28 Mar 2014

 
 “HIVI ujumbe aliotoa Rais Jakaya Kikwete alipohutubia Bunge la Katiba Ijumaa ulikuwa wa Rais? Mwenyekiti wa CCM? Mtanganyika au Mtanzania wa kawaida?”,  niliuliza swali hili katika mtandao mmoja wa kijamii baada ya kuchanganywa na hotuba hiyo.
Lakini siku chache baadaye, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, ‘alijibu’ swali hilo kwa namna fulani. Akizungumza na moja ya magazeti ya huko nyumbani, Salva aliushutumu Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kile alichoeleza kuwa ni kuendeleza propaganda, na kubainisha kuwa “Rais kama Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake.
Wakati ninakubaliana na maelezo hayo, sote tunafahamu kuwa shughuli iliyompeleka Rais Kikwete katika Bunge hilo la Katiba ni kulizindua, si kutoa maoni yake. Ninaamini kwamba kama ilivyokuwa kwa Watanzania wengine, Rais alikwishakupewa nafasi ya kutoa maoni yake huko nyuma, na hakukuwa na haja ya kutumia tukio hilo la uzinduzi wa Bunge la Katiba ‘kutoa tena’ maoni yake.
Kwa upande mwingine, binafsi sikushangazwa na msimamo wa Rais Kikwete hususan kwenye hoja ya muundo wa Muungano. Kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya, Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho tawala aliweka bayana msimamo wa CCM kuwa ni muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Sasa kwanini ilitarajiwa kwamba angebadili msimamo siku ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba?  Ni muhimu pia kukumbuka kwamba wazo lenyewe la mabadiliko ya Katiba halikuanzia CCM (angalau kipindi hiki, na tukiweka kando harakati za ndani ya CCM kama zile za kundi la G55) bali kwa vyama vya upinzani hususan, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kuna baadhi ya wachambuzi wanaokwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa hata huko kwa wapinzani kulikoanzia wazo hilo la Katiba mpya, msukumo ulikuwa zaidi katika mazingira ya chaguzi, hususan Uchaguzi Mkuu, baada ya kuonekana bayana kwamba Katiba iliyopo inatengeneza mazingira magumu ya ushindani halisi wa kisiasa (au kwa lugha nyingine, ni vigumu mno kukiondoa chama tawala madarakani katika mazingira ya Katiba iliyopo).
Mara kadhaa huko nyuma nimebainisha msimamo wangu kuhusu suala la Katiba mpya. Japo ninaafiki kwamba Katiba tuliyonayo ina mapungufu ya kutosha na kuna umuhimu mkubwa wa kuibadilisha, ninapata shida sana kuona jinsi kuja kwa Katiba mpya kutakavyoweza kumsaidia Mtanzania wa kawaida anayeandamwa na umasikini unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ufisadi.
Tatizo jingine linaloninyima shauku ya kuona Katiba mpya inapatikana ni ukweli mchungu kwamba kwa kiasi kikubwa tatizo linaloikabili nchi yetu si ukosefu wa sheria bali usimamizi na utekelezaji wake. Hivi tumewahi kujiuliza kwamba kama sheria zilizomo kwenye Katiba iliyopo (na ni muhimu kutambua kuwa Katiba ni ‘sheria mama’) hazisimamiwi ipasavyo na kupuuzwa mara kadhaa, kuna mwamana (guarantee) gani kwamba sheria zitakazokuwemo katika Katiba mpya zitaheshimiwa?
Kati ya sababu za msingi zinazochangia kero za Muungano ni hiyohiyo ya kupuuza sheria. Wakati Rais Kikwete anahubiri faida za Muungano wa serikali mbili, alishindwa kabisa kukemea uvunjifu wa sheria (Katiba) ulioruhusu Zanzibar kujipa hadhi ya nchi ndani ya nchi. Kwa makusudi, mjadala kuhusu muundo wa Muungano unakwepa kujadili Marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ambayo hayakuingizwa kwenye Katiba ya Muungano.
Uvunjifu huo wa Katiba kwa maana ya kuruhusu kuundwa kwa nchi yenye Rais wake, bendera yake, wimbo wake wa Taifa, Katiba yake, nk (Zanzibar) ndani ya nchi nyingine (Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania) ulifanyika wakati wa utawala wa Rais huyuhuyu tuliyenae sasa (Jakaya Kikwete), na si yeye wala washauri wake, kwa mfano ‘wakereketwa wa Muungano kama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, waliodiriki kukemea jambo hilo.
Japo binafsi sipingi wala siungi mkono muundo wa Muungano wa serikali mbili au tatu (au hata wa serikali moja) kwa sababu kwangu cha muhimu ni function (kazi) na sio form (muundo), kinachofanyika sasa kwa kung’ang’ania muundo wa serikali mbili uliogubikwa na matatizo yanayoweza kuepukika ni kuahirisha tu tatizo. Ni wazi tatizo hilo litarejea kwani busara zinaeleza kwamba haiwezekani kuua wazo ‘lililoiva’ (you can’t kill an idea whose time has come).
Hatuwezi kutatua tatizo kwa kuficha tatizo jingine. Katika mazingira ya kawaida tu, ilipaswa mjadala kuhusu muundo wa Muungano uambatane na kuwekwa wazi kwa nyaraka zilizounda Muungano huo (Articles of the Union) ambazo zimeendelea kufanywa siri kubwa.
Hata kwa sisi tusiohangaishwa sana na muundo wa Muungano tunadhani kwamba pengine chanzo kikubwa cha ‘kelele zisizoisha’ kuhusu Muungano ni ukweli kwamba waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Julius Nyerere na  Sheikh Abeid Karume, walifikia mwafaka wa kuunganisha nchi hizo kana kwamba yalikuwa makubaliano ya watu binafsi na si ya wananchi wote wa nchi hizo mbili. Sina hakika ni Watanganyika na Wazanzibari wangapi waliopewa fursa ya kuafiki au kupinga suala hilo la Muungano.
Na kama alivyofanya Rais Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba, uhai wa Muungano umeendelea kutegemea zaidi kuogopana, hadaa na vitisho (hususan ile ya takriban kila Rais kudai hayupo tayari Muungano uvunjike mikononi mwake).
Muungano katika muundo wake wa serikali mbili unaweza tu kusalimika iwapo matatizo yanayoukabili yatajadiliwa kwa uwazi pasi kuchelea matokeo ya kufanya hivyo. Iwapo kuujadili Muungano kwa uwazi kutasababisha uvunjike-alimradi kwa amani-basi na iwe hivyo. Iwapo kuujadili kwa uwazi kutauimarisha (na hii ndio njia mwafaka) basi tusipoteze muda na tufanye hivyo sasa.
Ni kichekesho kwa chama tawala CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, kujaribu kuuhadaa umma kuhusu utatuzi wa matatizo ya Muungano ilhali kimsingi kinachofanyika ni ‘kuvuta muda’ (buying time) pasipo jitihada zozote za makusudi kufanyika kuimarisha Muungano huo.
Kama tunataka tuwe na Muungano wenye maana halisi ya muungano basi ni muhimu kwa kila raia wa nchi hizi mbili ajisikie huru awapo upande wowote wa Muungano. Vilio vya Watanzania Bara kwamba wanapokuwa Zanzibar wanajiona kama ‘raia wa kigeni’ visipuuzwe, kwa sababu ni vitu kama hivi vinavyoweza kuzua ‘muundo wa lazima’ wa Muungano pasi kujali vitisho vya watawala.
Nihitimishe makala hii kwa kukumbushia kwamba muundo wa Muungano ni kimoja tu kati ya vipengele vingi vilivyomo kwenye Rasimu ya Katiba mpya. Ni muhimu pia kutambua kuwa matatizo ya msingi yanayoikabili nchi yetu- kwa mfano umasikini wa kupindukia na ufisadi unaoshamiri kwa kasi- hayatokani na muundo wa Muungano wa serikali mbili na pengine hata muundo wa Muungano wa serikali tatu hauwezi kuyatatua.
Wakati Watanzania wakitafakari na kujadili hotuba ya Rais Kikwete, baadhi ya magazeti mwanzoni mwa wiki hii yaliripoti taarifa za kigogo mmoja wa Ikulu kufanya jitihada ya kumtoa rumande mmoja wa wafanyabiashara watuhumiwa wakubwa wa madawa ya kulevya anayeshikiliwa na polisi huko Lindi. Je muundo wa Muungano unashughulikia vipi uhuni wa aina hii?
Masuala kama utawala bora, haki za makundi ‘ya wanyonge’ (vulnerable groups), haki za huduma muhimu kama afya, elimu, nishati, na habari yana umuhimu mkubwa pengine zaidi ya aina ya Muungano tunaotaka.
Ndiyo maana nimeeleza hapo juu kwamba la muhimu zaidi kwangu ni function(s) na si form(s) za serikali kama taasisi inayoongoza nchi.
Kuwa na serikali mbili, au serikali tatu, au serikali moja kuna faida tu kwa mwananchi kama kunamwezesha kujipatia mahitaji yake muhimu kwa haki na kumfanya ajione ‘mdau halisi’ wa nchi husika. Vinginevyo, badala ya serikali 2, 3 au 1, kwa mwananchi huyo asiye na uhakika wa mlo wake ujao na ambaye ustawi wake unatarajia kudra za Mwenyezi Mungu, anachoona ni kama kuna serikali 0.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.