TAMKO LANGU KWA UMMA JUU YA UZUSHI UNAOENEZWA DHIDI YANGU.

Ndugu wanahabari,

Baada ya kumshukuru na kumtukuza mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Natanguliza salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu mwanazuoni na mwanaharakati mwenzangu Dkt Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya Haki siku chache zilizopita huko Afrika ya kusini.

Ndugu zangu wanahabari,
Wengi mnanifahamu na kuifahamu vema historia yangu katika utendaji kazi na utumishi wa umma wa Watanzania. Nimekuwa nikiitumikia nchi yangu kwa kipindi kirefu katika Nyanja na sekta mbali mbali kuanzia Darasani mpaka kwenye siasa.

Kwa msingi huo, mimi Profesa Juma Kapuya, siku zote ninajikuta mwenye wajibu endelevu wa kuendelea kulitumikia Taifa langu kila siku mpaka kufikia mwisho wa Nguvu zangu.

Ndugu wanahabari,
Hivi karibuni nikiwa huku jimboni kuendelea na shuhuli za utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi kumezuka Tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yamgu zikiasisiwa na wanasiasa wenzangu wa ndani na nje ya chama changu ili kudhoofisha juhudi na utendaji wangu wa kila siku.

Tuhuma hizo zisizokuwa na kichwa wala miguu na pia kutokuwa na ukweli wowote, wamekuwa wakizitoa kwa kumtumia msichana anayedai amefanyiwa vitendo visivyofaa na mimi. Mimi simfahamu na sijui hizi shutuma zinatokea wapi.

Ndugu wanahabari,
Kwa tamko hili ninapenda kuwaambia kuwa nimefedheheshwa sana na uwezo mdogo wa kisiasa unaofanywa na hawa watu kwa kuwa dhamira yao haitatimia. Napenda niwakumbushe ndugu zangu kwamba tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na wapinzani wangu wameanza kunichafua ili nionekane sifai.

Ninapenda kuwaambia watanzania na wananchi wa jimbo langu kuwa wanatakiwa wazipuuze taarifa hizi kwa kuwa hazina ukweli wowote na kwamba ni za kutungwa zenye lengo la kunidharirisha na kuniondolea heshima yangu niliyojijengea kwenye jamii kwa kipindi kirefu sasa. Waswahili wanasema dawa ya mjinga ni kumpuuza.

Na hili linajidhihirisha zaidi kwa habari hii kuandikwa na chombo kimoja tu cha habari kinachotumiwa na chama kimoja cha siasa na baadhi ya wanasiasa wa chama changu wasiokitakia heri chama chetu, naomba kuwashukuru na kuwapongeza vyombo vingine vya habari kwa umakini wenu wa kuwa na nauelewa wa kutoandika kitu bila kukifanyia uchunguzi na kubaini ukweli ulivyo.

Chombo hiki cha habari kiliwahi kuripoti mwaka jana kuwa kuna mitambo imeingizwa nchini inayoweza kuandika ujumbe na kisha kuufanya uonekane umetoka kwenye namba Fulani, kwa kipindi kile sikuwaelewa, lakini sasa ninawaelewa na nimewaona kuwa wako sahihi na wao ndio waliouingiza mtambo huu na sasa wameamua kuutumia dhidi yangu kwa kutengeneza meseji na kuzihusianisha na mimi. Ninaamini ukweli utawaumbua muda si mrefu.

Ndugu wanahabari,
Nimeijenga heshima yangu na familia yangu kwa jamii yangu kwa kipindi kirefu mno, kwa hivyo siwezi kuruhusu heshima niliyoijenga kwa miongo kadhaa karibiwa na kupotezwa na watu wachache tena kwa muda mfupi namna hii.

Hivyo basi nimechukua hatua za kisheria kuhakikisha heshima yangu inaendelea kulindwa na utu wangu unaheshimiwa.

Nimemwagiza mwanasheria wangu afungue kesi na tayari amewashitaki watu wote wanaohusika kwenye mpango huu na tayari wameshapokea taarifa ya kuitwa mahakamani.

Nitaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaoendelea kutaka kujipatia umaarufu ama wa kisiasa au wowote ule kwa kutumia jina langu.

Hayo yote ni kwa kuzingatia ukweli kwamba nchi yetu inaendeshwa kwa misingi ya kisheria na kufuata na kuheshimu haki na wajibu wakila mmoja wetu.

Kwenye hilo ninawaambia ‘’janja yao nimeigundua, na hawatafanikiwa’’ 

Ninatoa Rai kwa yeyote mwenye kuona hilo jambo lina ukweli alipeleke kwenye vyombo husika ili lishuhulikiwe kwa mujibu wa sheria na sio kutumia vyombo vya habari kuchafuana.

Mwisho ninasisitiza kuwa nitaendelea kuilinda na kuitetea heshima yangu niliyojijengea kwa jamii kwa muda mrefu sasa na sitaruhusukuiona ikiharibiwa na wajanja wachache kwa maslahi yao binafsi. 

Tuendelee kuijenga nchi yetu, 

Mungu Ibariki Tanzania

Imetolewa leo tarehe 15.11.2013 nami
Prof. Juma A.Kapuya
Mbunge – urambo magharibi
S.L.P 45 Kaliua Tabora
Simu 0784993930