20 Apr 2012


Pinda kumfuata Lowassa

• HATMA YA MAWAZIRI WATANO MIKONONI MWA JK

na Mwandishi wetu

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, sasa yuko katika hatari ya kuondolewa madarakani kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kufuatia tuhuma nzito za ubadhirifu wa fedha za umma unaodaiwa kuwahusisha mawaziri watano wakiongozwa na Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo.

Akiwasilisha majumuisho ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, aliliambia Bunge kuwa kuanzia leo wataanza kukusanya saini za wabunge wenye nia ya kupiga kura hiyo na kwamba uamuzi wake utawasilishwa bungeni Jumatatu wiki ijayo.

Mwenyekiti huyo alisema ikiwa mawaziri hao ambao hata hivyo hakuwataja majina mmoja baada ya mwingine hawatakuwa wamejiuzulu wenyewe hadi kufikia siku hiyo, basi wabunge watamwondoa Pinda madarakani kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.

Kwa hali hiyo, Zitto alisema kuwa itakuwa ni jukumu la mawaziri hao kabla ya Jumatatu wiki ijayo kuamua wenyewe kujiuzulu au kumwacha waziri mkuu atimuliwe.

Hatua hiyo ya Zitto ilitokana na hoja iliyokuwa imetolewa mapema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ambaye aliwataka wenyeviti wa kamati za Bunge wakati watakapokuwa wanajumuisha hoja zao kupendekeza kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu Pinda ikiwa mawaziri wake hawatakuwa wamejiuzulu wenyewe.

Lissu alisema wakati wa kupiga kelele umekwisha, na sasa wanachotakiwa ni kuchukua hatua, kwani mamlaka hiyo wanayo kwa mujibu wa Katiba.

“Waziri Mkuu wajibika kwa madudu ya serikali. Nitaomba wenyeviti wa kamati hizi wanapomalizia mjadala huu kupendekeza kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu kwa kujenga mfumo wa siasa wa udokozi. Tukifanya hivyo wananchi watatuamini. Ninyi chama tawala ndio mnaosababisha haya kama mtatumia wingi wenu sawasawa tutafanikiwa, sisi tupo wachache.

“Badala ya kupiga makofi, chukua hatua kwa uozo huu. Mkifanya hivyo mtaheshimika na msipofanya hivyo mtaingia kwenye vitabu vya historia,” alisema.

Alisema masuala ya ufisadi yamekuwa yakizungumzwa na zaidi ya miaka 10 sasa, lakini hawajawahi kuona serikali ikichukua hatua.

“Wakati kila mwaka CAG anatuletea taarifa za wizi, hatujawahi kuona serikali ikichukua hatua dhidi ya wahusika. Hatujawahi kuona mtendaji amechukuliwa hatua wala waziri kuwajibika katika hili. Watu wanapata kupata nafasi za uwaziri ili kuhujumu nchi,” alisema na kuongeza mfumo uliopo ni wa kulinda wezi.

Tanzania sio ya CCM

Akichangia mjadala huo, asubuhi na pia jioni, Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) aliwafyatua mawaziri kadhaa akisema kuwa wanaongoza kwa kutafuna pesa za Watanzania na kumtaja Waziri wa Fedha Mustafa Mkullo kuwa kinara wa wizi huo.

Mbunge huyo alisema baadhi ya mawaziri wamegeuka kuwa mchwa wanaotafuta fedha za Watanzania bila woga na kuongeza kuwa sasa umefika wakati kwa wabunge kuweka tofauti za kisiasa pembeni na kuzungumza kwa umoja masuala yanayoliangamiza taifa, na katika hilo akadai kuwa hatakuwa tayari kuwaachia mawaziri wachache waangamize nchi.

“Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza na kusikitisha kuwa nchi inatafunwa. Wanaofanya haya ni mawaziri wetu. Nchi inakufa na tuelewe kuwa Tanzania sio mali ya CCM, ni ya Watanzania wote.

“Mawaziri wetu wamekuwa mchwa, wanaangamiza nchi na leo nitamtaja waziri anayeongoza kwa kutafuta fedha za Watanzania. Ni Waziri wetu wa Fedha, Mustafa Mkulo. Ameuza viwanja, amelidanganya Bunge baada ya kuivunja CHC,” alisema mbunge huyo.

Awali Filikunjombe alisema Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, alikuwa amelidanganya Bunge kwa kudai amefuata maagizo yote ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Alisema kuwa ana ushahidi wa kutosha jinsi mawaziri hao wanavyoitafuna nchi na kuhoji Bunge linachukua hatua gani inapobainika mawaziri wamelidanganya Bunge.

“Waziri Chami amedai kuwa ametekeleza agizo la kamati kuhusu uchunguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Uchunguzi ulifanywa wakati mkurugenzi alikuwa akiendelea na kazi, wakati kamati ilishauri wakati wa uchunguzi mkurugenzi huyo awekwe pembeni,” alisema.

Kutokana na kauli hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye pia ni mnadhimu mkuu wa shughuli za serikali bungeni, alimtaka kuthibitisha madai kuwa mawaziri wote ni wezi kwa kukabidhi ushahidi na kama hana uhakika na anachozungumza afute kauli hiyo. Hata hivyo, mbunge huyo alisisitiza kuwa alichosema ni kwamba mawaziri wengi ni wezi na si wote.

Mbunge wa Kasulu, Moses Machari, alisema wabunge wanaotaka mawaziri na wabadhirifu kunyongwa wanafanya hivyo wakiwa na akili timamu kwa sababu wamechoshwa na wizi wa waziwazi unaofanywa na mawaziri na baadhi ya viongozi wa serikali bila kuchukuliwa hatua yoyote.

Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), alitaja waziwazi majina ya vigogo wanaomiliki kampuni za ukaguzi wa magari ambazo zilitajwa bungeni kama ni za nje, hali iliyolifanya Bunge kuzizima kwa muda.

Nyerere alisema kuwa makampuni hayo yalilipwa mamilioni ya dola za Kimarekani kwa udanganyifu, na kibaya zaidi waziri mhusika akalidanganya Bunge akidai kuwa taarifa hizo zilikuwa za uongo. Alionyesha kushangazwa kwake na nguvu kubwa ya kumlinda Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Nchini (TBS) wakati ukweli wa mambo uko wazi.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, alisema kuwa dhana iliyojengeka kuwa wizara hiyo inaibena TBS na mkurugenzi wake, haina ukweli, kwani taarifa ya kamati ndogo ya uchunguzi wa shirika hilo aliipata jana na ameshaiagiza bodi ya shirika hilo kuifanyia kazi.

Hata hivyo, alisema yuko tayari kuweka rehani uwaziri wake iwapo mbunge huyo atathibitisha kuwa kuna kampuni hewa zinazokagua magari nje ya nchi na iwapo kampuni hizo zina uswahiba naye.

“Nimekosea wapi? Kila nilichoagizwa nimetekeleza. Wizara halindi uozo. Tukilazimishwa kufanya maamuzi bila kufuata taratibu tutakuwa tunakiuka sheria,” alisema.

Ujasiri huo hata hivyo, uliyeyuka kama nta jioni, baada ya Nyerere kumuumbua kwa kutaja majina ya wamiliki wa kampuni hizo, hali iliyompa wakati mgumu waziri huyo.

Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy (CCM), alishauri Rais Kikwete kuacha upole na kuwashughulia wote wanaotafuna mali za umma.

“Mawaziri walioshindwa kazi waondolewe na wawekwe wengine. Hakuna aliyesomea uwaziri kila mtu anaweza kuwa waziri. Unakuta kiongozi anatembea na msafara wa magari 40 unamtisha nani. Wakati watu hawana dawa wala chakula,” alisema.

Alisema kutokana na ubadhirifu huo, hata watendaji wa chini wa halmashauri wanakuwa na fedha nyingi kuliko halmashauri yenyewe, hali inayochangia kuiendesha serikali.

“Mafisadi wote tuwanyonge. Tukishanyonga 10 wataogopa. Leteni muswada mtu yeyote mwizi wa mali za umma anyongwe na mali itaifishwe. Tutaokoa nchi yetu. Wabunge tuwe wakali, lisiwe Bunge la mchezo mchezo,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, alisema kila wizara kuna mambo ya hivyo na kusema kinachoonekana mawziri hawajali suala hilo.

“Wabunge wa CCM twende kwenye Party Cacus tukafanye kazi tuliyotumwa. Kama kuna mtu atatulaumu basi, tuondoe waziri asiyefaa. Mbilinyi, Iddi Simba na Ngasongwa waliondolewa humu ndani. Tufanye kazi ya kibunge jamani. Nawaomba wabunge tufanye jukumu letu na tukifanya hakuna waziri atakayefanya mchezo,” alisema.

Wabunge waridhia vikao bila posho

Kutokana na uzito wa suala hilo, wabunge wameunga mkono hoja ya kuendelea na mjadala huo kwa kuongeza siku mbili zaidi hata kama vikao hivyo havitakuwa na posho.

Hoja hiyo ilitolewa na mbunge wa Buchosa, Dk. Charles Tizeba (CCM), ambaye alisema siku zilizotengwa kwa ajili ya kuchangia mjadala huo ni chache, hivyo wabunge wote walioomba kuchangia wanaweza wasipate nafasi.

“Mjadala huu ni muhimu sana, tunaomba kuongezewa siku mbili au tatu za kujadili suala hili hata kama hakuna posho tutafanya hivyo,” alisema Tizeba na hoja hiyo kuungwa mkono na nusu ya wabunge waliokuwapo ukumbini hapo.

Naibu Spika, Job Ndugai, alieleza kuwa hajawahi kuona hoja iliyoungwa mkono kama hiyo na kusema suala hilo atalifikisha kwa Spika, Anne Makinda, ambaye naye atajadiliana nayo na kamati ya uongozi na ndipo atakapotoa majibu kuhusiana na hoja hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Christowaja Mtinda (CHADEMA), alisema suala la mishahara hewa limekuwa sugu katika elimu ya juu na kwamba imefikia hatua jina lake limetumika katika suala hilo.

“Pale Open University kuna mtumishi anaitwa Christowanja Mtinda. Sijawahi kuomba kazi hapo wala kufanya kazi hata siku moja,” alisema.

Aidha, alisema makatibu wakuu hawakai katika nyumba zao zilizoko Dodoma na kusema kuwa wanazitumia wakati wa bikao vya Bunge na kuhoji kwa nini nyumba hizo wasipewe wabunge ambao wanapokuwa wanahudhuria vikao vya Bunge wanapata shida kupata nyumba za kuishi.

Naye Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa, alishauri wabunge wapitishe sheria ya kuwapo kwa kamati kwa ajili mawaziri wanaoshindwa kuwajibika.

“Wenzetu wa Kenya wameanzisha sheria kwa ajili ya mawaziri wanaotoa ahadi zisizotekelezeka. Baada ya miezi miwili anaulizwa ametekeleza ahadi kwa kiwango gani, akishindwa anatimuliwa. Kenya wameshafukuza mawaziri. Tukianzisha hiyo mawaziri watahakikisha ahadi zao zinatekelezeka. Ni lazima tuwe na mahali pa kuanzia,” alisema.

Aidha, alihoji wizara kutumia fedha nyingi katika maonesho mbalimbali kama Sabasaba, Nanenane na utumishi na kuhoji yameleta manufaa gani nchini. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imetumia sh bilioni 1.9 kwa ajili ya maonesho kama hayo katika kipindi cha mwaka 2009/2010.

Mapema asubuhi, Zitto alikuwa ameliomba Bunge kutoa kumbukumbu za mwaka jana kutokana na Waziri Aggrey Mwanri kuendelea kutoa ahadi bila kuwapo kwa utekelezaji.

“Ukichukua ‘hansard’ ya mwaka jana ukasoma maelezo ya majibu ya hoja hayana tofauti na haya anayotaka kutuaminisha leo. Mheshimiwa Naibu Spika naomba kupata mwongozo wako tupate hansard ya mwaka jana ya maelezo ya Mheshimiwa Waziri ili tulinganishe na maelezo ya sasa na aliyotolewa mwaka jana na tuone kama ametekeleza,” alisema Zitto.

Zitto alitoa kauli hiyo, baada ya Waziri Mwanri kueleza serikali imekuwa ikiingilia kati maeneo ambayo yanaona hayaendi na kusema kuwa watakapoanza kushughulikia masuala yanayolalamikiwa na wabunge wasianze kushikwa mikono.

“Tunaomba wabunge tusaidiane; tuseme hakuna kumhamisha mtumishi yeyote aliyekwenda kinyume na tutamchukulia hatua hapo hapo,” alisema.

Aidha, alisema baraza la madiwani limepewa nguvu kushughulikia matatizo yote ya halmashauri husika na kuongeza kwamba hiyo ni vita iliyopangwa na isiyopangwa.

“Hilo rungu tumeshapewa. Tuachieni. Mrema naomba tuamini. Tukitoka hapa kazi ni moja kashi kashi tu...lugha hii inatokana na mazungumzo ya hapa ndani. Halmashauri zilizopata hati chafu, zimeshakabidhiwa barua, haiwezekani sh bilioni 6 zinaondoka halafu mkurugenzi anaendelea kuwapo,” alisema.

Hatma ya mawaziri kwa JK

HATMA ya mawaziri watano wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali ya umma sasa iko mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, kufuatia hatua ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi kutaka watendaji hao wajiuzulu.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika jana mchana mjini hapa zimesema kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameamua kulifikisha suala hilo mikononi mwa Rais Kikwete kwa uamuzi zaidi.

Chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, kimewataja wabunge wanaotakiwa kujiuzulu kuwa ni pamoja na waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, na Naibu wake, Lazaro Nyalandu, Waziri wa Fedha, Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),George Mkuchika, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu na Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda.

Katika kikao hicho cha dharura kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Pinda, wabunge hao walisema mawaziri hao wameiaibisha serikali kwa kiwango kikubwa, hali iliyosababisha wananchi kukosa imani na serikali yao na kuichukia.

Kikao hicho kilichoanza saa 7 mchana na kumalizika saa 11 jioni kilikuwa na mvutano mkali kati ya wabunge hao na mawaziri.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube