14 Dec 2012JUMAPILI iliyopita niliungana na ‘somo wangu’ Tanzania Bara kusherehekea siku yetu ya kuzaliwa. Japo tulizaliwa miaka tofauti, na hivyo birthday yetu ya majuzi ilikuwa ni ya kutimiza umri tofauti pia, lakini kama ilivyo ada, siku ya kuzaliwa huwa na umuhimu mkubwa kwa mhusika.
Kinyume na wengi ambao huadhimisha birthdays kwa nderemo na vifijo, binafsi kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa hunipa fursa mwafaka ya kutafakari nilikotoka, nilipo na niendako, sambamba na kumshukuru Mungu na kumwomba uhai zaidi.
Kadri miaka inavyokwenda mbele, na kadri umri wangu na wa Tanzania Bara unavyozidi kuongezeka, ndivyo ninavyojikuta nikielemewa na mzigo wa tafakuri kuhusu ‘somo wangu’ Tanzania Bara (ninatumia jina hili badala ya ‘Tanzania’ kwa sababu wenzetu wa Tanzania Visiwani walipata uhuru siku tofauti na sisi wa Bara).
Lundo la mawazo linalozidi kukua kadri ninavyoadhimisha birthdays zangu na ‘somo wangu’ Tanzania Bara linatokana na ukweli kwamba kwa kiasi fulani yayumkinika kuhisi kwamba nchi yetu badala ya kwenda mbele ni kama inarudi nyuma.
Kuna wanaohoji kuhusu suala zima la uhuru. Tulimtimua mkoloni ili tujitawale, tunufaike na rasilimali zetu badala ya rasilimali hizo kumnufaisha mkoloni pekee. Lakini kinachoendelea sasa ni ukweli mchungu kwamba ‘mkoloni mweupe’ kaondoka, na nafasi yake imechukuliwa na ‘mkoloni mweusi, Mtanzania mwenzetu.’ Takriban skandali zote kubwa zilizotikisa (na nyingine zinazoendelea kutikisa) taifa letu zimehusisha Watanzania wenzetu.
Mara kadhaa nimekuwa nikitumia kauli hii: “”angalau wakati anatukandamiza na kutunyonya, mkoloni alikuwa na excuse (isiyokubalika) kuwa Tanganyika-wakati huo- haikuwa nchi yake. Hakuwa na uchungu nayo. Lakini sasa hawa wanaotafuna nchi yetu kwa kasi ni wenzetu. Ni wanafamilia wenzetu, ndugu, jamaa au marafiki zetu. Na kibaya zaidi, wengi wao wamesomeshwa kwa jasho la Watanzania haohao wanaofisadiwa kwa kasi.”
Kwa hiyo kimsingi, mafisadi wa Kitanzania hawana ‘excuse’ (kisingizio) kwa vile si tu wanayoiangamiza ni nchi yao pia lakini hata wahanga wa ufisadi huo ni watu wanaowahusu kwa karibu.
Lakini kuna jambo ‘jipya’ lililojitokeza mwaka huu wakati wa maadhimisho ya sherehe za uhuru wetu. Katika kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baadhi ya wanasiasa vijana walinukuliwa wakitoa kauli zinazoashiria kuwa wangependa kuona sheria za uchaguzi zinabadilishwa na kuwazuwia ‘wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru wasigombee urais.’
Huko nyuma nilishawahi kuandika makala ambayo, pamoja na mambo mengine, ilipingana na mtizamo wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CHADEMA, Zitto Kabwe, ambaye alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa harakati za kuleta maendeleo haziwezi kusimamiwa ipasavyo na watu waliozaliwa kabla ya Uhuru.
Katika makala hiyo nilitanabahisha bayana kuwa niliuona mtizamo huo wa Zitto kuwa ni wa kibaguzi. Na niliweka wazi hofu yangu kwamba tukianza kuwabagua wazee, tunaweza kuishia kuwabagua wanawake, wakristo/waislamu, wanene/wembamba, nk kwani sumu ya ubaguzi hutapakaa.
Kilichotokea baada ya Kongamano hilo ni kama mjadala wa umri wa mgombea urais kuhamia kwenye mtandao wa kijamii wa twitter ambako watu mbalimbali waliojitokeza kuchangia hoja zao, mie nikiwa miongoni mwao.
Binafsi, ninakubaliana na wenye mtizamo kuwa Katiba yetu inawabagua vijana kwa kulazimisha kuwa mgombea urais lazima awe na umri fulani na kuendelea. Na ubaguzi huo unakera kwa sababu hakuna uthibitisho wowote kuwa mtu mwenye miaka 40 ana uwezo bora zaidi wa kuongoza kuliko mwenye miaka 39.
Lakini binafsi ninaona hoja hii ya ‘vijana kubaguliwa’ inapindishwa makusudi na wanasiasa wenye uchu wa madaraka. Wanataka kuitumia ajenda ya umri/ujana/uzee kama turufu tu ya kufikia malengo yao ya kisiasa.
Na kutumia ajenda hiyo kusingekuwa tatizo laiti wasingeleta hoja kwamba watu waliozaliwa mwaka fulani wasiruhusiwe kugombea urais. Haiwezekani kupigania usawa kwa kuendesha ubaguzi.
Nadhani tatizo la msingi la wanasiasa wenye mtizamo huo ni ufinyu wa uelewa wao wa tatizo la msingi linaloisumbua na kuikwaza nchi yetu kuendelea. Na kinachonikera zaidi ni ukweli kuwa wapiga debe wa hoja hiyo ni wanasiasa wenye akili na uelewa mkubwa kabisa.
Tumefika hapa tulipo - yaani masikini wa hali ya juu huku nafsi zetu zikiwindwa na mafisadi wanaonekana kana kwamba wanataka kuhakikisha nchi yetu inakombwa hata kile kidogo tulichonacho- si kwa sababu ya waliozaliwa kabla au baada ya uhuru bali majambazi waliofanikiwa kupata nyadhifa ambazo wanazitumia kuifilisi nchi.
Majambazi hawa (samahani, sina neno mwafaka la kuwaelezea) ni wabinafsi wasio na uchungu na nchi yetu wala na Watanzania wenzao. Ni watu wasioguswa na ukweli kwamba kwa kuiba fedha zetu na kuzificha huko Uswisi na kwingineko, wanawaathiri pia ndugu, jamaa na marafiki zao.
Neno jepesi na mwafaka ni uhaba (wa makusudi au wa kimfumo) wa uzalendo. Kila mzalendo anajihangaisha kuifikiria nchi yake kwa hali ilivyo sasa na itakavyokuwa huko mbele. Na uzalendo hauna umri. Aliyezaliwa kabla ya uhuru au baada ya uhuru anaweza kuwa mzalendo alimradi atangulize maslahi ya nchi na wananchi mbele ya maslahi yake binafsi.
Hoja kwamba wazee wetu wameishiwa na uwezo wa kufikiri ni sawa na kuwatukana baadhi yao ambao bila wao leo hii tusingeweza hata kuwa na huo mwaka tunaodai uwe kipimo cha aidha kuruhusiwa au kutoruhusiwa kugombea.
Badala ya wanasiasa hao vijana kuhangaika na akina nani hawastahili kugombea urais kwa vile walizaliwa kabla ya uhuru ni vema wakielekeza jitihada hizo kutuambia ni akina nani wanaosababisha mgao ‘wa milele’ wa umeme, ni kina nani walioficha fedha zetu huko Uswisi, na mafisadi wengine wanaotuibia kila kukicha.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha wanasiasa hao vijana kwamba sumu wanayopanda ya ubaguzi haitoishia katika kuwabagua wazee tu bali inaweza kuelekezwa kwa makundi mengine ya kijamii yanayoonekana vikwazo kwa ‘vijana’ hao kutimiza malengo yao ya kisiasa.
UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UDHAIFU


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.