10 Mar 2012


FRIDAY, MARCH 9, 2012

Mamlaka ya Urais yawezeshe uwajibikaji kumaliza mgogoro wa Serikali na Madaktari


Jana tarehe 8 Machi 2012 asubuhi nilitoa tamko kwa niaba ya CHADEMA la kutaka kauli ya haraka ya Rais Jakaya Kikwete ya kutengua uteuzi wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hadji Mponda na Naibu Waziri wa wizara husika Dk. Lucy Nkya kutokana na udhaifu wao mkubwa wa kiongozi waliouonyesha katika kushughulikia mgogoro wa madaktari ambao umedumu kwa muda wa takribani miezi miwili. 

Nilieleza kusitikitishwa na ukweli kwamba Rais Kikwete toka mgogoro utokee hajatumia ipasavyo mamlaka yake ya kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 34 na 35 na tarehe 5 Februari 2012 aliahidi kwamba atazungumzia kwa kina suala la mgomo wa madaktari lakini badala yake akalizungumza kwa ufupi tarehe 29 Februari 2012 katika hotuba yake kwa taifa bila kuchukua hatua za msingi hali inayoashiria ombwe la uongozi. 

Nilieleza kuwa iwapo Rais Kikwete haitatoa kauli viongozi wakuu wa CHADEMA wataeleza hatua za ziada ambazo chama kitachukua kuiwajibisha serikali. Jioni Serikali ilieleza kuwa leo Rais angezungumza na wazee wa Dar es salaam, na leo imetolewa taarifa kuwa atazungumza nao kesho.

Jana usiku na leo asubuhi masuala kadhaa yameendelea kuhusu mgogoro huu, mosi; hukumu ya mahakama ya kazi, pili; uamuzi wa serikali na wadau wake kufanya propaganda dhidi ya madaktari tatu; uamuzi wa serikali kufanya mawasiliano na uongozi wa madaktari.

Mkakati wa kufanya propaganda hautaisaidia Serikali badala yake iwekeze katika mawasiliano na uongozi wa madaktari kabla ya Rais kuzungumza ili Rais atoe kauli baada ya kuchukua hatua za msingi ikiwemo za kuwezesha uwajibikaji wa viongozi waliotajwa na pia kuanza kushughulikia madai ya madaktari na yale yanayohitaji kuingizwa kwenye bajeti kuwe na makubaliano ya utekelezaji. 

Izingatiwe kwamba matatizo ya Wizara ya Afya pamoja na udhaifu wa kiutendaji yalichangiwa pia na ufinyu wa bajeti, na bajeti husika iliandaliwa na serikali na kupitia kwenye baraza la mawaziri ambalo Rais ni mwenyekiti wake kabla ya kuletwa bungeni na wengine tuliipinga tukitaka fedha zitoke kwenye matumizi mengine ya anasa na kuelekezwa kwenye huduma muhimu za kijamii. 

Pia; kutokana na matatizo katika serikali kwenye wizara mbalimbali yenye madhara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika taifa tunasisitiza umuhimu wa Rais Kikwete kulivunja baraza la mawaziri ili kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kuongeza uwajibikaji kama ilivyoazimiwa pia na kamati kuu ya CHADEMA katika mkutano wake wa tarehe 3 na 4 Machi 2012.

Tarehe 7 na 8 Machi 2012 Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa mara nyingine tena alitoa taarifa kinyume na kauli za awali za tarehe 9 Februari 2012 ambazo badala ya kushughulikia vyanzo vya mgogoro vimeendeleza mgogoro na kusababisha mgomo mwingine wa madaktari wenye athari kubwa kwa wananchi.

Ndio maana nikatoa kauli ya kumtaka Waziri Mkuu kuweka wazi kwa umma taarifa ya uchunguzi uliofanywa na serikali kuhusu tuhuma dhidi ya viongozi wakuu na watendaji waandamizi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, na kushughulikia madai ya msingi ya madaktari. 

Aidha, pamoja na kuunganisha nguvu za pamoja kuhakikisha mgomo unakwisha ili kuepusha athari zaidi kwa umma, ni muhimu hatimaye tathmini huru ikafanyika kuhusu matokeo ya mgogoro na mgomo toka ulipoanza mpaka sasa ikiwemo kueleza wazi idadi ya vifo vilivyotokea na madhara yaliyojitokeza katika hospitali za umma tofauti na kauli potofu iliyotolewa bungeni tarehe 3 Februari 2012 na Waziri husika.

Rais Kikwete alipaswa kabisa kuchukua hatua kuiongoza serikali kufanya maamuzi ya msingi mara baada ya matokeo ya kikao kati ya ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wanataaluma wa kada ya afya sanjari na mkutano kati ya madaktari na wawakilishi wa kada nyingine za sekta ya afya katika utumishi wa umma vilivyofanyika tarehe 9 Februari 2012; kwa kuzingatia pia ushauri tuliotoa tarehe 10 Februari 2012.

Kwa upande mwingine, jana nilirudia kutoa mwito tuliotoa tarehe 30 Januari 2012 kwa TUGHE, MAT na kamati ya muda ya madaktari kuendelea kutoa ushirikiano unaostahili kwa chama, kambi rasmi ya upinzani na wadau wengine ili kuweza kuunganisha nguvu ya pamoja katika kushughulikia madai ya msingi ya madaktari yenye kuathiri sekta ya afya nchini na maisha ya wananchi kwa ujumla. 

Naendelea kuwashukuru wanaharakati kwa kuunganisha nguvu katika kutaka uwajibikaji wa viongozi wa serikali katika kushughulikia mgogoro na madaktari na kinaitaka Serikali kuacha vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa madaktari na makundi mengine katika jamii yanapotumia uhuru wa kikatiba kwa kukusanyika, kujadiliana na kuhoji kuhusu uwajibikaji wa serikali na viongozi wake kwa kuzingatia ibara za 8, 18 na 20 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Kikwete anapaswa baada ya mawasiliano yanayoendelea kutoa hotuba yenye kuleta matumaini badala ya kurudia tena maelezo yasiyoridhika kama yale yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda tarehe 9 Februari 2012 na 7 na 8 Machi 2012 kuhusu namna ambavyo imeshughulikia mgogoro huu na madai ya madaktari, watumishi wengine wa umma katika sekta ya afya nchini pamoja na uboreshaji wa huduma katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini.

Narudia kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono madai ya msingi ya madaktari ili kuhakikisha kwamba hospitali za umma nchini zinakuwa mahali salama kwenye huduma bora za kulinda maisha ya wananchi hususan wasio na uwezo wa kudumu gharama za matibabu katika hospitali binafsi za ndani na nje ya nchi. 

Pamoja na madai ya maslahi ya madaktari ambayo ni kwa maslahi ya umma, madaktari wanataka pia serikali ichukue hatua za kuboresha huduma za afya. Serikali inaingia gharama kubwa kupeleka baadhi ya watanzania wengi wao wakiwa viongozi kwenda kutibiwa nje ya nchi huduma katika hospitali za umma zinazidi kuzorota kutokana na ukosefu wa madawa, vifaa tiba na wataalamu wa kutosha katika hospitali za umma. 

Aidha, serikali inashindwa kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kisingizio cha kutokuwa na uwezo wakati ambapo inafanya matumizi mengine ya anasa kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru. Serikali inachelewa kushughulikia madai ya posho za madaktari kama nyongeza ya posho ya kulala kazini (on call allowance) na posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (risk allowance) wakati huo huo serikali hiyo hiyo inazungumzia nyongeza ya fedha katika matumizi mengine ya serikali yasiyokuwa ya lazima. Serikali ishughulikie vyanzo vya migogoro ya kijamii badala ya matokeo.

MTEMBELEE MHESHIMIWA MNYIKA KATIKA BLOGU YAKE INAYOPATIKANA http://mnyika.blogspoti.com.PIA UNAWEZA KUMFUATA TWITTER www.twitter.com/jjmnyika NA UKURASA WAKE WA FACEBOOK NI http://www.facebook.com/pages/John-Mnyika/113913842009362

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.