Showing posts with label JOHN MNYIKA. Show all posts
Showing posts with label JOHN MNYIKA. Show all posts

24 Jun 2012Waheshimiwa Wananchi wenzangu,
Amani iwe kwenu,
Kwa kipindi cha wiki nzima kumekuwepo na mjadala mkali bungeni, kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na katika taifa kwa ujumla juu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13 sanjari na yaliyojiri kutokana na kauli niliyotoa bungeni juu ya udhaifu wa Rais katika usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti pamoja na mipango muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.
Aidha, kupitishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 bila marekebisho yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa kumedhihirisha kile nilicho tahadharisha tangu awali kwamba; kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na uendeshaji wa nchi, udhaifu wa Rais una athiri maisha ya wananchi. Ukweli ni Uhuru!.
Katika mazingira haya, udhaifu wa rais na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na serikali kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea pia migomo baridi ya watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kutokana pia na madai yao ya muda mrefu kutokuzingatiwa kwenye bajeti. Ukweli ni Uhuru!.
Kadhalika udhaifu wa kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia tu mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Pia, katiba imempa mamlaka makubwa Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge likikataa bajeti ya serikali kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja bunge suala ambalo huwapa hofu wabunge wengi hususani wa chama kinachotawala na kuwafanya wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika. Hivyo, udhaifu wa bunge unachangiwa na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais katika kuvunja bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo wabunge hawana uwezo wa kubadilisha na wakati huo huo wakikataa bunge linavunjwa, katika mazingira haya udhaifu wa Rais wa kushindwa kutumia nguvu hizo za kikatiba una madhara makubwa sana kwa nchi na maisha ya wananchi.  Ukweli ni Uhuru!.
Kwa mantiki hiyo, katika mchakato wa katiba mpya ni muhimu kwa wananchi kutoa maoni ya kuwezesha ukuu na uhuru wa bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. Wakati katiba mpya ikisubiriwa, ni muhimu kwa marekebisho ya haraka kufanyika katika kanuni za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka kanuni ya 107 ili kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa. Katika muktadha huo, nimeanza kufanya uchambuzi  ili kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Hata hivyo, hata kwa kanuni zilizopo sasa udhaifu wa bunge unaongezeka kutokana na maamuzi ya kizembe mathalani ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge, mfano Kanuni ya 94 inalitaka bunge ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano wake wa mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, kanuni ambayo toka niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa wakati hata mara moja pamoja na kuwakumbusha wanaohusika kusimamia kanuni. Ukweli ni Uhuru!.
Mwaka huu udhaifu umekuwa mkubwa zaidi kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sanjari na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni 2012 hali ambayo imechangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilfu mpango wa taifa wa miaka mitano. Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru kwamba Spika wa Bunge Anna Makinda amekiri bungeni tarehe 20 Juni 2012 kwamba kulikuwa na udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge kukamilisha kazi ya kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha serikali kuongeza vyanzo vya mapato kama wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na pendekezo hilo kurudiwa tena na kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni 2012. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa iwapo sheria ya fedha ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012 kama ilivyokuwa imepangwa awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia sehemu kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye bunge na waziri. Hivyo, michango na mapendekezo ya wabunge bila Rais mwenyewe kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa mapato kwa kuwa kwa kuwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) udhaifu wa bunge ni pamoja na kukatazwa kutoza kodi au kuongeza kodi. Ukweli ni Uhuru!.

Hivyo, Kamati ya Fedha na Uchumi itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3) kurejea maoni yake, ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne wa Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 na kufanya marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri Waziri. Ukweli ni Uhuru!.

Aidha, ili kuondoa udhaifu uliopo Rais Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu rasmi za bunge (Hansard) za tarehe 18 Juni mpaka 22 Juni 2012 na kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha Waziri wa Fedha ya 86 (10)  kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye kulenga kupunguza kodi katika bidhaa zenye kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni Uhuru!.
Izingatiwe kuwa nilipotolewa bungeni tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa ufupi nilichosema bungeni na nilichotarajia kusema na kuahidi kwamba nitatoa tamko kamili baadaye; baada ya kujipa muda wa kutafakari nimefikia uamuzi wa kutoa tamko husika wakati bunge litakapoelekea kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013; ambapo pamoja na masuala mengine nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa kwa watanzania kuweza kutekelezwa na serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa sasa niwashukuru wananchi wa Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na watanzania kwa ujumla walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni yao kwenye mitandao ya kijamii, simu za mkononi na katika vyombo vya habari. Nawashukuru pia viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya taifa.  Ukweli ni Uhuru!.
Nashukuru pia kwa mchango wa walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli niliyotoa juu ya udhaifu wa Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana na jazba na wengine wameeleza kuwa ningetumia lugha ya diplomasia kufikisha ujumbe ili kutodhalilisha taasisi ya urais na kwa kuzingatia utamaduni wetu wa heshima kwa wakubwa na wapo wachache waliosema kwamba ni matusi kutamka ‘udhaifu wa Rais’. Ukweli ni Uhuru!.
Wakati mjadala huu ukiendelea ni rai yangu kwamba rejea ifanyike katika mchango wangu wa tarehe 5 Julai 2011 wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili pia ifanyike kwenye mchango wangu wa tarehe 19 Juni 201; na ieleweke kwamba naheshimu taasisi ya urais na umri, naamini katika matumizi ya lugha ya kidiplomasia, hata hivyo nilitafakari na kuamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka zote zinazohusika na wauchukulie kwa uzito tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita. Ukweli ni uhuru!.
Niliamini, naamini na nitaendelea kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka; hata hivyo kwa kuwa pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa chanzo cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai bungeni wa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa; nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli ni uhuru!.
Katiba ya Nchi ambayo niliapishwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”. Toka nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010 kwa nyakati na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wa kawaida wakilalamika kuhusu udhaifu wa Rais na kutaka atumie nguvu na mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti serikali kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayolikabili taifa; niliamua kuendelea kusema bungeni kwa mara nyingine ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Ukweli ni Uhuru!.
Tarehe 19 Juni 2012 nilieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti na tarehe 22 Juni 2012 nilipiga kura ya hapana ya kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa ajili ya miradi ya barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais Kikwete na kuingizwa kwenye jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande wa miradi ya maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika bajeti ya 2012/2013. Ukweli ni Uhuru!.
Pamoja na utetezi uliotolewa na Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri kati ya kiingereza na Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua kuikataa bajeti kwa kuwa ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao uliwasilishwa na Rais Kikwete na ukapitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo kama zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli ni Uhuru!.
Naamini Rais Kikwete anayofursa ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake katika muswada wa sheria ya fedha kupanua wigo wa mapato na hatimaye kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 107 mapendekezo ya matumizi ya nyongeza ya fedha za serikali yenye kulenga kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo. Kwa upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam, serikali kwenye bajeti ya nyongeza inayopaswa kuwasilishwa iongeze fedha za miradi ya Maji kwa upande wa Ruvu Juu ikiwemo kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa Bwawa la Kidunda, kwa upande wa Barabara iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za pembezoni za mchujo na za mzunguko za kupunguza msongamano wa magari, na fidia ya ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la Mloganzila. Ukweli ni Uhuru!.
Kwa Wasemaji wa CCM waliodai kwamba nimetoa lugha ya matusi dhidi ya Rais na mwenyekiti wa chama chao wasome Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania cha mmoja wa waasisi wa TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere  ambapo wakati huo taifa likiwa katika mtanziko alimueleza Rais wa wakati huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’ katika ukurasa wa 50 na kuendelea kusema katika Ukurasa wa 51 na namnukuu “Kwa sababu ya minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize kipindi chake salama” . Ukweli ni Uhuru!
Naamini Mwalimu Nyerere hakumtukana Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu nimetukana ni kumtuhumu pia Marehemu Baba wa Taifa; narudia tena kusisitiza kuwa udhaifu uliojitokeza ni kutokana na Rais kutokutumia kwa uthabiti nguvu na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ibara za 33, 34, 35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji wa serikali na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni Uhuru!.
Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “ Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa.  Na msingi wa woga ni ubinafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho wa kunukuu:   Ukweli ni uhuru.

Wenu katika utumishi wa umma, 

John Mnyika
22 Juni 2012
Bungeni-Dodoma23 Jun 2012

MNYIKA HAKUKOSEA

Mara ya kwanza niliona mnyika amekosea sana kumwita rais Dhaifu, hii ni kutokana na ukweli kuwa kanuni za bunge hazimruhusu, lakini pia ameyasema yale mbele ya watanzania wote ambao wapo wenye mapenzi thabit kwa rais. Lakini kumbe rais amemruhusu mnyika aseme maneno yale

Hivi ni nani hajawahi ona watoto wa darasa la kwanza wanafunga barabara kwa kuwa mwenzao amegongwa mpaka matuta yawekwe, na siku hiyo hiyo matuta yanawekwa? Tumemfundisha nini mtoto huyu? Tumemfundisha serikali yako ni dhaifu lakini ukiishikia kiboko inatekeleza hapo hapo

Wakati wa mkapa wanafunzi udsm waligoma, mkapa akafunga chuo mwaka mzima, hatukusikia tena mgomo mpaka 2007 wakati wa kikwete, tuliposikilizwa tulichogomea, tuligoma kwa kila kitu hata kama hatukustahili

Kitendo cha mtu kusimama mbele ya bunge akapata courage ya kusema rais dhaifu, akarudia na kurudia peke yake inaprove kama rais ni dhaifu

USHAURI WA BURE KWA RAIS: 
Haiwezekani sovereign country tunaambiwa kuna muwekezaji ana passport tano, serikali imemshindwa, KWELI? Serikali ya watu mil 40, jeshi, police, na TISS, inaandikwa gazetini imemshindwa mtu mmoja? Vaa mkono wa chuma baba


Hakuna uhuru usio na mipaka mheshimiwa kikwete. He who wishes to be obeyed must know how to command, uhuru ukizidi sana tunaharibu nchi. Unatuachia saaaana mpaka tunaanza kukukosea heshima

Madaktari wamegoma, tukaambiwa rudini kazini haraka au tutawafukuza wote tutaleta wanajeshi wafanye kazi, then kesho tunawaita tunakaa nao mezani, baba watakupanda kichwani washajua una udhaifu, unawaogopa..

Machiavelli anasema If an injury has to be done to a man it should be so severe that his vengeance need not be feared..
Kwa mfano watoto wanagoma lazma matuta yawekwe, waagize walimu wao wawatandike viboko watoto warudi darasani, then baada ya mwezi weka tuta kuzuia ajali kwa kuwa hapo mwanzo walikaa miaka bila tu.
Tunagomagoma kila kitu kwa sababu unaturuhusu, lakini pia haujali.. Wanafunzi wagome, madokta wagome, walimu wagome, hivi nani anawapa kiburi? Hawa madokta nani anawapa kiburi cha kugomea serikali?

Men are so simple and so much inclined to obey immediate needs that a deceiver will never lack victims for his deceptions
Mtembelee Slimcony katika blogu yake inayopatikana HAPA

19 Jun 2012

 


Nitatoa tamko la kina baadae kuhusu kilichotokea lakini kwa ufupi ubovu wa bajeti hii ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, yeye ndiye aliyesaini Mpango wa Taifa wa miaka mitano kama Kiongozi Mkuu wa Nchi tena kwa wino mwekundu kama Amiri Jeshi Mkuu. Na yeye ndiye Mwenyekiti wa baraza la mawaziri, bajeti hii iliyoacha kuzingatia mpango wa Taifa imepita kwenye baraza alilloliongoza, pia kushindwa kutekelezwa kwa bajeti iliyopita ni matokeo pia ya udhaifu wa taasisi ya Urais.
Pia kwa mujibu wa Katiba Rais ndiye ambaye anapeleka bajeti bungeni, Waziri mwenye dhamana anapeleka tu kwa niaba. Rais amepewa mamlaka makubwa juu ya bajeti ibara ya 99 imeweka mipaka kuhusu mambo ambayo bunge lina mamlaka nayo huku ibara ya 90 inasema bunge likikataa bajeti rais ana mamlaka ya kuvunja bunge. Hivyo Rais Kikwete anapaswa kuagiza Waziri wa Fedha bajeti iondolewe irudi kwenye baraza la mawaziri ikafanyiwe marekebisho!


John Mnyika
19 Juni 2012

7 Jun 2012

Picha ya kwanza inamuonesha Mwenyekiti Freeman Mbowe akikata utepe wa kufungua Ofisi ya CHADEMA Kijiji cha Mkangaula. Ilikuwa ni baada ya Katibu Mkuu, Dkt. Slaa kutoa hotuba ya ufunguzi na John Mnyika kupandisha bendera ya chama nje ya ofisi hiyo, ikiwa ni ishara ya kupiga hatua katika mapambano ya awamu ya pili.

Picha zingine zinamuonesha Mnyika akitoa 'somo' kwa wanakijiji wa vijiji vya Kata ya Lumesule. Mapema kabla alikaribishwa na kuzungumza na Katibu wa Tawi wa CUF, Bi. Zaituni (pichani). Wananchi walimwelewa vyema. Kadi zikauzwa vizuri. Akaacha uongozi wa muda wa tawi lenye wanachama wa 34. Katika Kijiji hicho cha Lumesule, mwananchi mmoja kwa jina la Yasin Mohamed alihoji ilikuwaje CHADEMA wakaachia Dkt. Slaa ashindwe urais, wakati alichaguliwa kwa kura nyingi na wananchi na wao wanajua alishinda uchaguzi huo wa mwaka 2010.

Picha ZIFUATAZO zinamuonesha John Mnyika akiwa katika vijiji vya Kata za Makukwe na Mkwedu, wilayani Newala. Kwa George Mkuchika ambako alikutana na kiashiria cha wazi kuhusu udhaifu wa Waziri Mkuchika (Mbunge wa Newala) katika kusimamia majukumu yake, baada ya wananchi katika Kijiji cha Tengulengu, Kata ya Mkwedu kumlalamikia kuwa Diwani wa Kata hiyo, Juma Dadi hajawahi kufungua ofisi yake zaidi ya mwaka mmoja sasa. Pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwa barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Newala na kwa Mbunge wao, Mkuchika, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Unaweza kuona pia wanawake walivyonogewa na PIPOOOOOOOOOOZ POWER, nao wakaipiga ya nguvu kweli kweli kuonesha umoja na mshikamano katika Falsafa ya Nguvu ya Umma ya CHADEMA, katika kudai uwajibikaji, kupigania haki, uhuru na mabadiliko ya kweli ya mfumo na utawala nchini.

Unaweza pia kumuona Kamanda Alfonsi Mawazo akiendelea kupata uzoefu wa mikikimikiki ya kujenga hoja katika uwanja wa mapambano. Si ofisini.
Picha zifuatazo zinamuonesha John Mnyika akiwa katika vijiji vya Kata za Makukwe na Mkwedu, wilayani Newala. Kwa George Mkuchika ambako alikutana na kiashiria cha wazi kuhusu udhaifu wa Waziri Mkuchika (Mbunge wa Newala) katika kusimamia majukumu yake, baada ya wananchi katika Kijiji cha Tengulengu, Kata ya Mkwedu kumlalamikia kuwa Diwani wa Kata hiyo, Juma Dadi hajawahi kufungua ofisi yake zaidi ya mwaka mmoja sasa. Pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwa barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Newala na kwa Mbunge wao, Mkuchika, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Unaweza kuona pia wanawake walivyonogewa na PIPOOOOOOOOOOZ POWER, nao wakaipiga ya nguvu kweli kweli kuonesha umoja na mshikamano katika Falsafa ya Nguvu ya Umma ya CHADEMA, katika kudai uwajibikaji, kupigania haki, uhuru na mabadiliko ya kweli ya mfumo na utawala nchini.

Unaweza pia kumuona Kamanda Alfonsi Mawazo akiendelea kupata uzoefu wa mikikimikiki ya kujenga hoja katika uwanja wa mapambano. Si ofisini.
Pichani chini ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe akihutubia Masasi
Chini,wananchi wakigombea kadi za Chadema
Picha chini,wananchi wakisikiliza hotuba kwa makini
Picha zote zimetumwa na mdau SAJJO

27 May 2012Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Dk Wilbrod Slaa akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
 Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA  akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Singida Magharibi Mheshimiwa Tundu Lissu akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Mbunge Wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge  wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mbeya Mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi aka Mr II(SUGU) akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Viongozi wa chadema wakifurahia kadi nyingi za CCM zilizorudishwa leo jioni kwenye mkutano
Deo Munish Katibu mkuu wa BAVICHA akiteta jambo na mmoja aliyehudhuria mkutano wa CHADEMA Wa uzinduzi wa kampeni ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.
  Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwaaga wananchi waliokuwa wamefurika makao makuu ya chama kinondoni walikofika wakitokea jangwani usiku huu
 Mbowe akiwatania wanachama ofini kinondoni baada ya wananchi kuanza kudai chama kimfukuze John Shibuda.Alikuwa akijifanya hasikii wanachosema na hapa anajaribu kuwasikiliza zaidi.hata hivyo Mbowe aliwaondoa wasiwasi na kusisitiza kuwa chama kinao utaratibu wa kushughulika na viongozi wanaokiuka maadili ya chama na kuwaomba wawaamini kama viongozi kuwa wanaouwezo wa kulishughulikia jambo hilo na mengine
 Mh.Mbowe na Mnyika wakiwa wamesimama kwenye gari wakati wa matembezi wakitoka kwenye mkutano
Aliyekua Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA)Mheshimiwa Godbless Lema akiwa juu ya gari huku akishangiliwa na vijana jioni baada ya mkutano
 Sehemu ya umati uliowasindikiza viongozi wa chadema toka jangwani hadi kinondoni.wamesambaa yapata saa 2 usiku.

PICHA ZOTE NA MAELEZOKWA HISANI YA BLOGU YA MHESHIMIWA HAKI NGOWI

23 May 2012
WEDNESDAY, MAY 23, 2012


Hukumu kesho itakuwa mahakama kuu kivukoni na sio mahakama ya kazi akiba

Nimepokea taarifa kwamba hukumu ya kesi ya uchaguzi dhidi ya ushindi wetu Jimbo la Ubungo kesho tarehe 24 Mei 2012 itatolewa katika Jengo la Mahakama Kuu (Kivukoni- Court No. 1) badala ya jengo ilipo mahakama ya kazi (akiba) ambapo kesi iliendeshwa. Kama tulivyotafuta kura pamoja, tukapanga mstari kupiga kura pamoja na tukakesha kuzilinda pamoja tujumuike pamoja kujua hatma ya kura zetu. Hukumu ya kesi inatarajiwa kuanza kusomwa saa nne asubuhi hata hivyo ni muhimu kuwahi mapema zaidi asubuhi kwa ajili ya itifaki za kuingia mahakamani. Maslahi ya Umma kwanza

24 Mar 2012

Michango kwa ajili ya Barabara ya Maziwa-External Mandela, kifusi sasa; lami itafuata

Kwa watumiaji wa Barabara ya Mkato ya Maziwa mpaka External Barabara ya Mandela; tuunganishe nguvu ya pamoja kuwezesha matengenezo ya dharura ya kuweka kifusi wakati tukiendelea kufuatilia barabara husika ijengwe kwa kiwango cha lami.

Watendaji wa Manispaa ya Kinondoni wametueleza kuwa barabara ya External haiwezi kupitishwa grader kusawazishwa kwa kuwa ina mabaki ya lami; hivyo suluhisho ya muda mfupi linapaswa kuwa ni kuweka kifusi.

Manispaa imekubali kutoa malori kwa ajili ya kubeba kifusi; hata hivyo wameeleza kuwa hakuna bajeti ya kununua na kusambaza kifusi kwa haraka. Jana tarehe 20 Machi 2012 nilimjulisha Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob akutane na kamati ya wananchi iliyoanza jitihada mbalimbali kuangalia nini tunachoweza kufanya kwa kuunganisha nguvu ya umma.

Diwani amenijulisha kwamba gharama zinazohitajika kuweka na kusambaza kifusi ni milioni moja; nimeshampatia 10% ambayo ni sawa na laki moja kazi iendelee. Nawaandikia kuwaomba watumiaji wa Barabara hiyo ambayo ni ya mkato na yenye kupunguza foleni, tuunganishe nguvu za pamoja kukamilisha matengenezo yanayoendelea.

Wasiliana na Diwani 0712239595 kwa ajili ya maelezo na maelekezo ya kuwasilisha mchango wako; ukishaunganisha nguvu yako tafadhali tujulishe kupitia [email protected] ili kuhakikisha uwajibikaji.

Mtakumbuka kuwa gazeti la Habari leo la tarehe 18 Machi 2012 katika ukurasa 5 lilikuwa na habari “Wataka Ubungo-Mandela kutengenezwa”, Habari hiyo imeeleza kuwa “Wakazi wa Ubungo katika Manispaa ya Kinondoni, wamemuomba mbunge wa Jimbo hilo John Mnyika, kushughulikia tatizo la Ubovu wa Barabara inayounganisha eneo la Ubungo Maziwa na Barabara ya Mandela ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa kero”.

Kufuatia habari hiyo kwa kazi waliyonipa wananchi ya kuwawakilisha na kuisimamia serikali na vyombo vyake katika kuwezesha maendeleo nilitoa wiki moja kwa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutimiza wajibu wa kushughulikia ubovu wa barabara husika.

Nikaeleza kuwa iwapo baada ya wiki moja Manispaa itakuwa haijaanza kuifanyia matengenezo barabara iliyolalamikiwa basi nitachukua hatua za kuunganisha nguvu ya umma kuwezesha matengenezo yanayohitajika.

Kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi kazi za utekelezaji ziko chini ya vyombo vya serikali kuu na serikali za mitaa; kazi ya mbunge ni kuvisimamia vyombo husika kuwezesha maendeleo.

Wananchi wa kata ya Ubungo na maeneo mengine ya Manispaa ya Kinondoni wanalipa kodi na kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 kumetengwa fedha za matengenezo ya barabara hivyo ni wajibu wa Manispaa kutumia mafungu hayo kwa haraka kufanya ukarabati au kama Manispaa haina fedha itangaze kufilisika ili vyanzo vingine viweze kutumika.

Hivyo, kama katika kipindi hicho cha wiki moja nilieleza iwapo Manispaa itakuwa haijatoa kauli ya lini matengenezo ya barabara husika yataanza nitawajibika kwa kutumia nafasi yangu ya ubunge kuunganisha wananchi na wadau wa maendeleo katika eneo husika kuweza kuanza kushughulikia ubovu wa barabara husika kwa dharura kwa kutumia vyanzo vingine vya fedha nje ya kodi.

Aidha, wakati tukichukua hatua za dharura za kufanya matengenezo ili kupunguza kero , suluhisho muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami.

Kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.

Niliziandikia mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza barabara hiyo katika vipaumbele vyake na sasa imetengewa fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.

Hivyo, nichukue fursa hii pia kutoa mwito kwa TANROADS kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka huu wa 2012 ili kupata suluhisho la kudumu zaidi la kuondoa kero ya ubovu wa barabara husika na kuchangia katika kupunguza msongamano katika Jimbo la Ubungo.

Aidha, pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi 2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External.

Hivyo, ni muhimu watendaji wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao wakaeleza hatua ambayo imefikiwa katika kushughulikia maombi hayo kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Nitumie nafasi hii pia kurudia kutoa mwito kwa Wizara ya Ujenzi kueleza kwa wananchi hatua iliyofikiwa katika kupandisha hadhi barabara za Dar es salaam za kupunguza msongamano na kutumia nyongeza ya mapato iliyopatikana kwenye ushuru wa barabara kuanza kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami mwaka huu wa 2012. Maslahi ya Umma Kwanza.

John Mnyika at 12:1


19 Mar 2012WIKI YA MADAI YA MAJI

Mwito wa kushiriki wiki ya madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii:
Nimerejea toka Afrika Kusini nilipokuwa kikazi na kukuta Wizara ya Maji imezindua maadhimisho ya Wiki ya Maji kuanzia tarehe 16 Machi na kilele kitakuwa Siku ya Kimataifa ya Maji tarehe 22 Machi 2012.

Ujumbe wa mwaka huu ni “Maji na Usalama wa Chakula”, hata hivyo tunahimizwa kuadhimisha ujumbe mpya bila kuelezwa matokeo ya ujumbe wa mwaka mmoja uliopita wa “Maji kwa ajili ya Miji: Kukabiliana na changamoto mbalimbali mijini”.

Kazi ya wabunge na bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika kuwezesha maendeleo kwa kutumia rasilimali za umma na za wadau wengine.

Kwa nafasi hiyo natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo na wa Jiji la Dar es salaam kwa ujumla kwamba badala ya kuadhimisha sherehe za maji bila ya maji kila mmoja ashiriki kwa namna mbalimbali katika Wiki ya Madai ya Maji.

Kila mmoja anaweza kushiriki kwenye wiki hii ya madai ya maji kwa njia mbalimbali, njia mojawapo ambayo natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuitumia ni kushiriki madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii kwa kuandika barua pepe kwa bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) kuitaka ifanye kazi ipasavyo ya kuharakisha upatikanaji wa maji kwa mujibu wa sheria, kanuni, mipango na mikataba.

Waandikie wajumbe wa bodi ya DAWASA madai ambayo unataka wayafanyie kazi katika eneo lako na nakala ya barua pepe hiyo kuituma kwa[email protected] kwa ajili za hatua zaidi za kibunge za uwakilishi na usimamizi.

Bodi ya DAWASA ni kama ifuatavyo: Mwenyekiti Dr. Hawa E. Sinare([email protected]), Makamu Mwenyekiti-Alhaj Said H. El-Maamry[email protected], wajumbe: Bw. Laston Msongole ([email protected]),Bi. Mary Mbowe ([email protected]) , Bi. Christine Kilindu([email protected]), Bw. Daniel Machemba ([email protected],[email protected]), Alhaj Bakari Kingobi ([email protected]), . Mary G. Musira([email protected]), B. Florence S. Yamat ([email protected]), Mh. Amina N. Mkilagi (Mb), Mhandisi. Archard Mutalemwa-Afisa Mtendaji Mkuu ([email protected]).

Tuungane pamoja kutaka serikali kuu na serikali za mitaa zitumie wiki hiyo kutoa maelezo kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika kutekeleza miradi ya maji na pia kuharakisha uzinduzi wa miradi ilicheleweshwa.

Njia hii ya kuunganisha nguvu ya umma kwa kutumia TEHAMA (SMS, facebook, twitter, email na njia nyingine) tuliitumia tarehe 1 Disemba 2011 wakati wa kuhamasisha umma kushiriki mkutano wa wadau uliotishwa na EWURA kuhusu ombi la TANESCO kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa 155% (zaidi ya mara tatu ya bei iliyokuwepo).

Hatimaye umeme ulipandishwa lakini si kwa kiwango hicho cha awali bali kwa wastani wa 40% kwa kuzingatia pia viwango vya utumiaji. (Suala la Umeme nimeanza kuchukua hatua zingine kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kutokana na matatizo yanayoendelea kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa umeme na nitatoa kauli kuhusu mgawo wa umeme unaoendelea kinyemela).

Izingatiwe kuwa nilipanga kwenye wiki hii ya madai ya maji kuunganisha nguvu ya umma kwa kuwaongoza wananchi kukutana na serikali na mamlaka nyingine zinazohusika hata hivyo itabidi kutumia njia mbadala za kuwasilisha madai.

Hii ni kwa sababu kuanzia kesho tarehe 19 Machi 2012 nitakuwa mfululizo mahakamani kwenye kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Ubungo wa mwaka 2010. Hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea nitaendelea kutumia njia nyingine za kibunge kuchukua hatua kuhusu masuala ya maji lakini natoa mwito kwa wananchi nanyi kwa upande wenu kila mmoja kuchukua hatua zinazowezekana katika wiki hii ya madai ya ya maji. Umoja ni Nguvu.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji bila ya Maji
Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji kuwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.

Uchakavu na wa miundombinu kutokana na mabomba kutokarabatiwa ipasavyo pamoja na uharibifu katika mitandao ya maji wa kujiunganishia kinyemela na kiholela umesababisha ongezeko kubwa la upotevu wa maji mpaka kufikia kati ya asilimia 40 hadi 45.

Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni asilimia 18 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa kama Sinza mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Katika muktadha huo hakuna sababu ya kusherekea wiki ya maji bila maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla hivyo Wizara ya Maji na mamlaka nyingine husika zitumie wiki hii kutoa majibu ya msingi kwa wananchi kuhusu namna ambavyo wataongeza kasi ya kushughulikia kero ya maji.
Itakumbukwa kwamba akihutubia Bunge mwezi Juni mwaka 2010 wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka wa fedha 2010/11 Waziri Mark Mwandosya aliahidi kwamba usanifu wa bwawa la Kidunda linatarajiwa kutoa mchango mkubwa wa utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi wa Ubungo lingekamilika mwezi Septemba mwaka huo wa 2010; lakini mwezi Machi 2011 Waziri Mwandosya kauli tofauti kuwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bwawa hilo utakamilika mwezi Juni mwaka 2011 na ujenzi mwaka 2013.
Kwa sababu hiyo, ni muhimu kuendelea kuwasilisha madai ili taratibu zote za msingi zikakamilishwa mwaka huu wa 2012 kwa haraka; hivyo pamoja na kutenga bilioni sita kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa ajili ya ulipaji fidia iongeze fedha kwa ajili ya ujenzi kuanza. Maamuzi haya yafanyike pia kuhusu kuharakisha upanuzi wa Bomba la Ruvu Chini na ujenzi wa bomba jipya toka Ruvu Juu kama Serikali ilivyoahidi bungeni wakati wa kujibu swali langu la msingi tarehe 13 Aprili 2011.
Aidha, DAWASA ambayo ndiyo mamlaka yenye dhamana ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam ieleze ni lini maeneo ya pembezoni yenye mtandao wa mabomba maarufu kama mabomba ya wachina hususani ya Kimara Bonyokwa, King’ong’o, Mbezi kwa Msuguri, Malambamawili yataanza kutoa maji.

Kama hatua za dharura, DAWASA iharakishe kukamilisha uchimbaji wa visima virefu nane vyenye kuweza kuhudumia kwa ujumla wakazi zaidi ya elfu thelathini wa Kimara Mavurunza, Bonyokwa, Kilungule na King’ong’o kama ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Mei mwaka 2010.

Visima hivi ni suluhisho la dharura wakati tukiendelea kufuatilia suluhisho la kudumu linalopaswa kuhusisha pamoja na mambo mengine kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikataba, kudhibiti ufisadi unaofanywa katika mtandao ikiwemo kukabiliana na upotevu wa maji unaondelea na kupanua miundombinu.

DAWASA ieleze pia mpango ilionao wa kumalizia maeneo ambayo hayakufikiwa na mtandao wa mabomba ya maji hususani ya pembezoni ya Saranga, Makoka, Msakuzi, Kibamba, Kwembe, Msakuzi, Goba, Mpiji Magohe, Makabe, Msumi, Kilungule nk.

Kwanini madai ya sasa ya maji yaelekezwe DAWASA kwa niaba ya Serikali?
Ni muhimu ikazingatiwa kuwa kwa mujibu wa katiba ibara ya 8 mamlaka na madaraka yote ni ya umma, serikali na vyombo vyake vinafanya kazi kwa niaba; hivyo wiki hii ya madai ya maji iwezeshe kuongeza msukumo katika kazi za kuboresha upatikanaji wa maji kwa njia mbalimbali.

Njia mojawapo ni pamoja na kuwasilisha madai ya mamlaka husika na kutaka majibu kuhusu kazi ambazo zinafanyika na katika wiki hii ya madai ya maji, pamoja na kuwa wahusika wa masuala ya maji ni wengi kwenye sekta ya umma na sekta binafsi; ni muhimu nguvu zielekezwe kwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA).

Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya DAWASA (Dar es salaam Water and Sewerage Authority Act no.20 of 2001) kifungu cha 22 DAWASA ndio chombo kikuu cha utekelezaji wa mipango na sera za serikali kuhusiana na maji, ugavi wa maji, huduma za maji taka na uhifadhi wa maji katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla.

Tarehe 1 Julai 2005 DAWASA ilitoa mkataba wa ukodishaji (lease agreement) kwa DAWASCO ambao unaitaka DAWASCO kuendesha miundombinu ya maji na kuhakikisha matengenezo ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam.

Hata hivyo, uhusiano wa DAWASA na DAWASCO ni kama wa mwenye duka na muuza duka; ambao kunaweza kuwa na matatizo ya muuza duka lakini lakini panaweza kuwa na matatizo ya uhaba wa bidhaa na duka lenyewe ambayo kimsingi yanamhusu mwenye duka.

Hivyo, katika wiki hii ya madai ya maji nguvu zielekezwe kwenye kuisimamia DAWASA ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha sheria tajwa inatumia kodi za wananchi wote ikiwemo ambao hawapati huduma ya maji toka kwao na pia tozo za wateja wanaopata maji kwa mgawo, hivyo DAWASA inawajibika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa kuzingatia sheria, kanuni, mikataba na mipango.

Bodi ya DAWASA inapaswa kwa kuzingatia mamlaka yake kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Sheria tajwa na majukumu mengine ya DAWASA kwa kurejea vifungu vya 6, 7 na 8 vya sheria husika kuhakikisha huduma ya maji safi na maji taka inapatikana kwa wananchi.

Mtakumbuka kwamba Machi Mosi 2012 niliungana na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) katika kata saba Jimboni Ubungo kwenye kazi za kuboresha upatikanaji wa maji.

Tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na wanahabari na kutaka hatua za ziada kuchukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) na Wizara ya Maji.

Nashukuru kwa hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na DAWASCO na EWURA katika masuala kadhaa; hata hivyo sijaridhika na namna ambavyo DAWASA na Wizara ya Maji wanavyoshughulikia masuala ya maji katika maeneo mengi; hivyo wiki ya madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii itumike kuongeza msukumo wa umma kabla ya kuchukua hatua zaidi za kibunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 10 Aprili 2012.

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
18/03/2012

MTEMBELEE MHESHIMIWA MNYIKA KWENYE TOVUTI YAKE INAYOPATIKANA HAPA

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.