31 Aug 2014


Siku moja nilipokea barua-pepe kutoka kwa msomaji mmoja wa makala zangu katika jarida la Raia Mwema. Licha ya kupongeza kuhusu makala hizo, alinipa ombi ambalo kwa kiasi flani liliniacha na tabasamu. Namnukuu, "... tuna matatizo mengi huku kwetu, kila anayekuja anajali maslahi yake tu. Nakushauri ufikirie kuhusu kugombea katika jimbo letu mwakani." Nilimshukuru msomaji huyo kwa pongezi zake lakini nikamweleza bayana kuwa kamwe sintojiingiza katika uongozi wa kisiasa. Nilimfahamisha kuwa mie ni muumini wa falsafa kuwa yawezekana kuutumikia umma kwa ufanisi pasi haja ya kuwa kiongozi.

Falsafa hiyo inachangiwa na ukweli kwamba nimeshawahi kuwa kiongozi mara mbili, maishani mwangu. Mwaka 1991 nikiwa mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora (Tabora Boys') nilichaguliwa kuwa kiranja mkuu.Lakini kwa vile shule hiyo ilikuwa ya mchepuo wa kijeshi, wadhifa wa kiranja mkuu ulikuwa ukijulikana kama Kamanda Mkuu wa Wanafunzi (Students' Chief Commander), na sare ziliambatana na 'vijimkasi' viwili mabegani.

Japo wadhifa huo ulinipa fursa ya kwanza ya uongozi, tukio moja la mgomo wa wanafunzi lililojiri wakati nipo madarakani sio tu lilinipa mtihani mgumu sana bali pia lilinionyesha sura nyingine chungu ya uongozi. Kwa upande mmoja nilipaswa kuwa kiungo kati ya uongozi wa shule na wanafunzi, lakini wakati huohuo nami ni mwanafunzi na walitarajia niwe upande wao, huku walimu nao wakitaka niwe upande wao. Kwa busara na skills nilizopata kabla ya tukio hilo, mgomo huo ulimalizika salama na sikujenga maadui upande wowote kwa vile nilisimamia kwenye kanuni na taratibu na haki.

Fursa nyingine ya uongozi ilijitokeza mwaka 2000 nilipokuwa mtumishi wa taasisi flani ya serikali huko nyumbani. Niliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya kiutendaji (operational district/zone), nafasi niliyoshika hadi ninaondoka huko nyumbani miaka miwili baadaye. Ugumu mkubwa wa wadhifa huu ulikuwa kwenye 'kuwa macho masaa 24'...na wakati mwingine kukurupushwa usingizini na kuulizwa 'nifahamishe kilichotokea sehemu flani' ilhali sina habari ya nini kimetokea. Lakini jingine gumu lilikuwa kwenye kuwaongoza watu nilioanza ajira nao pamoja na wengine walionizidi miaka kadhaa ya uzoefu. Kadhalika, wasaidizi wetu mtaani walikuwa na matarajio makubwa ya 'uzalishaji' wao pamoja na maisha yao binafsi. Hata hivyo niliondoka nikiwa na rekodi ya kujivunia.

Kwa kifupi, fursa zote hio zilinifundisha kuwa uongozi ni mzigo mzito na unahitaji kujitolea kwa kiasi kikubwa. Ndio maana kila nikisikia mawazo ya kujihusisha na uongozi, jibu langu jepesi ni HAPANA.Not again. Sio kwamba ninakwepa majukumu lakini kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikijihusisha na uraia kama uongozi, kwa maana ya kutumainia nguvu za raia katika ujenzi wa taifa. Ndio hizo kelele tunazopiga magazetini, hapa bloguni na kwenye mitandao ya kijamii.

Lengo la makala hii sio kuelezea historia yangu au uwezo wa uongozi bali suala lililojitokeza katika mtandao wa kijamii wa Twitter juzi. Nadhani wengi wenu wasomaji mnafahamu kilichomsibu Betty Ndejembi, aliyetutoka juzi. Kabla ya kufariki kwake aliandamwa na unyanyasaji wa kutosha katika mtandao huo. Baada ya kifo hicho, mie niliungana na 'wenye mapenzi mema kwa jamii' kukemea unyanyasaji mtandaoni, kwa kimombo 'cyberbullying.' Hata hivyo, katika kuhamasisha mapambano hayo sikumtaja wala kumtuhumu mtu kuwa ni mnyanyasaji wa wenzie mtandaoni. Nilichohamasisha ndicho hicho nilichoeleza hapo juu: sie watumiaji wa mtandao kama wahanga wa unyanyasaji wa mtandaoni kuunganisha nguvu zetu dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo. Na kwa hakika mapokeo yamekuwa mazuri sana. Watu wengi wamewasiliana nami kunifahamisha jinsi walivyokuwa wahanga wa cyberbullying.

Wito wangu kwa jamii umekuwa sio kusubiri serikali au wanasiasa kuchukua hatua ya kukomesha tabia hiyo bali sie kama wananchi na wahanga wa tabia hiyo kuunganisha kuvu na kupambana nayo. Kwa lugha nyingine, sie wenyewe tuchukue uongozi wa mapambano dhidi ya wanyanyasaji wa mtandaoni.

Hata hivyo, jioni ya leo likaibuka kundi la watu waliaonza kunishambulia vikali kuhusiana na kampeni hiyo ya kupambana na unyanyasaji mtandaoni. Kikubwa ni tuhuma kwamba mie wanayeniita 'mwanaharakati wa cyberbullying' ni 'bully' (mnyanyasaji) pia. Na mmoja wao akapata ujasiri wa kupitia tweets zangu za nyuma na kuzi-screenshot ili 'kuthibitisha kuwa mie ni mnafiki nisyestahili kukemea cyberbullying.' Wakati mwingine huwa nashangazwa na 'ujasiri' wa aina hii ambao hata kwa mwenye uelewa mdogo tu wa sheria anaweza kujua athari zake.

Hadi hapo sikuona tatizo sana japo nilishangazwa na 'hasira' za watu hao ilhali sikuwahi kuwatuhumu kuwa wao ni bullies. Na hata asubuhi nilitwiti kuhoji ''kama tunapozungumzia ufisadi, hukasiriki kwa vile wewe si fisadi, kwanini tukizungumzia cyberbullying ukasirike ilhali wewe sio cyberbully?"

Lakini katika mwendelezo wa shutuma zao dhidi yangu, mmoja wao akavuka mstari wa kisheria. Siwezi kuliongelea kiundani suala hili kwa sababu za kisheria.

Awali nilipoamua kuungana na wengine kukemea unyanyasaji mtandaoni sikudhani kwamba itafika mahala pa kuchukua vitendo kulazimisha wanyanyasaji hao waache tabia hiyo. Hata hivyo, kwa kilichotokea leo, nimeamua kuhamia kwenye vitendo.

Tuna tatizo kama Watanzania, ni wepesi wa kulalamikia matatizo yanayotukabili lakini ni wagumu kuchukua hatua za vitendo kuyatatua. Mgao wa umeme, huduma mbovu za baadhi ya makampuni, tatizo la ajali zisizoisha, ufisadi, na kadhalika. Kwa kiasi kikubwa tumekuwa watu wa kulalamika tu kana kwamba malalamiko hayo yataleta mabadiliko.

Katika hili la unyanyasaji mtandaoni, asilimia kubwa ya watu wanaotaka 'kuishi kwa amani mtandaoni' wameunga mkono japo kwa maneno haja ya kukemea unyanyasaji mtandaoni. Lakini kama ilivyojitokeza leo jioni ambapo nimekuwa mhanga wa ushiriki katika harakati hizo, bado kuna wenzetu wanadhani wana hatimiliki ya kuwabughudhi watu mtandaoni watakavyo. Inabidi tuseme enough is enough. Kwa vile haijawahi kutokea huko nyumbani kwa mtu kuingia matatizoni kutokana na alichoandika mtandaoni, watu wengi tu wanaendelea kudhani kuwa akiwa mbele ya keyboard ya kompyuta yake ana uhuru wa kunyanyasa, kudhalilisha, kutukana na kufanya matendo mengine ambayo kimsingi ni makosa kisheria.

Ukweli ni kwamba tukiacha 'njia za asili' za kudhibiti 'wakorofi' kwenye mitandao ya kijamii, yaani aidha kuwa-mute, kuwa-unfollow au kuwa-block, kuna njia za ufanisi zaidi kama vile za kisheria alimradi kuna ushahidi wa kutosha.

Hatimaye nimefikia uamuzi wa kuchukua hatua za vitendo dhidi ya unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying). Sifanyi hivi kwa minajili ya kuingia kwenye vitabu vya historia kama Mtanzania wa kwanza kupambana na cyberbullies kwa vitendo bali ninafanya huduma kwa umma. Huhitaji kuwa kiongozi ili kuitumikia jamii. Na sihitaji madaraka ili niweze kupambana na tabia hii isiyofaa. Hakuna miujiza itakayowalazimisha wanyanyasaji wa mtandaoni kuacha tabia hiyo. Kitu pekee ni pale wanapofunzwa madhara ya vitendo vya aina hiyo.

Japo ningependa kuwa sehemu ya kundi linalopambana na suala hili, hadi sasa hakuna dalili zozote za uwepo wa mkusanyiko wa kukabiliana na tatizo hili ambalo kwa hakika linawasumbua wengi. Lakini tukisema tusubiri mpaka watu wajipange na kuunda kikundi, wenzetu wengi zaidi watazidi kuwa wahanga wa unyanyasaji huo wa mtandaoni.

Natambua ugumu wa mapambano haya lakini kila mapambano ni magumu. Natambua kutakuwa na lawama na kukatishana tamaa lakini liwalo na liwe lazima mtu flani awe mfano kwa wenzie kwamba cyberbullying is not just wrong but also a criminal offence. 

Lengo la makala hii sio kumtisha wala kumzuwia mtu kunituhumu kuwa nami ni cyberbully. Ninaheshimu uhuru wa kujieleza alimradi hauvuki mpaka.Na kitu ambacho kamwe siwezi kukivumilia  ni uvunjifu wa sheria dhidi yangu.

Ni matumaini yangu kuwa kama inavyofundisha Biblia Takatifu kuwa 'ukipiga mchungaji kondoo watasambaa,' kumwajibisha mmoja wa wanaodhani mitandao ya kijamii ni fursa ya kuwanyima wenzao amani kutapeleka ujumbe kwa wengine wanaoamini hivyo pia. Mafundisho ya Kiislam yanatueleza kwamba "ukiona jambo baya basi aidha lichukie, au likemee au liondoe." Nimeshachukia unyanyasaji mtandaoni vya kutosha, nimeukemea vya kutosha, na sasa ni wakati wa kuuondosha kwa vitendo. Haitokuwa rahisi lakini nina hakika nitafanikiwa. Inshallah!

Na mwisho, lengo la harakati ninazoanza si kumkomoa mtu au watu flani. Hao waliotumia muda wao kunishambulia ni dalili tu za tatizo, ninacholenga kupambana nacho ni chanzo cha tatizo. Mtu anaposkia baridi kwa vile ana homa, huwezi kumtibu kwa kumpa maji ya moto bali tiba ya homa. Kadhalika, unyanyasaji mtandaoni hauwezi kukomeshwa kwa kubana watu flani tu bali kulikabili tatizo lenyewe. Ifike mahala mtu ajiulize mara mbili kabla ya kuposti 'maneno yasiyofaa' dhidi ya mtu mwingine mtandaoni.

Ili mabadiliko ya kweli yatokee hasa ya kuondoa jambo baya ni lazima kujitoa mhanga. Iwapo uamuzi wangu wa kupambana na tabia hii utapelekea madhara kwangu basi na iwe. Ninaamini kuwa mwenye haki ataanguka saba mara sabini lakini hatimaye atasimama. Nikisema 'mwenye haki' simaanishi kuwa harakati hizi ni za kutafuta haki yangu bali ya wanyonge mbalimbali wahanga wa unyanyasaji mtandaoni. Tukiwakalia kimya bullies sio tu watadhani tunaridhia vitendo vyao bali pia wataendelea kutengeneza victims.

INAWEZEKANA, NA NITATIMIZA WAJIBU WANGU2 comments:

  1. kwenye uislam wanasema ukiona jambo baya unaliondosha kwa vitendo, ukishindwa unalikemea na haya mawili yakikushinda pia basi chukia rohoni na kwa hakika huko (kuchukia rohoni) ni udhaifu wa imani.

    wakati mwingine inabidi kuelewa kwamba sio watu wote wanokuwa mbele ya kompyuta zao (na wengi sio zao ni za kukodi huko cafe) wanakosa ile tunasema emotional control na kujikita wanashinswa kuwa na simile.

    pia, kuna hili la "mind set" nalo ni tatizo, itategemea sana msomaji kaelewa nini akihusianisha na nini ili ajione aidha kanyanyaswa na au kanyanyasa, ni kama vile kusema hisia wakati mwingine zinaweza leta mzozo.

    ReplyDelete
  2. nasemaa, kwenye uislam kuna unaambiwa ukiona jambo baya basi uliondoshe, (kwa vitendo) ukishindwa basi ulikemee na tatu basi ukishindwa yote hayo uchukie rohoni na hakika (kuchukia huko rohoni) ni udhaifu wa imani

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.