3 May 2012



RAIA MWEMA UGHAIBUNI
Wana usalama na nguvu yao kwa viongozi
Evarist Chahali
Toleo la 237
2 May 2012
MAKALA katika safu hii ya Novemba 2 mwaka jana ilianzisha uchambuzi wa nafasi za vyama mbalimbali vya siasa huko nyumbani katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Habari zilizotawala nchini Marekani hivi karibuni (na ambazo zinaendelea kuvuma japo si kwa kasi kubwa kama ilivyokuwa awali) ni kuhusu skandali iliyokikumba kitengo cha ulinzi wa Rais wa nchi hiyo, kinachofahamika kama Secret Service.
Kwa kawaida ya taratibu za kikazi, wanausalama hutangulia kukagua usalama wa sehemu inayotarajiwa kutembelewa na kiongozi wa juu wa nchi.
Msafara wa wanausalama hao unaweza kuweka makazi katika sehemu hiyo angalau mwezi mmoja kabla ya ziara husika kutegemea na hali ya usalama katika sehemu hiyo.
Sasa, kabla ya Rais Barack Obama kufanya ziara huko Amerika ya Kusini, jamaa wa Secret Service walishatangulia mapema kuhakikisha kwamba usalama wa kiongozi huyo muhimu si kwa Marekani bali dunia kwa ujumla, hauna mushkeli.
Pamoja na mashushushu waliotoka Marekani, walikuwako wenzao ambao kituo chao cha kazi ni eneo hilo la Amerika ya Kusini. Lakini katika mazingira yaliyosababisha mshtuko mkubwa, baadhi ya maafisa usalama hao walikumbwa na skandali ya kujihusisha na makahaba nchini Colombia.
Pengine skandali hiyo isingeibuka laiti mmoja wa mashushushu hao asingempunja ujira kahaba mmoja, ambaye katika harakati za kudai ‘haki yake’ alisababisha kuibuka kwa kashfa kubwa pengine kuliko zote kwa taasisi za usalama nchini Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa, kingine kilichochangia sakata hiyo kufichuka ni ushupavu wa mmoja wa viongozi wa Secret Service, mwanamama Mmarekani Mweusi, Paula Reid ambaye baada ya kupata taarifa za ‘madudu’ ya baadhi ya maafisa anaoongoza alimfahamisha Mkuu wa taasisi hiyo Mark Sullivan kuomba ruhusa ya kuwaondoa walioshiriki kwenye tukio hilo la aibu.
Duru za kisiasa, kiusalama na habari zimemwagia sifa lukuki mwanamama huyo ambaye amekuwa mtumishi wa Secret Service kwa miaka 21 sasa. Reid ni mmoja ya wanawake wachache kabisa Weusi kuwa viongozi kwenye taasisi hiyo nyeti.
Licha ya kulazimika kuchukua hatua alizochukua  kama kiongozi, ni wazi kuwa shushushu huyo wa kike alitambua bayana kuwa laiti ‘lingetokea la kutokea’, yeye kama kiongozi angebeba mzigo wote wa lawama.
Nimesimulia habari hii si tu kwa vile nimevutiwa sana na ujasiri wa Paula Reid bali pia ningependa kuitumia kama mfano katika kujadili mada ya leo: nafasi ya watendaji kazi katika kumjenga au kumbomoa kiongozi.
Nikiri kwamba kwa mara ya kwanza kabisa, katika siku chache zilizopita nimejikuta nikishawishika kuafikiana na kauli inayosikika mara kwa mara kumhusu Rais Jakaya Kikwete, kwamba ‘anaangushwa na wasaidizi wake.’
Labda kabla ya kuingia kwa undani kwenye mada hii ni muhimu kuwafahamu japo ‘kiduchu’ hao wanaoitwa wasaidizi wa Rais. Wakati kuna watumishi kadhaa walioteuliwa na Rais kufanya kazi naye kama wasaidizi wake, kuna idadi kubwa zaidi ya ‘wasaidizi wasioonekana’ na ambao kwa kiasi kikubwa hata Rais mwenyewe hawafahamu lakini wanawajibika zaidi ya hao wateuliwa wake kumpatia ushauri sahihi kila siku kuhakikisha kuwa nchi inakwenda vizuri. Hapa ninawazungumzia ndugu zetu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Wakati mara nyingi watu walioteuliwa na Rais kuwa wasaidizi wake huwa ‘waliobobea’ kwenye fani moja, wanausalama wetu ni watumishi wa umma ambao kwa mafunzo yao na utendaji kazi wao hubobea kwenye takriban kila eneo.
Kwa hiyo hadi hapo unaweza kubaini kuwa ‘wasaidizi’ muhimu wa Rais si mshauri wa uchumi, au siasa, nk bali ni Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambao kimsingi wanawajibika moja kwa moja kwa Rais.
Naomba ieleweke kuwa simaanishi kuwa ikitokea mshauri wa Rais ameboronga basi hilo litakuwa kosa la Maafisa Usalama. Hapana. Hapa ninajenga ‘picha pana zaidi’ kwa maana ya tija kutoka kwa watu wenye uelewa na ujuzi wa takriban kila eneo la maisha ya Mtanzania.
Turejee kwenye hoja ya kuwa Rais Kikwete anaangushwa na wasaidizi wake (ila hapa nitaangalia hao wasaidizi muhimu zaidi, yaani watu wa Idara ya Usalama wa Taifa).
Kwa mujibu wa taratibu, Idara hiyo ni wasaidizi wa Rais kwa njia ya ushauri tu. Japo wana namna ya kulazimisha ushauri huo utekelezwe, mazingira yetu yanafanya suala hilo kubaki la kinadharia zaidi kuliko vitendo.
Nitoe mfano. Kabla ya uvamizi wa Marekani nchini Iraki, wanasiasa wenye mrengo mkali wa kihafidhina wanaojulikana kama neo-conservatives au kwa kifupi neo-cons, walifanikiwa kuzishawishi taasisi za usalama za Marekani kufukua kila aina ya matishio ‘yaliyosababishwa na kuwapo kwa Saddam Hussein madarakani.
Japo Rais wa wakati huo, George Bush (mtoto) naye alikuwa muumini wa itikadi hiyo ya mrengo wa kulia kabisa wa uhafidhina, kwa kiasi kikubwa kilichompa nguvu ya kuamuru uvamizi wa nchi hiyo huko Iraki ni ‘uthibitisho’ (ambao baadaye ulibainika kuwa fyongo) kuwa Saddam ana silaha za maangamizi ya umma (weapons of mass destruction).
Kwa wanaofuatilia siasa za kimataifa watakumbuka kauli ‘maarufu’ ya mkuu wa Shirika la Kijasusi la nchi hiyo George Tenet  kuwa ‘ushahidi kuwa Saddam ana silaha za maangamizi ya umma ni sawa na 'kuchumpa' na mpira wa kikapu (slam dunk), yaani ni ushahidi wa wazi kabisa, japo baadaye ilibainika kuwa ushahidi huo ulikuwa na mushkeli mkubwa.
Nimetoa mfano huo kuonyesha jinsi gani taasisi ya usalama wa taifa inaweza ‘kulazimisha’ ushauri wake ufuatwe, hasa ikizingatiwa kuwa kimsingi uhai wa taasisi ya urais unategemea mno ufanisi wa idara ya usalama ya nchi husika.
Sasa, tukiangalia-kwa mfano-sakata la mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi na kutakuwa wajiuzulu (hadi wakati ninaandaa makala hii walikuwa hawajajiuzulu) tunaweza ‘kumhurumia’ Rais Kikwete kwa kutopewa usaidizi wa kutosha na watendaji wenye dhamana ya kufukua na kuweka wazi ‘madudu’ yote yanayodaiwa kufanywa na mawaziri hao.
Kwa kawaida, Idara ya Usalama wa Taifa hupenyeza watumishi wake katika taasisi mbalimbali kwa minajili ya kupata taarifa sahihi za kiusalama, ambazo hutengeneza msingi wa ushauri wao kwa Rais baada ya kuzichambua.
Je, inawezekana taasisi hiyo nyeti imeshindwa kupata taarifa hizo kiasi kwamba ikashindwa kumfahamisha Rais yanayofanywa na mawaziri wake? Je, inawezekana kuwa taasisi hiyo ilifanikiwa kukusanya taarifa hizo na kutoa ushauri mwafaka lakini ukapuuzwa? Nisingependa kubaishiri jibu kwani ukweli unafahamika kwa wahusika.
Lakini katika mazingira ya kawaida si rahisi kwa kiongozi wa nchi kuamua kupuuzia ushauri wa wasaidizi wake muhimu ambao si tu ‘wana macho kila eneo’ bali pia wanawezesha taasisi ya urais kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwa ujumla kuiwezesha nchi kuwa salama.
Katika namna fulani, wanausalama huhusika katika mchakato wa teuzi anazofanya  kiongozi mkuu wa nchi. Japo nisingependa kuingia kwa undani katika hilo, kwa kifupi ushauri wao ni muhimu sana (na pengine huzingatiwa) kabla Rais hajatangaza jina la anayemteua kushika wadhifa fulani.
Sasa, inapotokea baadhi ya wanaoteuliwa na Rais kuwa na walakini, inatubidi kujiuliza iwapo washauri walipotoka au aliyeshauriwa hakuzingatia ushauri husika.
Nimeshawishika kuafikiana na wanaodai kuwa Rais anaangushwa na wasaidizi wake kwa sababu, kwa uelewa wangu, tofauti na washauri wanaoteuliwa na Rais kwenye eneo moja, washauri muhimu kama wa Idara ya Usalama wenye uelewa wa takriban kila eneo wana namna wanayoweza kuitumia ‘kulazimisha ushauri wao ufuatwe kwa maslahi ya taasisi ya urais na taifa kwa ujumla.
Ikumbukwe kuwa Rais ni binadamu kama wengine, na si rahisi kufahamu kila kinachoendelea wizarani au mtaani. Wenye jukumu la kumsaidia kufahamu ni hao wasaidizi wake. Sasa kama hawatekelezi jukumu hilo ipasavyo itamwia vigumu Rais kufahamu kama ‘waziri fulani anafadhiliwa na mafisadi fulani’ au huko mtaani wananchi wanalalamikia hiki au kile.
Sawa, baadhi ya maamuzi yanapewa baraka na Rais kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri. Lakini katika mazingira ya kawaida tu ya kibinadamu, atawezaje kufahamu iwapo taarifa zinazowasilishwa kwenye vikao hivyo ni sahihi au la, pasipo wasaidizi wake wenye jukumu la ‘kusaka ukweli’ kumfahamisha mapema?
Nimalizie kwa kusisitiza kuwa ninapoizungumzia Idara ya Usalama wa Taifa katika namna yoyote ile ninasukumwa na imani yangu kwa taasisi hiyo na kutaka kuiona ikizifanyia kazi changamoto mbalimbali inazozikabili ili si tu iwe na msaada mkubwa kwa Rais na taasisi ya urais bali pia kwa Taifa kwa ujumla.
Taasisi hiyo ni uti wa mgongo wa kila nchi duniani, na kila mzalendo anapaswa kuisapoti kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na ‘kuishtua pale inapoonekana imesinzia’ kama ninavyofanya katika safu hii.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.