1 Aug 2013


TANGU niwasili kwa mara ya kwanza hapa Uingereza zaidi ya miaka 10 iliyopita, nimejijengea tabia moja ambayo ni mithili ya ‘ibada’ yangu kila asubuhi, kusoma habari za huko nyumbani katika vyanzo mbalimbali vya habari mtandaoni.
Na ni katika mwendelezo wa tabia hiyo, Oktoba 2006 nilikutana na habari moja iliyohusu ‘sakata la Richmond.’ Katika habari hiyo ndani ya gazeti moja la kila siku huko nyumbani (Tanzania), ilielezwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alikuwa anafanya jitihada za kuhamasisha wabunge wa CCM wawe na msimamo mmoja katika mjadala bungeni kuhusu sakata hilo.
Wakati huo nilikuwa nikituma makala katika gazeti moja la kila wiki huko nyumbani (sio hili), na kutokana na kuguswa na habari hiyo ambayo iliashiria uwepo wa harakati za kukwaza mjadala wa maana kuhusu skandali ya Richmond, niliifanya habari hiyo kuwa mada kwenye makala ya wiki iliyofuatia.
Makala hiyo ilinisababishia matatizo makubwa. Kwanza, mwandishi wa habari wa Waziri Mkuu (wakati huo) aliandika makala kali ya kunijibu, pamoja na mambo mengine aliniita mpotoshaji, huku akikanusha kwa nguvu mtizamo wangu kuwa ‘Lowassa alikuwa anajaribu kuwafumba mdomo wabunge wa CCM wasijadili suala la Richmond bungeni kwa ufanisi.’
Siku chache baadaye, nilipata simu kutoka kwa kiongozi mmoja wa juu wa taasisi niliyokuwa nikiitumikia wakati huo. Katika simu hiyo, bosi huyo alihoji iwapo nipo hapa Uingereza kimasomo au kisiasa. Alikwenda mbali zaidi na kunituhumu kuwa huenda wakati huo nilikuwa nikiitumikia Serikali ya Uingereza, kosa ambalo kwa mujibu wa kanuni za sehemu niliyokuwa mtumishi wakati huo ni sawa na kosa la uhaini (treasonable offence).
Kadhalika, kiongozi huyo, alinishambulia kuwa makala zangu zilikuwa zikiwapa hoja wapinzani wa CCM, na kisha kuniamuru niache mara moja kuandika makala zinazohusu masuala ya siasa za huko nyumbani. Nilijaribu kutii amri hiyo kwa muda mrefu lakini baadaye nikashindwa baada ya kuja huko nyumbani mwaka 2008 na kushuhudia jinsi mafisadi walivyokuwa wakiitafuna nchi yetu.
Kosa lililosababisha bosi huyo kufikia hatua ya kinipigia simu ya karipio ni makala hiyo niliyobainisha hapo awali, ambayo kimsingi ililenga kushauri uwepo wa mjadala huru na wa wazi kuhusu sakata la Richmond. Katika makala hiyo nilitahadharisha kuwa jitihada zozote za ‘kulifunika suala hilo chini ya kapeti’ zinaweza kuzua madhara huko mbele.
Miaka miwili baadaye, nilichobashiri katika makala hiyo kikatokea. Hatimaye Lowassa alilazimika kujiuzulu kutokana na skandali hiyo ya Richmond. Kama nilivyoitarajia, yule bosi aliyenikaripia mwaka 2006 hakunipongeza, na sidhani kama hadi leo (bado yupo madarakani) anatambua umuhimu wa nilichoandika wakati huo.
Kimsingi, tukio hilo ndio lilikuwa mwanzo wa uhusiano mbaya na mwajiri wangu, na picha iliyozidi kujengeka ni ya mie kuonekana msaliti kwa ‘kuisema vibaya’ CCM na serikali yake. Japo kimsingi nyingi ya makala zangu kuhusu siasa ziliendana na wajibu wa taasisi hiyo kwa umma, vitisho na manyanyaso mfululizo hatimaye vilisababisha ajira yangu katika taasisi hiyo ‘kutowezekana.’
Lengo la makala hii sio kumlaumu mtu au taasisi fulani. Pamoja na misukosuko kadhaa niliyopitia kutokana na dhamira yangu kunituma kujadili masuala mbalimbali yanayokwaza maendeleo ya nchi yetu, hususan ufisadi, bado ninaamini kwa asilimia 100 kuwa ninafanya jambo stahili, hata kama limeshanigharimu katika maisha.
Nilichokuwa ninafanya nilipokuwa mwajiri wa taasisi hiyo ndicho hasa kilichopaswa na kinachopaswa kufanywa na kila mwajiriwa na kiongozi wa taasisi hiyo ya umma, sambamba na kila Mtanzania mwenye upendo wa kweli kwa nchi yetu. Hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania, na tusipoilinda na kuienzi hatutokuwa na pa kukimbilia (hasa tukizingatia hivi sasa tuna uhusiano wa shaka na baadhi ya majirani zetu).
Kilichonisukuma kurejea mkasa huo ulionikumba miaka kadhaa iliyopita ni mawasiliano niliyofanya majuzi na mwalimu wangu mmoja wa zamani hapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Binafsi, mwalimu huyo ni kama mzazi wangu kielimu kwani ameniongoza tangu nikiwa mwanafunzi wake hapo ‘Mlimani,’ na kuniunga mkono kitaaluma hadi nikamudu kupata shahada nyingine mbili (licha ya niliyoipata UDSM), na ameendelea kuwa nguzo yangu muhimu wakati huu ninaposaka shahada ya nne – ya uzamivu (licha ya vikwazo mbalimbali vya kimaisha nilivyokumbana navyo).
Mwalimu huyo (ambaye ninaomba nihifadhi jina lake) alinieleza kuwa amekuwa akizungushwa na serikali kuongezewa mkataba wake kama mhadhiri katika kitivo kimoja chuoni hapo. Pengine msomaji unaweza kudhani nimeguswa na suala hili kwa vile tu mhadhiri huyo amekuwa na msaada katika maisha yangu kitaaluma. Ukweli ni kwamba takriban kila mwanafunzi aliyefundishwa na mhadhiri huyo atakubaliana nami kuwa mwanataaluma huyo ni mfano wa kuigwa kwa jinsi anavyojibidiisha kuhakikisha wanafunzi wake wanafaulu.
Na kujibidiisha huko hakumaanishi kuwapatia wanafunzi njia za mkato bali ni pamoja na kutumia muda wake binafsi hata katika siku za mapumziko kuwafundisha wanafunzi wake, iwe ni katika majengo ya chuo au nyumbani kwake.
Uzuri mwingine wa mhadhiri huyo ni ukweli kwamba yeye si muumini wa hizi dini zetu za ‘mapokeo’ yaani Ukristo na Uislamu. Ninasema ni ‘uzuri’ kwa sababu pamoja na mazuri ya dini zetu, kuna aina fulani ya ‘ubaguzi uliofichika’ unaotokana na mafunzo ya dini hizo, hususan katika kipengele cha ‘imani yangu ndio sahihi kuliko nyinginezo.’ Asiye muumini wa Ukristo au Uislam, kama ilivyo kwa mhadhiri huyo, ana ‘faida’ ya kuelezea mambo pasi kukwazwa na ‘sheria kali za kiimani’ zinazotawala dini zetu.
Katika kubobea kwenye taaluma ya Sosholojia (elimu-jamii), mwongozo mkubwa wa kitaaluma na kimaisha kwa mwalimu huyo ni jamii. Na ndio maana, kama ilivyo katika masuala ya dini, yeye amekuwa ‘neutral’ (asiyefungamana na upande wowote) katika itikadi za kisiasa. Kwake, jamii ndio nyanja muhimu zaidi katika maisha ya mwanadamu.
Mhadhiri huyo anashangaa kwa nini serikali imekuwa ikisuasua kumwongezea mkataba wake hasa ukizingatia kuwa utendaji kazi wake ni wa hali ya juu hadi amefikia hatua ya kupata Uprofesa. Na kwa kila anayemfahamu, kusita kwa serikali kumwongezea mkataba mwanataaluma huyo kunaashiria jambo moja tu; kutothamini michango ya Watanzania wenzetu wanaojitolea kwa maslahi ya taifa letu.
Bahati nzuri amefanikiwa kupata chuo kikuu cha kufundisha katika nchi moja barani Afrika, lakini hata hivyo anajisikia uchungu kuona anakwenda kutoa mchango wa kielimu katika nchi nyingine ilhali taifa letu lina mahitaji makubwa ya wataalamu katika nyanja mbalimbali, hususan elimu ya juu.
Sitaki kujifananisha na mwanataaluma huyo mahiri, lakini kwa kiasi flani, yanayomsibu yanashabihiana na kilichonikumba huko nyuma. Unatumikia umma kwa nguvu na moyo wako wote lakini wenye mamlaka wanakuona kama surplus to requirements (ziada isiyohitajika)
Athari kubwa ya kutothamini wenzetu wanaojitolea kwa ajili ya taifa letu ni ile hisia kuwa “ah, bora ujali tu maisha yako...mbona fulani alijiweka kimbelembele na angalia yaliyomfika.” Kwa lugha nyingine, uzalendo unakwazwa na vitimbi vinavyowaandama wenzetu wanatanguliza maslahi ya umma mbele ya maslahi yao binafsi.

Kwa mwenendo huu, basi tutazidi kushuhudia wataalamu mbalimbali wakiamua aidha kukimbilia kwenye ‘ulaji’ katika siasa au, kama ilivyo kwa mhadhiri huyo, kwenda kutumia utaalamu wao nchi nyingine, na kuliongezea taifa letu uhaba wa wataalamu katika sekta mbalimbali.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/imebaki-kazi-moja-tu-kuipigania-tanzania#sthash.QVeXmYgZ.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.