Vigogo dawa za kulevya watajwa

Written by Mwananchi 
Monday, 18 September 2006

*Majina yao yapelekwa kwa Rais Kikwete
*Ni orodha ndefu ya majina ya watu 58
*Wamo wafanyabishara, wanasiasa, viongozi wa dini
*Mbinu wanazotumia nazo zaanikwa hadharani

WITO wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka wananchi wajitokeze kutaja majina ya wahalifu nchini, umepata mwitikio mpya, safari hii watu kadhaa wakijitokeza kutaja majina ya vigogo wanaoongoza kwa biashara ya dawa za kulevya nchini.

Majina hayo yako katika barua iliyoandikwa na wananchi 15 kwenda kwa Rais Kikwete, ambamo wanadai kwamba walikuwa wakitumiwa na vigogo hao kufanya biashara
hiyo, lakini sasa wameamua kuachana nayo. Barua hiyo iliandikwa Septemba 8, mwaka huu na wahusika wanadai wamekwisha kuiwasilisha Ikulu.

Kwa mujibu wa barua hiyo, majina 58 yameorodheshwa yakiwa katika makundi matatu makubwa, la kwanza likiwa ni waagizaji wakubwa wa dawa hizo; la pili ni
wafadhili ambao majina yao hutumika kusafirisha dawa hizo; na la tatu ni wauzaji walioko Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.

Katika orodha ya waandishi wa barua hiyo wanaodai kusukumwa na uzalendo na uchungu kwa nchi yao, yamo majina ya wafanyabiashara maarufu nchini na wanasiasa,
wakuu wa taasisi nyeti, baadhi ya viongozi wa dini na maafisa wa juu serikalini.

Kundi la kwanza lina majina 12, miongoni mwao ni wafanyabiashara maarufu katika miji ya Dar es Salaam, Morogoro, Zanzibar, Arusha na Bagamoyo na baadhi ya
 viongozi wa dini wa madhehebu fulani.

Kundi hili linadaiwa kuwa linaingiza dawa za kulevya kwa njia mbalimbali zikiwamo, kutumia mipira ya kondomu, majokofu, vifaa vya hospitali, meli na
 marobota ya mitumba.

Katika kundi la pili kuna watu 19, miongoni mwao wamo wanasiasa wakubwa nchini wakiongoza kundi hili, kutoka taasisi ya fedha nchini na wafanyabiashara maarufu wa
Dar es Salaam na Zanzibar.

Kundi la tatu lina majina 27, ambao si ya watu wenye majina makubwa, lakini ndio wanaotumika kusambaza mitaani kwa watumiaji wa dawa za kulevya.
 

Mbali ya kushiriki katika kusambaza dawa za kulevya, kundi hili pia lina baadhi ya majina ya watu waliotajwa kushiriki katika kuingiza silaha nzito
 zinazotumika kwa ajili ya ujambazi kutoka nchi jirani.

Ufukwe wa Pwani ya Bahari ya Hindi eneo la Muhoro wilayani Rufiji inaelezwa kuwa linatumika kuingizia silaha hizo kutoka nchi jirani pamoja na dawa za
 kulevya chini ya ufadhili wa mmoja wa wanasiasa nchini.

Uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K. Nyerere unatajwa kuwa unatumiwa na watu hawa kuingiza dawa hizo nchini kutokea nchi za nje, huku baadhi ya maafisa wa polisi
 watatu wakitajwa kuwa ndio wanaotoa ulinzi kwa watu wanaopitisha dawa hizo.

Nyumba ya afisa wa juu mstaafu katika idara nyeti iliyopo jijini Dar es Salaam inatajwa kuwa inatumika katika kuhifadhi vijana wanaoingiza dawa za kulevya
 nchini, huku nyumba ya mfanyabiashara mmoja iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam ikitajwa kuwa ndiyo inayotumika kama kituo cha kutolea pipi tumboni kwa vijana wanaotumika kuingiza dawa hizo kutoka nje ya nchi.

Vile vile, katika kundi hili mwanamke mmoja anayefanya kazi katika taasisi moja ya fedha anatajwa kuwa anashiriki katika kuhujumu uchumi wa nchi kwa
 kusafirisha kwenda nje fedha nyingi za kigeni akitumiwa na mfanyabiashara mmoja maarufu wa dawa za kulevya nchini.

Mipaka ya Tunduma mkoani Mbeya, Horohoro mkoani Kilimanjaro na Namanga mkoani Arusha, nayo imetajwa kuwa inatumika kupitisha dawa za kulevya kwa kutumia
 mabasi na magari mengine. Kuna kampuni mbili za mabasi nchini zinazotajwa kuongoza kutumika katika usafirishaji.

Barua hiyo ya kurasa 10, pia inamtaja mwanamke mmoja ambaye anatumika kupitisha dawa za kulevya uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kuwa ni sugu; aliwahi
 kuhukumiwa kifungo cha miaka 35 jela kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya, lakini hivi sasa yupo mitaani kifungo chake akitumikia mtu mwingine.

Alipoulizwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, alisema hajapata barua hiyo na kwamba atalizungumzia
 baada ya kuipata.

Naye Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, alisema hana taarifa za kuwako kwa barua hiyo. Hata hivyo, alisema kuna tume ya dawa za kulevya iliyopo
 chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inayoshughulikia zaidi suala hilo.

Alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi za kukamata watu wanaojihusisha na dawa hizo na kwamba mikakati mingine ya kupambana na watumiaji inafanywa na tume
 hiyo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza Jeshi la Polisi liongezewe uwezo wa kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha vituo vya kazi askari
 waliokaa kituo kimoja kwa muda mrefu.

Pia alilitaka Jeshi hilo lijisafishwe lenyewe kutokana na madai kwamba polisi wanahusika na baadhi ya matukio ya uhalifu nchini.
 

Rais alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa zozote za uhalifu, na wanaojua waliko majambazi wazipeleke taarifa hizo kwake kama wanaogopa kuzipeleka polisi.
 

Katika kuitikia wito huo, wananchi kadhaa waliandika barua iliyooroshesha majina ya polisi 20, wakiwamo baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa na kuikabidhi kwa Waziri wa Usalama wa Rais, Bakari Mwapachu.

Tangu wakati huo, mabadiliko makubwa yameshuhudiwa yakifanywa kwenye jeshi hilo, hata hivyo hii ni mara ya kwanza kwa watu kujitolea kuandika barua yenye
 majina na maelezo ya kina kama hii kuhusu biashara ya kulevya na kuipeleka kwa Rais.