19 Mar 2012



WIKI YA MADAI YA MAJI

Mwito wa kushiriki wiki ya madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii:
Nimerejea toka Afrika Kusini nilipokuwa kikazi na kukuta Wizara ya Maji imezindua maadhimisho ya Wiki ya Maji kuanzia tarehe 16 Machi na kilele kitakuwa Siku ya Kimataifa ya Maji tarehe 22 Machi 2012.

Ujumbe wa mwaka huu ni “Maji na Usalama wa Chakula”, hata hivyo tunahimizwa kuadhimisha ujumbe mpya bila kuelezwa matokeo ya ujumbe wa mwaka mmoja uliopita wa “Maji kwa ajili ya Miji: Kukabiliana na changamoto mbalimbali mijini”.

Kazi ya wabunge na bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika kuwezesha maendeleo kwa kutumia rasilimali za umma na za wadau wengine.

Kwa nafasi hiyo natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo na wa Jiji la Dar es salaam kwa ujumla kwamba badala ya kuadhimisha sherehe za maji bila ya maji kila mmoja ashiriki kwa namna mbalimbali katika Wiki ya Madai ya Maji.

Kila mmoja anaweza kushiriki kwenye wiki hii ya madai ya maji kwa njia mbalimbali, njia mojawapo ambayo natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuitumia ni kushiriki madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii kwa kuandika barua pepe kwa bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) kuitaka ifanye kazi ipasavyo ya kuharakisha upatikanaji wa maji kwa mujibu wa sheria, kanuni, mipango na mikataba.

Waandikie wajumbe wa bodi ya DAWASA madai ambayo unataka wayafanyie kazi katika eneo lako na nakala ya barua pepe hiyo kuituma kwa[email protected] kwa ajili za hatua zaidi za kibunge za uwakilishi na usimamizi.

Bodi ya DAWASA ni kama ifuatavyo: Mwenyekiti Dr. Hawa E. Sinare([email protected]), Makamu Mwenyekiti-Alhaj Said H. El-Maamry[email protected], wajumbe: Bw. Laston Msongole ([email protected]),Bi. Mary Mbowe ([email protected]) , Bi. Christine Kilindu([email protected]), Bw. Daniel Machemba ([email protected],[email protected]), Alhaj Bakari Kingobi ([email protected]), . Mary G. Musira([email protected]), B. Florence S. Yamat ([email protected]), Mh. Amina N. Mkilagi (Mb), Mhandisi. Archard Mutalemwa-Afisa Mtendaji Mkuu ([email protected]).

Tuungane pamoja kutaka serikali kuu na serikali za mitaa zitumie wiki hiyo kutoa maelezo kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika kutekeleza miradi ya maji na pia kuharakisha uzinduzi wa miradi ilicheleweshwa.

Njia hii ya kuunganisha nguvu ya umma kwa kutumia TEHAMA (SMS, facebook, twitter, email na njia nyingine) tuliitumia tarehe 1 Disemba 2011 wakati wa kuhamasisha umma kushiriki mkutano wa wadau uliotishwa na EWURA kuhusu ombi la TANESCO kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa 155% (zaidi ya mara tatu ya bei iliyokuwepo).

Hatimaye umeme ulipandishwa lakini si kwa kiwango hicho cha awali bali kwa wastani wa 40% kwa kuzingatia pia viwango vya utumiaji. (Suala la Umeme nimeanza kuchukua hatua zingine kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kutokana na matatizo yanayoendelea kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa umeme na nitatoa kauli kuhusu mgawo wa umeme unaoendelea kinyemela).

Izingatiwe kuwa nilipanga kwenye wiki hii ya madai ya maji kuunganisha nguvu ya umma kwa kuwaongoza wananchi kukutana na serikali na mamlaka nyingine zinazohusika hata hivyo itabidi kutumia njia mbadala za kuwasilisha madai.

Hii ni kwa sababu kuanzia kesho tarehe 19 Machi 2012 nitakuwa mfululizo mahakamani kwenye kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Ubungo wa mwaka 2010. Hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea nitaendelea kutumia njia nyingine za kibunge kuchukua hatua kuhusu masuala ya maji lakini natoa mwito kwa wananchi nanyi kwa upande wenu kila mmoja kuchukua hatua zinazowezekana katika wiki hii ya madai ya ya maji. Umoja ni Nguvu.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji bila ya Maji
Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji kuwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.

Uchakavu na wa miundombinu kutokana na mabomba kutokarabatiwa ipasavyo pamoja na uharibifu katika mitandao ya maji wa kujiunganishia kinyemela na kiholela umesababisha ongezeko kubwa la upotevu wa maji mpaka kufikia kati ya asilimia 40 hadi 45.

Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni asilimia 18 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa kama Sinza mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Katika muktadha huo hakuna sababu ya kusherekea wiki ya maji bila maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla hivyo Wizara ya Maji na mamlaka nyingine husika zitumie wiki hii kutoa majibu ya msingi kwa wananchi kuhusu namna ambavyo wataongeza kasi ya kushughulikia kero ya maji.
Itakumbukwa kwamba akihutubia Bunge mwezi Juni mwaka 2010 wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka wa fedha 2010/11 Waziri Mark Mwandosya aliahidi kwamba usanifu wa bwawa la Kidunda linatarajiwa kutoa mchango mkubwa wa utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi wa Ubungo lingekamilika mwezi Septemba mwaka huo wa 2010; lakini mwezi Machi 2011 Waziri Mwandosya kauli tofauti kuwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bwawa hilo utakamilika mwezi Juni mwaka 2011 na ujenzi mwaka 2013.
Kwa sababu hiyo, ni muhimu kuendelea kuwasilisha madai ili taratibu zote za msingi zikakamilishwa mwaka huu wa 2012 kwa haraka; hivyo pamoja na kutenga bilioni sita kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa ajili ya ulipaji fidia iongeze fedha kwa ajili ya ujenzi kuanza. Maamuzi haya yafanyike pia kuhusu kuharakisha upanuzi wa Bomba la Ruvu Chini na ujenzi wa bomba jipya toka Ruvu Juu kama Serikali ilivyoahidi bungeni wakati wa kujibu swali langu la msingi tarehe 13 Aprili 2011.
Aidha, DAWASA ambayo ndiyo mamlaka yenye dhamana ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam ieleze ni lini maeneo ya pembezoni yenye mtandao wa mabomba maarufu kama mabomba ya wachina hususani ya Kimara Bonyokwa, King’ong’o, Mbezi kwa Msuguri, Malambamawili yataanza kutoa maji.

Kama hatua za dharura, DAWASA iharakishe kukamilisha uchimbaji wa visima virefu nane vyenye kuweza kuhudumia kwa ujumla wakazi zaidi ya elfu thelathini wa Kimara Mavurunza, Bonyokwa, Kilungule na King’ong’o kama ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Mei mwaka 2010.

Visima hivi ni suluhisho la dharura wakati tukiendelea kufuatilia suluhisho la kudumu linalopaswa kuhusisha pamoja na mambo mengine kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikataba, kudhibiti ufisadi unaofanywa katika mtandao ikiwemo kukabiliana na upotevu wa maji unaondelea na kupanua miundombinu.

DAWASA ieleze pia mpango ilionao wa kumalizia maeneo ambayo hayakufikiwa na mtandao wa mabomba ya maji hususani ya pembezoni ya Saranga, Makoka, Msakuzi, Kibamba, Kwembe, Msakuzi, Goba, Mpiji Magohe, Makabe, Msumi, Kilungule nk.

Kwanini madai ya sasa ya maji yaelekezwe DAWASA kwa niaba ya Serikali?
Ni muhimu ikazingatiwa kuwa kwa mujibu wa katiba ibara ya 8 mamlaka na madaraka yote ni ya umma, serikali na vyombo vyake vinafanya kazi kwa niaba; hivyo wiki hii ya madai ya maji iwezeshe kuongeza msukumo katika kazi za kuboresha upatikanaji wa maji kwa njia mbalimbali.

Njia mojawapo ni pamoja na kuwasilisha madai ya mamlaka husika na kutaka majibu kuhusu kazi ambazo zinafanyika na katika wiki hii ya madai ya maji, pamoja na kuwa wahusika wa masuala ya maji ni wengi kwenye sekta ya umma na sekta binafsi; ni muhimu nguvu zielekezwe kwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA).

Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya DAWASA (Dar es salaam Water and Sewerage Authority Act no.20 of 2001) kifungu cha 22 DAWASA ndio chombo kikuu cha utekelezaji wa mipango na sera za serikali kuhusiana na maji, ugavi wa maji, huduma za maji taka na uhifadhi wa maji katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla.

Tarehe 1 Julai 2005 DAWASA ilitoa mkataba wa ukodishaji (lease agreement) kwa DAWASCO ambao unaitaka DAWASCO kuendesha miundombinu ya maji na kuhakikisha matengenezo ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam.

Hata hivyo, uhusiano wa DAWASA na DAWASCO ni kama wa mwenye duka na muuza duka; ambao kunaweza kuwa na matatizo ya muuza duka lakini lakini panaweza kuwa na matatizo ya uhaba wa bidhaa na duka lenyewe ambayo kimsingi yanamhusu mwenye duka.

Hivyo, katika wiki hii ya madai ya maji nguvu zielekezwe kwenye kuisimamia DAWASA ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha sheria tajwa inatumia kodi za wananchi wote ikiwemo ambao hawapati huduma ya maji toka kwao na pia tozo za wateja wanaopata maji kwa mgawo, hivyo DAWASA inawajibika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa kuzingatia sheria, kanuni, mikataba na mipango.

Bodi ya DAWASA inapaswa kwa kuzingatia mamlaka yake kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Sheria tajwa na majukumu mengine ya DAWASA kwa kurejea vifungu vya 6, 7 na 8 vya sheria husika kuhakikisha huduma ya maji safi na maji taka inapatikana kwa wananchi.

Mtakumbuka kwamba Machi Mosi 2012 niliungana na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) katika kata saba Jimboni Ubungo kwenye kazi za kuboresha upatikanaji wa maji.

Tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na wanahabari na kutaka hatua za ziada kuchukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) na Wizara ya Maji.

Nashukuru kwa hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na DAWASCO na EWURA katika masuala kadhaa; hata hivyo sijaridhika na namna ambavyo DAWASA na Wizara ya Maji wanavyoshughulikia masuala ya maji katika maeneo mengi; hivyo wiki ya madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii itumike kuongeza msukumo wa umma kabla ya kuchukua hatua zaidi za kibunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 10 Aprili 2012.

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
18/03/2012

MTEMBELEE MHESHIMIWA MNYIKA KWENYE TOVUTI YAKE INAYOPATIKANA HAPA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.