7 Nov 2013

KATIKA moja ya makala zangu huko nyuma nilitaja kitabu fulani ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikinipa mwongozo katika mazingira tofauti. Kitabu hicho kinaitwa ‘48 Laws of Power’ (Kanuni 48 za nguvu, kwa tafsiri isiyo rasmi).
Robert Greene, mwandishi wa kitabu hicho ambacho miongoni mwa ‘waumini’ wake wasanii Will Smith na Jay-Z, ambao ni maarufu nchini Marekani na duniani kwa ujumla, anakanusha vikali madai kuwa kitabu hicho ni ‘Biblia ya mwendawazimu.’
Anasema tofauti na Biblia Takatifu ambayo inategemea zaidi kwenye upendo na mambo mema, hali halisi duniani ni tofauti: kuna maadui na watu wenye roho mbaya; kuna maharamia ambao ukifuata mafundisho ya Biblia kuwa “mtu akikupiga kofi shavu la kushoto, mgeuzie na shavu la kulia” watakumwagia tindikali uso wako kama si kung’oa meno na kucha.
Kwa kifupi, kitabu hicho kinatoa mwongozo wa jinsi ya kupata nguvu, kutathmini nguvu, na jinsi ya kujikinga dhidi ya nguvu za wengine.
Kwa nini nimeanza makala hii kwa kukumbushia kuhusu Kanuni 48 za Nguvu? Jibu ni kwamba dhima ya makala hii ni kujadili harakati za kusaka nguvu ndani ya chama kikuu cha upinzani huko nyumbani (Tanzania), yaani CHADEMA.
Kanuni ya 4 ya Nguvu (4th Law of Power) inaonya: “ Usiongee sana zaidi ya inavyopaswa: kadri unavyojaribu kuridhisha watu kwa maneno, ndivyo kadri utakavyoongea zaidi, na kuonekana ‘mtu wa kawaida’... Watu wenye nguvu hujenga heshima na kuogofya kwa kuongea maneno machache. Kadri unavyoongea maneno mengi ndivyo kadri unavyokuza uwezekano wa kuonekana mpumbavu.”  
Mbunge Godbless LemaKanuni ilipaswa kuzingatiwa na Mbunge wa CHADEMA, Godbless Lema ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa katika malumbano makali na mbunge mwenzie kutoka chama hicho, Zitto Kabwe, kuhusu suala la posho kwa wabunge.
Kilichonikera kuhusu Lema ni ukweli kwamba alipotoa taarifa katika mtandao wa Jamii Forums kuwa kesho yake angeandika makala kuhusu ‘Unafiki wa Zitto kuhusu suala la posho’ nilimjibu kwa kumtafadhalisha kutofanya hivyo, nikimkumbusha kuwa malumbano hayo hayana manufaa kwa chama chao. Kwa bahati mbaya au makusudi alipuuza ushauri wangu.
Labda nimuulize Lema, baada ya kuandika makala hiyo ya ‘kumsuta’ Zitto, CHADEMA imejipatia wapiga kura wangapi kwa minajili ya kukiingiza chama hicho Ikulu mwaka 2015? Kwa kuutangazia umma kuwa Naibu Katibu wake Mkuu (Zitto), Lema ameisaidiaje CHADEMA kujenga dhana kwa Watanzania kuwa ni chama kilicho tayari kuwa mbadala wa CCM pindi chama hicho tawala kiking’oka madarakani?
Hivi kulikuwa na ugumu gani kwa Lema kumtafuta Zitto baada ya vikao vya Bunge au kwenye simu na kujadili tofauti zao ‘ki-utu uzima’? Pamoja na kuthamini mchango wake katika siasa za upinzani huko nyumbani, ninaomba kuhitimisha kuwa alichofanya Lema ni dalili za ‘utoto wa kisiasa’ (political immaturity).
Kanuni ya 9 ya Nguvu (9th Law of Power) inausia: “Ushindi unaopatikana kupitia malumbano una madhara yake. Chuki itakayozalishwa kutokana na ‘ushindi’ huo itadumu kwa muda mrefu...Ni vema kuwafanya watu waafikiane nawe kutokana na matendo na sio maneno yako.” Yawezekana Lema akahisi ameshinda katika hoja yake ya kujenga picha kuwa ‘Zitto ni mnafiki,’ lakini kwa gharama ipi, kwa manufaa ya nani na hatma ya ‘ushindi’ huo ni ipi?
Hivi baada ya malumbano hayo ya mitandaoni kati ya Lema na Zitto kuna uwezekano wowote wa wanasiasa hao kusimama jukwaa moja kunadi mgombea wa chama chao? Je, wanaweza kukaa pamoja kujenga hoja yenye maslahi kwa chama chao au wapigakura wao?
Kanuni ya 19 ya Nguvu (19th Law of Power) inafundisha; ‘Kuna aina mbalimbali za watu ulimwenguni na kamwe usidhani kuwa kila mtu atafanya mambo kulingana na matarajio yako. Msaliti au mwajibishe mtu wa aina fulani basi mtu huyo atatumia uhai wake wote akisaka fursa ya kulipa kisasi...Chagua maadui zako kwa makini, na kamwe usimkosee mtu asiyestahili kukosewa.”
Hata kwa mie ambaye si ‘shabiki wa Zitto,’ aliyoyaandika Lema huko mitandaoni yangeweza kuniacha na kinyongo dhidi yake. Pengine Zitto ni ‘malaika’ ambaye atachukulia kauli za Lema kama sehemu tu ya maisha ya kisiasa, lakini kuna mashabiki wake (Zitto) ambao huenda si ‘malaika’ kama yeye. Je, vinyongo vyao havina madhara kwa mustakabali wa CHADEMA?
Na tutarajie nini iwapo hata Zitto si ‘malaika’ (kwa maana kwamba akifanyiwa jambo baya analea kinyongo)?
Lakini kosa jingine la Lema ni kupuuzia Kanuni ya 43 ya Nguvu (43rd Law of Power) inayofundisha “Ubabe hupelekea matokeo yatakayokuwa dhidi yako. Ni lazima uwashawishi watu watake kufuata mwelekeo wako. Mtu aliyeshawishika kufuata mwelekeo wako anakuwa mfuasi wako mtiifu...Lainisha upinzani kwa kufanyia kazi hisia zao, kwa ‘kucheza’ na kile wanachokithamini na wanachokiogopa. Puuza matamanio ya wengine, basi nao watakupuuza.”
Mpende au mchukie, Zitto ana turufu kubwa zaidi ya Lema katika ajenda kuu ya CHADEMA ya kupambana na ufisadi. Kuna Watanzania wengi tu wanaomwona kama ‘mpiganaji halisi’ wa maslahi yao: kuanzia ‘ishu’ ya Buzwagi hadi kwenye kufuatilia ‘mabilioni yaliyofichwa Uswisi’ sambamba na ‘vita yake mpya’ dhidi ya ukwepaji kodi.
Kwa Lema kutumia ‘ubabe’ kwenye mitandao ya kijamii ilhali hana ‘kete muhimu’ ya kuwafanya Watanzania wengi zaidi wampende, anaweza kuwa amewapa sababu baadhi yao kumchukia kwa ‘kumwandama shujaa wao Zitto.’
Kadhalika, Lema angeweza kabisa kusaka kuungwa mkono na Watanzania katika hoja yake ya ‘unafiki kuhusu posho za wabunge’ kwa kuwashawishi Watanzania (badala ya kumwandama Zitto) kuwa tatizo sio posho bali mantiki yake (yaani kuwajali wabunge na kuwapuuza watumishi wengine wa umma).
Vile vile Lema alipaswa kutambua kuwa ajenda zinazompa umaarufu Zitto sio kususia posho huko bungeni bali masuala muhimu zaidi kama kufuatilia mabilioni ya Watanzania yaliyoibwa na kufichwa huko Uswisi. Iwe Zitto amedhamiria kwa dhati ‘kufa na mafisadi wa mabilioni hayo’ au anatumia suala hilo kama mtaji tu wa kisiasa, ukweli unabaki kuwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa ‘kulainisha’ upinzani kwa kufanyia kazi hisia zao, kwa kucheza na kile wanachokithamini (stahili zao) na wanachokiogopa (ufisadi).”
Kwa Lema ku-“puuza matamanio ya wengine (walalahoi wanaotamani kuona Zitto anapambana na mafisadi), basi nao watampuuza (hasa kwa vile utetezi wowote kwa posho za wabunge unatafsiriwa kuwa ni usaliti kwa walalahoi).”
Huko nyuma, kiongozi mmoja wa vitengo vya CHADEMA aliniomba msaada wa kusaidia kukijenga chama hicho huku Ughaibuni. Niliafiki ombi hilo kwa vile ninaunga mkono ajenda za CHADEMA dhidi ya mafisadi. Hata hivyo ningefanya hivyo kama Mtanzania mwenye mapenzi kwa nchi yake lakini sio mwanachama wa chama hicho. Sijui hakupenda msimamo wangu au vipi, akapotea moja kwa moja.
Baadaye akajitokeza kijana mmoja aliyepo kwenye kitengo fulani nyeti cha chama hicho. Kwa kuridhishwa na utendaji kazi wake, nikatoa ‘ofa ya msaada wa kitaalamu.’ Nikampatia ‘jukumu fulani,’ na huo ndio ukawa mwisho wa mawasiliano yetu.
Mifano hiyo miwili, ukijumlisha na ushauri wangu kwa  Lema kumsihi asibandike ‘post’ ya kumkosoa kiongozi mwenzie wa CHADEMA (Zitto) mtandaoni kisha akapuuza, inanifanya nikitazame chama hicho kama ambacho aidha kinajiamini sana kiasi kwamba hakioni umuhimu kwa kujijenga au kinadhani kimekamilika katika nyanja zote kiasi kwamba misaada japo ya ushauri tu haina umuhimu kwake.
Nihitimishe makala hii kwa Kanuni nyingine ya Nguvu (5th Law of Power) inayotahadharisha “Kila kitu kinategemea hadhi yako: ilinde kwa nguvu zako zote maishani...Hadhi ni msingi wa nguvu. Hadhi peke yake inaweza kukufanya ushinde au uogopwe, lakini ikiponyoka itakudhoofisha na utaandamwa kila upande...” Kinachoendelea ndani ya CHADEMA sasa hivi sio tu kinakishushia hadhi chama hicho bali pia kinawafanya Watanzania walioanza kukiamini chama hicho wajione kama ‘wameingizwa mkenge’ (wamesalitiwa). Usipoziba ufa utajenga ukuta

- See more at: http://raiamwema.co.tz/mbunge-lema-mfuasi-wa-siasa-nyepesi#sthash.v91YhgAj.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube