30 Jul 2014

signalapp
Mie ni miongoni mwa waumini wakubwa wa filosofia ya 'ishu binafsi shurti zibaki kuwa za binafsi' (private things should always remain private). Na ninaposema 'ishu binafsi' ninamaanisha pia masuala nyeti yasiyopaswa kusikizwa na yeyote yule asiyehusika nayo. Siwezi kufafanua zaidi ila naamini kwamba kuna nyakati tunakuwa na masuala yanayopaswa kufahamika kwa wahusika tu.

Sasa iwapo unatumia iPhone,kuna app moja inaweza kuwa na manufaa makubwa kwako pindi ukijikuta katika mazingira ambapo unataka kuwasiliana na mtu pasi maongezi hayo 'kunaswa' na watu wengine. Labda kama hadi hapa hujanielewa vizuri, ni vema ukafahamu kuwa taarifa za hivi karibuni kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Vodafone inaonyesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi inayoshika nafasi za juu duniani kwa mashushushu wake kunasa mawasiliano binafsi ya simu za wananchi.

App husika inaitwa SIGNAL, na inapatikana bure kwenye App Store.

Kwa kutumia teknolojia inayoruhusu wahusika tu wa ujumbe husika kuupata ukiwa kamilifu (encryption), app hiyo ya Signal inayafanya maongezi katika iPhone kuwa ya faragha kiasi kwamba mtu asiyehusika hawezi kuyanasa.

Jinsi ya kui-set up App hiyo ni rahisi kabisa, na unahitaji kuingiza namba yako ya simu tu na kuithibitisha kwa kuingiza tarakimu 6 (6-digit code), ambazo zitatumwa kwako kwa SMS au simu, na utakuwa tayari kuitumia app hiyo. Namba za simu ulizohifadhi katika simu yako zitahamia kwenye app hiyo mara moja, lakini zitakazoonekana ni zile tu ambazo mtumiaji naye anatumia app hiyo. Ukimpigia simu mtu asiyetumia app hiyo,atatumiwa ujumbe wa ku-install app hiyo kwenye simu yake.

Unapopiga simu kwa kutumia app hiyo kwa mtu ambaye simu yake nayo ina app hiyo, faragha ya mawasiliano yenu inahakikiwa kwa kutumia maneno yanayoonekana katika screen ya simu ya anayepiga na anayepigiwa.Kisha mnafananisha maneno hayo kuhakikisha kuwa yanalingana, na yakilingana basi mawasiliano yenu yanakuwa ya siri. Yasipolingana basi inamaanisha kuna mtu anaingilia (anasikiliza) maongezi yenu.

Wakati kwa sasa app hiyo inaweza tu kuyafanya maongezi ya simu kuwa ya siri, kampuni iliyotengeneza app hiyo imeeleza kuwa ipo mbino kuwezesha hata mawasiliano ya SMS nayo kuwa ya siri.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube