18 Jul 2014

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe
NIANZE makala hii kwa kuwatakia ndugu zangu Waislamu mfungo mwema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, japo salamu hizi nimechelewa kidogo, ambapo sasa mfungo huo umeingia kumi la pili (Maghfirah).
Ni matarajio yangu kuwa ndugu zetu Waislamu watatumia mwezi huu wa toba kuliombea taifa letu kwani mwelekeo wake si mzuri.
Sisi kama Watanzania tuna tatizo kubwa la kupuuzia masuala ya msingi kwa mustakabali wa taifa letu. Hivi katika mazingira ya kawaida tu, inawezekana vipi nchi iandamwe na matukio ya ‘kigaidi’ ya milipuko kadhaa ya mabomu na kupelekea vifo na majeruhi kadhaa lakini hakuna japo mtu mmoja aliyewajibishwa?
Majuzi nimemsikia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe akihojiwa na Radio France International kuhusu matukio hayo ya ‘kigaidi.’ Ninaomba kuwa mkweli, majibu ya Waziri huyo si tu yalikuwa ya kibabaishaji bali pia yalizidi kuonyesha ombwe kubwa linaloukabili utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Waziri Chikawe alieleza kuwa tayari kuna watu sita waliotiwa nguvuni kufuatia tukio la awali la mabomu jijini Arusha, na wengine wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio la hivi karibuni. Alidai kuwa inadhaniwa kuwa makundi hayo mawili yana uhusiano. Lakini alipoulizwa ni kundi gani hasa linahusika na mashambulizi hayo, akaishia kudai kuwa ni magaidi.
Kadhalika, Waziri huyo alidai kuwa hatua madhubuti zimechukuliwa kudhibiti matukio hiyo, ambapo “takriban mitaa yote imedhibitiwa kuhakikisha vitendo hivyo vya kigaidi havitokei tena.”
Vilevile alithibitisha kuwa wahusika ni Watanzania, baadhi kutoka Arusha na wengine Tanga, lakini walipata mafunzo ya ugaidi ‘kwingineko’ (bila kusema ni ndani au nje ya Tanzania).
Ndugu msomaji, huhitaji kuwa mtaalamu wa masuala ya usalama kuhitimisha kwamba Waziri Chikawe alikuwa akitimiza tu wajibu wake kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa. Busara ndogo tu yaweza kukufahamisha kwamba kama wakati tukio la hivi karibuni linatokea tayari kulikuwa na watuhumiwa sita mbaroni basi kwa hakika kuna mapungufu makubwa mahala flani.
Waziri Chikawe hawezi kukwepa lawama kwa vile Wizara yake inahusika moja kwa moja na usalama wa raia kupitia Jeshi la Polisi, kimsingi wanaopaswa kubebeshwa lawama kubwa zaidi ni Idara ya Usalama wa Taifa. Moja ya majukumu makuu ya taasisi hiyo ni kukabiliana na vitendo vya ugaidi, kwahiyo ‘mafanikio’ ya magaidi-kwa maana ya mwendelezo wa vitendo vyao vya kinyama huko nyumbani-ni dalili ya kushindwa kazi kwa Idara hiyo.
Ninafahamu bayana kuwa wahusika hawatopendezwa na lawama hizi lakini ni muhimu kwao kuelewa kwamba kamwe tusitarajie miujiza kumaliza tatizo hili linalozidi kukua. Ugaidi una sifa ya kupata hamasa kutokana na mafanikio ya mashambulizi yaliyotangulia. Na kwa maana hiyo, pasipo hatua madhubuti, ni wazi tutaendelea kushuhudia matukio hayo yakijirudia.
Mara kadhaa tumeishia kusikia watu flani wamekamatwa kutokana na matukio ya mabomu lakini hadi muda huu vyombo vya dola havijawahi kuona japo umuhimu wa kuufahamisha umma maendeleo ya uchunguzi wao kufuatia kukamatwa kwa watu hao.
Majuzi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento, alitoa maoni yake kwamba Jeshi la Polisi linapaswa kubebeshwa lawama kutokana na matukio ya mabomu, kwa kushindwa kuyazuia yasitokee tena.
Jaji Manento alisema katika tukio la kwanza la mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA jijini Arusha, Jeshi la Polisi lilishindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kusikiliza kauli za viongozi wa kisiasa. Alihusisha hali hiyo na ukiukwaji wa haki za binadamu .
Na siasa za kihuni zimechangiwa sana ustawi wa matukio haya ya mabomu. Wengi tunakumbuka jinsi Mwigulu Nchemba alivyofanya kila jitihada kuwahadaa Watanzania kwamba tukio la mabomu katika mkutano wa CHADEMA huko Arusha lilisababishwa na CHADEMA wenyewe.
Hiyo ilikuwa baada ya jitihada mufilisi za CCM kumtwisha kiongozi mwandamizi wa CHADEMA Wilfred Lwakatare kesi ya ugaidi.
Mwanzoni mwa makala hii nimewalaumu Watanzania kwa kupuuzia mambo ya msingi kwa mustakabali wa taifa letu. Pasi haja ya kutoa mifano mingi, rejea jinsi wananchi walivyokubali kwamba mgao wa milele wa umeme ni kama haki yao ya kikatiba, huku licha ya kuambiwa kuwa kuna mabilioni ya fedha zao zilizoibiwa na kufichwa huko Uswisi, hakuna harakati zozote za angalau kupigia kelele ufisadi huo.
Majuzi nimeshuhudia picha kadhaa zinazoonyesha jinsi hali ilivyo mbaya katika hospitali ya taifa Muhimbili. Nikajisemea moyoni, kama hali ipo hivi katika hospitali ya taifa, hali ikoje huko kwenye hospitali teule, za mikoa, wilaya au kwenye vituo vya afya?
Lakini nani anajali? Ushindi wa Ujerumani katika Kombe la Dunia mwishoni mwa wiki iliyopita unaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa Watanzania wengi kuliko hatma ya usalama wao kutokana na matukio mfululizo ya mabomu, mgao wa umeme, hali mbaya katika hospitali zetu, nk.
Ndio, wenye jukumu la kushughulikia yote hayo ni viongozi tuliowakabidhi dhamana ya kutuongoza, lakini ni wajibu wa kila mwananchi kuwabana viongozi wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo. Ninaamini kuwa kinachowapa jeuri viongozi wengi kutowajibika ipasavyo ni ukweli kwamba aliyewateua hatowawajibisha na wananchi hawatojali.
Nikirejea kwa watu wa Usalama wa Taifa, angalau wanapohusishwa na kushamiri kwa ufisadi huko nyumbani, wanaweza kuwa na ‘excuse isiyokubalika’ kuwa labda wananufaika kimaslahi. Lakini wanaweza kuwa na maelezo gani wanaposhindwa kudhibiti janga hili la ugaidi?
Nihitimishe makala hii kwa kumshauri Rais Kikwete kuchukua hatua stahili dhidi ya watendaji wake wanaozembea kukabili tishio na matukio ya ugaidi.
Asisubiri mpaka bomu limdhuru kiongozi ndio atambue kuwa ugaidi ni hatari (na sifa nyingine ya ugaidi ni kuwa haubagui -haichagui kati ya mlalahoi au kigogo japo hadi sasa wahanga wamekuwa walalahoi pekee).
Japo inampendeza kusikia Rais wetu anawathamini wasanii kiasi cha kuwaletea mastaa kutoka Marekani ‘kuwapa somo kuhusu sanaa’ lakini angewatendea haki Watanzania wote laiti angeweza pia kuwaletea wataalamu wa masuala ya ugaidi ili kuwasaidia wanausalama wetu ambao kwa hakika wameshindwa kazi.
Mungu Ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube