27 Dec 2013

NIANZE makala haya kwa kuomba radhi kutokana na kutoweza kuwaletea safu hii katika toleo la wiki iliyopita, kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Wiki iliyopita kulisikika kishindo kikubwa katika medani ya siasa za huko nyumbani, baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri wanne (japo mmoja alitangaza kuwa amejiuzulu).

Uamuzi huo wa Rais ni matokeo ya ripoti iliyosomwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika utekelezaji wa operesheni ya kupambana dhidi ya ujangili inayofahamika kama Operesheni Tokomeza Ujangili.

Mawaziri ambao ‘tunaambiwa kwa lugha ya kistaarabu kuwa nyadhifa zao zimetenguliwa’ (neno halisi ni kufukuzwa) ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki.

Hadi wakati ninaandaa makala haya bado kuna vuguvugu la kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, naye aachie ngazi kwa madai kuwa utendaji kazi wake hauridhishi. Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) ameanzisha jitihada za kukusanya saini kwa minajili ya kumng’oa Pinda, kwa kura ya kutokuwa na imani naye.Hata hivyo, hadi sasa waliotoa saini hizo ni wabunge wa Kambi ya Upinzani pekee ilhali wale wa chama tawala CCM wakionekana kusita ‘kumtosa’ mwana-CCM mwenzao.

Lengo la makala haya ni kujadili kwa undani kuhusu tukio hilo kubwa na pengine la kufungia mwaka huu 2013 unaoelekea ukingoni. Kwa upande mmoja, ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili ni hukumu nzito kwa vyombo vyetu vya habari (pengine sio vyote japo sina uhakika).

Katika nchi yenye ‘utitiri’ wa magazeti, rundo la blogu na idadi kubwa tu ya vituo vya redio na televisheni, iliwezekana vipi unyama uliofanywa na watekelezaji wa operesheni hiyo ukafanyika pasipo vyombo hivyo kuripoti?Huu sio tu uzembe bali pia ni sawa na usaliti wa ‘mhimili huo wa nne wa dola’ (Fourth Estate) kwa wananchi. Angalau vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali vinaweza kujitetea isivyostahili (unacceptable excuse) kuwa “mara nyingi haviripoti mabaya ya serikali na taasisi zake.”

Ninasema isivyostahili kwa sababu uendeshaji wa vyombo hivyo unategemea kodi za wananchi na kuegemea kwake kwa serikali kwa kila jambo hata kama ni baya ni kutowatendea haki wananchi na kodi wanayolipa.

Lakini vyombo vya habari binafsi havina utetezi wowote (labda kuhofia kufungiwa na serikali kwa madai ya uchochezi. Lakini sababu hiyo haina mashiko kutokana na ukweli kwamba hata kama chombo cha habari kingefungiwa baada ya kuripoti unyama ulioambatana na operesheni hiyo, tayari ukweli ungekuwa umefahamika kwa umma.

Binafsi, nadhani chanzo cha maovu yaliyoambatana na Operesheni Tokomeza Ujangili kutosikika katika vyombo vyetu vya habari ni shauku ya matukio hususan yanayohusu wanasiasa binafsi, badala ya utendaji kazi wao au taasisi wanazoongoza.

Kwa zaidi ya mwezi mzima, vyombo vingi vya habari huko nyumbani vimelowea kwenye mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kana kwamba suala hilo ni sehemu ya uhai wa kila Mtanzania.Japo natambua uzito wa habari zinazokihusu chama hicho kikuu cha upinzani, lakini kuna masuala mengine ya muhimu zaidi, kama hilo la Operesheni Tokomeza Ujangili, yanayopaswa kupewa umuhimu.

Hebu msomaji pata picha, laiti taarifa za maovu hayo zingeibuliwa mapema zingeokoa uhai wa watu wangapi kutokana na unyama ulioambatana na operesheni hiyo?

Lakini jambo jingine ni lile linalokwepwa kusemwa na wengi, uchovu katika utendaji kazi wa Rais Jakaya Kikwete. Ninatambua kwa kutamka ukweli huu bayana ninajijengea mazingira ya kuitwa msaliti, mwenye chuki kwa Rais, nisiye na nidhamu kwake, lakini ukweli sharti usemwe na kuuchukia ukweli hakuufanyi uwe uongo.

Kweli Pinda ni mchovu kiutendaji lakini kuna tunaoutafsiri uchovu wake kama ‘sponji’ linalonyonya uchovu wa bosi wake, yaani Rais Kikwete. Ni hivi, uamuzi mwingi wa Waziri Mkuu humshirikisha na huwa na ridhaa ya Rais. Vinginevyo, kama tunataka kuaminishwa kuwa tatizo ni Pinda pekee, basi Rais angeshamfukuza kazi.

Lakini huenda nafsi ya Kikwete ‘inamsuta’ kumwajibisha Pinda kwa vile anatambua kuwa Waziri Mkuu huyo anatekeleza maagizo yake (Rais Kikwete).

Ni rahisi kuwabebesha lawama mawaziri waliofukuzwa iwapo tutapuuza kanuni muhimu ya uwajibikaji wa pamoja serikalini. Je, mawaziri hao walishiriki katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili pasipo Rais kufahamu? Sitaki kuamini hivyo.Kimsingi, Rais hupewa taarifa kila siku kuhusu takriban kila jambo linaloendelea nchini. Sasa, vinginevyo waliokuwa wanampatia taarifa za utekelezaji wa Operesheni hiyo walikuwa wakimdanganya, basi kwa namna moja au nyingine naye anahusika.

Na hata tukiamini kuwa mawaziri hao ni wachovu kiutendaji, ukweli unabaki kuwa hawakujiteua wenyewe bali waliteuliwa na Rais kwa kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa iliyowafanyia uchunguzi (vetting). Na kama alivyoshauri mwanasiasa mkongwe Peter Kisumo kuhusu umuhimu wa ‘vetting’, ni muhimu kwa teuzi za viongozi wetu zikazingatia uwezo wao badala ya urafiki au fadhila za kisiasa.

Na kwa vile nimeitaja Idara ya Usalama wa Taifa, swali la msingi ni; je, walikuwa wapi wakati unyama ulioambatana na Operesheni Tokomeza Ujangili unaendelea? Kwa nini Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wawajibishwe lakini si waziri mwenye mamlaka na Idara hiyo (ambaye kimsingi ni Rais mwenyewe)?

Naomba ieleweke kuwa hapa sijengi hoja ya kutaka Rais awajibishwe. Badala yake, ninapanua mtazamo kuhusu suala hili na kuepusha uwezekano wa “kutoa majibu mepesi kwenye maswali magumu,” ugonjwa unaoisumbua Tanzania yetu kwa muda mrefu.

Ni muhimu kujiuliza tutaendelea kushuhudia mabadiliko ya mawaziri hadi lini. Na ni muhimu pia kutambua kuwa mabadiliko hayo yana gharama kubwa iliyofichika hasa ikizingatiwa kuwa stahili za viongozi wetu haziendani na hali ngumu ya uchumi wetu.

Ni rahisi kukenua meno kwa furaha baada ya kusikia mawaziri wanne wamefukuzwa pasipo kutambua kiasi gani cha fedha za mlipakodi kitatumika sambamba na hatua hiyo.

Lakini jingine ambalo pia aidha linapuuzwa au kukwepwa ni ukubwa wa Baraza la Mawaziri. Ni ukweli usiopingika kuwa fukuza fukuza hii ya mawaziri katika utawala wa Kikwete ni uthibitisho mmojawapo kwamba kuwa na rundo la mawaziri hakumaanishi ufanisi katika kazi.Busara kidogo tu yatosha kutujulisha kuwa wingi wa idadi ya mawaziri wasiojua kwa nini wamepewa uwaziri ni sawa na kutokuwa na mawaziri kabisa.

Mwisho, ninaomba nimalizie makala hii kwa kukumbusha kuwa maovu yaliyofanywa katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili ni uhalifu.Ni matarajio yangu kuwa kufukuzwa kwa mawaziri hao ni hatua ya kwanza tu na hatimaye sheria itachukua mkondo wake.

Katika hili ninatoa changamoto kwa taasisi za kutetea haki za binadamu, ndani na nje ya nchi kuhakikisha haki inatendeka kwa wahanga wa operesheni hiyo kwa kuwafikisha wahusika wote mahakamani (hata Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - ICC).

Mwisho, nimenong’onezwa kuwa kilichojiri katika Operesheni Tokomeza Ujangili ni kidogo mno kulinganisha na yanayotokea katika Operesheni Kimbunga inayoshughulikia wahamiaji haramu.Natoa wito kwa watu na taasisi mbalimbali kutupia macho katika operesheni hiyo ninayoambiwa inaambatana na rushwa, unyanyasaji wa kijinsia na kibinadamu na ubaguzi mbaya zaidi ya ule aliopambana nao Nelson Mandela katika zama za utawala wa makaburu nchini Afrika Kusini.

Heri na baraka ya Sikukuu ya Krismasi


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube