12 Aug 2013

Sijui ilikuwaje, jana nimeshinda Twitter takriban kutwa nzima pasi kutambua kuwa mmoja wa wanaharakati wa haki za jamii, msanii wa Bongoflava, BABU SIKARE a.k.a ALBINO FLANI, yu mgonjwa. Katika maelezo ya picha aliyoweka katika mtandao wa kijamii wa Instagram, msanii huyo ameeleza kuwa anasumbuliwa na kansa ya ngozi, na sasa anapata matibabu.

Katika maelezo hayo, anaeleza (namnukuu), "kWAHIYO, NIMEGUNDULIWA NINA KANSA YA NGOZI. KWA MWEZI SASA NIMEKUWA NIKIFANYIWA OPERESHENI NA MATIBABU MAKUBWA YA KANSA YA NGOZI. SI MUHIMU KUELEZEA MAUMIVU YALIVYO LAKINI NI MUHIMU KUJADILI JINSI MAALBINO WASIOJIWEZA WATAKAVYOWEZA KUPAMBANA NA KANSA PASIPO MATIBABU NCHINI TANZANIA.

Pole sana, mpambanaji. Natambua pole pekee haitoshi, na ndio maana ninatoa wito kwako msomaji wa blogu hii kuungana nami kumwombea ndugu yetu huyo apate uponyaji, si kwa ajili yake tu bali pia kwa jamii nzima ya maalbino ambayo amekuwa mstari wa mbele kuipigania.

Nimefahamiana na ALBINO FULANI huko Twitter, katika mijadala mbalimbali ya mustakabali wa taifa letu. Ni msanii mwenye upeo na uelewa wa hali ya juu. Na katika majadiliano yetu, amejitanabaisha waziwazi kuwa ni mtu mwenye kuguswa sana na haki za jamii (social justice). Na ndio maana namwita MPAMBANAJI.

Basi pamoja na sala zangu kwa Mungu, naamini mpambanaji utashinda mtihani huu wa maisha. Naamini pia maradhi yako yataifungua macho jamii kuhusu wajibu wetu kuwasaidia wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albinism), sambamba na kupigani haki zao, hususan za matibabu stahili.

MUNGU AKULINDE NA KUKUBARIKI. 


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube