13 Oct 2013


NIANZE makala hii kwa pongezi zangu za dhati kwa Ubalozi wetu nchini Kenya ambao juzi ulitangaza kuwa umejiunga na mtandao wa kijamii wa Twitter. Kadhalika, naushukuru ubalozi huo kwa heshima waliyonipatia kwa ‘kunitwiti’ kuhusu habari hiyo njema.
Lilipotokea shambulio la kigaidi nchini Kenya hivi karibuni, nilihoji kama Ubalozi huo unatumia mtandao wa Twitter kuwafahamisha Watanzania waliopo nchini humo au/na huko nyumbani kuhusu usalama wao au wa ndugu, jamaa au marafiki zao.
Kwa nchi nyingi duniani, hususan za Magharibi, balozi zao na hata Wizara zao za Mambo ya Nje, hujihangaisha sana kwenye mitandao ya jamii na tovuti zao kuwafahamisha wananchi kuhusu hali ya usalama, na hasa wakati wa majanga kama tukio la ugaidi jijini Nairobi.
Ni matumaini yangu kuwa balozi zetu nyingine zitaiga mfano wa ubalozi wetu wa Kenya na kuanza kutumia vyombo mbalimbali vya habari, na hasa mitandao ya kijamii kusambaza na kurahisisha mawasiliano.
Baada ya pongezi hizo, nibaki huko huko Twitter kwa ajili ya mfano unaohusiana na mada yangu wiki hii. Majuzi nilikuwa na maongezi ya utani na mbunge mmoja wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi (mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi).
Pasi kuingia kiundani kuhusu maongezi yetu hayo, mbunge huyo alinieleza (kwa utani) kwamba namnukuu: “Chahali, you are very cynical...” (akimaanisha mie ni mtu mwenye kuyaangalia mambo kwa mashaka, kwa tafsiri isiyo rasmi).
Ninapenda kukiri kuwa mara nyingi mtizamo wangu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa taifa letu, umetawaliwa na mashaka. Pengine tabia hiyo, ni matokeo ya kujihusisha na fani moja huko nyuma ambayo inasisitiza kuliangalia kila jambo kwa mashaka, sambamba na dhana kuwa imani itapelekea mauti yako (trust will get you killed).
Ni katika hali hiyo, mtizamo wangu kuhusu mchakato mzima wa kuelekea kupata Katiba Mpya, umetawaliwa na mashaka. Na huenda nikieleza sababu zinazonipa mashaka hayo, wasomaji wangu wanaweza kushawishika kukubaliana nami kwamba japo ni vema kuwa na matarajio mema, lakini ni muhimu matarajio hayo yakatokana na misingi imara na ya kuleta matumaini.
Kwa wanaofuatilia kwa karibu suala la Katiba Mpya, watakuwa wanafahamu kuwa kimsingi ajenda hiyo iliasisiwa na chama cha upinzani cha CHADEMA, kabla ya kuporwa na CCM.
Lakini, jambo la msingi si nani aliyeasisi hoja hiyo au nani aliipora, bali umuhimu wake kwa taifa letu. Hata hivyo, ukweli kwamba awali CCM ilionyesha upinzani dhidi ya wazo hilo la CHADEMA kuhusu Katiba mpya, unaweza kutupa mwanga kuhusu sokomoko linaloendelea katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Kwa wanaofuatilia makala zangu kwa karibu, wanaweza kubaini kwamba sijalitilia maanani sana suala la Katiba mpya. Kwanini? Jibu langu ni jepesi tu, ambalo pengine linachangiwa na kile alichokieleza Mmbunge Mwinyi kuwa ninayaangalia mambo mengi kwa mashaka, ni kwamba ninapata shida sana kuamini kwamba CCM ipo tayari kujitundika kitanzi kwa kuruhusu Katiba Mpya yenye maslahi ya wananchi, badala ya utaratibu uliozoeleka miaka nenda rudi, wa kuweka mbele maslahi ya kibinafsi na/au kiitikadi.
Kwamba CCM iruhusu nchi iongezwe na Katiba badala ya Chama kushika hatamu (hata kama tupo kwenye mfumo wa vyama vingi)? Ninapata shida kuamini hilo, kama ambavyo siamini kuwa chama hicho tawala kitaruhusu kundi lolote lile, iwe ni Tume ya Warioba, wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii na kadhalika, kuongoza mchakato huo badala ya CCM yenyewe.
Ni hivi; kwa viongozi wengi wa CCM, kila suala linaloihusu nchi yetu, lipo chini ya hakimiliki yake. Ukiwasikiliza viongozi mbalimbali wa chama hicho wanapozungumzia masuala yanayohusu nchi yetu, unaweza kudhani wanazungumzia kitu wanachokimiliki binafsi na si cha umma.
Na japo ni rahisi kuwalaumu kwa ubinafsi huo, lakini tutarajie nini kutoka kwa wanasiasa ambao wengi wao wametumia mamilioni ya fedha kuingia kwenye nyadhifa walizonazo sasa?
Kwa watu wa aina hiyo, siasa ni zaidi ya ajira; ni njia ya mkato ya kujinufaisha na hata kupata utajiri wa haraka, kama si kinga kwenye matendo yaliyo kinyume cha sheria.
Lakini, hata kama CCM ingekuwa chama ‘kisafi’ bado kinakabiliwa na tatizo moja kubwa la haiba ya viongozi wakuu wa chama hicho. Tangu ‘utotoni,’ chama hicho kilitegemea sana nguvu na busara za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ingawa wengine wanatafsiri kuwa alikuwa mbabe, ambapo alimudu kwa asilimia kubwa kukipa dira na mwongozo chama hicho tawala.
Kila anayeifahamu CCM ya sasa anajua fika kuwa japo Rais Jakaya Kikwete anapewa heshima zake kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, lakini yayumkinika kuhitimisha kuwa kuna wanasiasa wawili-watatu wenye nguvu kubwa zaidi yake ndani ya chama hicho.
Tetesi kadhaa zinaeleza kuwa hata hali ya sintofahamu au upinzani katika masuala kadhaa yanayohusiana na mchakato wa Katiba hiyo mpya, vinachangiwa na kiongozi mmoja ‘mwenye nguvu za ajabu’ ndani ya CCM, ambaye inaelekea ameapa kuwa lazima aingie Ikulu mwaka 2015 ‘no matter what’ (iwe, isiwe).
Inaelezwa kwamba mwanasiasa huyo, ambaye sihitaji kumtaja jina, amekuwa akiongoza CCM kwa namna anavyotaka, pengine kutokana na habari kwamba ametumia fedha zake nyingi kuwaingiza madarakani viongozi mbalimbali wa chama hicho, ikiwa ni pamoja na wale waliopo ngazi za juu.
Kwa hiyo, ingawa ningetamani kuandika maneno tofauti na haya, binafsi sidhani kwamba tutaishia kupata Katiba tunayoitamani. Ninashindwa kabisa kuamini kuwa ‘walafi’ ndani ya CCM, wataruhusu mwanya unaoweza kupunguza uwezekano wao wa ‘kuifakamia keki ya taifa.’
Naam, mengi ya mapendekezo yaliyomo katika Katiba hiyo yanaweza angalau kupunguza mianya ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na ukandamizwaji wa haki.
Ingawa ninatamani sana kuona nchi yetu inapata Katiba yenye kujali maslahi ya kila Mtanzania na taifa letu kwa ujumla, historia na uzoefu wangu binafsi, vinanikwaza kuamini kwamba chama tawala, hususan genge la wanasiasa wanaoendekeza maslahi binafsi, kitaruhusu tufikie ndoto hiyo.
Na pia, ninaomba kuwa mkweli, hata kama ukweli wenyewe ni mchungu, Rais Kikwete anaweza kuwa na nia nzuri kwa taifa letu kuhusiana na suala hili la Katiba mpya, lakini amezungukwa na wanasiasa wabinafsi na wenye nguvu kubwa, ambao kwa namna moja au nyingine, wanaweza kumzidi kete na hatimaye tukaishia kuwa na Katiba iliyo mpya, si kwa kilichomo ndani yake, bali mpya kwa mwaka ilipopitishwa rasmi.
Labda, mimi ni ‘cynical’ kama alivyotania Mbunge Mwinyi, lakini labda hii ndiyo hali halisi tunayopaswa kujiandaa nayo kisaikolojia. Lakini kinachonisumbua zaidi, ni kukosekana kwa njia bora. Waingereza wanasema ‘foolproof’ itakayozuia uwezekano wa mchakato huu wa Katiba mpya kuishia kuwa zoezi la gharama kubwa, kifedha na kimatumaini, litakaloishia kuwa sehemu ya historia isiyo na manufaa kwa mwananchi wa kawaida.
Nihitimishe makala hii kwa ushauri unaoweza kuonekana hauna maana. Imani zetu za kidini kwa asilimia kubwa zimekuwa sehemu muhimu ya maisha yetu.
Na kwa vile dua na sala zina umuhimu wa kipekee, na hasa katika mazingira yanayokatisha tamaa, basi pengine ni vema tukiwekeza nguvu zetu katika dua/sala kumwomba Mola aangamize vikwazo vya kila mwenye malengo mabaya dhidi ya Katiba Mpya, sambamba na kuwajaalia ujasiri wale wote wanaopigania kupatikana kwa tunu hiyo muhimu kwa taifa letu. Katika Mungu, yote yanawezekana!
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tujiandae-kisaikolojia-kupata-katiba-mpya#sthash.dTZXvHqP.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.