11 Apr 2014

KWA familia nyingi huko nyumbani, takriban kila usiku huambatana na kukusanyika mbele ya runinga kuangalia tamthilia mbalimbali.
Hali kama hiyo hujitokeza pia mchana wa mwisho wa wiki ambapo tamthilia hizo hurejewa kwa kujumuisha ‘vipande’ vya wiki nzima.
Nyingi ya tamthilia hizo huwa katika lugha ya kigeni, lakini wengi wa wanaozifuatilia wanamudu kuzielewa bila matatizo. Hata hivyo, yayumkinika kuhisi kwamba hata magwiji wa ufuatiliaji wa tamthilia hizo sasa wanapata wakati mgumu si tu kufuatilia bali hata kuelewa ‘tamthilia’ nyingine ndefu inayoendelea huko Dodoma. Hapa ninamaanisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba.
Pengine ni vema nikawakumbusha wasomaji msimamo wangu kuhusu suala la Katiba mpya, ambao nimeutanabahisha katika makala zangu kadhaa zilizopita.
Kwanza, pamoja na kutambua haja ya kuwa na Katiba bora zaidi ya tuliyonayo sasa, ukweli kwamba matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu hayatokani na ukosefu wa sheria bali usimamizi na utekelezaji wake, sioni jinsi Katiba mpya (kama itapatikana) itakavyoweza si tu kuwa ‘mwarobaini’ wa matatizo yetu bali pia kuheshimiwa.
Pili, muundo wa Muungano ndio suala linaloonekana kutawala mjadala wa Katiba mpya, na ninarejea tena kukiri kwamba ninachoona muhimu kwangu si idadi ya serikali zinazounda Muungano- ziwe mbili kama ilivyo sasa, tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, au hata serikali moja kama inavyodaiwa kuwa ndio ‘muundo halisi’ wa Muungano- bali jinsi serikali husika inavyoweza kutimiza majukumu yake na kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi.
Kwahiyo basi, kwa lugha nyepesi, msimamo wangu katika suala hili la muundo wa Muungano ni “wowote ule utakaowapatia Watanzania wanachostahili.” Na kwa hakika, malumbano yanayoendelea kuhusu suala hili la muundo wa Muungano yamegubika masuala mengine muhimu yaliyoleta haja ya kuwa na Katiba mpya.
Sasa, kwa vile mazingira yanaashiria kwamba kupatikana au kutopatikana kwa Katiba mpya kunategemea muafaka katika suala hilo la muundo wa Muungano, basi hata sie ‘tusiolitilia maanani sana’ tunalazimika kulijadili kwa marefu na mapana. Hiki ni kikwazo ambacho bila kukivuka chaweza kuondoa uwezekano wa kupatikana Katiba mpya.
Mwanzoni mwa makala hii, nimefananisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba na tamthilia. Lakini kichekesho ni kwamba wakati tamthilia nyingi za kigeni zinazotawala kwenye runinga za huko nyumbani zinaeleweka licha ya kuwa katika lugha za kigeni, hii ya Bunge la Katiba si tu inazidi kutoeleweka bali inapoteza ladha kila kukicha.
Hakuna haja ya kurejea mlolongo wa matukio yaliyokwishakujitokeza katika Bunge hilo, hasa kwa vile takriban yote yanakera; kuanzia madai ya nyongeza ya posho hadi Bunge hilo kugeuka ulingo wa kuonyeshana umahiri wa vijembe na lugha zisizopendeza.
Lakini sasa kuna suala jipya ambalo si tu linazidisha ugumu wa mjadala wa muundo wa Muungano bali pia linatishia hata uhai wa Muungano wenyewe. Suala hili ni nyaraka mbalimbali za kuthibitisha uhalali/uhalisia wa Muungano.
Ningependa kukiri kwamba sielewi nyaraka hizo za Muungano ni ngapi, lakini ninachofahamu ni kwamba moja ni hiyo inayofahamika kama Hati ya Muungano. Sasa, katika mazingira yanayoweza tu kuonekana katika filamu ya kutisha (horror movie), sahihi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere inaonyesha dalili ya ‘kuchakachuliwa.’ Mlolongo wa maswali unaibuka hapo: je, sahihi hiyo imechakachuliwa au hati nzima imechakachuliwa na ndiyo maana sahihi inazua utata? Nani aliyefanya ‘uhuni’ huo? Na kubwa zaidi, kwa nini?
Lakini ukidhani kizaazaa pekee ni katika suala hilo la sahihi ya Nyerere tu, basi subiri mpaka utakapofahamu kwamba madai kuwa Hati ya Muungano ambayo awali ilidaiwa ipo Umoja wa Mataifa (UN) nayo yana walakini baada ya UN kudai haina hati hiyo. Swali jingine, iko wapi? Kwa nini ilidaiwa ipo UN ilhali si kweli? Nani huyo anayedanganya? Kwa nini?
Kabla ya kuandika makala hii nimekutana na maelezo ya mchambuzi mmoja kwenye mtandao mmoja wa kijamii akieleza kwamba kwa uelewa wake, hati iliyowasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma, na yenye sahihi za Nyerere na Pius Msekwa sio ‘Hati ya Muungano’ (Articles of the Union) bali ni Sheria ya Muungano (the Act of the Union) iliyotungwa na Bunge wakati huo kupitisha Articles of the Union, na kusainiwa na Nyerere na Msekwa (kama Katibu wa Bunge wakati huo).
Na hata hati hiyo ingekuwa ndio Hati halisi ya Muungano, bado kuna tatizo jingine la sahihi za Nyerere na Msekwa kuwa na walakini. Kadhalika, inaelezwa kwamba hati hiyo imeongezwa maneno ‘kwa kompyuta’ japo kila mwenye uelewa anafahamu kwamba kompyuta hazikuwapo nchini katika miaka hiyo ya 1960.
Mchambuzi huyo anahitimisha kwamba hati ‘zilizotoweka’ ni nakala halisi ya Serikali ya Tanganyika, nakala halisi ya SMZ, nakala halisi ya Bunge la Tanganyika, nakala halisi ya Baraza La Wawakilishi, nakala halisi ya Mwanasheria Mkuu, nakala halisi ya Nyerere, na nakala halisi ya Karume.
Maswali kadhaa yanajitokeza, ikiwa ni pamoja na, je nakala hizo ‘zimetoweka’ kweli au hazijawahi kuwapo? Nani anahusika na kutoweka huko? Kwa nini? Na maswali mengine lukuki.
Vilevile, gazeti moja la Kiingereza la huko nyumbani, katika toleo lake la juzi, liliripoti kwamba aliyekuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Salum Rashid, alieleza kwamba Mzee Karume hakuwahi kusaini hati yoyote kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Utata huo unaogubika uhalali na/au uhalisia wa Muungano umenifanya kuhisi kwamba kuna mtu/watu fulani mahala fulani anadanganya/wanadanganya. Swali: ni nani? Na kwa nini anadanganya/wanadanganya?
Niliwahi kuandika katika moja ya makala zangu huko nyuma kwamba pamoja na nia nzuri ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, Nyerere na Karume walikosea kufanya suala hilo kama la ‘wao binafsi’ na si la Watanganyika na Wazanzibari wote.
Pamoja na dhamira zao nzuri, sidhani kama viongozi hao waliangalia mbali zaidi ya ajenda ya umoja na mshikamano, hivyo kutotilia maanani uwezekano wa matatizo ya kisheria au hata ridhaa ya wananchi huko mbele. Na, binafsi naona mapungufu haya kama moja ya vyanzo vikuu vya matatizo ya Muungano.
Lakini pengine badala ya kuwalaumu waasisi hao wa Muungano ni muhimu kutambua mazingira ya kisiasa ya wakati huo. Hicho kilikuwa kipindi cha kujenga Taifa, huku mfumo wa kisiasa ukiwa hauruhusu mawazo tofauti na ya watawala. Hivi tumeshawahi kujiuliza wazo la kuunganisha Tanganyika na Zanzibar lilikuwa la kidemokrasia kiasi gani, kwa maana ya kusaka ridhaa ya wadau halisi wa Muungano huo, yaani Watanganyika na Wazanzibari?
Kwa bahati mbaya (au kwa makusudi), kwa kiasi kikubwa chama tawala CCM kinataka kurejea kosa hilohilo lililopelekea kuzaliwa Muungano ‘wenye matatizo.’ Wanataka kulazimisha matakwa yao ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Kuna busara moja inafundisha hivi, “Si kila tendo jema ni sahihi. Kwa mfano, kumpa chakula ‘kigumu’ mtu mwenye njaa ni tendo zuri, lakini kumpa chakula kingi kigumu mtu mwenye njaa kali ni hatari kwani inaweza kumfanya mtu huyo kuvimbiwa na hata kupoteza maisha.”
Dhamira ya CCM kutaka kunusuru muundo wa sasa wa Muungano (wa serikali mbili) inaweza kuwa nzuri. Lakini kulazimisha dhamira hiyo (pasi kujali uzuri wake) ni jambo hatari. Na hata kama CCM walitaka kulazimisha dhamira yao hiyo basi angalau wangejiandaa vya kutosha badala ya kukurupuka, na sasa tunashuhudia matatizo mengine makubwa zaidi yanayozua utata wa Muungano mzima wanaotaka kuinusuru.
Nihitimishe kwa kuishauri CCM na wote wanaotaka kulazimisha muundo wa Muungano wa serikali mbili, kwamba suluhu pekee ni kwa suala hilo kupelekwa kwa wananchi ili hatimaye waamue kuhusu muundo wa Muungano wanaotaka. Na si tu kulipeleka suala hilo kwa wananchi bali pia kutowatisha kwa minajili ya kuwalazimisha wafuate matakwa ya chama hicho tawala.
Ni ushauri mwepesi lakini kila anayeijua CCM anafahamu kuwa ni chama ‘kisichoshaurika’ wala ‘kuambilika.’ Kwao, wapo tayari Watanzania wakose Katiba mpya iwapo dhamira ya chama hicho kung’ang’ania muundo wa Muungano wa serikali mbili itakwama.
Kama ambavyo hata tukipata Katiba mpya inaweza kutokuwa na manufaa pasipo nia ya dhati kuiheshimu na kuitekeleza kwa ufanisi, pasipo nia ya dhati ya kusaka muafaka katika suala la muundo wa Muungano na hatma ya Katiba mpya kwa ujumla, kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kitaishia kuwa tamthilia ambayo si tu inakera bali pia ya gharama kubwa kwa wananchi.
PENYE NIA PANA NJIA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube