9 Feb 2012

Nani anasema ukweli kuhusu posho za wabunge?

WIKI iliyopita inaweza kuingia katika vitabu vya historia ya nchi yetu kufuatia mlolongo wa matukio yanayozidi kuashiria kuwa hali si shwari katika uongozi wa nchi yetu.

Tukio la kwanza lilikuwa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kukanusha habari kwamba Rais Jakaya Kikwete ameshasaini kuridhia ongezeko la posho za wabunge kutoka shilingi 70,000 kwa siku hadi shilingi 200,000.

Kukanusha huko kulifuatia taarifa kwamba Spika Anne Makinda aliwaambia wandishi wa habari kwamba Rais alikuwa ameridhia posho hizo, na kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwaaambia wabunge kwamba Rais alikubali posho zilipwe.  

Binafsi, nilibahatika kufanya maongezi yasiyo rasmi na Rais Kikwete kwenye mtandao wa  jamii wa Twitter. Kama ilivyoeleza taarifa ya Kurugenzi ya Ikulu, Rais Kikwete alieleza kwamba (namnukuu), “Upo mkanganyiko na upotoshaji mkubwa kuhusu jambo hili. Wengi hawaelewi bado. Litatolewa ufafanuzi kwa kina.

Jibu hilo lilitokana na ombi langu kwa Rais ambapo niliandika (ninajinukuu), “Mheshimiwa Rais, ninakusihi umwajibishe ‘mtoto wa mkulima (Waziri Mkuu Pinda) kwa kukuchonganisha na umma eti umebariki posho...

Kadhalika, Rais alifafanua kwamba (namnukuu) “Nilitoa maelekezo kuhusu suala la posho za wabunge. Maelekezo hayo hayakuwa kuridhia jambo hilo.” Baada ya tweet hiyo Rais aliongeza, “Nilikubali haja ya kuangalia upya posho kwa wabunge na niliwataka wabunge kutumia busara na hekima katika kutafakari hili...Wabunge watumie kikao cha Februari cha Bunge kulizungumzia suala hili. Ni muhimu.

Kabla ya kuendelea na mjadala kuhusu suala hili sina budi kumpongeza Rais, si tu kwa majibu yake ya kistaarabu bali pia kuchukua muda wake kusoma na kujibu tweets mbalimbali zinazoelekezwa kwake.
Kwa tabia ya kimungu-mtu iliyozoeleka miongoni mwa viongozi wetu wengi wa Kiafrika, ni nadra sana kwa Rais kufanya mawasiliano na wananchi wa kawaida hasa katika mitandao ya jamii.

Yawezekana kabisa kuwa maelezo yake hayajakidhi shauku ya Watanzania wengi kufahamu nani anasema ukweli lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba kwa kutumia muda wake adimu kulizungumzia suala hilo ‘katika maongezi yasiyo rasmi’ ni jambo linalostahili pongezi.

Lakini pamoja na majibu hayo mazuri ya Rais, wananchi wengi bado wanatatizwa na mkanganyiko wa kauli za viongozi kuhusu posho za wabunge.

Kuna maswali kadhaa ambayo hayana majibu hadi sasa (licha ya ufafanuzi wa Rais).Hivi inawezekana kweli Waziri Mkuu kuzusha kuwa Rais aliridhia ongezeko hilo la posho? Ukisoma maelezo ya Rais ‘kati ya mistari’ (between the lines) unaweza kuhisi kuwa labda Pinda hakuyaelewa vizuri maelekezo ya ‘bosi’ wake. Lakini kama ukweli ndio huo, kwanini basi Makinda aje na maelezo mapya? Na kwanini Pinda amekuwa kimya hadi leo?

Binafsi ninaona kuwa suala hili linaweza kumalizwa na Rais Kikwete kwa kuwakumbusha wabunge kuwa japo maombi ya nyongeza ya posho zao yanaweza kuwa ya msingi, ukweli ni kwamba hayaendani na hali halisi ya uchumi wetu.

Na majuzi Rais Kikwete ameeleza waziwazi kuwa serikali yake inakabiliwa na hali ngumu kifedha alipozungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria, ambapo miongoni mwa wageni waalikwa alikuwa Spika Makinda. Je, inawezekana Rais alikuwa anafikisha ujumbe ‘kistaarabu’ kwa Spika?
Wito wa safu hii kwa Rais Kikwete ni mwepesi na mfupi: huko nyuma alishaweka bayana kuwa tabasamu lake lisitafsiriwe vibaya, na urais wake hauna mbia. Kutegemea hekima na busara za wabunge kujadili maslahi yao ni sawa kabisa na kuwasihi mafisadi waionee huruma nchi yetu. Wabunge wanaopiga kelele kutaka nyongeza ya posho wapo ‘out of touch’ na hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Haiwezekani kuwasihi watumie hekima na busara wakati wameshaonyesha tangu mwanzo kuwa wana uhaba wa vitu hivyo linapokuja suala la posho.

Mwanzoni mwa makala hii nimeandika kuwa wiki iliyopita ilikumbwa na mlolongo wa matukio na hadi muda huu nimeongelea tukio moja tu. Kwa kifupi, matukio mengine yanayoweza kuonyesha kuwa ombwe la uongozi wa taifa letu linazidi kuwa kubwa ni pamoja na habari zilizopatikana kutoka bungeni Dodoma kuwa Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo ‘aligoma’ kujibu swali aliloulizwa na Spika. Kichekesho ni kwamba japo Spika Makinda amejijengea umaarufu kwa kuliendesha Bunge kwa ‘mkono wa chuma’ dhidi ya wabunge wa vyama vya upinzani katika tukio hilo hakuchukua hatua yoyote dhidi ya Waziri Mkulo.

Kana kwamba hiyo haikuwa ‘kali kubwa ya wiki,’ taarifa zinaeleza kuwa wabunge wa CCM waligoma kukutana na Rais Kikwete kuzungumzia muswada wa mabadiliko ya Katiba, ambapo inasemekana wabunge hao wamedhamiria kuikwamisha.

Je, wabunge hao wamegoma kwa sababu wamechukizwa na kauli ya Rais kuwa hajaridhia matakwa yao ya nyongeza ya posho? Taarifa zinaeleza kuwa sababu iliyopeleka hatua hiyo ni mtizamo wa wabunge hao kuwa marekebisho yaliyofanywa kwenye muswada huo yatapelekea CCM kuangushwa na CHADEMA. Pia inaelezwa kuwa wabunge hao hawajapendezwa na kitendo cha Rais kukubaliana na mapendekezo ya CHADEMA katika maboresho ya muswada huo.

Japo sisi tusio wana-CCM hatuna haki ya kuingilia mambo ya ndani ya chama hicho, lakini kwa vile ni chama tawala na chochote kinachokihusu kinamgusa takriban kila Mtanzania, ni muhimu kukemea utovu huo wa nidhamu ambao unaweza kutafsiriwa tu kuwa ni njama za wazi za kumkwaza Rais kuleta mwafaka wa kitaifa utakaosaidia kuiongoza nchi yetu katika njia sahihi.

Nimalizie makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete kuwa licha ya kuwa Mwenyekiti wa taifa wa CCM yeye ni Rais wa Watanzania wote.

Kamwe asiruhusu maslahi ya waroho na walafi wachache yaathiri maslahi ya Watanzania wote pasipo kuangalia itikadi zao za kisiasa.

Kadhalika, ninawasihi wazalendo wote (bila kujali tofauti zetu) kumuunga mkono Rais Kikwete katika masuala yenye maslahi kwa Watanzania wote hata kama yeye mwenyewe amelea matatizo haya na sasa yanataka kutupeleka kubaya.

Lakini ili Rais aweze kupata sapoti hiyo ni muhimu na yeye aamue ‘liwalo na liwe,’ lakini Tanzania kama nchi ni muhimu kuliko mtu binafsi au kikundi cha walafi wachache.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.