22 Feb 2013

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Rashid Othman


UENEZAJI CHUKI ZA KIDINI:
Wanausalama Tanzania wamelala usingizi wa pono?

NIANZE kwa kutoa shukrani za dhati kwa wengi waliojitokeza kunipa pole na kunifariji kufuatia taarifa niliyobainisha kwenye makala yangu katika toleo lililopita la jarida hili kwamba nimehabarishwa na wanausalama wa hapa Uingereza kuwa kuna tishio la kuaminika dhidi ya uhai wangu.
Wengi walionitumia ujumbe wa barua-pepe, simu na ujumbe mfupi, walinipa moyo, walinitia nguvu zaidi kwa kumhusisha Mungu na nguvu zake dhidi ya udhalimu kwa wasio na hatia. Nikiri kwamba baada ya kupata ujumbe huo si tu nimefarijika lakini pia nimetambua kuwa jukumu nililojipa la kukemea maovu katika (hususan ufisadi) lina umuhimu kwa wengi.
Lakini si wote walioipokea makala hiyo kwa mtizamo huo chanya. Kuna wachache ambao si tu walipingana na nilichoeleza (baadhi wakidai ni uzushi tu) lakini pia wapo walioona kuwa ninastahili ‘adhabu’ hiyo kutokana na walichokiita ‘kimbelembele’ changu.
Miongoni mwa ‘Tomaso’ hao, wapo waliohoji mie ni nani hasa mpaka niwindwe ili kudhuriwa, huku wengine wakinituhumu kuwa ninajiona mtu muhimu sana kiasi kwamba ninaweza kuhisi ninawindwa kwa minajili ya kufanyiwa kitu kibaya. “Kwani wewe ndio Mtanzania pekee uliyepo Ughaibuni mpaka watake kukuuwa?” walihoji baadhi yao.
Wengine walikwenda mbali zaidi na kuhitimisha kuwa huenda ninasumbuliwa na maradhi ya kisaikolojia yanayonifanya kuamini kuwa kuna watu wanataka kunidhuru ilhali ni ‘ndoto za alinacha’ tu.
Kwa vile lengo la makala hiyo halikuwa kusaka huruma ya wasomaji bali kuhabarisha tu kilichonisibu, nimezipokea salamu za pole na hizo za kebehi/kashfa kwa moyo mkunjufu.
Mimi ni muumini mkubwa wa tofauti za kimtizamo, na kamwe katika zaidi ya miaka 10 niliyojihusisha na uandishi wa makala magazetini sijawahi kudhamiria maandiko yangu yawe kama kumshikia mtutu wa bunduki msomaji ili aamini ninachoandika.
Lakini wakati ninaendelea na ‘maisha ya tahadhari’ (hadi sasa feedbacks kutoka kwa wanausalama zinaonyesha kuendelea kwa uwepo wa tishio hilo), Jumapili iliyopita nilipokea taarifa za kusikitisha na kutisha maradufu ya tishio ninalokabiliana nalo.
Vyombo mbalimbali vya habari, vya ndani na nje ya Tanzania, viliripoti tukio la mauaji ya kinyama ya padre wa Kanisa Katoliki huko Zanzibar, marehemu Evaristus Mushi.
Nilipatwa na mshtuko mkubwa si tu kwa vile marehemu alikuwa wajina wangu (sote ni Evarist) lakini pia wote tunafahamu kuwa tukio la mtumishi wa Mungu kuuawa wakati anajiandaa kuendesha Misa Takatifu linaogofya na kutia uchungu mwingi, sambamba na kujenga picha tofauti dhidi ya imani tuliyojijengea kuwa nchi yetu ni kisiwa cha amani na utulivu.
Kwa kiasi kikubwa, tukio hilo la kigaidi (naam, kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi kuwa mauaji hayo si uhalifu bali ugaidi) limenirejesha katika hisia nilizowahi kuandika katika makala kadhaa huko nyuma nikihoji ufanisi wa utendaji kazi wa wanausalama wetu.
Haihitaji japo kozi ya dakika chache ya usalama wa taifa kwenda kwenye mtandao wa kijamii wa video wa YouTube kukumbana na sumu kali inayomwagwa na baadhi ya wanaojiita viongozi wa dini wakichochea ugaidi kama huo uliofanywa dhidi ya Padre Mushi.
Kuna waungwana wanalipwa mishahara minono na posho nzuri tu kuhakikisha kuwa matishio ya usalama dhidi ya nchi na wananchi yanadhibitiwa (pre-empted) kabla hayajaleta madhara lakini yayumkinika kudhani kuwa labda wahusika wapo kwenye likizo ndefu, tukizingatia hali ya usalama wa nchi inavyozidi kudumaa huko nyumbani.
Wanausalama wetu wamekuwa mahiri mno kuwa na ‘taarifa za kiintelijensia dhidi ya wakorofi wanaotaka nchi yetu isitawalike’ (na kutumia taarifa hizo kunyanyasa baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani, wanahabari, wanaharakati, nk) lakini wapo katika usingizi wa pono linapokuja suala la kutambua MATISHIO HALISI ya usalama wa nchi yetu na wananchi wake.
Hivi wanausalama wamekuwa wapi wakati taifa ‘linaingizwa mkenge’ kwenye skandali kama ya Richmond? Je, walikuwa likizo wakati majambazi wanaofahamika wakikwapua fedha za EPA? Na je, wanausalama wetu wamezibwa akili kutambua kuwa kuna mabilioni yetu yamefichwa huko Uswisi na watu wanaofahamika?
Tatizo la wazi ni kuwa na vipaumbele fyongo, ambapo dhana ya usalama wa taifa letu inatafsiriwa ‘ndivyo sivyo’ kuwa kuhakikisha ombwe la uongozi linalomomonyoa taifa letu halinyooshewi kidole, majambazi wanaobaka uchumi wetu hawakemewi, na chama tawala kina haki ya kudumu kutawala na upinzani dhidi yake ni uhaini.
Huu ni ukweli ambao wahusika hawatopenda kuusikia. Moja ya kanuni kuu za usalama wa taifa lolote lile duniani ni hii, “uimara au udhaifu wa amani katika taifa husika ni kiashirio cha uimara au udhaifu wa taasisi ya/za usalama katika nchi husika.”
Kwa hakika, mahala fulani kuna watu hawawajibiki ipasavyo. Kwa nini hawawajibishwi? Jibu jepesi ni kuwa kutowajibika kwao kwa taifa si muhimu kwa watawala ukilinganisha na uwajibikaji katika kuhakikisha kuwa wakorofi wanadhibitiwa, na keki ya taifa inaendelea kufakamiwa na wateule wachache pasi bughudha.
Sitaki kujifanya mjuzi wa masuala ya usalama, lakini siku moja kabla ya kifo cha Padre Mushi, ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook wa kikundi cha UAMSHO ulikuwa na picha ya maiti ikisindikizwa na ujumbe ‘wasia wa leo: kila nafsi itaonja mauti.’Innocent coincidence or statement of intent (ilitokea tu au ilikuwa ‘kauli thabiti’)? Labda wanausalama wetu watakuwa na jibu.
Lakini pamoja na kauli mbalimbali za kulaani mauaji hayo ya Padre Mushi na ahadi za kuwasaka wahusika kwa nguvu zote, sote twakumbuka kauli na ahadi kama hizo lilipotokea tukio jingine la kigaidi dhidi ya Padre Ambrose Mkenda huko huko Zanzibar.
Taifa letu halijawahi kuwa na upungufu wa viongozi wanaonekana kuguswa sana pindi yakitokea majanga (ikiwa ni pamoja na yale ya kuzuilika kama milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto) lakini wanaozembea kudhibiti kutokea kwa majanga hayo.
Kuna mtu anaitwa Ustaadh Ilunga Hassan, ambaye hotuba zake zinazochochea waziwazi mauaji dhidi ya mapadre, maaskofu na walei zimetapakaa huko YouTube, lakini yupo huru kana kwamba serikali na vyombo vyake vya dola vinaafikiana nae.
Kuna vyombo vya habari vya kidini (magazeti na redio) ambavyo ni kama vimeruhusiwa kuchochea vurugu za kidini lakini serikali na wanausalama wake ni kama hawana habari.
Nikiri kuwa hadi majuzi nilikuwa sifahamu jinsi chuki ya kidini ilivyotapakaa kwa baadhi ya Watanzania wenzetu lakini upeo wangu ulifunguka baada ya muda mfupi tu wa kusoma maoni kwenye habari ya kifo cha Padre Mushi iliyobandikwa kwenye ukurasa wa Facebook wa kikundi cha UAMSHO. Hivi mashushushu wetu wamekuwa vipofu kiasi cha kutoona sumu hii hatari inayomwagwa huko mtandaoni?
Imekuwaje tumefika hapa? Moja, tumeruhusu dini itumiwe na wanasiasa muflisi, si katika namna baadhi ya viongozi wa CCM wanavyodai, bali kwa maslahi binafsi ya wanasiasa hao. Sote tunakumbuka ajenda ya ‘upadre wa (Dk. Wilbroad) Slaa’ ilivyotumika kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita kana kwamba ni sehemu ya manifesto ya CCM, au upadre ni uhaini fulani.
Pili, vipaumbele vya wanausalama wetu vipo kwingineko. Ufisadi unashamiri na matishio ya usalama wa taifa yanaongezeka na hakuna kinachoonekana kufanyika.
Nimalizie kwa kutoa angalizo kuwa kuna haja ya haraka ya kukabiliana na hali hii ya uchafuzi wa amani, vinginevyo tutarajie majanga makubwa zaidi (God forbid!) Wenzetu mahali fulani wameshindwa kazi; wawajibike au wawajibishwe. Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube