8 Mar 2012


Tanzania nchi ya vituko na viporo vya utatuzi wa kero

Kitendawili bila majibu kwa mgomo wa madaktari
Arumeru wanausalama walinda ‘usalama wa rushwa’
MIONGONI mwa habari zilizogusa hisia za wengi wiki iliyopita ni tishio la madaktari kuwa ifikapo Jumatano hii (Machi 7)  watarejea kwenye mgomo iwapo viongozi wawili wa Wizara ya Afya, Waziri Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya hawatakuwa wameng’olewa kwenye nyadhifa hizo.
Ni vigumu kuelewa kwa nini Rais Jakaya Kikwete anaendelea kuwalinda Mponda na Nkya, lakini uzoefu unapaswa kutukumbusha kuwa ni nadra kwa watawala wetu kusikia vilio vya watawaliwa, isipokuwa nyakati za uchaguzi.
Kimsingi, kilichofanywa na Serikali hapo awali kuwashawishi madaktari kusitisha mgomo wao na kurejea kazini ni sawa na kuahirisha tatizo pasipo kujihangaisha namna ya kulikabili litaporejea tena.
Msimamo wa madaktari hao ulikuwa wazi kwa Serikali, ambapo pamoja na kutaka watimiziwe madai ya kutaka kuboreshewa maslahi na mazingira yao ya kazi, walitamka bayana viongozi wanne wa Wizara ya Afya waondolewe madarakani.
Lakini kabla ya Serikali kuamua kukaa chini na madaktari, ilishajichanganya kwa kujaribu kutumia ubabe kama njia ya kumaliza mgomo. Awali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa tishio kwamba daktari atakayegoma kurejea kazini, angekuwa amejifukuzisha kazi huku ikiahidiwa kwamba madaktari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wangeziba pengo kubwa lililojitokeza.
Pengine kwa kutambua kuwa katika siku za hivi karibuni kauli za Pinda zimekuwa kama za mtu anayesema kwa minajili ya kusikia tu sauti yake mwenyewe, madaktari walipuuza tishio hilo na nguvu kazi iliyoahidiwa kutoka jeshini ikiishia kuwa kituko kama si utani mbaya (bad joke).
Baada ya kugundua kuwa ‘imeshikwa pabaya’ ndipo Serikali kupitia Pinda ikajirudi na kuwaahidi madaktari kuwa ingetimiza matakwa yao. Na siku chache baadaye, ikatangaza kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa.
Japo uamuzi huo wa kuwasimamisha kazi Nyoni na Mtasiwa ulipokewa na kueleweka vizuri, bado inaniwia vigumu kuelewa kwa nini Mponda na Nkya walisalimika na wanaendelea kukumbatiwa hadi leo.
Kwa kiasi kikubwa, kusita kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya Waziri huyo na Naibu wake ndio kumesababisha kurejea tena kwa sakata hili la mgomo. Lakini kingine kinachokera zaidi ni ukweli kwamba japo Nyoni na Mutasiwa wamesimamishwa kazi, hakuna taarifa zozote kutoka serikalini kuhusu hatua zaidi dhidi yao.
Yayumkinika kuhisi inasubiriwa ‘upepo utulie’ kabla watendaji hao hawajapangiwa madaraka mengine. Ndio Tanzania yetu ilivyo.
Kilio cha madaktari na tishio lao la mgomo ni dalili tu ya tatizo kubwa linalohitaji dhamira ya dhati ya Serikali kulishughulikia. Asilimia kubwa ya watumishi wa umma wanakabiliwa na matatizo kama hayo yanayowasibu madaktari, kubwa zaidi likiwa maslahi na mazingira ya kazi duni.
Lakini kilio cha watumishi wa umma ni mithili ya ‘tone kwenye bahari’ ukilinganisha na hali ngumu ya maisha inayowakabili asilimia kubwa ya Watanzania. Cha kusikitisha zaidi ni kukosekana kwa dhamira ya dhati kwa upande wa Serikali kuboresha maisha ya Mtanzania, awe mtumishi wa umma au sekta binafsi, aliyejiajiri au mkulima, na kila kundi katika jamii.
Mara zote nimekuwa nikiamini kuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo yetu si kukosekana kwa sera nzuri na mipango mizuri, au mawazo mazuri. Kinachotukwaza zaidi ni kutokuwapo nia ya kutekeleza sera, mipango au mawazo hayo, sambamba na usimamizi mbovu pale tunapojaribu kuitekeleza.
Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005 sio tu aliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia alibainisha kuwa suala hilo (la maisha bora) linawezekana. Na hakuwa anatania (angalau kwenye ukweli wa mambo) kuwa maisha bora yanawezekana katika nchi iliyojaliwa kila aina ya utajiri japo tunaendelea kuwa masikini wa kutupa huku tukiwa nchi ya tatu kwa kupokea misaada mingi zaidi duniani (mbele ya Iraq na Afghanistan).
Rais Kikwete hajajihangaisha kupima ufanisi wa dhamira yake ya kuwaletea maisha bora Watanzania, lakini ninachokumbuka kuna wakati kauli mbiu hiyo ya maisha bora kwa kila Mtanzania ‘ilikarabatiwa’ na kuongezwa vikorombwezo kama ‘maisha bora hayawezi kushuka kutoka mbinguni.’ Unaweza kujiuliza kwa nini kaulimbiu hiyo ilipotolewa mara ya kwanza haikuwa ‘maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana lakini hayawezi kushuka kutoka mbinguni.’
Kwa kutathmini dhamira hiyo ya Kikwete tangu aitangaze hadi leo hii, yayumkinika kuhitimisha kuwa ilikuwa ni porojo tu za kutaka kura za Watanzania. Ninasema hivyo kwa sababu ni rahisi kupata idadi ya safari za Rais kwenda nje ya nchi kuliko kuwa na takwimu sahihi za uboreshwaji wa maisha ya Mtanzania. Hapa ninazungumzia takwimu halisi za mtaani na sio kauli za kisiasa za akina (Waziri wa Fedha) Mustafa Mkulo kuwa uchumi unakua.
Hivi kuna ugumu gani kujifunza kutoka kwa majirani zetu wa Rwanda, taifa lililojitutumua na kutoka kwenye mauaji ya kimbari na kuibuka kuwa moja ya mifano adimu ya mafanikio ya kiuchumi barani Afrika.
Nchi hiyo ambayo sasa inafananishwa na economic tigers wa Kusini Mashariki mwa Asia (kwa mfano Malaysia) imepiga hatua kubwa katika kupunguza umasikini huku uchumi wake ukikua kwa kasi.
Rwanda imediriki kufika ilipo sasa kwa sababu Rais Paul Kagame yupo makini, sio kufanya safari za kuzunguka dunia, bali kuhakikisha kuwa nchi yake inapiga hatua kimaendeleo. Sidhani kama Wanyarwanda watakuwa na tatizo iwapo Kagame ataamua ‘kushindana na Kikwete kufanya safari za nje ya nchi’ kwa sababu uchumi unaokua nchini humo unaweza kumudu gharama kubwa zinazotokana na safari za aina hiyo.
Kwa bahati mbaya, shinikizo la madaktari kuitaka serikali iboreshe maslahi na mazingira yao ya kazi linakuja wakati tunaelekezea kwenye msimu mwingine wa kuteketeza fedha katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Na dalili za awali za uteketezaji fedha za umma ni taarifa za uwepo wa makachero wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wenzao wa Idara ya Usalama wa Taifa kwenye mchakato wa CCM kupata mgombea wake kwenye uchaguzi huo.
Licha ya ukweli kwamba taasisi hizo sio za kisiasa na hivyo hazikupaswa kuwepo kwenye shughuli hiyo ya ndani ya CCM, uwepo wao ambao umegharimiwa na fedha za umma haukuweza kuzuia utoaji na upokeaji wa rushwa.
Siwezi kuilaumu sana TAKUKURU kwa vile kuwepo au kutokuwepo kwake hakuna faida kwa Mtanzania zaidi ya kumwongezea hasira na mzigo wa kugharamia uendeshaji wa taasisi hiyo butu. Lakini nina swali au changamoto kwa Idara ya Usalama Taifa; hivi haioni kama inajidhalilisha inapotuma maofisa wake kwenda kwenye chaguzi za ndani za CCM, kisha rushwa ikamwagwa kana kwamba ni halali, na hatimaye maofisa hao wakarejea ofisini kuripoti tu jinsi rushwa ilivyotawala?
Zamani, sio tu kuwa uwepo wa maofisa Usalama wa Taifa ulitosha kuwatisha wahalifu (kwa mfano hao wanaomwaga rushwa kwenye michakato ya uchaguzi ya CCM) lakini ilikuwa sio rahisi kubaini uwepo wao (na hivyo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi).
Lakini siku hizi imekuwa kama desturi kusikia wakijazana kwenye vinyang’anyiro vya kupata wagombea wa CCM lakini wakiishia kuwa watazamaji tu kwani rushwa imeendelea kuwa turufu muhimu kwa wanachama wa chama hicho tawala kumudu kupata kura za kutosha.
Fedha zinazotumika kugharimia uwepo wa wanausalama hawa zingeweza kuelekezwa kwenye maeneo mengine muhimu, na hilo licha ya kupunguza migongano kati ya serikali na watumishi wake na wananchi wengine kwa ujumla, ingesaidia pia kuepusha aibu ya wanausalama hao kuwa waangalizi wa namna rushwa inavyofanikisha ushindi wa wanaowania kuteuliwa.
Tutashuhudia katika kampeni za uchaguzi huo mdogo wa Arumeru Mashariki jinsi Serikali itakavyotapanya fedha za Watanzania (pasipo kujali ukweli si kila mlipakodi wa nchi yetu ni mwana-CCM) kuhakikisha inashinda uchaguzi huo. Tutashuhudia pia nyenzo za umma (kama magari) zikitumika kisiasa na kuwabebesha Watanzania mzigo wasiostahili. Chama kinachopata wagombea kwa njia ya rushwa hakina njia nyingine ya kuomba kura zaidi ya kutoa rushwa.
Ni mazingira haya ya serikali yetu kumudu gharama zisizo muhimu (kama safari mfululizo za Rais Kikwete nje ya nchi na matumizi makubwa ya fedha za umma kwenye shughuli za kisiasa za CCM), yanayofanya vilio vya madaktari (na watumishi wengine wa umma pamoja na wananchi kwa ujumla) kuwa sio tu vya msingi bali pia vya lazima.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.