7 Feb 2012


WAFANYAKAZI WA HAZINA, TANESCO NA WIZARA YA NISHATI WAHUSIKA, NGELEJA ATHIBITISHA UCHUNGUZI KUFANYWA
Mwandishi Wetu
SERIKALI inawachunguza baadhi ya maofisa wake waandamizi kwa tuhuma za wizi wa dola50 milioni za Marekani sawa na Sh86 bilioni, zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta mazito ya kuzalishia umeme kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), katika kipindi hiki nchi inapokabiliana na tatizo la uhaba wa nishati hiyo.

IPTL inayozalisha megawati 100 za umeme iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco), lakini utendaji wake umekuwa na mkanganyiko.Chanzo kutoka serikalini kililiambia gazeti dada la The East African la Februari 12, kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwamba baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Hazina na Tanesco, wanahusika katika mpango huo wa wizi.

Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alipoulizwa alijibu, “Ndiyo naweza kuthibitisha upo uchunguzi unaoendelea, lakini ndiyo kwanza upo katika hatua za awali.” Tayari taarifa za awali za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), zinaonyesha kumekuwa na maelezo yaliyokiuka utaratibu wa fedha zilizolipwa na Serikali kwa ajili ya usambazaji wa mafuta mazito kutoka kampuni za ndani.

Ukosefu wa nishati ya umeme unaoikabili nchi kwa sasa unaifanya Tanesco kulipa IPTL dola12 milioni za Marekani sawa na Sh19.2 bilioni kila mwezi, kwa uzalishaji wa megawati 60 badala ya megawati 100.

Mwaka 1995, Tanesco iliingia mkataba na IPTL, mkataba ambao uliihusisha kampuni ya nchini Malaysia , Mechmar Corporation na wawekezaji wa ndani, na VIP Engineering and Marketing Company kwa ajili ya kuzalisha megawati 100 kwa kutumia mitambo inayotumia dizeli kwa miaka 20.Katika mkataba huo, VIP ina hisa ya asilimia 30 na ile ya Mechmar ya Malaysia ikiwa na hisa ya asilimia 70.Serikali ilikubali kulipa kwa ajili ya uzalishaji huo kwa kuwa haikuwa na njia nyingine.

Mpango wa kuifilisi IPTLTayari hivi karibuni Mahakama iliamua IPTL ifiilisiwe na jukumu hilo lilikabidhiwa kwa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (Rita).Hata hivyo, baadhi ya benki zinazoidai IPTL ziliweka zuio mahakamani zikitaka kwanza kulipwa fedha zao ambazo kampuni hiyo ilikopa.IPTL inakadiriwa kuwa na Sh200 bilioni zilizopo Benki Kuu (BoT) ambazo kama ikifilisiwa zingeangukia mikononi mwa Serikali. Kampuni hiyo imekuwa ikiitafuna Tanesco mabilioni ya shilingi tangu kuingia mkataba huo ambao umekuwa ukitajwa kama wa kifisadi, kuliko hata wa Richmond.


Wakati fedha za umma zikitafunwa bila huruma,mgomo wa madaktari unaoendelea kwa siku kadhaa sasa umeingia katika hatua mpya baada ya madaktari bingwa nao kujiunga na mgomo huo,kama inavyoripotiwa hapa chini:

Geofrey Nyang’oro na Florence Majani
WAKATI Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ikianza kazi ya kuzungumza na madaktari walio kwenye mgomo, madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na walio katika Taasisi ya Mifupa (MOI) wamegoma. Mgomo huo wa jana ulihusisha vitengo vyote huku wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo wakipewa taarifa za kuondoka katika wodi walimolazwa.

Azimio la mgomo huo lilifikiwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa na jopo la madaktari bingwa wakiongozwa na Dk James Rwehabura ambaye ni daktari bingwa wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu.

Habari za ndani kutoka katika kikao cha dharura cha wanataaluma hao, zilisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha madaktari hao kilichoanza mapema asubuhi jana na kumalizika saa 6:00 mchana. “Kwa pamoja tumekubaliana kuweka vifaa chini, hii ni kutokana na ukweli kuwa hali ya utoaji huduma katika hospitali hii ni mbaya huku taarifa za Serikali zikiwa siyo za kweli,” alidokeza mmoja wa madaktari bingwa.

Daktari huyo aliyekataa kutaja jina lake, alisema, “Tumekubaliana kugoma hadi hapo Serikali itakapotoa majibu ya madai yote yaliyowasilishwa na jumuiya ya madaktari inayoongozwa na Dk Stephen Ulimboka kwa Serikali.” Jumuiya hiyo iliwasilisha madai mbalimbali likiwamo la kuitaka Serikali kupeleka vifaa na dawa katika hospitali za Serikali ili madaktari hao waweze kutoa huduma bora kwa jamii.

Pia, madaktari hao walitaka kusitisha safari za vigogo kwenda kutibiwa nje kwa magonjwa yanayotibika ndani kwa kile walichodai, hali hiyo inachangia wao kudharauliwa na pia kuzorotesha jitihada za Serikali katika uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa madaktari hao.

Kwa nyakati tofauti, madaktari hao walibainisha sababu ya mgomo wao na kudai kuwa, kikubwa ni mazingira magumu ya kazi. Daktari mwingine ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini alisema, licha ya mishahara na posho ndogo, lakini mazingira ya kufanyia kazi yamekuwa magumu mno.

“Tumeshaamua , ‘tools down’ hospitali haina kitu, hata ‘mask’ hakuna badala yake tunavaa gozi tunapofanya upasuaji, acha hiyo, hata nyuzi za kushonea wakati wa upasuaji hakuna,” alisema daktari huyo. Daktari huyo alisema, hawawezi kufanya kazi katika mazingira hayo kwa sababu yatawasababisha kuwa na utendaji mbovu na baadaye taifa kuwalalamikia.

Alisema hapa nchini madaktari bingwa ni wachache, kwa hiyo kitendo cha wao kufanya kazi peke yao bila wasaidizi, yaani madaktari wa mafunzo na wale wanaomaliza, wanaelemewa na mzigo wa kazi. Dk Henry Mwakyoma, Mhadhiri Mkuu wa Chuo cha Udaktari Muhimbili, (MUHAS) ambaye hakuwapo katika kikao hicho cha dharura alidai kuwa, yeye kama mhadhiri hajagoma, lakini alikiri kuwapo kwa mazingira magumu ya kazi.

“Mpaka sasa hatujalipwa mishahara ya mwezi uliopita, halafu kazi yetu ndiyo kama hii tunatakiwa tufanye utafiti, unategemea tutafanya kazi kwa umakini kweli? Tutawafundisha madaktari kwa umakini?” alihoji Dk Mwakyoma.

Mwakyoma alisema, Serikali haiwezi kudai kuwa haina fedha za kutosha wakati imetumia mamilioni ya shilingi katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru na uchaguzi wa Igunga. Alisema ni vyema Serikali ikajipanga na kuamua kushughulikia masuala ya madaktari kwa hekima kwani kukaa kimya bila kutoa suluhu ni sawa na kufanya ushindani usio na maana.

Hata hivyo, Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH Aminael Aligaesha alisema jana jambo hilo lilikuwa likishughulikiwa kwani vipo vikao vinavyoendelea.

Wagonjwa watimuliwa wodini
Wodi mbalimbali hospitalini hapo zilitawaliwa na vilio kutokana na wagonjwa na ndugu za wagonjwa kupewa taarifa za kuondoka katika eneo hilo mara moja, kutokana na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika wodi ya Sewahaji, Sadick Dimoso (35) mkazi wa Morogoro alisema hali sasa MNH ni mbaya.

“Tumeambiwa tuondoke wodini bila ya kuruhusiwa na daktari, hii ni hatari tena wanasema tuondoke tukakae huku hadi wiki mbili ndio turudi kuangalia,” alisema Amina Ramadhani, aliyekuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji wa jicho. Alisema hatua ya kutakiwa kuondoka hospitalini hapo imekatisha matarajio yao ya kuendelea kuwa hai na kuitaka Serikali kufanyia kazi madai ya madaktari.

Wakati kundi la watu wengine wakililia huduma hosptalini hapo, baadhi ya ndugu za wagonjwa waliingia katika mgogoro na walinzi wa wodi hiyo ya Sewahaji wakitaka waandishi wa habari kuingia wodini.

Vikao vya Kamati Wakati hayo yakijiri, vikao baina ya madaktari na Kamati ya Kudumu ya Huduma za Bunge, viliendelea jana katika ofisi ndogo za Bunge huku taarifa zake zikiwa ni siri.

CHANZO (Habari zote mbili): Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.