21 Jun 2012



NIANZE makala hii na ‘mchapo’ ambao nimeshawahi kuusimulia katika makala zilizopita. Ninaurejea mchapo huo kwa sababu ninaamini utasaidia kuwa mfano mzuri katika mada ninayozungumzia leo.
Nilianza uandishi magazetini katika namna ya ‘mzaha.’ Makala zangu za mwanzo kabisa zilihusu ‘unajimu uliosheheni utani.’ Nikiandikia moja ya magazeti ya mwanzo kabisa ya udaku-Sanifu-niliandika ‘utabiri’ kuhusu masuala mbalimbali kuendana na alama za kawaida za kinajimu.
Kwa mfano, niliweza ‘kutabiri’ kuwa “wiki hii usimzuwie mwanao kucheza barabarani kwani atagongwa na gari la ubalozi wa nchi moja inayojiweza. Ajali hiyo haitomsababishia madhara mwanao bali italeta neema kubwa, kwani Ubalozi husika utaamua kuifidia familia yako kwa kumpatia mwanao huyo makazi katika nchi yao tajiri duniani.
Ulikuwa utani tu, na lengo lilikuwa kuchekesha. Lakini, amini usiamini, baadhi ya wanafunzi wenzangu pale Chuo Kikuu sehemu ya Mlimani walikuwa wanachukulia unajimu huo kuwa una ukweli. Mara kadhaa wapo waliodiriki kuniuliza kuhusu nyota zao.
Na katika kuongeza hamasa katika ‘unajimu huo feki’ nikajipachika ‘jina la kinajimu, nikajiita Ustaadh Bonge (jina ambalo hadi leo linatumiwa na baadhi ya marafiki zangu wa tangu enzi hizo). Baada ya kutoka Sanifu niliendeleza ‘unajimu’ wangu kwenye gazeti la Kasheshe na baadaye Komesha (yote ya udaku, na ninadhani kwa sasa hayachapishwi tena).
Nimesimulia mchapo huo kuonyesha kuwa ni rahisi sana kuwaghilibu baadhi ya Watanzania wenzetu. Nitatoa mifano mingine mitatu kupigia mstari hoja yangu. Mfano mwingine ni tukio lililojitokeza wakati nikiwa bado mwanafunzi hapo Mlimani (kati ya 1996-1999). Siku moja nilifuatwa na mwanafunzi mwenzangu aliyenifahamisha kuwa “kuna dili imeibuka hapa Dar...ni njia ya mkato ya kupata utajiri. Unawekeza kiasi kadhaa cha fedha kisha baada ya muda mfupi kinazaa zaidi ya mara tatu ya kiwango hicho. Na kuipata watu wengi kujiunga basi unaweza kupata hata mara 10 ya kiwango ulichowekeza mwanzo.”
Hapa ninazungumzia kitu kilichofahamika kama Dollar Jet. Lakini kama ilivyo kwa ‘mazingaombwe’ mengine, ‘mbinu hiyo ya utajiri wa chap-chap’ ikazua kitu kingine kilichokuja kufahamika kama Shilingi Jet. Yaani hadi muda huu nikikumbuka ‘usanii’ huo ninaishia kucheka. Yaani hao wa Shilingi Jet walijifanya kama wazalendo fulani ambao wanaithamini sarafu yetu, na hivyo kuepuka neno ‘Dollar’ ambalo ni sarafu ya kigeni.
Haikuchukua muda mrefu, 'michezo' hiyo ikawaacha mamilioni ya Watanzania wakiwa na majonzi. Kimsingi, ‘michezo' hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa mtindo wa piramidi, ambapo wanufaika huwa wachache waliowekeza mwanzo, na lazima ifike mahala watu fulani wataambulia patupu. Ninaomba kukiri kuwa ushawishi wa mwanafunzi mwenzangu kuhusu michezo hiyo ulipelekea mie kuwekeza shilingi 10,000.Uzuri ni kwamba fedha ‘niliyowekeza’ haikuwa yangu bali ilitolewa na ‘mhamasishaji’ huyo. Lakini mwisho wa yote, mie na yeye tuliambulia patupu. Sikuumia kwa vile haikuwa hela yangu.
Mfano mwingine uliohusisha fedha pia ni ule wa ‘mchezo’ wa DECI. Ninadhani mfano huu unaweza ‘kutonesha vidonda ambavyo bado havijapona’ kwani piramidi hili lilitokea miaka tu machache iliyopita. Nina ndugu na marafiki ambao walikuwa wahanga wa ‘mchezo’ huo ulioendeshwa na watu waliokuwa wakihusishwa na taasisi moja ya kidini. Ninaamini kwamba moja ya kilichowavutia wengi kuiamini DECI ni kuhusika kwa watumishi wa Mungu.
Kilichotokea kwa wana-DECI kila mmoja anakifahamu. Hadi leo kuna wanaozilaumu baadhi ya taasisi za Serikali kwa madai kwamba walifahamu uwepo wa ‘mchezo’ huo (huku wengine wakienda mbali na kudai baadhi ya vigogo walikuwa washiriki, na walipovuna faida wakaamua kupiga marufuku) lakini hawakuchukua hatua katika muda mwafaka. Sijui kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa DECI imefia wapi, lakini kilicho wazi ni kuwa DECI imewaacha watu na madeni na umasikini kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake Dollar Jet na Shilingi Jet.
Mfano wa mwisho ni suala la ‘tiba ya miujiza ya kikombe cha Babu wa Loliondo.’ Hii ndio ilikuwa ‘kubwa kuliko zote’ kwani hata viongozi wa kitaifa hawakuona aibu kupigwa picha wakiwa na Kikombe cha Babu kilichodaiwa kutibu baadhi ya maradhi sugu ikiwa ni pamoja na Ukimwi.
Hadi wakati ninaandika makala hii haijafahamika ni watu wangapi waliopoteza maisha kutokana na mradi huo. Mimi nauita utapeli kwa sababu hakuna uthibitisho wowote kuwa Kikombe cha Babu kimemtibu mtu yeyote yule. Hata wakati habari hiyo ilipopamba moto, tulichosikia zaidi ni habari za misururu ya watu na magari kuelekea Loliondo lakini taarifa za ushuhuda wa waliopona zilikuwa haba.
Taratibu ‘uzushi kuhusu tiba hiyo’ ukafifia na, kama ilivyo kawaida ya Watanzania, hakuna aliyewajibishwa kwa kupotosha umma katika kiwango cha kihistoria (historical proportion).Viongozi waliopewa kikombe wamekuwa kimya kabisa kutujulisha kama maradhi yamepona au la. Kama walikuwa na ujasiri wa kupiga picha hadharani kutuonyesha kuwa wanaamini ‘tiba’ hiyo sijui kwa nini wamekosa ujasiri wa kutufahamisha ufanisi au udanganyifu wake.
Sasa baada ya mifano hiyo, nigeukie mada ya leo. Kilichonisukuma kuzungumzia mada hii ni habari niliyoiona mtandaoni kuwa msanii maarufu wa muziki wa Bongofleva, Hamisi Mwinjuma (anayefahamika kwa jina la kisanii kama ‘Mwanafalsafa’ au ‘MwanaFA’) amekanusha kuwa mafanikio yake katika usanii yametokana na uumini wa jumuiya (fraternity) ya Freemason.
Pasipo kurejea kanusho la ‘Mwanafalsafa’, kila anayemfahamu kijana huyo hatoshindwa kuelewa kwanini ameendelea kuwa mmoja wa wasanii waliofanikiwa sana katika fani yake. Na siku chache kabla hajakanusha habari hizo, mmoja wa wadau wakubwa wa muziki, Boniface Kilosa (anayefahamika zaidi kwa jina la ‘Bonny Luv’) alitamka bayana (alipohojiwa na kipindi cha runinga cha ‘Mkasi TV’ kuwa “msanii anayemkubali sana katika Bongofleva ni Mwanafalsafa...kwani anajituma na kuthamini sana fani yake.” Kwa wanaomfahamu Kilosa, kauli yake hiyo ilikuwa ni kama tamko rasmi la wataalamu waliobobea kwenye ‘muziki wa kizazi kipya.’
Ninamfahamu Mwinjuma kwa kiasi fulani (nilishawahi kufanya mahojiano naye) na ni mmoja ya watu tunaojadiliana takriban kila siku huko Twitter kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu nchi yetu.
Kwa vile kuna hisia kuwa wasanii wana uelewa mdogo wa mambo yasiyo ya burudani, ukisoma ‘majadiliano kati yetu unaweza kudhani msanii huyo ni mhadhiri au mtafiti fulani. Kwa kifupi, maendeleo yake ni matokeo ya mchanganyiko wa kipaji, akili, ubunifu na nidhamu ya kazi, na wala sio imani katika u-Freemason.
Kwa bahati mbaya (au makusudi) suala la Freemasonry limegeuka kuwa kama uzushi ule wa Dollar JetDECI na Kikombe cha Babu wa Loliondo. Kuna wanaoamini kabisa kuwa kujihusisha na Jumuiya hiyo ni njia ya mkato ya kupata mafanikio katika fani yoyote ile. Na ndiyo maana mafanikio ya akina ‘Mwanafalsafa’ yanahusishwa naFreemasonry.
Lengo la makala hii sio kuilaani au kuipinga Jumuiya hiyo hasa kwa vile kila mtu ana uhuru wa kuamini anachotaka alimradi kufanya hivyo hakumkwazi mwingine. Kinachosikitisha ni jitihada za makusudi za baadhi ya watu (na kile ninachokiita’ taasisi za kidaku’) kufanya jitihada za kuuaminisha umma kuwa mafanikio yanaweza kumwangukia mtu kama ‘Mana’ kwa kujihusisha na Freemasonry.
Nilisoma maoni ya wasomaji katika gazeti moja la huko nyumbani ambapo baadhi yao walidiriki kutamka bayana kuwa ‘wanataka kujiunga na Freemasonry kwa vile maisha yamekuwa magumu, na hiyo ndiyo njia rahisi ya kubadili hali zao kimaisha.’
Katika hili, utapeli sio Freemasonry bali hizo imani potofu zinazochochea kubweteka kwa matarajio kuwa kujihusisha na Jumuiya hiyo kutashusha neema kutoka kusikojulikana.
Naomba nieleze hili: kwa hapa Uskochi, mmoja wa marafiki zangu ni mshiriki wa ngazi ya juu katika Jumuiya hiyo, lakini ajira yake ni mfagizi (cleaner). Na kupitia yeye, ninawafahamu watu wengine wachache ambao licha ya ushiriki wao katika Jumuiya hiyo, hali zao kimaisha ni za kawaida tu. Sasa kama huku ambapo Jumuiya hiyo ipo wazi zaidi ya huko nyumbani kuna washiriki ambao ni hohehae kama mie, kwanini iwe tofauti huko?
Ninaomba ieleweke kuwa lengo langu si kushawishi watu wasijiunge na Freemasonrykama wanataka kufanya hivyo. Sina tatizo na Jumuiya hiyo kwa vile fraternities ni vitu vya kawaida katika nchi zilizoendelea. Tatizo langu ni hao wanaochochea uzembe kupitia uzushi unaohusisha Freemasonry na utajiri. Uwepo wa matajiri katika Jumuiya hiyo haumaanishi kuwa ni kama Benki ya wazi ya kwenda kujizolea utajiri.
Nimalizie kwa kuwasihi vijana wenzangu kuwa hakuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio. Ukikaa kijiweni kutwa nzima na kudhani u-Freemason utakuletea utajiri, utakufa masikini.
Ndiyo, hali ya maisha huko nyumbani ni ngumu lakini ndoto za alinacha haziwezi kuwa sehemu ya ufumbuzi wa hali hiyo. Na badala ya kutumia muda mwingi kuyahusisha mafanikio ya watu kama ‘Mwanafalsafa’ na imani fulani, pengine ni vema kujifunza kutoka kwao katika namna wanavyojibidisha na kuzichukulia fani zao kama sehemu muhimu ya maisha yao.
Penye nia pana njia.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.