17 Jul 2013

NIANZE kwa kutoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa askari wetu saba mashujaa waliouawa huko Darfur, Sudan wakiwa sehemu ya jeshi la kimataifa la kulinda amani nchini humo. Damu ya askari hao haijapotea bure kwani kilichowapeleka huko ni kusaka amani, na kama tujuavyo sote, kila dini inasisitiza amani. Kwa hiyo ni matarajio yetu kuwa Mwenyezi Mungu atazimpumzisha roho zao kwa amani.
Pili, niwatakie mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wasomaji wote wa gazeti hili la Raia Mwema. Kila Ramadhan ni ushahidi mzuri kuwa Watanzania tuna umoja na udugu, licha ya tofauti zetu za kiimani, kwani wengi tusio Waislam tunawaunga mkono ndugu hao.
Na tatu, ningependa kukipongeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa ushindi wao katika uchaguzi wa madiwani katika kata zote nne huko Arusha.
Itakumbukwa uchaguzi huo uliahirishwa baada ya kutokea shambulio la bomu katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za CHADEMA kuwania viti hivyo vya udiwani.
Lakini hata kabla ya kutokea janga hilo la kusikitisha, uchaguzi huo ulivuta hisia za Watanzania wengi hasa kutokana na ushindani mkubwa uliojitokeza kati ya CHADEMA na CCM.
Kama kuna kubwa tulilojifunza katika uchaguzi huo ni ukweli kwamba matumizi ya fedha, ubabe, vitisho na hadaa yanaweza kushindwa kuwarubuni wapiga kura wanaolewa wanataka nini. Japo uchaguzi huo ulikuwa wa ngazi ya kata tu, lakini matokeo yake yanaweza kuwa na maana kubwa zaidi, kwa CHADEMA na CCM, kwani kuna uwezekano, hata kama ni mdogo, wa matokeo hayo kujiakisi kwenye chaguzi nyingine, na pengine hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Lakini kati ya picha mbaya zilizojitokeza katika uchaguzi huo ni namna chuki inavyokua kati ya CCM na CHADEMA. Japo hadi muda huu hakuna maendeleo ya maana katika uchunguzi wa chanzo cha bomu la Arusha katika mkutano wa CHADEMA, yayumkinika kuhisi chuki hizo za kisiasa zinaweza kuwa miongoni mwa sababu kuu za tukio hilo la kinyama.
Na kwa kuthibitisha chuki hiyo, vifo vya Watanzania wanne vilivyotokana na shambulio hilo vilionekana kama ‘vimetokea nchi nyingine,’ tulishuhudia Bunge likishindwa angalau kuahirisha kikao cha bajeti japo kwa saa chache tu kuwakumbuka marehemu na majeruhi.
Kadhalika, tukio hilo liligeuzwa turufu muhimu kwa baadhi ya wanasiasa ‘hamnazo’ wa CCM ambao walidai CHADEMA wanahusika kwa minajili ya kusaka huruma ya wapigakura.
Kibaya zaidi, hata Rais Jakaya Kikwete naye hakuona haja ya kwenda Arusha kuhani misiba ya waliouawa kinyama na hadi leo hajaona umuhimu huo.
Kana kwamba haitoshi, majuzi ubalozi wa Marekani huko nyumbani umeliumbua Jeshi la Polisi kwa kubainisha kuwa wapelelezi wa Shirika la Upepelezi la nchi hiyo FBI hawapo Arusha kupeleleza tukio hilo, tofauti na taarifa za awali za jeshi hilo. Sijui polisi wetu walikuwa wanataka kumhadaa nani.
Kimsingi, ushindi wa CHADEMA katika uchaguzi huo wa ngazi ya kata una umuhimu mkubwa kwa chama hicho kwa sababu wafuasi wake wamekuwa wakipewa wakati mgumu na CCM pamoja na vyombo vya dola. Hali hiyo imekuwa ikijitokeza takriban katika kila chaguzi.
Pasi aibu, Jeshi la Polisi limekuwa likiwanyanyasa CHADEMA kana kwamba jeshi hilo ni sehemu ya kikundi cha ulinzi cha CCM kinachofahamika kama Green Guard.
Na ni suala hilo la Green Guard ambalo ndio dhima ya makala hii. Majuzi, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alieleza dhamira ya chama chake kuanzisha kikosi cha ulinzi, Red Brigade, kwa ajili ya ulinzi wa mikutano ya chama hicho.
Kauli hiyo ya Mbowe imezua mzozo mkubwa huku Rais Kikwete akikemea hadharani, Jeshi la Polisi likiapa kupambana na dhamira hiyo ya CHADEMA, na muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amenukuliwa akidai ataifuta CHADEMA iwapo wataanzisha kikosi cha ulinzi.
Kati ya ‘upinzani’ wote huo dhidi ya Red Brigade, ulionigusa ni ule wa Rais Kikwete. Binafsi, hainiingii akilini kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM hafahamu chama chake kina kikundi cha ulinzi kama hicho wanachotaka kuanzisha CHADEMA. Kikwete hafahamu kikosi hicho, kinaitwa GREEN GUARD.
Nisiume maneno, kama Rais Kikwete, ambaye pia Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, hafahamu chama chake kina kikosi cha ulinzi kiitwacho Green Guard basi yayumkinika kusema haistahili kuendelea kuwa kiongozi wa juu wa chama hicho.
Bila kujali suala la vyama vya siasa kuwa na vikosi vya ulinzi ni sahihi au la, ukweli kwamba kwa muda mrefu tu CCM imekuwa na Green Guard, CUF nayo imekuwa na Blue Guard, na si Kikwete, Jeshi la Polisi wala Tendwa, waliokemea suala hilo, lakini ghafla CHADEMA kutangaza ina nia ya kufuata ‘mkumbo’ huo inakuwa nongwa, basi nchi yetu imekosa mwelekeo.
Huu sio upendeleo au uonevu bali ni ubabaishaji. Ukisikiliza kwa msingi hoja za CHADEMA kuhusu dhamira yao ya kuwa na kikosi chao cha ulinzi kama wenzao wa CCM na CUF, utaafikiana nao mara moja. Sio siri Jeshi la Polisi sio tu limeshindwa kukipatia chama hicho ulinzi unaostahili bali pia limekuwa mstari wa mbele kuwapiga, kuwanyanyasa na hata kushindwa kuzuia vifo vya wana-CHADEMA.
Ifahamike kuwa Katiba ya nchi inatoa ruhusa kwa raia kupatiwa ulinzi na kujilinda inapobidi. Sasa kama polisi sio tu hawataki kuwalinda CHADEMA bali pia wanashiriki kuwanyanyasa, chama hicho kifanye nini?
Niliwahi kuandika mfululizo wa makala huko nyuma kuhusu kampeni ya chuki inayoongozwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM (nikawataja Steven Wassira, Mwigulu Nchemba, Nape Nnauye, Spika Anne Makinda na Naibu wake Job Ndugai). Katika makala hizo nilibainisha angalau Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete amekuwa akiepuka kauli za chuki dhidi ya wapinzani, hususan CHADEMA.
Lakini kwa kushindwa kwenda kuwapa pole waathirika wa shambulio la bomu katika mkutano wa CHADEMA Arusha, na kauli yake ya majuzi kuituhumu CHADEMA kuhusu wazo la chama hicho kuanzisha Red Brigade, ilhali CCM anayoongoza Kikwete nayo ina Green Guard, naanza kushawishika pengine akina Wassira, Nape, Mwigulu na wengineo wanaomwaga sumu ya chuki dhidi ya CHADEMA wana idhini ya Mwenyekiti wao.
Nihitimishe makala hii kwa kumsihi Rais Kikwete atafakari upya mwenendo wa chama chake katika siasa hizi za chuki dhidi ya CHADEMA. Badala ya kukimbilia kudhibiti matokeo, ni vema kuchunguza chanzo cha ‘tatizo’ (yaani kwa nini CHADEMA ‘inaisumbua’ CCM).
Badala ya kudhani kuwa uungwaji mkono wanaopata CHADEMA ni matokeo ya chama hicho ‘kuhamasisha vurugu’ au ‘kufanya nchi isitawalike,’ ni rahisi tu kwa Kikwete na CCM kubaini kwamba turufu kubwa ya CHADEMA ni utambuzi wa matatizo yanayomkabili Mtanzania hivi sasa, na kushauri njia mwafaka za kuyatatua. Na matatizo makubwa zaidi ni ufisadi na umasikini, licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali katika nchi yetu.
Mfano mwepesi, mwananchi wa kawaida tu hahitaji uelewa wa juu wa utendaji kazi wa vyombo vya dola kutambua kuwa haiwezekani kilo 150 (zaidi ya gunia la lumbesa) za dawa za kulevya ziweze kupita kwenye mipaka yetu na kukamatwa Afrika Kusini kama hakukuwa na msaada wa vigogo fulani. Na kama kawaida, si Waziri, Naibu wake, IGP au kiongozi yeyote yule mwenye dhamana aliyechukuliwa hatua kuhusiana na skandali hiyo inayochafua sifa ya Tanzania kimataifa. Je, kuzubaa huko kuwajibishana katika tukio kama hilo si hatua muhimu ya kuwapa CHADEMA pointi a bure?
Niihadharishe CCM kuwa chuki na hujuma zake dhidi ya CHADEMA zinarahisishia safari ya chama hicho kuingia Ikulu mwaka 2015. Hivi sasa, CHADEMA inavuna wafuasi wengi sio tu kwa sababu wanakihurumia chama hicho kwa jinsi kinavyonyanyaswa kila kukicha, lakini pia wanakerwa kuona ajenda pekee ya CCM sasa hivi ni kuidhibiti na pengine ‘kuichinja’ CHADEMA. Huu ni mithili ya mpambano kati ya babu mtu mzima mwenye ‘miguvu’ tele (CCM) dhidi ya mjukuu wake ‘dhaifu’ (CHADEMA). Sote tunajua uungwaji mkono wa wapenda haki utaelekezwa upande gani.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube