30 Nov 2012


NILIPOSIKIA Abdulrahman Kinana ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hisia zangu zilikwenda kwa Karl Rove, Mmarekani anayeweza kuelezwa kama gwiji la mikakati ya siasa (political strategist) katika duru za siasa za Marekani.
Kwa uelewa wangu wa siasa za Marekani na za huko nyumbani, Rove na Kinana wanafanana kwa karibu katika utendaji kazi wao. Wote wawili ni watu waliopata mafanikio makubwa katika majukumu yao ya kuhakikisha ushindi wa mgombea waliyekuwa wakimuunga mkono; George W. Bush kwa upande wa Rove, na Rais Jakaya Kikwete kwa upande wa Kinana.
Hata hivyo, wakati Kinana amefanikiwa katika chaguzi mbili ‘kumpatia’ ushindi Kikwete, Rove alijaribu na kushindwa kupata ushindi wa mgombea zaidi ya Bush, harakati zake kwa kutumia taasisi za American Crossroads na Crossroads GPS (Grassroots Political Strategy) na mikakati wa ‘kumwaga’ dola bilioni moja kumuunga mkono aliyekuwa mgombea wa Republicans, Mitt Romney, kumwangusha Rais Barack Obama, hazikuzaa matunda.
Kimsingi, baadhi ya wachambuzi wa Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka huu wanayumkinisha kuwa ukiachilia mbali kushindwa kwa Romney, wahanga wakubwa wa uchaguzi huo ni Rove na baadhi ya wachambuzi wa siasa (political pundits).
Wakati Rove, ambaye pia ni miongoni mwa pundits hao, ‘aliangukia pua’ licha ya matumizi makubwa ya fedha kupitia taasisi alizokuwa akiongoza, wachambuzi wengine wa kisiasa wanatafsiriwa kuwa ‘walipigwa bao’ na magwiji wa takwimu wakiongozwa na Mmarekani nguli wa ubashiri kwa kutumia takwimu, Nate Silver.
Katika ubashiri wake, Silver alisema Obama angepata kura za uchaguzi (electoral college votes) 313 (akapata 332) na Romney 225 (akapata 206). Kwenye uchaguzi wa Seneti, Silver alibashiri Democrats wangepata viti 52.5 (wakapata 53) na Republicans viti 47.5 (wakapata 45). Kitakwimu, ubashiri huo unaweza kuitwa sahihi. Hiyo ni kinyume kabisa na Rove aliyebashiri Romney angeshinda kwa angalau kura za uchaguzi 279 dhidi ya Obama.
Nirejee kwa Kinana. Baada ya kuteuliwa kwa mwanamikakati (strategist) huyo wa CCM kunikumbusha kuhusu Rove, nikakumbana na swali jingine kichwani: baada ya mafanikio makubwa kwa awamu mbili za Kikwete (2005 na 2010), je, uamuzi wa Kinana kuingia kwenye ‘active politics’ utadumisha rekodi yake au ndio political suicide (kujiua mwenyewe kisiasa) yake?
Kimsingi, japo nimemfananisha Kinana na Rove kana kwamba siasa za uchaguzi huko nyumbani ni za uwazi kama za Marekani, lakini pengine tukiingia kwa undani na kuangalia vigezo vingine vilivyosaidia ushindi wa Kikwete - kwa mfano nafasi ya ‘Wanamtandao’ na ‘usaidizi’ wa Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi kwa CCM - inawezekana kazi ya Kinana ilikuwa nyepesi tu kwa vile mazingira yalikuwa mwafaka kwa mgombea wa CCM kushinda.
Lakini wakati ninajaribu kumtendea haki Kinana kwa kutoihukumu rekodi yake kwa vitu ambavyo havipo wazi kirekodi (yaani kama vigezo nilivyovitaja hapo juu), Jumapili iliyopita zikapatikana habari na picha zikimwonyesha anagawa leseni 21 za uchimbaji madini kwa wananchi huko Mugusu, Geita.
Kwa kweli sikuamini kwamba Kinana niliyefikia hatua ya kumlinganisha na Rove angeweza ‘kuingia mkenge’ wa kuigeuza CCM kuwa Wizara ya Nishati na Madini. Hivi kweli Kinana hatambui kuwa kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hakumaanishi kupora majukumu ya Wizara? Kama hatambui hilo basi hapaswi kuwa japo mwenyekiti wa serikali ya mtaa, achilia mbali huo ukatibu mkuu wa CCM.
Kwa upande mmoja kitendo hicho cha Kinana kinarejesha ‘machungu’ ya ufisadi wa Kampuni ya Meremeta ambapo Watanzania walidanganywa kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilijihusisha na biashara ya madini. Ninasema hivi, hili la Kinana kugawa hati za vitalu vya kuchimba madini lina kila dalili ya kuturejesha kwenye skandali kama hiyo ya Meremeta.
Hivi leseni alizotoa Kinana ziliombwa na nani huko wizarani? Yeye Kinana, CCM au hao wananchi waliokabidhiwa leseni? Kama Kinana ana uchungu na wachimbaji wadogo wa madini basi angeanza na hizo kampuni kubwa za madini ambazo kila mmoja wetu anatambua zinavyonufaika kutokana na udhaifu wa serikali yetu katika sera ya madini.
Hivi Kinana atanilaumu nikizua ‘conspiracy theory’ kuwa hao wananchi waliopewa leseni za kuchimba madini ni mwendelezo tu wa ufisadi ambapo walalahoi hutumiwa kwa maslahi ya mafisadi (yaani jina kwenye leseni ni la mlalahoi lakini mnufaika ni kigogo fulani)?
Leo CCM ‘mpya’ ya Kinana inapora jukumu la Wizara ya Nishati na Madini na kugawa leseni za uchimbaji madini, kwa nini kesho isipore jukumu la Ofisi ya Rais na kuiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuangamiza vyama vya upinzani vinavyoonekana tishio kwa CCM?
Naam, Waingereza wana msemo ‘once a cheater always a cheater’ (yaani, ukishawahi kuwa msaliti kwenye uhusiano wa kimapenzi utabaki kuwa msaliti wa mapenzi milele). Kama Kinana na CCM yake wameshaonja ‘utamu wa kuhonga leseni za uchimbaji madini’ (na yayumkinika kuamini kuwa hakuna mwenye uwezo wa kubadilisha kashfa hiyo ya kikatiba) kwa nini ‘asichonge mzinga’ na kupora majukumu ya wizara na idara/taasisi nyingine za serikali?
Laiti ningekuwa ninafahamiana na Kinana ningemshauri hivi: “Kinachoifanya CCM ionekane adui wa maendeleo ya Mtanzania wa kawaida ni uamuzi wa chama hicho kutelekeza msingi wake kama chama cha ‘jembe na nyundo’ (yaani wakulima na wafanyakazi) na kugeuka chama cha ‘bunduki na kisu’ (yaani hifadhi ya mafisadi na waporaji wa rasilimali zetu).”
CCM haiwezi kupendwa na Watanzania kwa kuingilia majukumu ya wizara. Kwamba wizara hizo zipo chini ya serikali ya CCM haimaanishi chama hicho kiingilie utendaji kazi wake.
Nimalizie makala hii kwa utabiri, sio ‘fyongo’ kama wa Rove niliyemlinganisha na Kinana, bali wa Nate Silver: kwa mwenendo huu wa Kinana kupora majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini na kutoa leseni za uchimbaji madini kwa wananchi, ninabashiri kuwa anaweza kuishia kukumbukwa zaidi si kwa kuwa mmoja wa wanamikakati wa kisiasa mahiri kabisa katika historia ya Tanzania bali kwa ‘madudu’ (kama ya Karl Rove mwaka huu) ya kuwapa sababu za ziada wapiga kura wa Tanzania ‘kuizika’ CCM ikiwa bado hai hapo mwaka 2015.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.