11 Jan 2013


 
NI kitu kimoja kupima maendeleo kwa vigezo vilivyowekwa kutoka nje, na kitu kingine kabisa kupima maendeleo kwa kuzingatia hali halisi ya maisha katika eneo husika.
Hii ni nukuu ya tafsri yangu kutoka katika kitabu kilichochapishwa mwaka 1998; kiitwacho ‘The Making of a Periphery: Economic Development and Cultural Encounters in Southern Tanzania’ kilichohaririwa na Pekka Seppata na Bertha Koda.
Kitabu hiki ni muhimu sana katika wakati huu ambapo mjadala wa suala la gesi huko Mtwara umekuwa ukitawala vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni.
Takriban kila anayefuatilia maendeleo ya nchi yetu, atakuwa anatambua hisia kwamba mikoa ya kusini mashariki mwa nchi yenu, yaani Lindi na Mtwara, ni eneo ambalo si tu limegubikwa na umasikini, bali pia limesahaulika kimaendeleo.
Hata hivyo, kama nukuu ya mwanzo wa makala haya inavyoonyesha; dhana ya maendeleo inaweza kuwa na maana tofauti kati ya mkazi wa Masaki, Dar es Salaam, na yule wa Tanganyika Masagati, kule Morogoro.
Na suala hili limekuwa ni tatizo katika uchambuzi usio wa kitaaluma kuhusu maendeleo ya nchi yetu. Kuna msemo mmoja maarufu wa ‘Bongo tambarare’ ambao kwa namna fulani unajaribu kujenga picha kwamba taarifa kwamba Tanzania ni moja ya nchi masikini kabisa duniani, ni kama porojo tu ikilinganishwa na utitiri wa maghorofa unaochipuka kwa kasi jijini Dar es Salaam, na au mfumuko wa kasi wa viota vya starehe katika jiji hilo la maraha.
Kwa mtizamo wa juu-juu, taarifa kwamba Tanzania ni masikini, ni kama chuki binafsi tu kwa mtu anayetafsiri maendeleo kwa kigezo cha wingi wa magari ya thamani barabarani, kujaa kwa bidhaa za thamani madukani, na kadhalika.
Wengi wa wenye mtizamo huu potofu, ni wale wanaoiangalia nchi yetu kupitia kinachowazunguka mijini, hata kama wao si sehemu ya wamiliki wa vitu hivyo. Kuna Watanzania wengi tu wasiotaka kuiangalia nchi yetu zaidi ya kilichopo jijini Dar es Salaam au mijini kwa ujumla.
Bahati nzuri kwa mimi mzaliwa wa kijijini, ili nifike mahali nilipozaliwa (Ifakara), kwa kutumia basi kwa mfano, hunigharimu takriban saa 10 ya kukatiza mikoa mitatu, kwa maana ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro. Uzuri wa safari hiyo, kwa mtu mwenye kiu ya kuielewa nchi yetu, inatoa picha isiyo na chenga, ya tofauti ya hali ya maisha kati ya mjini na kijijini.
Taswira ambazo zinaendelea kubaki kichwani mwangu hadi leo, ni zile za watoto walio pekupeku ambao mara nyingi huwaangalia wasafiri waliomo kwenye basi kama watu waliokwepa ugumu wa maisha wanaopitia watoto hao.
Ni nyuso zinazoonyesha kukata tamaa, huku baadhi ya watoto wakijaribu kushirikiana na wazazi wao kuuza bidhaa moja au nyingine kwa wasafiri, mara nyingi muda ambao watoto hao wanapaswa kuwa shuleni.
Katika upeo wa kawaida, maendeleo ya kiuchumi yanamaanisha wastani kati ya raslimali zilizopo na idadi ya wakazi katika eneo husika. Ndiyo maana, kuyaangalia maendeleo ya nchi yetu kwa kigezo cha sehemu tu ya wenzetu wanaoishi mijini, kunatoa picha isiyo sahihi.
Lakini hata hivyo, maana hiyo ya maendeleo ya uchumi, inazua hoja nyingine ya muhimu. Raslimali nyingi zilizopo nchini mwetu hazipo mijini. Wakati pengo kati ya Dar es Salaam na Morogoro limetawaliwa na umasikini, eneo hilo (la Morogoro) lina utajiri mkubwa wa maliasili katika Hifadhi ya Selous, na ardhi yenye rutuba katika Bonde la Mto Ruvu.
Kati ya Morogoro mjini na Ifakara, kuna utajiri mkubwa wa raslimali, kuanzia mbuga ya wanyama ya Mikumi, taswira kama za kwenye postikadi kutoka milima ya Udzungwa, maporomoko ya maji maeneo ya Ruaha, ardhi lukuki inayorutubisha miwa, mpunga, mahindi na kadhalika, orodha ni ndefu!
Lakini wengi wa makazi ya maeneo hayo ni masikini kupindukia. Na hiki ndicho kinachonifanya niafiki kilio cha wana-Mtwara wanaopinga mpango wa gesi iliyopo eneo lao kusafirishwa kwenda Dar es Salaam. Binafsi, tatizo si gesi hiyo kusafirishwa, kwani thamani ya kitu ni matumizi, na haitokuwa busara kuwa na gesi ya kuringia tu pasipo kuitumia kwa manufaa ya wakazi wa eneo husika na nchi kwa ujumla.
Tatizo ni pale raslimali katika eneo husika inapokuwa haina manufaa yoyote kwa wakazi wa eneo husika. Ushahidi ni mwingi. Angalia maeneo ya migodini. Zaidi ya kuachwa na mashimo makubwa ya migodi, wengi wa wakazi katika maeneo yenye migodi wanaendelea kuwa masikini.
Kipaumbele kikubwa kwa Serikali kwenye maeneo kama hayo, kimekuwa kama alivyofanya mkoloni. Kuwezesha raslimali husika kusafirishwa kutoka zilipo hadi kwingiepo pasipo kutilia mkazo kutengeneza mazingira ya kuwawezesha wakazi wa sehemu husika kunufaika na raslimali husika.
Mikoa ya kusini, na hususan Mtwara, ni mifano hai ya namna raslimali zinazopaswa kuwanufaisha wakazi wa eneo husika zinavyoshindwa kuleta maendeleo ya kiuchumi katika eneo husikao. Licha ya utajiri wa zao la korosho, kilimo cha mihogo, misitu ambayo baadhi ya miti iliyopo humo hutumika kutengenezea vinyago, na sasa utajiri wa gesi, vijana wengi kutoka maeneo hayo wameamua kwenda kusaka maisha mijini, hususan Dar es Salaam, na kugeuka kuwa wamachinga.
Wakati ninaafikiana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete, ya kwamba raslimali za eneo moja la nchi lazima ziwe na manufaa kwa nchi nzima, lakini haikubaliki kuona raslimali hizo zikinufaisha maeneo mengine huku eneo lenye raslimali hizo likiendelea kudumaa kimaendeleo.
Suala hili la gesi ya Mtwara, ni kielelezo tu cha namna raslimali za nchi yetu zinavyonufaisha wachache. Hivi laiti utajiri lukuki tulionao huko nyumbani ungetumika kwa maslahi ya nchi yetu nzima, muda huu tungekuwa na deni la ndani la taifa la Sh trilioni 22, achilia mbali nafasi yetu kama nchi masikini kabisa duniani inayotegemea huruma ya nchi na mashirika wafadhili?
Nihitimishe makala haya kwa ubashiri huu mchungu. Wakati sitarajii kuona Serikali ikitambua kwamba utajiri huo wa gesi ya Mtwara ni fursa ya kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja; yaani kuifanya Mtwara kuwa hub ya sekta ya gesi nchini na papohapo kuifufua na kuiendeleza Bandari ya Mtwara, sintoshangaa kusikia kwamba gesi hiyo inayopigiwa kelele, ilishauzwa tayari na mafisadi kabla hata haijaanza kuchimbwa!
Ninajua utabiri wangu huu haupendezi, lakini huo ndio ukweli mchungu wa Tanzania yetu ya sasa ambapo badala ya Waziri wa Fedha na Uchumi kuguswa na deni la matrilioni ya Shilingi, yeye anadai bado tunakopesheka.
Kama ukubwa wa deni hilo hausumbui vichwa vya watawala wetu, kwanini wasumbuke kuona utajiri wa gesi haumnufaishi mkazi wa Mtwara, bali ukiishia kuongeza vijisenti kwenye akaunti za wateule wachache kule Uswisi, visiwa vya Jersey na kwingineko?


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.