8 Oct 2012NIMEKUWA nikiulizwa swali hili takriban kila wiki baada ya makala zangu kuchapishwa katika jarida hili maridhawa: Hivi kuna wakati unaishiwa na cha kuandika? Na siku zote jibu langu linakuwa lile lile; Tanzania yetu haiishiwi mambo yanayopaswa kujadiliwa-iwe gazetini, mtandaoni, kijiweni au popote pale. Kuweka rekodi sawia, kila ninapoingia mtandaoni huwa ninakumbana na wastani wa angalau habari tano zinazoweza kutengeneza mada za makala zangu.
Wiki hii nitazungumzia matukio mawili makubwa yanayoihusu CCM na CHADEMA. Kwa namna moja au nyingine, matukio yote mawili yanahusiana, na nitajitahidi kuonyesha uhusiano wao mwishoni mwa makala haya.
Tukio la kwanza ni kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwamba CCM haitokufa, na pengine wanaodhani hivyo wanaweza kufa wao kabla ya chama hicho tawala kufa.
Kwa baadhi yetu tunaosoma siasa kama eneo la taaluma, tunatambua ukweli mmoja, kwamba chama cha siasa kinazaliwa, kinakua, na kama ilivyo kwa binadamu, kinaweza kufa. Na tofauti na binadamu ambao hatuna udhibiti mkubwa wa kurefusha au kufupisha maisha yetu (kuna watenda dhambi na wanaotumia kila aina ya ‘sumu’-pombe, dawa za kulevya na kadhalika ama kumkera Muumba au kuharibu afya zao-lakini si tu wapo hai bali pia wana afya za kuridhisha, huku wengine mambo yao yakizidi kuwanyookea, huku upande mwingine kukiwa na wacha Mungu, wanaojali afya zao lakini wanataabika muda huu); Vyama vya siasa vinaweza kurefusha maisha yao kwa kuitumikia jamii kulingana na matarajio ya jamii husika au ikaipuuza jamii hiyo na kujichimbia kaburi.
Pamoja na heshima yangu kubwa kwa Rais Kikwete, ninaomba kutofautiana naye katika kauli hiyo kuwa CCM haitokufa. Si tu kuwa vyama vya siasa hufa, bali pia ninaamini kuwa kila Mtanzania anayefuatilia kwa karibu historia na mwenendo wa chama hicho anaweza kabisa kubashiri kuwa ama mwanzo wa mwisho wake unakaribia au kinaharakisha kifo chake.
Simlaumu Rais Kikwete kwa kauli hiyo kwa sababu kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chama anachoongoza ana jukumu kubwa la kuwahakikishia viongozi na wanachama wenzake kuwa ‘mambo si mabaya’ kama inavyoelezwa na wapinzani wao.
Binafsi, nasema kinachoweza kuiua CCM kabla ya wakati wake, ni pamoja na mtizamo huo wa Rais Kikwete wa kwamba ‘chama hicho kipo imara na kinaendelea kupendwa na Watanzania wengi-uthibitisho (kwa mujibu wao) ni idadi ya wana-CCM waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwenye chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho.
Ni kweli kwamba idadi ya waliojitokeza kugombea inaweza kujenga picha kuwa CCM bado kinapendwa na wengi. Lakini haihitaji ufahamu mkubwa wa siasa zetu kumaizi kuwa baadhi ya wanaokimbilia uongozi ndani ya chama hicho wana ajenda zao binafsi. Ikumbukwe kuwa huko nyuma chama hiki kilishaonyesha dhamira ya kutenganisha biashara na siasa, hatua iliyotafsiriwa na wengi kuwa ni kutambua kuwa kuna kundi la wafanyabiashara wanaokimbilia kwenye siasa si kwa minajili ya kuutumikia umma, bali kusaka ‘kinga’ ya kuwalinda katika biashara zao.
Binafsi, nilikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa wazo hilo, si tu kwa sababu siafikiani na aina yoyote ya ubaguzi, bali pia sikuona kuwa tatizo ni wafanyabiashara kujihusisha na siasa bali wafanyabiashara ‘wachafu’ kuruhusiwa kujihusisha na siasa. Kwa kuharamisha biashara kwenye siasa kungeweza kuwa na hatari ya kuwakwaza wazalendo wazuri tu ambao walichagua kujihusisha na biashara kabla ya kuingia kwenye siasa.
Na ingekuwa ubaguzi wa wazi kuwazuia wafanyabiashara kujihusisha na siasa, lakini kuwaruhusu askari wastaafu, wasomi na wanajamii wengineo kufanya hivyo. Sawa, wanasema samaki mmoja akioza basi wote wameoza, lakini usemi huu hauzingatii ukweli kwamba binadamu hutofautiana.
Kwa mfano, kwa vile Mndamba wa kwanza kumfahamu ni mie ambaye pengine ninakukera na kwa mtizamo wangu haimaanishi kuwa kila Mndamba utakayekutana nae maishani atakukera. Waingereza wana msemo kuwa “people vary because we differ” yaani watu huwa na tofauti kwa sababu wanatofautiana, na kwa mantiki hiyo hiyo, mfanyabiashara anayeingia kwenye siasa kwa minajili ya kujitengenezea kinga katika ufisadi wake kwa taifa, haimaanishi kuwa kila mfanyabiashara anayeingia kwenye siasa ana malengo hayo.
Ninaamini kilichopelekea CCM kudhamiria kumtenganisha biashara na siasa ni historia na uzoefu iliopata kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara walioingia kwenye siasa. Na wazo lilikuwa zuri, kwamba mfanyabiashara atakayeamua kuingia kwenye siasa achague moja: biashara au siasa.
Tukirejea kwenye tamko la Kikwete kuwa CCM haitokufa, yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo ni ya kujipa matumaini tu na kukwepa ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa chama hicho kinaonekana machoni mwa baadhi ya Watanzania kuwa ni chanzo cha matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu. Kwa kifupi, kitakachoiua CCM si kauli za hao wanaoikitabiria kifo bali matendo ya chama hicho ambayo kimsingi ndio ‘pumzi’ inayokifanya kiwe hai.
Tukio jingine ambalo kwa namna moja au nyingine linahusiana na uhai wa chama cha siasa (kwa maana ya kuwa hakitokufa au la) ni tamko la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA), ya kwamba hatogombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015, bali atagombea urais.
Kwanini ninalinganisha tamko la Zitto na kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Kikwete? Jibu fupi ni kwamba matamko yote mawili yanaelekea kupuuza hali halisi ya mwenendo wa siasa za huko nyumbani.
Wakati Mwenyekiti Kikwete anajigamba kuwa CCM haitokufa japo kuna mamia kwa maelfu ya wana-CCM wanaokihama chama hicho kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake, huku pia baadhi ya viongozi wa chama hicho kama kina Samuel Sitta wakionyesha hadharani ‘maovu’ ya chama hicho, Zitto hataki kujihangaisha kutambua wengi wa Watanzania wanamtaka mwanasiasa gani kutoka chama chake ili kubeba dhamana ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Kabla sijaendelea kuijadili kauli ya Zitto, ningependa kuweka bayana masuala matatu ya msingi. Kwanza, Zitto ana kila haki si tu ya kutaka kuwa Rais wa Tanzania, bali pia kutangaza kuwa ana nia hiyo. Ni haki yake ya kidemokrasia, hasa ikizingatiwa kuwa anatoka katika chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Pili, ni suala la kukubalika kwa wapiga kura watarajiwa (potential voters). Kila mara ninapomsikia Zitto akielezea dhamira yake ya kutaka kuwa Rais, huwa ninajiuliza swali moja la msingi; ni lini amefanya ‘utafiti’ wa kutambua Watanzania wanamhitaji awe rais wao?
Wenzetu huku Magharibi, kabla mwanasiasa hajakurupuka kutangaza kuwa anataka kuwa rais huwa inamlazimu kujihangaisha ‘kusoma upepo,’ yaani kufahamu iwapo wapigakura wanamhitaji.
Sawa, Tanzania si nchi ya Magharibi, na pengine hakuna umuhimu wa kusaka mtizamo wa wapigakura. Lakini kwa mwanasiasa anayejali maslahi ya chama chake na wananchi kwa ujumla, yayumkinika kuamini kuwa atajihangaisha kufahamu iwapo dhamira yake ya kugombea ni kwa maslahi ya chama chake na umma kwa ujumla au ni kwa ajili ya kutimiza ndoto zake binafsi tu.
Suala la tatu, na ambalo kwangu si tu ni la msingi zaidi bali pia linanishawishi kuamini kuwa dhamira ya Zitto kugombea urais ni sawa na kubariki ushindi wa CCM hapo 2015, ni uadilifu wa mwanasiasa huyo.
Ninamfahamu Zitto vizuri, na si kupitia social media. Ni mmoja wa wanasiasa wachache wenye kipaji cha hali ya juu katika ujenzi wa hoja. Lakini, kama mwanadamu mwingine, mwanasiasa huyo ana mapungufu fulani. Kwa wanaomfahamu kupitia social media (hususan Twitter) wanaweza kuafikiana nami kuwa si mwepesi sana wa kuafikiana na watu wenye mtizamo tofauti na wake.
Ni rahisi kumhukumu kuwa ana jazba (japo sitaki kuamini hivyo) pindi mtu anapotofautiana naye katika anachoamini yeye kuwa ni sahihi. Nafasi haitoshi kutoa mifano halisi, lakini waliotofautiana nae kimtizamo ndani ya Twitter wanaweza kuwa mashahidi wazuri.
Tatizo la msingi kuhusu Zitto ni ‘tuhuma’ zilizowahi kuandikwa na jarida moja la kila wiki kwamba katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, jarida hilo lilinasa mawasiliano kati ya mwanasiasa huyo na mmoja wa viongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Katika mazingira ya kawaida, mwanasiasa wa chama cha upinzani kuwa na mawasiliano na mtumishi wa taasisi hiyo nyeti (ambayo ilishutumiwa na CHADEMA-ambayo Zitto ni mbunge wake-kuwa ilikihujumu chama hicho kwenye uchaguzi huo) inazua maswali kadhaa.
Ndio, watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ni Watanzania wenzetu kama ilivyo kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani. Lakini mawasiliano kati ya mwanasiasa wa chama cha upinzani kama Zitto na kiongozi wa idara hiyo, yanaweza kuibua maswali mengi. Kibaya zaidi, Zitto hajawahi kutoa ‘maelezo ya kueleweka’ kuhusu mawasiliano hayo.
Kimsingi, Zitto anatambua bayana hisia zilizojengeka baada ya habari hiyo kuchapishwa. Kuna waliotafsiri kuwa mawasiliano hayo yalilenga kukihujumu chama hicho, na kwa kuzingatia mantiki ya kawaida tu hatuwezi kuwalaumu kwa hisia hizo.
Lakini pengine kubwa zaidi ni kwanini bado kuna idadi kubwa tu ya wafuasi wa CHADEMA wanaotafsiri uamuzi wa Zitto kutaka urais kama ‘tamaa ya madaraka.’ Hivi akiweka kando imani yake kuwa ana uwezo na uadilifu wa kuongoza taifa la Tanzania, Zitto ameshawahi kufikiria kuwashawishi sceptics hawa hata kama hoja zao hazina mashiko?
Kubwa zaidi ni ukweli kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita yanaonyesha bayana jinsi mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, alivyokubalika kwa idadi ya kuridhisha tu wapiga kura. Kama dhamira ya Zitto ni kuona CHADEMA inaingia Ikulu, kwanini asiwekeze jitihada kumsapoti Dk Slaa katika uchaguzi ujao na kusubiri ‘zamu yake’ hasa kwa vile umri bado unamruhusu hata kwa miaka mingine 15 ijayo?
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, mgombea urais sharti awe na miaka 40. Mwaka 2015 Zitto atakuwa na umri pungufu na huo. Hivi kung’ang’ania kuwa anataka kugombea ilhali akijua Katiba haimruhusu si ni dalili ya tamaa ya madaraka?
Nimalizie makala haya kwa kulinganisha matukio mawili haya niliyozungumzia. Kama ambavyo Rais Kikwete hataki kujiuliza kwanini baadhi ya watu wanaitabiria kifo CCM, Zitto hataki kujiuliza kwanini baadhi ya watu wanatafsiri dhamira yake ya kutaka urais mwaka 2015 kama mikakati wa kuirejesha CCM madarakani na kuinyima CHADEMA nafasi hiyo.
Suluhisho katika masuala hayo mawili, linaweza kupatikana katika busara hii ya Waingereza isemayo “never ever put emotions in front of common sense” (kwa tafsiri isiyo rasmi, kamwe usitangulize hisia mbele ya tabasuri/ busara).


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.