Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu,makala yangu katika jarida la Raia Mwema toleo la Jumatano iliyopita (Agosti 8, 2012) haikuwekwa mtandaoni japo ipo gazetini.Kwa faida ya wasomaji,nimelazimika kuiweka hapa (inaweza kuwa na tofauti chache na iliyopo gazetini ambayo imehaririwa)
MAKALA
YA RAIA MWEMA TOLEO LA AGOSTI 8
Kwa zaidi ya wiki
moja sasa kumekuwepo habari zisizopendeza kuhusiana na tatizo la muda mrefu la
mpaka kati ya Tanzania na Malawi.
Ningependa kukiri
hadharani kwamba pamoja na kiu yangu kubwa ya ufahamu wa masuala mbalimbali
sikuwahi kujibidiisha kufuatilia kwa undani chanzo cha tatizo hilo. Na pengine
kuliita suala hilo ‘tatizo’ ni kulipunguzia uzito kwani ukichambua kwa makini
kauli mbalimbali kutoka kwa baadhi ya viongozi wetu na wenzao wa Malawi, kinachoendelea
hivi sasa kinaweza kabisa kuitwa ‘mgogoro wa mpaka kati yetu na Malawi.’
Katika baadhi ya
mitandao ya jamii, ambayo baadhi yetu inatusaidia sana kufuatilia mambo
mbalimbali huko nyumbani kumeanza kujitokeza hofu ya vita kati ya nchi hizi
ambazo licha ya ujirani zina ukaribu mkubwa kwa sababu ya mwingiliano wa
makabila.
Hata hivyo, wakati
hofu hiyo ya vita kati yetu na Malawi ikianza kukua, kuna mambo kadhaa
yanayopaswa kujadiliwa kwa uwazi. Lakini pia ningependa kuweka wazi msimamo
wangu kuwa ninaamini ufumbuzi pekee na wenye manufaa katika mgogoro huu ni kwa
njia za amani.
Na moja ya sababu
kubwa ya kutaka mgogoro huu utatuliwe kwa njia za amani ni kumbukumbu
niliyonayo ya vita pekee nilivyowahi kushuhudia katika uhai wangu hadi sasa.
Bado nina kumbukumbu nzuri ya vita ya Kagera kati yetu na Uganda, ambapo wakati
huo nilikuwa mtoto mdogo ninayeishi na wazazi mkoani Kigoma.
Moja ya kumbukumbu
zinazoniogofya hadi leo ni pale wakazi wa mji huo walipotakiwa kuchimba
mahandaki kama hatua ya kujilinda. Kulikuwa na taarifa kwamba ‘swahiba’ wa
nduli Idi Amin wa Uganda, aliyekuwa Rais wa ‘Zaire’ (sasa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Congo-DRC) dikteta Mobutu, alikuwa na mpango wa
kumsaidia Amin kushambulia Kigoma hasa kwa vile mkoa huo unapakana na DRC.
Ninakumbuka hofu
tuliyokuwa nayo kila tuliposikia mlio wa ndege angani, tukidhani ni ndege za
Mobutu zimekuja kutuangamiza. Bahati nzuri hadi vita hiyo inamalizika hakukuwa
na shambulio lolote kwa mji huo.
Kwa kuzingatia
kumbukumbu hizo, nisingependa kuona Watanzania wenzangu wakirejea kwenye hofu
kama hiyo iliyotukumba sie wakati wa vita hiyo kati yetu na Uganda.
Lakini kuna jambo
jingine linalonipa hofu zaidi. Katika moja ya shahada zangu za Uzamili nimesoma
Stadi za Vita (War Studies), na
katika kozi hiyo tulitumia muda mwingi mwanafilosofia mahiri wa masuala ya vita,
Mchina Sun Tzu. Moja ya mambo yanayousiwa na Sun Tzu kuhusu maandalizi ya vita
ni hili
“Sanaa ya vita inatufundisha sio kutarajia kuwa
adui hatotuvamia bali maandalizi yetu katika kukabiliana nae, na sio katika
uwezekano kuwa (adui) hatoweza kutuvamia bali uimara wa nafasi yetu
‘kutohujumika’ (unassailable).”
Licha ya sote kuwa
na mapenzi kwa nchi yetu, tukiangalia mwenendo wa mambo huko nyumbani kwa sasa,
jambo tusilotaka kabisa kusikia kwa sasa ni vita. Mmoja wa ukweli mchungu ni
kwamba hadi sasa tumeshindwa kukabiliana na maadui kadhaa wa ndani ambao hawana
silaha bali fedha na porojo zao. Hapa ninawazungumzia mafisadi na maharamia
wengine wanaoifanya Tanzania yetu kuwa katika umasikini tusiostahili.
Lakini pia uimara
wetu kukabiliana n adui si wenye kutoa matumaini. Katika siku za karibuni
tumeshuhudia migomo ya madaktari na baadaye walimu, wote wakidai kuboreshewa
maslahi yao. Wakati watawala wetu wanadai serikali haina fedha za kuboresha
maslahi ya watumishi wake, imemudu kupandisha mishahara ya wabunge hadi kufikia
shilingi milioni 11 kwa kila mmoja wao.
Je inawezekana
chokochoko kutoka Malawi zinachangiwa na uelewa wa nini kinachoendelea nchini mwetu?
Lakini hata kama hiyo si sababu, je katika mazingira haya ya kuendekeza anasa
kwa tabaka dogo huku wengi wa wananchi wakizidi ‘kupigika’ kutokana na uchumi
dhaifu unaozidi kudhoofeshwa na majambazi wanaopora raslimali zetu kila
kukicha, tunaweza kweli kukabiliana na adui huku tukiwa na uhakika wa
kumshinda?
Ninatambua kuwa
ninaweza kuonekana msaliti kwa nchi yangu kwa kubainisha hoja hizo hapo juu
lakini kama nilivyotanabaisha hapo awali, ningependa, na ninataraji, mgogoro
huu utamalizwa kwa njia za amani.
Nimeeleza hapo
mwanzo kuwa sikuwahi kujishughulisha kufuatilia chanzo cha mgogoro ‘wa muda
mrefu’ wa mpaka kati yetu na Malawi. Lakini jitihada kidogo tu ziliniwezesha
kukutana na makala ya kitaaluma, ambayo licha ya kuwa ilichapishwa mwezi
Disemba mwaka 1973, bado ina maelezo muhimu kuhusu mgogoro huo.
Katika makala hiyo, The
Malawi-Tanzania Boundary Dispute (mgogoro wa mpaka
wa Malawi na Tanzania) iliyoandikwa na James Mayall, na ambayo ni mapitio ya
kitabu (book review) kuna taarifa
ambazo kwa namna flani zinatoa taswira ya ‘msimamo wa kukanganya’ kwa baadhi ya
viongozi wetu, ikiwa ni pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Kwa mujibu wa makala
hiyo, awali viongozi wetu wakiongozwa na Nyerere waliridhia kuwa Ziwa si letu
bali la Malawi. Kwa kiasi kikubwa msimamo huo ulionekana kuchagizwa na dhamira
ya nchi yetu katika umoja wa nchi za Afrika.
Japo sitaki
kuchukulia makala hiyo kama ukweli halisi kuhusu chanzo cha mgogoro huo,
mwandishi alijitahidi kwa kiasi kikubwa kubainisha jinsi suala hilo
lilivyochukuliwa kuwa la kiutawala zaidi kuliko la kisheria.
Inavyoelekea, kwa
mujibu wa Mayall, moja ya sababu zilizopelekea nchi yetu kubadili msimamo wake
wa awali kuwa Ziwa hilo si letu ni uhusiano wa karibu kati ya aliyekuwa Rais wa
Malawi, dikteta Kamuzu Banda na utawala wa makaburu. Kama ambavyo inaelezwa
kuwa moja ya vipaumbele vilivyopelekea Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar
ni sababu za kiusalama, umuhimu wa sehemu ya Ziwa hilo kumilikiwa nasi
unaelekea kuchangiwa na sababu kama hizo.
Kadhalika, makala
hiyo inajenga picha moja ambayo yayumkinika kuhisi kuwa inaweza kurandana na
sababu za sasa za kurejea kwa mgogoro huo. Mwandishi Mayall alieleza kuwa
katika wakati flani huko nyuma kulikuwa na hisia kwamba hoja ya Malawi kumiliki
Ziwa lote ilihamasishwa na utawala wa Makaburu (waliokuwa wakitawala baadhi ya
nchi za kusini kabisa mwa Afrika) na Wareno (waliokuwa wakitawala Msumbiji).
Kisichopendeza kwa
Mtanzania yeyote kuhusu makala hiyo ni ukweli kwamba msimamo wa awali wa nchi
yetu ulikuwa ni pamoja na kuwaachia Wamalawi waamue wenyewe ‘kutuachia’ sehemu
ya Ziwa Nyasa na pia kauli mbalimbali zilizoonyesha kuafiki kuwa Ziwa hilo si
sehemu ya nchi yetu, japo baadaye msimamo huo ulibadilika.
Ningependa
sana kuitafsiri makala hiyo nzima kwa Kiswahili lakini nafasi hairuhusu, na
pengine kufanya hivyo kunaweza kuwavunja moyo baadhi ya Watanzania wenzangu na
pengine kuanza kuamini kuwa sie ndio chanzo cha chokochoko zilizopelekea
mgogoro huo kufikia hatua ya sasa. Hata hivyo, iwapo kuna msomaji atahitaji
nimsaidie kutafsiri makala hiyo ya Kiingereza, nipo tayari kufanya hivyo.
Wakati ninajipa
matumaini kuwa mgogoro huo utamalizwa kwa amani, ninajikuta nikikabiliana na
maswali kadhaa ambayo ninachelea hata kudadisi majibu yake. Kwa mfano,
itakuwaje iwapo Malawi watapuuza onyo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje
Bernard Membe kuwa makampuni yanayojihusisha na uchimbaji raslimali katika Ziwa
hilo yasitishe kazi mara moja?
Wakati viongozi
kadhaa huko Malawi wametoa kauli za kuleta matumaini kuwa kilichopo si mgogoro
kwa vile nchi zetu zipo katika mahusiano mazuri, takriban wote wanaonekana kuwa
na msimamo unaorandana kwamba Ziwa Nyasa lote ni la nchi hiyo.
Hapo huhitaji uelewa
wa mambo ya diplomasia kuhitimisha kuwa kinachoongelewa na viongozi hao ni
kupunguza tu hofu kwa wananchi lakini pasipo kurudi nyuma katika msimamo kuwa Ziwa
hilo ni lao lote na hawapo tayari kuliachia.
Lakini kuna swali
jingine la msingi zaidi. Je jeuri ya Malawi inatoka wapi? Je inachangiwa na
makampuni yanayochimba raslimali katika Ziwa hilo? Je inachangiwa na uelewa
kuwa nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na ‘mizigo mikubwa’ kiasi cha kuiaminisha
nchi hiyo kuwa hatuna uwezo wa kuwakabili? Na swali ambalo pengine ni gumu
zaidi, je tuna uwezo wa kurejea ‘tulichomfundisha Nduli Idi Amin mwaka 1978-79?
Ili uingie vitani ni
lazima uwe na taarifa sahihi dhidi ya adui yako. Je taasisi zetu zinazoonekana
kama zimesalimu amri kwa mafisadi wanaotafuna nchi yetu zina uwezo wa kukusanya
taarifa muhimu za kiusalama ili pindi tukiamua ‘liwalo na liwe’ dhidi ya Malawi
tusiishie kujilaumu?
Vyovyote
itakavyokuwa (huku tukiamini kuwa hakutokuwa na haja ya matumizi ya nguvu
kutatua mgogoro huo) suala moja muhimu ni kuutumia mgogoro huu kama fursa ya
kusaka suluhisho la kudumu.Kama ambavyo matatizo ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar unavyoendelea kuzalisha matatizo hususan kutokana na kukosekana utashi
wa kisiasa kumaliza matatizo yaliyopo, mgogoro huu kati yetu na Malawi ambao
umedumu kwa takriban nusu karne sasa unahitaji kumalizwa. Lakini ili hilo
liwezekane ni muhimu kwa watawala wetu kuelewa vipaumbele vya taifa letu.
Na kwa vile katika
mazingira tuliyonayo tunalazimika kuwa kitu kimoja (na kuweka kando ukweli kuwa
baadhi ya wenzetu wameigeuza nchi yetu kuwa kitegauchumi chao) na tunalazimika
pia kuwaamini watu walewale ambao ‘wanadai hawajui chanzo cha umasikini wetu’,
basi ni muhimu Tuweke kando tofauti zetu na tuwe tayari kulinda na kutetea kile
tunachoamini ni halali yetu.
Nimalizie kwa kutoa
wito kuwa suala hili nyeti lisigeuzwe turufu ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi
wa mwaka 2015.Tusiruhusu wababaishaji wakurupuke na kauli za kusaka umaarufu
pasipo kuwa na mikakati ya namna ya kutatua mgogoro huu kwa njia za amani.
Kwa jirani zetu wa
Malawi na hususan Rais Banda, wito wangu kwao ni huu: amani ni muhimu kwetu
sote, lakini wakati mwingine inalazimu kutumia mabavu ili kuleta amani ya
kudumu. Pamoja na matatizo yetu, mie na pengine kila Mtanzania anaamini kuwa kamwe
hatutoruhusu Ziwa Nyasa ligeuzwe ‘uwanja wa kutupima ubavu.’ Tulimsambaratisha
Nduli Amin kwa sababu nia tulikuwa nayo, sababu tulikuwa nazo, na uwezo pia
tulikuwa nao. Hata kama itaonekana kwa Wamalawi kuwa nia, sababu na uwezo wetu
ni hafifu kwa sasa, hakuna Mtanzania aliye tayari kuona ardhi ya nchi yake
ikimegwa au mipaka yetu ikichezewa.
Mwanafalsafa Sun Tzu
anaonya; “gharama ya vita ni kubwa kuliko
ushindi wowote utakaopatikana” na “wanaoingia
vitani hufanya hivyo wakiongozwa na ‘miscalculations’ hasa imani kuwa
watashinda...lakini vita ikimalizika hujikuta wana hasara kubwa kuliko kabla
hawajaingia vitani.”
Mungu Ibariki
Afrika
0 comments:
Post a Comment