushwa aliyezingatia deadline hiyo bali pia baadhi ya watendaji wake wamepata ujasiri kutokana na upole wa kupindukia wa ‘bosi’ wao ambaye yayumkinika kuhitimisha kuwa ni mwoga wa kutumia ipasavyo mamlaka yake aliyopewa na Katiba kuchukua hatua stahili dhidi watendaji wabovu.
Laiti Kikwete angekuwa ‘mkali japo kidogo’ kwa watendaji wake basi ni wazi Magufuli angefikiri mara mbili kabla ya kuwabwatukia watumiaji wa kivuko cha Kigamboni.
Ikumbukwe kuwa moja ya turufu muhimu kwa Kikwete wakati anagombea nafasi ya urais mwaka 2005 ilikuwa ni hoja kuwa ni ‘mtoto wa mjini’ na ni ‘mtu wa watu.’
Japo si lazima kila kiongozi awe ‘mtoto wa mjini’ lakini sifa hiyo inaweza kuwa ya msaada mkubwa kwa kiongozi kwani inamwezesha kuelewa mambo mbalimbali hata pasipo kutegemea taarifa mbalimbali anazoletewa na wasaidizi wake.
Naomba kusisitiza kuwa neno ‘mtoto wa mjini’ hapa limetumika kwa maana chanya likiashiria mtu anayelielewa Jiji la Dar es Salaam kwa marefu na mapana.
Kwa maana hiyo inatarajiwa kuwa Kikwete anafahamu fika kuwa kauli ya waziri wake Magufuli sio tu ni mithili ya matusi kwa wakazi wa Dar es Salaam wanaokitegemea kivuko cha Kigamboni kwa maisha yao, bali pia inatia mawaa kwa utawala wake.
Hivi ni vigumu kiasi gani kwa Rais Kikwete kumwita Magufuli na kumfahamisha kuwa lugha aliyotumia si nzuri, na anapaswa kuwaomba msamaha aliowatukana?
Hivi Rais hafahamu kuwa ukimya wake katika suala hili unaweza kutafsiriwa kama kumuunga mkono waziri wake au yeye kuwa na mtizamo kama wa Magufuli kuwa wasiomudu nauli hiyo wapige mbizi?
Japo Kikwete hakumtuma Magufuli kutoa kauli hiyo chafu lakini kwa vile ni yeye aliyemteua kushika wadhifa huo, na kwa vile kama ‘mtu wa watu’ anaelewa kuwa kauli ya waziri wake si nzuri, kwa nini basi ‘asijikongoje’ na kumsaidia mtendaji wake na kuisadia Serikali yake isionekane ina watendaji wanaopuuza vilio vya wananchi?
Kama nilivyoandika katika makala yangu kwenye toleo lililopita kuwa mwaka huu 2012 utaendelea kuwa wa machungu kwa Watanzania kwa vile moja ya kasoro za Rais wetu ni kusita kuchukua hatua za haraka pale mambo yanapokwenda mrama, hususan chanzo kinapokuwa mmoja wa watendaji wake.
Ukweli mchungu ni kwamba kama kauli ya kebehi ya Magufuli itaachwa kama ilivyo inaweza kuzalisha kasumba kwa viongozi wengine kuwatukana wananchi pasipo hofu ya kukemewa na aliyewapa nyadhifa husika.
Kwa upande mwingine siafikiani kabisa na sababu alizotoa Waziri Magufuli kuhusu ongezeko hilo la nauli. Kigezo kuwa nauli za awali ni pungufu kulinganisha na nauli katika vivuko vingine ni ya kipuuzi kwa sababu hata kama kiwango cha nauli katika kivuko kilichopo mkoani ingekuwa Sh. 500 lakini kinatumiwa na watu 200 kwa siku, kivuko cha Kigamboni kinatumiwa na watu wengi zaidi kiasi kwamba hata kiwango cha nauli cha Sh. 200 kwa watu 5,000 kwa siku kingezalisha fedha zaidi.
Kadhalika, hakuna uthibitisho wowote kuonyesha kuwa ongezeko hilo la viwango vya nauli kwa kivuko cha Kigamboni litaongeza mapato zaidi kwa Serikali kwani busara nyepesi tu inabainisha kuwa, kama mafisadi walimudu kuiba kidogo kilichopatikana kutokana na nauli ya awali, itakuwa rahisi zaidi kwao kuiba mapato yanayotarajiwa kupatikana kutokana na viwango vipya.
Kwa lugha nyingine, kama walikuwa wanaiba kila Sh. 50 katika nauli, sasa wataweza kuiba hata shilingi 100 katika kila nauli.
Tatizo la msingi linalokabili vyanzo vya mapato ya Serikali halijawahi kuwa katika viwango vidogo vya nauli au kodi bali usimamizi wa matumizi ya mapato hayo.
Yayumkinika kubashiri kuwa laiti mapato yanayopatikana kutokana na vivuko vyetu yangesimamiwa na kutumiwa vizuri, basi ndoto za ujenzi wa madaraja kwenye vivuko hivyo zingekuwa zimekwishatimia.
Nirejee kwa Rais Kikwete. Ninaamini anahesabu siku zilizosalia kabla muda wake wa kuwa madarakani haujafikia mwisho hapo mwaka 2015. Kwa hakika bado ana nafasi nzuri ya kuwafanya Watanzania wasahau (ambao kimsingi ni wepesi wa kusahau mabaya) upungufu wote unaoendelea kuufanya utawala wake kuwa dhaifu zaidi ya tawala zilizotangulia.
Lakini hata tukiweka suala hilo la kuwaachia wananchi kumbukumbu nzuri, Kikwete anaweza kuuthibitishia umma kuwa alipotoa hadhari kwamba tabasamu lake lisieleweke vibaya alikuwa serious na sasa ameamua kutafsiri hadhari hiyo kwa vitendo.
Anaweza kuanza na Magufuli; kama kumwambia ana kwa ana kutakinzana na huruma yake kwa watendaji wake basi anaweza kumfikishia ujumbe kupitia kwa makamu wake au waziri mkuu.
Amueleze kuwa ujumbe mzuri unaweza kusababisha matatizo makubwa kama hautowasilishwa kwa lugha ya kistaarabu.
Kwa upande mwingine, Rais Kikwete anaweza kujipatia umaarufu mkubwa iwapo atamwacha Magufuli na jeuri yake lakini akitumia mamlaka yake kama mkuu wa nchi na kubatilisha uamuzi wa waziri huyo kwa kurejesha nauli ya awali.
Na pengine baada ya kufanya hivyo, anaweza 'kufunga bao la kisigino’ kwa kutangaza kuwa uamuzi wa wabunge kujiongezea posho hauendani na hali halisi ya uchumi wetu na Serikali yake haina fedha za kumudu mahitaji yao ya kifahari.
Sababu ya kuchukua uamuzi wa aina hiyo anazo, na mamlaka aliyonayo yanampa uwezo wa kufanya hivyo. Kinachohitajika ni nia tu ya kufanya hivyo.
Laiti akizingatia ushauri huu na kufanya hivyo, sio tu Watanzania wengi watarejesha imani kuwa ‘Kikwete ni mtu wa watu’ bali hata wale waliosema yeye ni chaguo la Mungu wanaweza kupata ujasiri wa kurejea kauli hiyo (kwa vile kiongozi ambaye ni chaguo la Mungu hawezi kulea mafisadi, viongozi wazembe na hao wenye kauli za kebehi kama ya Magufuli).


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube