7 Dec 2012


MOJA ya kumbukumbu muhimu katika uchaguzi mkuu uliopita wa Marekani, ni ile ya Mitt Romney, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republicans, kuwa mgombea tajiri kabisa katika historia ya chaguzi za nchi hiyo. Hata hivyo, pamoja na utajiri wake, Romney aliishia kubwagwa na mgombea wa Democrats, Rais Barack Obama.
Licha ya utajiri wake binafsi, Romney pia alipata sapoti ya kutosha kutoka kwa matajiri mbalimbali ndani ya chama chake, huku wengi kati yao wakiweka bayana kuwa wangekuwa tayari kutumia kiasi chochote kile cha fedha kuhakikisha wanamng’oa madarakani Rais Obama. Kama ilivyokuwa kwa Romney, matajiri hao na fedha zao, hawakuweza kumwangusha Obama.
Kama kuna fundisho kubwa zaidi la muhimu kutoka katika uchaguzi huo wa Marekani kwa siasa zetu huko nyumbani, hasa kipindi hiki ambacho baadhi ya wanasiasa wanahangaika kumwaga fedha kujijengea mazingira ya ushindi katika uchaguzi mkuu ujao 2015, basi ni ukweli kwamba fedha si kila kitu katika kusaka ushindi wa kisiasa.
Wengi wa wachambuzi wa siasa za Marekani, wanaafikiana kwamba moja ya sababu kuu mbili zilizopelekea Romney kushindwa uchaguzi huo, ni kwanza; mwonekano wake kama tajiri aliye tofauti na Wamarekani wengi wanaokabiliwa na hali ngumu ya uchumi kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia, na pili; chama cha Republicans kutokuwa na mvuto kwa makundi mbalimbali katika jamii ya Wamarekani.
Walipokuwa wakipita huko na kule kujinadi, Obama na Romney walionekana kama wanasiasa wanaotoka sayari mbili tofauti. Wakati ilikuwa rahisi kwa Obama kuonekana ni ‘mwenzetu’ kutokana na historia ya maisha yake, mtu aliyetoka familia ya kawaida na ambaye ni ushuhuda mwafaka wa ndoto ya Amerika (The American Dream), Romney alionekana kama mtu asiyejua maana ya ugumu wa maisha kwani alizaliwa na kukulia kwenye familia tajiri.
Kana kwamba historia kumhukumu kama mgombea tajiri asiyejua shida zinazowakabili wengi wa wapiga kura haikutosha kuwa kikwazo kwa Romney, chama chake chaRepublicans kimeendelea kuonekana kama kinawatenga wapigakura wengi wa Marekani. Kwa taifa linalojigamba kwamba linaheshimu uhuru wa mtu kujiamulia mambo yake mwenyewe, alimradi havunji sheria za nchi, upinzani wa chama hicho dhidi ya utoaji mimba, haki za mashoga, bima ya afya bure (Obamacare) na masuala mengine muhimu wa walalahoi wa Marekani, umezidi kukifanya chama hicho kijiweke mbali na mpigakura wa kawaida katika nchi hiyo.
Kadhalika, kuibuka kwa kundi la wahafidhina wenye msimamo mkali linalofahamika kama‘Tea Party,’ kimezidi kuwafanya Republicans waonekane kama chama cha kibaguzi, na hasa kwa upinzani wao mkali dhidi ya marekebisho ya mfumo wa Uhamiaji ambao kwa sasa unaathiri takriban wakazi milioni 12 ndani ya nchi hiyo ambao kimsingi hawana haki ya makazi hadi sasa.
Wakati Obama amekuwa na mtizamo wa kujenga dunia ya maelewano, kwa mfano kwa kujaribu kujenga mahusiano bora kati ya Marekani na nchi za Kiislam, Republicanswalitafsiri jitihada hizo kama udhaifu wa Rais huyo.
Kadhalika, sera ya nje ya kibabe ya kutanguliza vitisho na vita badala ya kuipa fursa diplomasia, imeendelea kuwafanya wengi wa wapigakura wa Marekani kuwaonaRepublicans kama chama cha kuwabebesha mzigo wa gharama za kuendesha vita moja baada ya nyingine, bila kusahau gharama za uhai kutokana na vifo vya askari wa nchi hiyo.
Kwa huko nyumbani, siasa zetu za uchaguzi zimezidi kutawaliwa na matumizi makubwa ya fedha, hususan katika michakato ya kupata nafasi ya kugombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na hatimaye katika kupambana na vyama vya upinzani kwenye uchaguzi mkuu.
Ninaamini kila msomaji anafahamu kuhusu matumizi makubwa ya fedha kwenye chaguzi za Jumuiya za CCM, ambapo kimsingi fedha hizo zimelenga zaidi kujenga mazingira mazuri ya ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Tofauti na Marekani ambapo matumizi makubwa ya fedha yanalenga zaidi katika kumnadi mgombea kwa njia ya matangazo, huko nyumbani kwa kiasi kikubwa fedha zinatumika kununua kura. Kwa lugha ya moja kwa moja, fedha zinajenga uwezo wa mgombea kutoa rushwa kununua kura.
Matokeo yake sote tunayaona. Tumeendelea kuwa na wanasiasa ambao baada ya kununua ushindi kwenye chaguzi, wanakuwa ‘bize’ zaidi kujirejeshea fedha hizo kwa njia za kifisadi. Ninakumbuka wakati nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1996, takwimu zilikuwa zinaonyesha ili mgombea aweze kushinda uchaguzi katika jimbo lililopo jijini Dar es Salaam, alikuwa anahitaji takriban Shilingi milioni 100.
Sijawahi kupata takwimu za chaguzi za mwaka 2005 na 2010, lakini yayumkinika kuhisi kuwa kiwango cha mwaka 2006 kimeongezeka mara kadhaa. Sasa, kama huko Marekani ambapo hali ya maisha ni bora mara kadhaa kulinganisha na huko nyumbani, wapigakura wengi wameweza kukataa kuhadaiwa na mamilioni ya dola zilizotumika kumnadi Romney, kwanini Watanzania tuendelee kuwa watumwa wa pishi za mchele, doti za khanga, kilo za sukari na kadhalika zinazotumika kununua kura kisha kutupatia viongozi wasiojali maslahi yetu, na hivyo kuendeleza umasikini na ufisadi unaogubika taifa letu?
Ifike mahala tuweze kutofautisha mahitaji ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Kweli kilo moja ya sukari itamwezesha mpigakura kunywa chai kwa siku kadhaa, lakini rushwa hiyo itamgharimu mpigakura huyo kwa miaka mitano mfululizo.
Ingawa utajiri si dhambi, hususan ule uliopatikana kihalali, na ambao ni nadra katika nchi nyingi za Afrika, ni muhimu kwa wapigakura kuhoji huyo mgombea anayepita huko na kule kumwaga fedha, anazitoa wapi? Ni ukweli usiopingika kuwa wengi wa wanasiasa wanaotoa rushwa ili wapate uongozi, wanapata fedha hizo kupitia njia ambazo kimsingi ndizo zinafanya maisha ya wananchi kuwa magumu.
Kwa lugha nyingine, wanasiasa wa aina hiyo ni sawa na majambazi wanaotuibia, kisha wanatumia fedha zilizotokana na ujambazi wao kununua haki zetu za kupata wagombea sahihi, kisha wakishaingia madarakani wanaendeleza ujambazi wao huo!
Waingereza wanasema ‘once a thief always a thief’ (mtu akishakuwa mwizi ataendelea kuwa mwizi). Mwanasiasa anayehonga fedha kwa kutumia fedha zilizopatikana kwa ufisadi, lazima ataendeleza ufisadi wake pindi akiingia madarakani.
Nihitimishe makala haya kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kubadilika. Tuweke kando haiba za wagombea. Tuweke kando tamaa ya vitu vya msimu kama vile sukari, mchele, khanga na kadhalika. Tuweke mkazo katika kuwachagua viongozi wenye kujua matatizo yetu na wenye nia ya dhati kuyatatua matatizo hayo. Inawezekana, timiza wajibu wako!


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.