18 Apr 2014

NIANZE kwa kutoa pole kwa Watanzania kwa janga la mafuriko ambalo linaendelea kusababisha madhara makubwa katika maeneo mbalimbali huko nyumbani.
Japo taarifa zinazosikika zaidi kuhusu mafuriko hayo ni za hali ilivyo Jijini Dar es Salaam, taarifa zinaonyesha kuwa janga hilo linaendelea kusababisha madhara katika sehemu nyingine mbalimbali za nchi yetu.
Kwa vile Taifa bado lipo katika kipindi cha majonzi kufuatia wenzetu kadhaa waliokwishapoteza maisha kutokana na mafuriko hayo, sambamba na maelfu waliopoteza mali zao, inaweza kuwa si wakati mwafaka sana kuanza kunyoosheana vidole. Hata hivyo, kituko kimoja kilichojitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita kinaleta haja ya kuwekana sawa wakati tunakabiliana na janga hili.
Jumamosi iliyopita, kulipatikana taarifa iliyoambatana na picha inayomwonyesha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, akiwasili mjini Mwanza kwa shughuli za kichama. Ikumbukwe kwamba siku hiyo hali ilikuwa mbaya sana Jijini Dar es Salaam kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kuonyesha sehemu mbalimbali huko nyumbani.
Ili kukupa mlolongo sahihi wa matukio, naomba ninukuu kauli husika kuhusiana na tukio hilo. Awali, kutokana na kushangazwa na uwepo wa Meya Silaa jijini Mwanza huku wananchi wake wakikabiliwa na janga la mafuriko, nilibandika picha iliyoambatana na maelezo
Meya wa Ilala Jerry Silaa katika shughuli za kichama muda huu huko Mwanza,” na kuuliza “Mheshimiwa, una taarifa za mafuriko Dar?” Kisha nikaandika tena, “Hawa ndio viongozi wenu. Manispaa ya Ilala ipo katika mafuriko, Meya wa Ilala Jerry Silaa yupo kichama Mwanza.
Baada ya muda mfupi, Meya Silaa alijibu, namnukuu,
Nakuomba radhi kama ungependa niwe Dar nikizuwia mvua isinyeshe.” Kisha akaandika tena “I hate cheap politics (nachukia ‘siasa nyepesi’). Mabonde yote yamejengwa. Mnategemea mito itapumulia wapi? I have remarkable record kwenye rescue missions (nina rekodi ya kupigiwa mfano kwenye jitihada za uokoaji.)” Lakini hakuishia hapo, akaendelea kudai kwamba, “Kwangu wahanga (wa mafuriko) ni kwa wanaoathirika kwa madaraja kukatika iliyosababishwa na watu kujenga mabondeni.” Na katika ‘kuhitimisha’ mjadala huo, Meya Silaa akatoa tuhuma kwamba “Najua viongozi wengi huwa wanaombea watu hata wafe wakabebe jeneza kuonekana wanajali lakini ni unafiki.”
Naomba niweke wazi ya kuwa sina tatizo na Meya Silaa binafsi ila kwa hakika kauli zake zilizosheheni dharau na kiburi zilinikera sana. Na si mimi pekee bali Watanzania kadhaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii pia walishutumu kauli za kiongozi huyo wa Manispaa ya Ilala.
Hata hivyo, pamoja na ushauri wa wengi kwamba hata kama hakuwa na nia mbaya katika kauli hizo basi labda aombe radhi, Mheshimiwa huyo alipuuzia ushauri huo. Mie ni muumini mkubwa wa uhuru wa kujieleza. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba uhuru pasi nidhamu ni uhuni. Japo kila kiongozi ana uhuru wa kujieleza kama mwananchi yeyote yule, uhuru huo unaambatana na wajibu wa kiongozi husika kwa umma.
Kwa busara za kawaida tu, shughuli za kichama zilizompeleka Meya Silaa huko Mwanza hazikuwa na uzito mkubwa zaidi ya janga la mafuriko Jijini Dar es Salaam ambapo manispaa ya mheshimiwa huyo ilikuwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa sana.
Lakini busara zaidi zingeweza kutumika baada ya mheshimiwa kutambua kuwa suala hilo limezua hisia hasi miongoni mwa wananchi, na angeweza kujibu kistaarabu tu, kwa mfano, “ninatarajia kurejea Dar es Salaam  haraka kushirikiana na wananchi wenzangu katika janga hili” badala ya kauli ya kebehi kuwa ‘anaomba radhi kwa anayependa awepo Dar es Salaam  kuzuwia mvua isinyeshe.’
Hivi Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara ya maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mafuriko hayo alifanya hivyo ili kuzuwia mvua au mafuriko hayo? Na je Makamu wa Rais Dk. Bilal na viongozi wengineo walionusurika katika ajali ya helikopta wakati wakitaka kuanza ukaguzi wa athari za maafa ya mafuriko walitarajia wangezuwia mafuriko hayo?
Ninaamini Meya Silaa anafahamu fika kwamba tunapokwenda kuwajulia hali wagonjwa haimaanishi kuwa tutawaponyesha, tunapokwenda misibani haimaanishi kuwa tutawafufua marehemu. Kumjulia hali mgonjwa au kujumuika msibani ni ustaarabu tuliyojijengea katika mila zetu kuonyesha kuwa TUNAJALI. Na kisaikolojia inaonyesha kuwa mhanga wa tukio lolote lile hupata faraja pindi anapotambua kuwa kuna wanaomjali.
Katika moja ya majibu yangu kwake, nilimfahamisha bayana Meya Silaa kwamba tatizo kubwa la wengi wa viongozi wetu ni kuzowea kusifiwa tu lakini wakikosolewa hukimbilia kudai ni ‘cheap politics.’
Waingereza wanasema “wrong is just that, wrong” (kisicho sahihi kipo hivyo hivyo, hakipo sahihi). Kiongozi kuzipa kipaumbele shughuli za kichama ilhali wananchi wanahangaika na janga la mafuriko si sahihi, na hakuna excuse katika mazingira ya aina hiyo.
Japo Meya Silaa anaweza kuwa sahihi kulaumu ujenzi wa mabondeni kama moja ya sababu zinazochangia mafuriko, lakini kwa hakika mamlaka husika kwa mfano Manispaa ya Ilala inayoongozwa na Meya Silaa zinahusika kwa namna moja au nyingine. Kuwalaumu tu wakazi wa mabondeni hakuwezi kuleta ufumbuzi wa tatizo. Ni muhimu kuelewa kwanini wakazi hao wa mabondeni wanaendelea kuishi maeneo hayo licha ya tishio la mafuriko.
Kwa uelewa wangu, wengi wao ni masikini ambao wanaoishi katika ‘nyumba za mbavu za mbwa’ na ni vigumu mno kwao kumudu kununua ama kujenga nyumba bora katika maeneo salama, achilia mbali huo uwezo wa kununua japo kiwanja.
Lakini eneo jingine ambalo pengine Meya Silaa hawezi kuligusia ni ujenzi unaokiuka taratibu za mipango-miji, unaofanywa na matajiri ambao fedha zao zinawawezesha kupindisha kila aina ya sheria. Wanaoishi mabondeni ni wahanga wanaathiriwa zaidi na kanuni za kiasili za maji kujaa kwenye mabonde, lakini ujenzi holela unaoathiri mfumo wa maji taka ni uingiliaji wa makusudi wa jitihada za binadamu kukabiliana na mafuriko.
Mvua ikinyesha maji yanajaa, na kwa vile mitaro inayopaswa kuyaongoza maji hayo katika maeneo maalumu imezibwa, maji hayo yatamwagikia eneo lolote lile, hata kama si bondeni.
Kuhusu kauli za Meya Silaa, nilimfahamisha kwamba ana bahati ni meya wa manispaa nchini Tanzania kwani laiti angekuwa  meya kwa hapa Uingereza, kisha akaenda mji mwingine kwa shughuli za kichama ilhali wananchi wake wanakabiliana na janga la mafuriko, kungekuwa na uwezekano mkubwa wa harakati za kumng’oa madarakani. Moja ya sifa ya uongozi si tu kujali wananchi bali pia kuonyesha uongozi hasa katika nyakati za majanga.
Kauli hizo zisizopendeza za Meya Silaa zimekuja katika kipindi ambacho Taifa letu lipo katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Pengine tukio hili laweza kuwa angalizo muhimu kuhusu Katiba hiyo mpya.
Kwa mfano, je, Katiba hiyo itamwezesha mwananchi wa kawaida kumwajibisha kiongozi ‘mwenye kauli zisizofaa’? Suala hapa si tu katika kauli za kiongozi (iwapo zinafaa au la) bali suala zima la uwajibikaji.
Nimalizie makala hii kwa kurejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete wakati alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali kuangalia athari za mafuriko, kwamba “mafuriko hayaepukiki na wajibu wa Serikali ni kuwasaidia waathirika.”
Mafuriko kama maji kujaa kutokana na wingi wa mvua hayaepukiki, lakini mafuriko kama ukosefu wa miundombinu bora ya kukabiliana na mafuriko ni suala lililo ndani ya uwezo wetu. Kuna tofauti kati ya mafuriko yanayosababishwa na maji kuvuka kingo za Mto Kilombero huko Ifakara, na mafuriko katika maeneo yasiyo mabondeni jini Dar yanayochangiwa na mfumo duni wa kushughulikia majitaka.
Na japo ninaafikiana na kauli ya Rais kwamba wajibu wa serikali ni kuwasaidia waathirika (sijui ni wapi hao tukirejea kauli ya Meya Silaa) lakini kuna mengi yaliyo ndani ya uwezo wa serikali yanayoweza kupunguza idadi ya waathirika wa majanga kama mafuriko. Kubwa zaidi ni kujijengea uwezo wa kukabiliana na majanga badala ya kusubiri janga litokee ndipo tuanze kutafutana. 


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube