9 Mar 2013
KATIKA moja ya mambo ambayo yanaweza kubaki kwenye kumbukumbu kuhusu utawala wa Rais Jakaya Kikwete ni utaratibu aliojiwekea wa kulihutubia taifa takriban kila mwisho wa mwezi.
Bila kujali kama hotuba hizo zinakuwa na mapya au zina manufaa kwa taifa, kitendo cha mkuu wa nchi kuongea na wananchi wake mara kwa mara kinastahili pongezi. Binafsi, nimekuwa nikizisoma hotuba zote za Rais Kikwete, na moja ya sifa kuu za hotuba hizo ni lugha inayopendeza kuisoma au kuisikiliza.
Nyingi ya hotuba za Rais hutawaliwa na busara zaidi kuliko jazba, ingawa kama ilivyo ada ya siasa za Chama cha Mapinduzi (CCM) kuna wakati hotuba hizo zimekuwa na vijembe vya hapa na pale vya kisiasa. Hilo ni la kawaida kwenye ulingo wa kisiasa.
Lakini kutoa hotuba yenye mvuto ni jambo moja, na hotuba husika kuwa na mantiki ni suala jingine. Katika makala haya ningependa kuijadili hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa Ijumaa ya Februari 28 mwaka huu. Na katika kujadili huko nitaegemea kwenye kipengele cha uhusiano wa Waislam na Wakristo.
Kwanza, nimpongeze Rais Kikwete kwa kutambua uzito wa suala hilo la kuwapo dalili za kuchafuka kwa uhusiano kati ya Waislam na Wakristo, na kuchukua hatua ya kulizungumzia. Kwa kufanya hivyo, Rais ni kama amefungua na kuruhusu mjadala wa kitaifa kuhusu suala hilo.
Pengine, baadhi ya wasomaji wangu wanaweza wakadhani kwamba pongezi zangu hizi kwa Rais si stahili yake, lakini ni vema kuelewa kuwa mara nyingi katika siasa za Afrika, kwa kiongozi au raia yeyote kuzungumzia masuala ya dini, imekuwa ni kama mwiko Fulani hivi.
Viongozi wengi hukwepa kuzungumzia dini, hasa kwa vile wenyewe huwa ni waumini wa dhehebu fulani, na ni rahisi kueleweka vibaya na kudhaniwa ama wanapendelea imani zao au kulaumiwa kuwa wanasaliti imani zao.
Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo kwa Rais Kikwete, moja ya mapungufu makubwa katika kipengele hicho cha uhusiano wa Waislam na Wakristo, ni swali alilouliza mwenyewe. Namnukuu: “Watanzania hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini?”
Binafsi, ninadhani kwamba ingawa ilikuwa sahihi kwa Rais Kikwete kuuliza swali hilo, lakini alikosea walengwa halisi wa swali hilo. Nitafafanua. Rais ndiye mkuu halisi wa Idara ya Usalama wa Taifa, au ‘sponsor’ kwa lugha ya kitaalamu. Yeye ndiye mlaji (consumer) wa taarifa zote za kiusalama zinazosakwa na kuchambuliwa na mashushushu wetu.
Ninadhani swali hilo lingekuwa na maana zaidi kama lingeelekezwa kwa wanausalama wetu maana kimsingi wao ndio wenye jukumu la si tu kulinganisha hali ilivyokuwa huko nyuma na kwanini sasa ni tofauti, bali pia wana jukumu la kubashiri kwa kuzingatia uchunguzi wao, nini kinaweza kujiri pindi hiki au kile kisipofanyika.
Ni uwezo huo wa kuangalia tulikotoka, tulipo na tuendako, unaowezesha vyombo vya usalama kumudu kuzuia matukio mbalimbali yanayoweza kutishia usalama wa taifa letu.
Rais Kikwete anasema: “Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia nchi yetu hii nzuri. Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na walahawazitakii mema dini zetu na nchi yetu.
Inawezekana anachosema Rais Kikwete ni kweli, lakini hata hivyo hatuambii ‘wenzetu’ hao ni kina nani, tukiamini kuwa wana usalama wetu wamemudu kuwatambua na hatimaye kumfahamisha Rais. Sasa kama ‘wenzetu’ hao wanafahamika, kwanini hawajachukuliwa hatua hadi tumefika katika hatua tulipo sasa?
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete aliweka wazi dhamira ya Serikali kwa kusema: “Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine na wanaokejeli dini nyingine.
Hata hivyo, Rais amechelea kusema kuwa Serikali yake pia itachukua hatua dhidi ya watendaji wake watakaozembea majukumu yao katika kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama.
Rais amefanya vyema kuwakumbusha polisi na mamlaka nyinginezo kuwa wasifanye ajizi kwenye matukio kama hayo yanayotishia amani ya nchi yetu. Hata hivyo, haitoshi kuwakumbusha tu pasipo kuchukua hatua stahiki dhidi ya wanaozembea majukumu yao!
Labda kwa kukumbushia tu, muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka 2005, Rais Kikwete alitoa onyo kali na ‘deadline’ kwa wala rushwa huku akiwatahadharisha kuwa wasitafsiri tabasamu lake vibaya. Miaka minane baadaye, yayumkinika kuhitimisha kuwa wala rushwa hao ‘wamepuuza’ onyo hilo la Rais, na kuna uwezekano wa hali kuendelea kuwa hivyo hadi atakapomaliza muhula wake wa pili mwaka 2015.
Kwa mantiki hiyo hiyo, kuwakumbusha wanausalama wetu kuwa wasifanye ajizi ilhali kuna ajizi za waziwazi ambazo zimekuwa zikiendelea, kwa mfano kutojihangaisha na wanaomwaga sumu za udini kwa kutumia mitandao ya kijamii, inaweza kuturudisha kule kule kwenye ‘deadline’ yake kwa wala rushwa.
Kuhusu swali la Rais Kikwete, la kwamba ‘kumetokea nini?’ Jibu rahisi tu. Ni kwamba hali hiyo imeachwa na (Serikali yake) pasi kuchukua hatua na tunayoshuhudia sasa ni matokeo ya kuzembea huko.
Ni muhimu kutambua kuwa imani ya dini inaweza kujenga umoja na pia inaweza kubomoa umoja. Kimsingi, kama nilivyobainisha kwenye mfululizo wa makala zangu zilizochambua vurugu za kidini kule Mbagala, zipo tofauti za kimsingi za kiimani kati ya Waislam na Wakristo. Na tofauti hizo, pengine kwa bahati mbaya, ndizo misingi mikuu ya dini hizo.
Lakini pia, dini hizo zina maeneo kadhaa ya muafaka wa kiimani ambayo kimsingi ndiyo yanayowezesha waumini wake kuishi pamoja. Kwa hiyo, katika mazingira ambamo kuna vitu ambavyo vipo ‘readymade’ kuwatenganisha watu, ingawa pia kuna vingine ambavyo vinaweza kuwaunganisha, njia pekee ni kuhakikisha watu hao wanaishi kwa umoja na amani. Kung’ang’ania kwa nguvu zote hayo yanayowaunganisha. Hilo limewezekana kwa miaka kadhaa, hata sasa kwa kiasi kikubwa bado linawezekana.
Hata hivyo, kuwezekana huko hakumaanishi kwamba yale yanayowatenganisha waumini wa dini hizo yamefutika. Yapo na yataendelea kuwapo. Kuyazuia kunahitaji mchanganyiko wa busara na utashi wa kuweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi ya kiimani. Kinadharia, hilo ni rahisi, lakini kivitendo, linaweza kuwa gumu zaidi ya inavyofikirika.
Nimalizie makala haya kwa kurejea pale nilipoanzia kwamba angalau Rais Kikwete ameongelea suala hilo la udini na amefungua mjadala kuhusu hatma ya taifa letu katika kipindi hiki ambacho tofauti zetu kiimani zinaelekea kuanza kuzidi nguvu muafaka wetu kiimani. Uislam na au Ukristo unaanza kuchukua nafasi muhimu kwenye utambulisho (identity) ya mtu badala ya Utanzania wetu!
Mwaka 2010 tuliruhusu baadhi ya wanasiasa mufilisi kutumia tofauti zetu za dini kama turufu ya kupata kura kutoka kwa wananchi, labda hao ndio ‘wenzetu’ aliowataja Rais kwenye hotuba yake. Sumu waliyomwaga haijafutika, lakini tunaweza kuidhibiti tukiunganisha nguvu zetu kama Watanzania pasi kujali Uislam au Ukristo wetu, pamoja na wanausalama wetu kutekeleza majukumu yao ipasavyo. United we stand, divided we fall (Tunasimama tukiwa wamoja, tunaanguka tukitengana).


1 comment:

  1. Mwandishi ningekuona makini sana kama ulivyowaambia usalama wako wapi? kama ungelirudisha tena kwake na chama chake kuwa WAO CCM ndiyo waliopandikiza chuki hizo kwa kuwa walitumia hiyo agenda ya UDINI kukidhoofisha CUF 2000 na 2005 na wakatumia tena 2010 kuidhoofisha CHADEMA. ni Rais na chama chake wamekuwa wakisimama kwenye majukwaa na kusema kuna vyama vya UDINI hali ya kuwa wanajua fika katiba hairuhusi kitu hicho kwa hiyo hakipo isipokuwa kwa matakwa ya chama chao, na TENDWA msjili wa vyama kwa kipindi chote hicho hunyamzia maneno hayo kana kwamba anazungumza mambo mazuri sanaaaa. Hivi kwa akili ya kawaida unapomwambia mtu chama fula ni cha Waislamu alafu yeye ni Muislamu ataacha. au umwambie CHADEMA cha wakristo kinaongozwa na Padre Slaa ataacha kukifuata...! Je hujawatenga watu kwa imani zao...?

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube