28 Feb 2014

HUYU naye vipi? Mhasibu mzima anapenda basi la wafanyakazi! Hana japo pikipiki na bado anaishi nyumba ya kupanga. Ama kweli kwenye miti hakuna wajenzi...”.  Hii ilikuwa kauli ya mfanyakazi mwenzangu wakati nilipokuwa mwajiriwa wa taasisi moja ya umma huko nyumbani.
Mhasibu aliyekuwa akiongelewa ni kijana mmoja ambaye baada ya kuhitimu masomo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kurejea kazini alipandishwa cheo katika idara ya uhasibu katika taasisi hiyo. Yayumkinika kuhitimisha kuwa miezi kadhaa ya mwanzo baada ya kuwa mhasibu, kijana huyo aliandamwa sana na wengi wa wafanyakazi wenzake, ‘kosa’ lake pekee likiwa ‘kuishia maisha ya kawaida kulingana na kipato chake.’
Tofauti na kijana huyo, katika taasisi hiyo kulikuwa na jamaa mmoja ambaye japo hakuwa mhasibu kitaaluma, ndiye aliyekuwa na jukumu la usimamizi wa fungu la fedha kwa ajili ya matumizi ya mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, hususan safari za nje ya nchi. Sehemu kubwa ya fedha alizokuwa akisimamia ndugu huyo zilikuwa za kigeni.
Huyu bwana alikuwa na uwezo mkubwa mno kifedha japo mshahara wake ulikuwa wa ‘kawaida’ tu. Alikuwa na misururu ya magari ya thamani huku ikidaiwa kuwa alikuwa na idadi kubwa ya nyumba jijini Dar es Salaam. Mfanyakazi huyu alikuwa akinyenyekewa hata na baadhi ya mabosi wake.
Baada ya muda, inaelekea huyo mhasibu kijana alizidiwa na kebehi dhidi yake, na akaanza ‘kuishi kihasibu,’ na taarifa zilizopatikana zilionyesha kuwa alianza kununua nyumba, magari na hata matumizi yake yalibadilika yakawa makubwa. Na sifa zikaanza kumiminika kwake, na kama ilivyokuwa kwa yule ‘mhasibu’ wa mkurugenzi mkuu, naye akaanza kunyenyekewa.
Ninakumbuka kuhusu ‘kituko’ hiki kwa vile kilitokea mbele ya macho yangu katika taasisi niliyokuwa nimeajiriwa. Lakini kimsingi hali hiyo ilikuwa kama ya kawaida kwenye taasisi nyingi tu, za umma na za binafsi.
Huo ndio ‘ukweli mchungu’ kuhusu Tanzania yetu. Mhasibu atakayeishi kulingana na kipato chake (na mishahara ya wahasibu wengi ni ya kawaida kwa vile uhasibu si ‘fani adimu’- rare profession- kama urubani yenye mshahara mkubwa.
Huko mitaani hali ni mbaya zaidi ambapo wahalifu wanatukuzwa; wauza madawa ya kulevya wamepachikwa ‘uzungu’ na kuitwa ‘wazungu wa unga.’ Wananyenyekewa kama miungu-watu. Kwa hakika Tanzania yetu inaweza kuwa sehemu muafaka ya kuthibitisha ule msemo wa Kiingereza kuwa crime pays (uhalifu unalipa).
Utakutana na mtu ambaye hana shughuli ya kueleweka lakini ana fedha nyingi mno; hajaachiwa urithi mkubwa, hajawahi kushinda bahati nasibu, na kubwa zaidi hana kazi wala biashara ya kueleweka. Uwezekano pekee wa ‘utajiri’ wa mtu huyu ni kujihusisha na uhalifu kwa sababu fedha hazianguki kutoka hewani kiasi cha kuwa na mtu mwenye fedha nyingi lakini hana chanzo cha mapato.
Nikirejea kwenye uzoefu wangu huko nyumbani, kuna wakati niliwahi kufanya kazi na watumishi wa chombo kimoja cha dola (yaani kazi iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya chombo hicho na taasisi niliyokuwa nikiitumikia wakati huo). Hali huko ilikuwa mbaya zaidi ambapo mtendaji aliyechukia rushwa alionekana kama adui wa watendaji wenzie.
Kisingizio kikubwa kilikuwa maslahi madogo na mazingira magumu ya kazi. Nilichojifunza kwao ni kwamba ilikuwa vigumu sana kuwa mzalendo katika chombo hicho cha dola kwa sababu rushwa ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya watumishi wake.
Mara nyingi tumekuwa tukiilaumu serikali na taasisi zake, wanasiasa na watawala wetu kuhusu kuporomoka kwa uadilifu sambamba na kushamiri kwa uhalifu. Lakini pengine mara nyingi zaidi ni nadra kwetu kama wananchi kujiuliza kuhusu nafasi zetu kupambana na au kuchochea kuporomoka huko kwa maadili na kushamiri kwa uhalifu. Ni vigumu kuuchukia uhalifu, kwa mfano, ilhali ndoto zako ni kuishi maisha ya kifahari kama anavyoishi mhalifu fulani.
Ninaambiwa kwamba baadhi ya wahalifu huko nyumbani wamekuwa na nguvu kubwa zaidi ya watawala wetu kiasi kwamba vyombo vya dola vinaogopa kuwagusa wahalifu hao. Na bahati nzuri kwao, baadhi yao wamefanikiwa kujenga ushirikiano na watu wa karibu wa familia za watawala wetu ambao wanatumiwa na wahalifu hao kama kinga dhidi ya hatua za kisheria.
Sasa kama katika hali inayokera na kukatisha tamaa tunaelekea kuruhusu na kuhalalisha upatikanaji kipato kwa njia zisizo halali, na kisha kuwaabudu wahalifu kana kwamba ni miungu-watu na kuwaenzi kwa ‘nyadhifa kama ‘mzungu wa unga’ au ‘pedejee,’ kwanini tunatahayari kusikia taarifa kwamba wajumbe wengi wa Bunge la Katiba wanalalamika kuwa posho ya shilingi 300,000 kwa siku haitoshi?
Hivi katika mazingira ya kawaida tu, tutarajie lipi kwa mjumbe wa Bunge la Katiba aliyeteuliwa na Rais  ‘anapogusana mabega’ (rubbing shoulders) na wajumbe walioingia katika Bunge hilo kama wabunge ‘wa kawaida’ wanaolipwa zaidi ya shilingi milioni 10 kwa mwezi?
Kwamba kama serikali ina uwezo na jeuri ya kulipa mamilioni hayo kwa wabunge zaidi ya 300 kila mwezi kwa miaka mitano, kwanini basi nao wasidai japo ‘kipande kiduchu cha keki hiyo ya taifa’?
Naomba ieleweke bayana kwamba si kuwa ninaafiki madai ya wajumbe hao wa Bunge la Katiba wanaodai waongezewe posho, bali ninachojaribu kubainisha hapa ni ukweli kwamba kelele za wajumbe hao zinaakisi hali halisi huko mtaani. Kama ni sahihi kwa wahalifu kuenziwa huko mtaani, kwanini basi ‘waheshimiwa hawa wa muda mfupi’ wasitumie fursa hiyo kujinufaisha?
Nchi yetu imekuwa kama msitu (jungle) ambapo kanuni pekee inayotawala ni ubabe: kula au uliwe. Na katika mazingira ya namna hiyo ni vigumu kweli kwa uzalendo au wazalendo kusalimika. Ndiyo maana niliposikia jina la mwanadada mzalendo, Maria Sarungi, kuwa miongoni mwa wajumbe walioteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba nilitamani kungekuwa na angalau makumi kadhaa ya watu kama yeye.
Simsifii bali mwanadada huyu amekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya mtandaoni inayoitwa 'Badili Tanzania' (Change Tanzania), ambayo kimsingi inahimiza mabadiliko ya kifikra, kitabia na vitendo kwa jamii badala ya kutilia maanani kuwategemea wanasiasa au taasisi za kisiasa kuleta mabadiliko chanya kwa nchi yetu.
Ikumbukwe kuwa kati ya mafanikio makubwa ya kampeni ya Change Tanzania ni kupinga ongezeko la kodi kwa kadi za simu (SIM card tax) ambapo hatimaye ilifutwa baada ya kilio cha umma kupitia kampeni hiyo kusikika kwa watawala.
Alipotajwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba sikumpongeza, na hadi leo sijatoa pongezi zangu kwake. Sababu kubwa ya kuhifadhi pongezi zangu ni kwamba yeye ni mithili ya mwanasoka bora ambaye kwa hakika ni lazima achaguliwe katika timu ya taifa. Na tunapoongelea soka, kuna mfano mzuri hapa: mwanasoka Mtaliano Mweusi, Mario Balotelli, aliwahi kunukuliwa akisema kwamba anapofunga bao huwa hashangilii kwa sababu hiyo ni kazi yake. Na akasema ‘umeona wapi msambazaji barua wa posta anashangilia anapofikisha barua kwa mhusika? Huwezi kumshangilia kutimiza jukumu lake.”
Bunge la Katiba lilipaswa kuundwa na wazalendo wanaofikiria hatma ya taifa letu na si ‘nani atalipwa ada ya mwanangu wakati ninashughulikia mchakato wa Katiba mpya’ au wanaodhani posho ya ujumbe wa Bunge la Katiba ni fursa ya kuwabadilishia maisha yao (iwe kuwaongezea fedha au kuongeza idadi ya nyumba ndogo).
Tumeruhusu ‘uhuni’ katika shughuli hiyo muhimu kwa hatma ya taifa letu, na ndiyo maana tunashuhudia mtu kama Emmanuel Makaidi akigeuza mchakato wa kupata Katiba mpya kuwa fursa ya kiuchumi kwa familia yake kwa kumteua mke wake kuwa mjumbe mwenza katika Bunge hilo.
Bunge la Katiba lilihitaji akina Maria Sarungi wengi, yaani watu ambao historia ‘inawapendelea’ (kwa maana kwamba kuna mifano hai ya uchungu wao kwa Watanzania wenzao)’.  Bunge hilo halikustahili kuwa fursa kwa wababaishaji wanaodai eti waongezewe posho kwa vile wameambatana na wanasheria wa kuwashauri wakati wa mjadala wa Katiba mpya.
Kwa vile uteuzi wa wajumbe wa Bunge hilo haukufanywa kwa mtutu wa bunduki kuwa ‘lazima uwe mjumbe hata kama posho haitoshi’ ni vema kwa wanaodhani posho haitoshi wakajiuzulu na kurejea makwao.
Nimalizie makala hii kwa kuwaasa Watanzania wenzangu kujiandaa kisaikolojia kupokea Katiba mpya ‘fyongo au ‘bomu’ kwa sababu wengi wa wanaotuwakilisha katika mchakato wa kupata Katiba hiyo wapo huko Dodoma kwa maslahi yao binafsi. Yayumkinika kuhisi kwamba mjadala wa Katiba huo utakuwa mrefu, si kwa minajili ya kupata muafaka wenye maslahi kwa taifa bali ukweli kwamba urefu wa mjadala utamaanisha urefu wa posho pia.
Ningetamani sana kuhitimisha makala hii na ‘pendekezo la maana’ lakini nafsi inanisuta: ukipanda upupu shambani kamwe usitarajie kuvuna maharagwe.' Kinachojiri katika Bunge la Katiba Dodoma kinaakisi kinachojiri katika maisha yetu ya kila siku mtaani, na tusipoamua kwa dhati kubadili mtizamo wetu dhidi ya ‘wazungu wa unga’ na ‘mapedejee’ basi tusitarajie miujiza kwa watu wanaoteuliwa katika ‘nafasi za ulaji’ kama ujumbe wa Bunge la Katiba.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube