31 Jul 2012



Mara nyingi kwa wenzetu huku nchi za Magharibi kila jambo linapotokea watu wa kada mbalimbali hujihangaisha kusaka maelezo yanayojitosheleza kuhusu chanzo cha tukio husika na jinsi linavyoweza kuzuiwa mbele ya safari.
Ukiangalia nchini Marekani, kwa mfano, mara baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001, taasisi mbalimbali zilikuna vichwa kusaka chanzo cha mashambulizi hayo na jinsi nchi hiyo itakavyoweza kuzuia uwezekano wa mashambulizi kama hayo kujirudia.
Ninaamini kwa wanaofuatilia siasa za kimataifa watakumbuka kazi iliyofanywa na Kamisheni ya Septemba 11 ambayo kwa kiasi kikubwa ilifukua kila eneo kuhakikisha inapata taarifa sahihi kuhusu mashambulizi hayo ya kigaidi na usalama wa nchi hiyo kwa ujumla.
Yayumkinika kuhitimisha kwamba jinsi Marekani ilivyoshughulikia ‘aftermath’ ya mashambulizi hayo imesaidia kwa kiasi kikubwa si tu kuuawa kwa mtuhumiwa nambari moja, Osama bin Laden, bali pia imesaidia kuepusha mashambulizi mengine.
Kwa hapa Uingereza, matukio ya vurugu za mwezi Agosti mwaka jana yaliyoanzia kitongoji cha Tottenham, jijini London, na kusambaa maeneo kadhaa yalisababisha taasisi na watu mbalimbali kuhangaika kusaka chanzo cha matukio hayo, zoezi ambalo hadi sasa linaendelea.
Na kutokana na umuhimu wa jiji la London-na Uingereza kwa ujumla-kwa dunia, vurugu hizo zilivuta hisia hadi nje ya mipaka ya nchi hii. Ripoti kuhusu vurugu hizo zilikamata vichwa vya habari kuanzia Zimbabwe hadi India, Amerika ya Kaskazini hadi Kusini, na kwingineko.
Lakini binafsi niliguswa zaidi na maelezo ya gazeti la mrengo wa kushoto la Ujerumani la Berliner Zeitung ambalo lilihitimisha ifuatavyo kuhusu vurugu hizo (ninanukuu)
The country has lost faith in every authority: the banks, politicians, the media, the police. The corruption has reached even the smallest unit - the family. There is a generation growing up without values of any kind.” (Tafsiri isiyo rasmi: nchi imepoteza imani kwa kila mamlaka: benki, wanasiasa, vyombo vya habari, polisi. Rushwa imetamalaki hadi kwenye eneo dogo la chini kabisa, yaani familia. Kuna kizazi kinachokua kisichokuzwa katika maadili ya aina yoyote ile)
Gazeti hilo likaendelea kueleza (ninanukuu tena) “In the economic crisis the financial establishment declared bankruptcy, and British politicians became mired in the expenses scandal of 2009. Then this year the media and politicians have been damaged by the Murdoch scandal...When the country's elites don't take the law seriously, why should we? No question is more dangerous for a society.” (Tafsiri isiyo rasmi: katika mtikisiko wa kiuchumi, taasisi za fedha ziliishia kutangaza kuwa zimefilisika, na wanasiasa wa Uingereza wakakumbwa na skandali ya posho mwaka 2009. Kisha, mwaka huu kashfa ya Murdoch imeathiri sana taswira ya vyombo vya habari na wanasiasa...Sasa kama wasomi wa nchi wanapuuza sheria, kwanini sie tuijali? Hakuna swali la hatari kwa jamii kama hili.”
Nukuu hizo mbili kuhusu vurugu za London zinaweza kabisa kutumika kuelezea mwenendo wa baadhi ya mambo huko nyumbani kwa sasa. Kimsingi, mwananchi wa kawaida anakumbana na matarajio makubwa kutoka kwa watawala wetu lakini licha ya Watanzania wengi kukidhi matarajio hayo ya tabaka tawala, wameendelea kushuhudia watawala na mamlaka za utawala zikishindwa kwa makusudi kuthamini matarajio na mahitaji ya wananchi.
Moja ya taasisi za utawala ambazo zimekuwa zikiwaangusha ambayo imekuwa ‘ikiwaangusha’ sana Watanzania ni Bunge, tunaloambiwa ni tukufu. Katika siku za hivi karibuni, Bunge letu limekuwa likifanya kila jitihada kujivunjia heshima na imani kubwa waliyonayo wananchi kwa taasisi hiyo.
Kimsingi, Bunge letu limegeuka zaidi ya kituko. Lakini baya zaidi, taasisi hiyo ya kutunga sheria imegeuka pia kuwa ‘utani mbaya’ (a bad joke), ambapo watu wanaotubebesha mzigo mkubwa kumudu maslahi yao ambayo kwa mwananchi wa kawaida ni ya kufikirika tu wameamua kuigeuza taasisi hiyo kuwa uwanja wa mipasho, vijembe, matusi na tabia nyingine unazoweza kuzikuta maeneo ya vijiweni tu.
Lakini tukirudi nyuma, Bunge ‘liliharibiwa’ tangu zamani, na tunachoshuhudia sasa ni mwendelezo tu wa uharibifu huo. Tukiangalia Bunge la mfumo wa chama kimoja tunabaini kuwa lilikuwa mkusanyiko wa watu waliopaswa kuwa na fikra za aina moja, kupitisha kila kinacholetwa na serikali ya chama kimoja kilichoshika hatamu, na mawazo yoyote yaliyokinzana na mtizamo wa watawala yalichukuliwa vibaya, lakini walau wakati huo zilikuwapo pia sauti zilizokuwa zikisema ukweli kwa jinsi ulivyokuwa.
Hatimaye tukapata Bunge la vyama vingi chini ya Spika Pius Msekwa. Kimsingi, Bunge hili liliendelea kuwa mithili ya lile la mfumo wa chama kimoja kwani wabunge wachache wa upinzani hawakupewa fursa yoyote ya maana kuipa changamoto serikali, na Bunge likaendelea kuwa kibaraka wa serikali kwa kutumia wingi wa wabunge wa chama tawala.
Lakini kama awamu zilizotangulia zilikuwa mbaya, basi zilizofuatia zilikuwa zaidi ya mbaya. Bunge lililokuwa chini ya Uspika wa Mheshimiwa Samuel Sitta lilizaa kile kinachofahamika sasa kama siasa za majitaka. Nisingependa kuingia kwa undani ni jinsi gani Sitta alifanikiwa kupata uspika lakini ninachoweza kusema pasi uoga ni kuwa Bunge hilo lililogubikwa na migongano lukuki ya kimaslahi, lilifanikiwa kupigia mstari hoja kuwa ni rahisi sana kuwaghilibu Watanzania.
Lakini ukidhani ‘Bunge la Sitta’ lilikuwa hivyo lilivyokuwa, na kama unakumbuka kituko kikubwa zaidi (tuhuma za ushirikina bungeni?) basi subiri tulichambue kidogo ‘Bunge la sasa la Spika Anne Makinda.’ Pengine hili litamkera Spika Makinda lakini moja ya maelezo mepesi ya utawala wake ni kuwa anaiendesha taasisi hiyo kidikteta ‘kupita maelezo.’
Kuna hoja moja ya kisiasa inayodai kuwa kuna nyakati udikteta ni muhimu. Kwamba kuna udikteta wa aina mbili: kwa ajili ya watu na dhidi ya watu. Udikteta mbaya ni huo wa aina ya pili (dhidi ya watu) kwani ni kwa ajili ya maslahi ya wachache. Lakini udikteta kwa ajili ya watu unaweza kuwa muhimu na lazima hususan pale maslahi ya wengi yanapoelekea kusipofaa.
Spika Makinda amekuwa ‘mungu-mtu’ wa Bunge letu, akitumia kila aina ya ubabe dhidi ya wabunge wa vyama vya upinzani, akiwatimua nje ya Bunge kadri apendavyo huku akiwaacha watu kama Mwigulu Nchemba kuigeuza taasisi hiyo kuwa mithili ya kituo cha mafunzo ya vijembe, mipasho, matusi na upuuzi mwingine.
Lakini tatizo si Makinda tu bali hata kiti cha Uspika. Yayumkinika kuhitimisha kuwa kiti hicho ni kama ‘kimerogwa’ kwani kila anayekikalia anajisikia mwenye nguvu zisizomithilika na kama ni lazima awathibitishie wabunge wa vyama vya upinzani kuwa wao ni sawa na kile Waingereza wanakiita ‘evil necessity’ (yaani jambo la kishetani ambalo inabidi liendelee kuwapo kwa vile tu ni muhimu, angalau kwa mujibu wa taratibu za kimaandishi na si kivitendo).
Kabla sijaandaa makala hii nimesoma habari katika gazeti moja inayomnukuu Waziri wa Makazi, Prof Anna Tibaijuka, akitoa wito kwa Watanzania kuwaombea viongozi wa ngazi zote wakiwamo wabunge ili wapate hekima na busara kutoka kwa Mungu.
Japo wazo la Waziri Tibaijuka lina maana laini sidhani kama Watanzania ambao tayari wanabebeshwa mzigo kumudu maslahi ya viongozi kama wabunge wapo tayari kujitwika ‘gunia jingine la misumari’ kufanyamaombi kwa ajili ya watu walioko bungeni kuendekeza mipasho na vijembe badala ya kuzungumzia kero za wananchi.’
Tuwaombee ili wapate busara za kusaka vina (verses) kali zaidi za mipasho yao ya kila siku? Tuwaombee ili waendelee kupigania kuboreshewa maslahi yao ambayo hayaendani kabisa na hali halisi ya uchumi wetu? Ninaamini kabisa kuwa hakuna Mtanzania mwenye ‘muda mchafu’ wa kuwaombea watu hawa. Wajiombee wenyewe ili wapatwe na akili ya kutambua kuwa ‘utoto’ wa vijembe, kashfa na matusi si tu unaisukuma taasisi hiyo kwenye lindi la ukosefu maadili bali pia unaweza kuzua mjadala kama kuna umuhimu wa kuwaita watu hawa waheshimiwa ilhali baadhi yao wana kauli chafu zaidi ya zile za vijiweni. Kwanini tuwe na waheshimiwa wasiojiheshimu?
Nimalizie makala hii kwa kukumbushia nukuu ya Berliner Zeitung kuwa kama ‘waheshimiwa’ hawajali sheria na taratibu kwanini basi wananchi waone umuhimu wa kuzijali? Kwa bahati mbaya, kufanya hivyo ni kukaribisha uvunjifu wa amani zaidi ya huo uliojiri hapa Uingereza mwaka jana.
Nihitimishe kwa kutoa wito kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa marekebisho tarajiwa ya Katiba yetu kuangalia uwezekano wa wapigakura kuwadhibiti wabunge ‘wasio na heshima’ kutokana na kauli au/na vitendo vyao, sambamba na kutengeneza mazingira ya kudhibiti udikteta wa Spika na/au kiti cha uspika.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.