20 Apr 2012

Waziri Mkuu Pinda akifanya usanii wa kulia bungeni katika sakata la maalbino.Je hatorejea tena mbinu hii?

Tusiume maneno.Tanzania hivi sasa inayomba kwa vile Rais tuliye nae,Jakaya Kikwete,ni mithili ya mtu asiyejua kwanini Watanzania walimpa dhamana ya kuongoza nchi yetu-moja ya nchi masikini kabisa duniani licha ya utajiri luluki ilionao.

Kikwete alifanya uzembe kwa kuteua rundo la mawaziri (ambapo ukubwa tu wa Kabineti yake ni mzigo mzito kwa nchi yetu masikini) lakini kana kwamba hiyo haitoshi,akajaza wababaishaji kibao ambao aidha ni maswahiba wake au kwa busara zinazomtosha yeye pekee aliwaona wababaishaji hao kama sehemu muhimu ya timu yake ya kuwaletea Watanzania MAISHA BORA.

Hivi Rais mwenye busara angeweza kumkabidhi Mustafa Mkulo Uwaziri wa Fedha ilhali historia yake huko nyuma inafahamika vyema?Well,Kikwete hakumpa Mkulo nafasi hiyo kimakosa bali kwa sababu maalum.Teuzi za Mawaziri wa Fedha Barani Afrika huzingatia sana ushkaji kati ya Rais na mteuliwa.Kimsingi,wengi wa mawaziri wa fedha wa Afrika ni kama wahasibu binafsi wa Rais.

Si kwamba Kikwete hajui ufisadi wa Mkulo na mawaziri wengine.HAPANA.Anafahamu fika ila hawezi kuchukua hatua kwa vile Mkulo hafanyi hivyo pasipo uelewa wa bosi wake.Hapa ninamaanisha kuwa kwa kiasi kikubwa,kinacholalamikiwa kuhusu Mkulo kina baraka za Kikwete.

Sijui Tanzania itakuwa katika hali gani wakati huyu mtu anamaliza muda wake hapo 2015!Cha kusikitisha zaidi,wakati nchi inazidi kuangamia yeye yuko bize kushindana na Christopher Columbus kwenye 'safari za uvumbuzi.'

Majuzi kapewa ripoti ya ukaguzi wa fedha za serikali na CAG Ludovick Utouh.Kana kwamba kilichomo kwenye ripoti hiyo ni salamu za hepi bethdei,siku chache baadaye Kikwete huyooo safarini Brazil.Hana habari kuwa nchi inaangamia.Yey na safari,safari na yeye.Basi bora amwondoe Waziri wa Mambo ya Nje,Bernard Membe,kisha yeye Kikwete ajiongezee wadhifa wa uwaziri huo ili akisafiri hata kila wiki tujue moja.

Back to the point ya kumwajibisha Pinda na/au mawaziri,well,kama wabunge watafanikiwa kutekeleza hilo itakuwa vema.Waiwasi wangu mkubwa ni unafiki wa wengi wa wabunge wa CCM.Japo Tanzania yetu inaanza kuonyesha dalili za watu kuchoka kuiona nchi ikigeuzwa shamba la bibi,napatwa na wasiwasi kama wabunge wa CCM watakauwa tayari kumtosa Pinda au kushinikiza mawaziri mafisadi wajiuzulu.Pinda ni msanii anayeweza kuwahadaa wabunge wa chama chake kwa kulia tena hadharani....nao wakalainika.

Lakini,hata kama Pinda na mawaziri mafisadi waking'olewa,bado tutaendelea kuwa na tatizo hapo juu kabisa-yaani Kikwete na urais wake wa sandakalawe (wa kubahatisha).Ameshauthibitishia umma wa Watanzania kuwa sio tu yeye ni dhaifu wa uongozi bali pia hana nia ya kurekebisha chochote dhidi ya kansa inayoitafuna nchi yetu.

Anyway,kama kura ya kutokuwa na imani na Pinda itafanikiwa nadhani hatua itakayofuata ni kura ya kutokuwa na imani na Kikwete mwenyewe.Actually,ni kwa sababu tu ya hizi taratibu za kirasimu za kupiga kura.Sidhani kama kuna Mtanzania yeyote mwenye akili timamu ana imani na Kikwete-hasa baada ya kushindwa kutekeleza hata ahadi alizojiwekea mwenyewe pasipo shinikizo lolote lile.Kitu pekee ambacho amefanikiwa kukitekeleza kwa ufanisi mkubwa ni mashidano yake dhidi ya Vasco da Gama na Christopher Columbus.

MUNGU INUSURU TANZANIA (kwa namna yoyote ile...hata kama ni kwa majonzi) 

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube