28 Jun 2013

WAKATI Watanzania wakiendelea na maombolezo ya wenzao waliopoteza maisha katika shambulizi la bomu kwenye mkutano wa CHADEMA jijini Arusha, mambo mawili makubwa yamejitokeza wiki iliyopita: moja la wazi na jingine ‘lililofichika.’

Tuanze na hilo la pili. Itakumbukwa baada ya shambulio la bomu kanisani jijini Arusha, tulielezwa kwamba Rais Jakaya Kikwete alikatisha ziara yake nchini Kuwait ili kushughulikia janga hilo ikiwa ni pamoja na kuhani misiba ya watu wawili waliofariki (kwa mujibu wa taarifa) na kuwajulia hali majeruhi kadhaa.

Hata hivyo, baadhi yetu tulihoji kama kweli Rais alikatisha ziara hiyo au ilikuwa imefikia ukingoni. Kuhoji kwetu huko hakukuwa na uzito sawa na ukweli kuwa Rais alionyesha kuwajali Watanzania wenzake waliokumbwa na janga hilo.

Safari hii pia, tukio la shambulio la bomu katika mkutano wa CHADEMA lilitokea wakati Rais akiwa nje ya nchi (alikuwa hapa Uingereza kuhudhuria mkutano wa nchi tajiri zaidi duniani za G8). Katika kile kilichoashiria kuwa ameguswa na tukio hilo, alitumia salamu za rambirambi kwa wafiwa na pole kwa majeruhi.

Lakini pamoja na pongezi hizo, katika makala yangu ya wiki iliyopita, moja ya masuala niliyozungumzia ni pamoja na kuhoji kwa nini safari hii Rais ‘hakukatiza ziara’ kama ilivyokuwa katika tukio la shambulio la bomu kanisani huko Arusha.

Nilihoji kama tukio hili la hivi karibuni lililosababisha vifo vya watu wanne hadi sasa (kwa mujibu wa taarifa) lina umuhimu mdogo kulinganisha na lile la awali ambalo lilisababisha vifo vya watu wawili. Huhitaji kufahamu vyema hisabati kuelewa kuwa vifo vya watu wanne ni vingi zaidi ya vifo vya watu wawili japo vyote ni vifo, na hakuna kifo ‘kidogo’ au ‘kikubwa.’

Je, Rais alikatisha ziara huko Kuwait kwa vile tukio la awali lilihusu imani ya kidini kwa maana ya shambulio kufanyika kanisani? Je, Kikwete alifanya hivyo kuepusha hisia kuwa yeye kama Muislam amepuuza vifo na majeraha ya Watanzania Wakristo katika shambulio hilo? Na je, aliporudi nchini na kwenda kuhani na kutoa pole huko Arusha alikuwa na lengo la ‘kuwapoza hasira’ Wakristo hasa ikizingatiwa kuwa bado kulikuwa na kumbukumbu za mauaji ya Padri Evaristus Mushi, Zanzibar?

Ni Kikwete pekee na wasaidizi wake wanaoweza kuwa na majibu ya maswali hayo ya msingi, lakini jambo moja la kusikitisha ni ukweli kuwa hadi ninapoandika makala hii Rais hajatoa mguu jijini Arusha kuhani misiba ya Watanzania wanne waliouawa na kadhaa waliojeruhiwa katika shambulio hilo. Je, Rais ‘amepuuza’ tukio hilo kwa sababu linakihusu CHADEMA?

Pengine ni kuwa na ushauri mbovu wa wasaidizi wake au pengine ni uamuzi wake tu usio sahihi wa kutozuru Arusha hadi muda huu, lakini kimsingi suala hilo linazidi kujenga hisia zisizopendeza kuwa CCM na serikali yake ina chuki kubwa kwa CHADEMA na kila Mtanzania anayejihusisha nayo. Tumeshuhudia Bunge la Jamhuri likiendelea na vikao vyake pasi kujali kuwa taifa lipo msibani, na tumeshuhudia pia baadhi ya viongozi wa serikali na wabunge wa CCM wakipuuza uhai na majeruhi ya Watanzania wenzao waliokuwa waathirika wa shambulio hilo la kigaidi, na kuligeuza hoja muhimu ya kuishambulia CHADEMA.

Na hapa ndipo inabidi tuzungumzie tukio la pili (kama nilivyobainisha mwanzoni mwa makala hii). Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa kauli ya ajabu na ya kutisha ya kuliruhusu Jeshi la Polisi kuendelea kuwapiga wananchi wanaoleta vurugu na kuwataka polisi kuwapiga.

Kilichonisikitisha na kunikera zaidi kuhusu kauli hiyo ya Pinda ni ukweli kwamba huko nyuma alilazimika kumwaga chozi bungeni baada ya kukurupuka na kauli isiyo na busara wala kuzingatia utawala wa sheria ya kuruhusu wananchi kuwaua wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na vifo vya albino. Hatari ya tamko hilo ni kwamba lingeweza kusababisha vifo vya wananchi wasio na hatia kwa kisingizio cha “uhusika wao katika vifo vya albino.”

Badala ya kushurutishwa ajiuzulu, Watanzania wakalainishwa na machozi ya kinafiki ya kiongozi huyo. Naam, ni machozi ya kinafiki kwa sababu kwa mara nyingine amerejea kosa lile lile lililomfanya amwage chozi bungeni: kuruhusu polisi wavunje sheria kwa kuwapiga (tena zaidi) wananchi kwa kisingizio cha kuwashughulikia wavunja sheria.

Hivi kwa busara zake, polisi hao ambao Pinda anawapa ruhusa ya kuwapiga wananchi watakavyo watakuwa wanatumia kipimo gani kutofautisha mvunja sheria na mwananchi asiye na hatia? Inawezekana, Pinda hajui kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likilaumiwa mno kwa matumizi makubwa ya nguvu (ambayo baadhi yamesababisha vifo) hata pale inapohitajika busara tu?

Pinda, anayefahamika kama ‘mtoto wa mkulima, si tu mcha Mungu (angalau kwa mujibu wa mwenendo wake) bali pia kiujuzi ni afisa usalama wa taifa. Inanitatiza sana kuona Pinda atageuka mcha Mungu asiye na huruma kwa Watanzania wenzake watakaoendelea kupigwa na polisi zaidi kutokana na ruhusa waliyopewa na Waziri Mkuu huyo. Pia inanikera mno kuona kiongozi mwenye ujuzi wa usalama wa taifa anapuuza usalama wa raia kwa kuruhusu polisi kuwapiga raia zaidi.

Rafiki yangu mmoja mwanasheria huko nyumbani (Tanzania) ameninong’oneza kuwa kuna jitihada zinaendelea kumchukulia hatua za kisheria Pinda kutokana na kauli yake hiyo ambayo kimsingi inavunja Katiba ya nchi yetu. Lakini wakati tunasubiri hatua hizo za kisheria- iwapo zitafanikiwa- inabidi ‘tuwe wapole tu’ kwani inaelekea ni wazi kuwa Pinda sio tu hatoomba radhi kwa kauli hiyo ya uvunjifu wa sheria lakini tusitarajie kuona filamu nyingine ya Waziri Mkuu kudondosha chozi la kinafiki.

Na kwa vile majuzi tu tumeshuhudia Rais Kikwete ‘akimzawadia’ Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema kwa kumwongezea mkataba wa ajira yake licha ya miito mbalimbali kumtaka aachie ngazi kwa kushindwa kazi, ni dhahiri Kikwete sio tu hatomkemea Pinda bali hatomwajibisha pia.

Japo hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoweza kumhusisha Kikwete na chuki za wazi za baadhi ya viongozi wa serikali (kwa mfano Waziri William Lukuvi na Steven Wassira) au CCM (kwa mfano Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba), ukimya wake katika kukemea matamshi yao unaweza kuashiria kuwa anaafikiana nao kama sio anayewatuma kutoa matamshi hayo ya chuki (kwa mfano kuituhumu CHADEMA kuwa inahusika na tukio la milipuko kwenye mkutano wake huko Arusha).

Pinda aombe msamaha (na siamini kuwa atafanya hivyo) au akae kimya, Kikwete amwajibishe (pia sioni hili kutokea) au amwache tu, Pinda achukuliwe hatua za kisheria au aachwe tu, ukweli mchungu unabaki kuwa kauli hiyo ya Waziri Mkuu ina madhara makubwa na huenda tukaanza kuyashuhudia hivi karibuni tu. Na madhara hayo si kwa raia tu bali hata kwa polisi wenyewe maana kama Pinda ameruhusu polisi kupiga raia ni wazi pia raia watajiruhusu wenyewe kujilinda dhidi ya vipigo vya polisi. Huu sio uchochezi bali ni ukweli usioepukika.

Nimalizie makala hii kwa kumwomba Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda kuisoma mojawapo katika gazeti la Guardian la hapa Uingereza inayoeleza kuwa licha ya maendeleo ya teknolojia kuwa nyenzo muhimu kwa umma kupambana na tawala dhalimu, wananchi katika nchi mbalimbali duniani sasa wana uelewa mkubwa kuhusu nguvu za dola (power) na jinsi zinavyotumika isivyo (abuse) kiuchumi na kisiasa.

Natoa wito kwa Balozi wa Marekani nchi Tanzania, Alfonso Lenherdt, kumfikishia ujumbe Rais Barack Obama anayetarajiwa kuzuru nchi yetu wiki ijayo, kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu (kama unavyothibitishwa na kauli ya Pinda) sambamba na kukua kwa tishio la ugaidi huku serikali ikionekana kuzembea kuchukua hatua mwafaka. Wakati takriban kila Mtanzania anasikia fahari kwa Rais Obama kuzuru Tanzania, ni matarajio ya wengi kuwa kiongozi huyo wa taifa lenye nguvu kubwa kabisa duniani, na muumini wa haki za binadamu na uhuru wao atawakumbusha watawala wetu juu ya haja na umuhimu wa kuzingatia masuala hayo muhimu (haki na uhuru wa binadamu).

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.