27 Sept 2012NINAAMINI takriban kila msomaji wa magazeti ameshawahi kukumbana na sentensi hii inayokera ya “jina linahifadhiwa kwa sasa.”
Kinachokera si tu kuhifadhiwa kwa jina la mhusika mkuu katika habari bali ukweli kwamba mara nyingi habari husika hugeuka kuwa mithili ya mtihani uliojaa mafumbo, na pasipo msomaji “kujumlisha 2 na 2 kupata 4” hakuna uwezekano wa habari hiyo kuleta maana yoyote.
Mifano ni mingi lakini mfano mwafaka ni katika habari ambayo nitaizungumzia pia kwenye makala hii. Kwa siku kadhaa, magazeti mbalimbali yalikuwa yakiripoti taarifa kuhusu mke wa kigogo wa Jeshi la Polisi, ambapo utambulisho wa kigogo huyo na mkewe umebaki kuwa “umehifadhiwa,” akihusishwa na utapeli wa mamilioni ya shilingi kwa ahadi ya kuwapatia watu ajira kwenye vyombo vya dola.
Kabla ya kujadili tukio hilo la utapeli wa aina yake, tuendelee na mjadala wa tabia inayozidi kuota mizizi kwenye magazeti yetu ya “jina limehifadhiwa.” Japo uelewa wangu wa sheria ya kumkashifu mtu/taasisi (Defamation Law) ni wa wastani, siku zote kama mwandishi wa blogu na makala nimekuwa makini kuhakikisha kuwa ninapotaja jina la mtu au taasisi kwenye habari husika, nina uhakika na ushahidi ninao.
Kwa msingi huo, sioni haja ya kutumia sentensi “jina linahifadhiwa kwa sasa” (na mara nyingi hiyo ‘sasa’ hugeuka kuwa ‘milele’) kwa sababu iwapo mtajwa katika andiko husika ataamua kunipeleka mahakamani kwa madai ya kumkashifu, nitapambana naye vilivyo.
Nadhani sababu kubwa ya waandishi wetu kusaka hifadhi ya “jina linahifadhiwa kwa sasa” kwenye kuficha majina ya wahusika katika maandiko yao ni uoga wa kuburuzwa mahakamani kwa madai ya kashfa dhidi ya mtajwa. Na sababu pekee inavyoweza kusababisha uoga huo ni ukosefu wa facts au ushahidi kamili.
Ni wazi kwamba sheria ipo upande wa mwandishi pindi anapoandika habari ambayo imejitosheleza, kwa maana ya kuwa na ushahidi usiopingika kuhusu mtajwa katika habari husika.
Kimsingi, taaluma ya uandishi wa habari inashabihiana kwa kiasi kikubwa na ushushushu katika namna habari inayotafutwa. Katika taaluma zote lengo ni kupata habari kwa minajili ya kuziwasilisha sehemu fulani: kwa msomaji kwa upande wa wanahabari, na kwa mwajiri kwa upande wa mashushushu.
Tofauti za msingi katika utafutaji na matumizi ya habari ni kwamba wakati mara nyingi wanahabari wanapaswa kuwa ‘wazi’ wanaposaka habari (kupata habari kwa udanganyifu kunaweza kuwa kosa la jinai), takriban mara zote mashushushu husaka habari kwa kificho (na kwa mujibu wa sheria, shushushu kujiweka wazi-au kujiumbua-ni kosa).
Kwa upande wa matumizi ya habari zilizopatikana, wanahabari wanatarajiwa kuziwasilisha kwa msomaji (tukiweka kando taratibu za kiuhariri ndani ya chombo habari husika) ilhali kwa mashushushu habari, ambayo wakati huo hugeuka kuwa taarifa, huwasilishwa kwa chombo husika kwa hatua nyinginezo.
Kwa hiyo, tofauti ya kimsingi ya mwanahabari na shushushu ipo zaidi kwenye ‘habari’ na ‘taarifa.’ Wakati habari ni kitu cha wazi na kwa ajili ya matumizi ya umma, taarifa ni kitu cha siri na ni kwa ajili ya matumizi ya taasisi ya kishushushu tu.
Sasa tunachoshuhudia katika uandishi wetu wa “jina limehifadhiwa kwa sasa” ni mithili ya ‘mchanyato wa habari na taarifa,’ kwa maana ya ‘kuwasilisha habari nusu kama mwanahabari lakini pia nusu kama shushushu - nusu wazi nusu siri.’
Ni adhabu kubwa kwa msomaji anapokutana na habari iliyoandikwa kwa mfumo huu “kigogo mmoja (jina linahifadhiwa) wa taasisi moja (jina linahifadhiwa) anadaiwa kulimbikiza fedha zilizopatikana kifisadi katika nchi moja (jina linahifadhiwa).” Kimsingi, habari hii haina umuhimu zaidi ya kuuza gazeti husika na kusumbua ubongo wa msomaji.
Kwa nini mwandishi husika asihakikishe anapata facts zote kuhusu mhusika katika habari hiyo kabla ya kukurupuka kuiripoti nusu nusu? Ninatambua kuwa baadhi ya wanahabari wanaweza kujitetea kuwa wanafanya hivyo kwa minajili ya ‘kumshtua mhusika’ kwamba matendo yake yanafahamika lakini kimsingi hilo si jukumu la chombo cha habari. Kama kuna maovu yasiyoandikika gazetini basi yawasilishwe kwa taasisi za dola badala ya kuwachosa wasomaji na ‘habari za kificho.’
Turejee kwenye sakata la utapeli unaodaiwa kufanywa na mke wa kigogo wa polisi ambao kwa pamoja “majina yao yameendelea kuhifadhiwa” na vyombo vya habari vilivyokuwa vinaripoti habari hiyo.
Awali iliripotiwa kuwa mke wa kigogo huyo alijipatia mamilioni ya shilingi kwa ahadi ya kuwapatia ajira vijana 120 kwenye Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU).
Habari zaidi zilizeleza kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa likimlinda mke huyo wa kigogo (na hii si ajabu kwani yeyote anayefahamu utendaji kazi wa vyombo vyetu vya dola anatambua kuwa viongozi wake na watu wanaowahusu ni miungu-watu wasiopaswa kusumbuliwa kwa aina yoyote ile).
Kwa mantiki hiyo, Polisi kumlinda mke wa kigogo wa jeshi hilo ni jambo la kutarajiwa japo si sahihi.
Baadaye ikaripotiwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa Othman Rashid amelitaka Jeshi la Polisi kumkamata na kumchukulia hatua mwanamke huyo. Katika hatua ya nadra mno, Othman alisema (ninanukuu) “Nimewasiliana na IGP (Said) Mwema ili aweze kunipa ufafanuzi kuhusu mke wa kigogo huyo, lakini nashukuru amenipa ushirikiano na kuniambia kuwa suala hilo wanalishughulikia kisheria zaidi. Watanipa taarifa pindi watakapokuwa wamekamilisha.”
Lakini katika kile unachoweza kudhani ni tamthiliya isiyopendeza machoni, habari hiyo ikageuka sarakasi na kugeuka kuwa (ninanukuu) “Wakazi wawili wa jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na makosa 12 ya kujipatia sh milioni 102 kwa njia ya udanganyifu wa kuwatafutia vijana kazi katika Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi.”
Miongoni mwa wanaotajwa ‘kutapeliwa’ ni mke wa Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja, aliyatajwa kwa jina moja tu la Happyphania, ambaye inadaiwa alitapeliwa shilingi milioni 5 “kwa madai kuwa ni malipo ya maombi ya usajili wa mafunzo ya POLISI (herufi kubwa kwa sababu maalumu), TAKUKURU na Idara ya Usalama wa Taifa.
Swali la kwanza, hivi kweli inaingia mke wa Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi atoe fedha kwa ‘matapeli’ ili kumpatia nafasi ya usajili wa mafunzo ya Jeshi la Polisi ambako mumewe si tu ni mmoja wa vigogo wa ngazi za juu bali pia ndiye mwenye dhamana ya MAFUNZO kwa wanaojiunga na jeshi hilo?
Swali la pili, tukiamini kuwa watu hao wawili waliokamatwa na kufungulia mashtaka (wote si wanawake), kwanini basi Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa alimtaka IGP kushughulikia suala la “mke wa kigogo wa polisi”? Hivi kweli inaingia akilini “mke wa kigogo wa polisi” awe “hao washtakiwa wawili wa kiume”?
Maswali ni mengi, ikiwa ni pamoja na kitendo cha mke wa Kamanda Chagonja kutoa fedha kwa matapeli hao. Pasi kuuma maneno, hivi kutoa fedha kwa ajili ya kupata huduma inayotolewa bure si rushwa? Kwanini basi waliopokea fedha hizo washtakiwe lakini waliotoa fedha wasishtakiwe kwa kutoa rushwa?
Ninatambua uwezekano wa utetezi wa “waliotoa fedha hizo ni victims (majeruhi) wa utapeli.” Hiyo inaweza kuwa kweli tu kwa watu wasiofahamu utaratibu wa kujiunga na taasisi hizo. Sitaki kabisa kuamini kuwa mke wa Kamishna Chagonja hafahamu utaratibu huo hadi kushawishika kutoa fedha kwa washtakiwe hao.
Katika moja ya habari inayomnukuu kigogo wa polisi ambaye kama kawaida jina lake lilihifadhiwa, alisema “…Hata mke wangu ni mmoja wa waliotapeliwa. Alikusudia kuwapeleka wanafamilia watatu akiwemo mtoto wake, mke wa kaka yake na wifi yake ambaye tunamlea.” Mke wa kigogo wa polisi anatapeliwa kuingiza nduguze kwenye jeshi hilohilo analofanya kazi muwewe? Huu ni utani mbaya kabisa.
Kama ilivyo desturi, habari hiyo ndio imeishiwa hapo. Magazeti yaliyokuwa yakiripoti kuhusu mke (jina limehifadhiwa) wa kigogo wa polisi (jina limehifadhiwa) yamemaliza kazi yao na kumwachia kazi msomaji kujumlisha 2 na 2 apate 4.
Na tabia hii ya kukera ya “jina limehifadhiwa” inachangia kuonyesha ubaguzi wa wazi wa kimatabaka. Sijawahi kuona sentensi ya “jina linahifadhiwa” ikitumika kwa tuhuma zinazowahusu walalahoi bali ni kwa vigogo pekee.Ni kwa vile uwezekano wa walalahoi hao kwenda mahakamani kudai wamekashifiwa na gazeti husika ni mdogo au ni kupuuza tu haki zao za kibinadamu?
Mwisho, wakati nina uhakika kuwa majina ya kigogo wa polisi na mkewe anayedaiwa kutapeli yataendelea kuhifadhiwa ‘milele’ (habari yenyewe ni kama imeshakufa kifo cha asili), harakati za kupigania uhuru wa vyombo vya habari hazitozaa matokeo tarajiwa kama vyombo vya habari vitaendeleza kasumba ya “jina linahifadhiwa” ambayo inainyima jamii uhuru wa kuelewa habari husika.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.