13 Dec 2013



KATIKA simulizi za Biblia Takatifu, mara baada ya Yesu Kristo kufariki msalabani pazia la hekalu lilipasuka vipande viwili, nchi ikatetemeka, miamba ikapasuka na makaburi yakafunguka. Askari waliokuwa wanamlinda wakakiri kuwa "kwa hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu." Niliyakumbuka maneno haya mara baada ya kupatikana taarifa za kifo cha Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, Nelson Mandela.
Habari za kifo cha Mandela sio tu zilikuwa za kushtusha licha ya ukweli kwamba afya yake ilikuwa imedhoofika kitambo, lakini pia ziligusa hisia za watu wengi duniani kote. Nilikesha takriban usiku mzima baada ya taarifa hiyo na vituo vyote vikubwa vya televisheni duniani vilikatiza matangazo ya kawaida na kuonyesha 'breaking news' ya kifo cha Mandela.
Ninaomba kukiri kuwa japo nilikuwa ninampenda na kumheshimu Mandela, lakini nimetambua zaidi ukubwa wa upendo na heshima hiyo baada ya kifo chake. Pengine ni kwa vile vyombo vya habari vimekuwa vikitumia muda mwingi kumzungumzia, lakini kikubwa zaidi kwangu ni kupata wasaa kupitia busara mbalimbali za mwanasiasa huyo mahiri duniani.
Nukuu yangu kutoka katika Biblia hailengi kumlinganisha Mandela na Yesu Kristo.
Na pia maana ya nukuu ifuatayo ya kiongozi huyo haimaanishi kwa namna yoyote mie kujilinganisha na 'Madiba';  "I was made, by the law, a criminal, not because of what I had done, but because of what I stood for, because of what I thought, because of my conscience" (tafsiri isiyo rasmi, sheria iliniona mhalifu sio kwa sababu ya nilichofanya bali nilichosimamia, nilichoamini na utashi wangu). Nukuu hii ni maneno ya Mandela wakati wa kesi aliyofunguliwa na utawala dhalimu wa makaburu mwaka 1962.
Kwa nini nukuu hii inanigusa sana? Binafsi ninajiona kama mwathirika wa kutumia haki zangu za kibinadamu na kikatiba kuwa na msimamo katika masuala fulani, kuamini katika msimamo huo, na utashi unaoniongoza katika msimamo huo. Kwa bahati mbaya, kama ilivyokuwa kwa Mandela huko Afrika Kusini, msimamo pekee unaokubalika kwa tawala dhalimu ni ule unaoendana na mtizamo wao, hata kama sio sahihi.
Kwa yeyote atakayesimama kupambana na udhalimu, basi na awe tayari kukumbana na nguvu kinzani dhidi ya mapambano hayo. Mandela alidhamiria kupambana na mfumo dhalimu uliowabagua watu kwa asili ya rangi zao, na hakuishia katika kudhamiria tu bali alitafsiri dhamira hiyo katika vitendo.
Ni muhimu kutambua kuwa mapambano dhidi ya mfumo dhalimu wa kikaburu yalikuwa mithili ya tembo na sisimizi. Makaburu licha ya kuwa watawala, walikuwa na kila nyenzo dhidi ya wapigania uhuru. Lakini licha ya 'faida' hizo kwa utawala huo wa kibaguzi, moja ya nyenzo zake muhimu za kiutawala ilikuwa matumizi ya nguvu na ubabe wa hali ya juu, na maelfu ya raia wasio na hatia waliuawa au kujeruhiwa katika mapambano ya kudai haki na uhuru.
Huu ni wakati wa maombolezo ya mwana-Afrika muhimu, ambaye wakati huu ninapoandaa makala hii, anatarajiwa kuagwa na idadi ya kihistoria ya viongozi wa dunia. Kwa mfano wakati Marekani inawakilishwa na Rais Barack Obama na marais wastaafu George W Bush, Bill Clinton na Jimmy Carter, Uingereza inawakilishwa na Waziri Mkuu David Cameron na watangulizi wake Gordon Brown, Tony Blair na John Major. Viongozi hao muhimu duniani watajumuika na waombolezaji wanaotarajiwa kufikia 80, 000.
Lakini kama ambavyo mara kadhaa tumekuwa tukinyoosheana vidole kuhusu unafiki wa baadhi ya viongozi wetu katika kumwenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Mandela, itakuwa ni unafiki mwingine kumlilia Mandela bila kuzingatia kazi yake kubwa aliyoifanya kwa Waafrika Kusini na dunia kwa ujumla.
Machozi tunayotoa kumlilia Mandela yatakuwa kazi bure kama hatutounga mkono imani yake kuwa hakuna fursa ya aina yoyote kwa mwanadamu kubaguliwa na mwanadamu mwenzake au mfumo.
Lakini pengine kubwa zaidi kutokana na kifo cha Mandela ni changamoto kwa wanasiasa na viongozi wetu katika nyanja mbalimbali, iwe kisiasa, kidini na kijamii. Hivi wakati tunashuhudia takriban dunia nzima ikimlilia Mandela, je siku ya kifo chako utakumbukwa kwa lipi, iwe ni katika ngazi ya mtaa, wilaya, mkoa, taifa au hata kimataifa? Sababu kuu ya dunia kumuenzi Mandela sio tabasamu lake la kudumu usoni mwake bali kuwa mfano hai hata katika udhalimu mkubwa kiasi gani, haki inaweza kupatikana palipo nia thabiti.
Kuna changamoto nyingine muhimu kwa Watanzania hasa baada ya maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru wetu Jumatatu iliyopita. Je uhuru wetu unaendana na uhuru halisi aliopigania Nelson Mandela na hatimaye kufanikiwa kuuangusha utawala dhalimu wa makaburu? Je, miaka 52 ya uhuru wetu imefanikiwa kuondoa 'ukaburu' kati ya walio nacho isivyo halali na wasio nacho isivyo halali? Je, rasilimali za taifa letu hazifuati 'ukaburu wa kiuchumi' kwa kunufaisha wachache badala ya kila mmoja wetu?
Naomba nihitimishe makala hii kwa kukiri kwamba nimepata wakati mgumu sana kuiandaa. Ni vigumu kuomboleza kifo cha mtu muhimu kama Mandela, na ni kama jambo lisilowezekana kumuenzi kwa makala fupi kama hii. Kwa upande mwingine ninamuaga Mandela kwa maneno haya: "….ulikuwa mtu mwema uliyeamini katika haki na usawa wa binadamu. Dunia itakukumbuka kwa jitihada zako. Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi, Amina"
KWAHERI NELSON MANDELA


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.