12 Sept 2014

Judge Thokozile Masipa delivers her judgement  in court  in Pretoria, South Africa, Friday, Sept. 12, 2014. Masipa ruled out a murder conviction for the double-amputee Olympian, Oscar Pistorius, in the shooting death of his girlfriend, Reeva Steenkamp, but said he was negligent, and convicted him of culpable homicide

Mwanamama mweusi aliyeendesha kesi ya Pistorius ana historia ya kutia moyo kama ya mwanariadha huyo mlemavu.

Kesi mbili zimemalizika jijini Johannesbugh, Afrika ya Kusini: moja, ya wazi na ambayo dunia nzima ilikuwa ikiifuatilia, ya mwanariadha mlemavu, Oscar Pistorius, aliyekuwa kizimbani kwa kosa la kumpiga risasi mpenzi wake, mrembo Reena Steenkamp, na kumuua, na ya pili ni dhidi ya mwanamke mweusi mwenye miaka 66, Jaji Thokozile Masipa, aliyekuwa na dhamana ya kutoa hukumu katika kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi duniani.

Yaliyojiri kwa upande wa Pistorius sote twayafahamu, lakini wengi hawafahamu kuhusu mwanamama Masipa, ambaye licha ya kuangaliwa kwa jicho 'kali' na familia za mwanariadha huyo na ya marehemu Reena, macho ya dunia yaliyokuwa yakifuatilia kesi hiyo nayo yalielekezwa kwake.

Ile kuwa mtu mweusi, achilia mbali uanamke wake, ilikuwa ni mtihani tosha katika nchi ambayo licha ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi bado inaugulia vidonda vya mfumo huo. Kwa mtu mweusi kuwa jaji wa kesi ya 'wazungu' wawili, ni mtihani mkubwa wenye kugusa hisia.

Lakini hata kama Afrika Kusini isingekuwa bado na makovu ya mfumo wa ubaguzi wa rangi, na pamoja na ukweli kwamba nchi hiyo imeendeleza mara kadhaa zaidi ya nchi nyingine za Afrika, bado ipo Afrika na ni nchi ya Kiafrika. Na sote twafahamu mtizamo wetu wa Afrika kwa wanawake. Tukubali, tukatae, wengi wetu tuna kasumba ya kudhani ni wanaume pekee wenye uwezo wa 'kufanya mambo makubwa.' Kwahiyo mtihani mwingine kwa Jaji huyo ulikuwa uanamke wake katika jamii inayomtizama mwanamke kwa jicho la kutokuwa na imani kuhusu uwezo wake.

Mtoto wa kwanza katika familia ya watoto 10, watano kati yao wakiwa marehemu na mmoja aliuawa wa kuchomwa kisu, Masipa alizaliwa katika nyumba ya vyumba viwili katika eneo la mafukara katika kitongoji cha Soweto. Katika utoto wake, alilala sebuleni, na wakati mwingine kulazimika kulala sakafuni jikoni pindi nyumba yao ilipopata ugeni. Japo alikuwa mwenye akili na mwenye malengo ya kimaisha tangu udogoni, alilazimika 'kupoteza muda' kwa kufanya kazi kama housegirl. Ni hadi alipotimiza miaka 20 hivi ndipo alipopata fedha za kutosha kugharamani masomo yake chuo kikuu kusoma digrii ya 'kazi za jamii' (social work).

Baadaye alikuja kuwa mwandishi wa habari, akiwekea mkazo habari za  masuala ya wanawake, na unyanyasaji dhidi wa watu weusi nchini humo.Mwaka 1977 alitiwa nguvuni wakati wa maandamano dhidi ya kukamatwa kwa mwandishi wa habari mwenzie, na mmoja wa askari alimnong'oneza "Leo unakwenda kukutana na Steve Biko," mwanaharakati aliyepigwa na polisi wa Makaburu hadi kuuawa.

Alisalimika, lakini kwa mara nyingine alijikuta akilala tena sakafuni kama alipokuwa mdogo, lakini safari hii ni katika sakafu chafu ya rumande, na kuamriwa kusafisha vinyesi vya mahabusu wengine waliokuwa humo rumande. Alikaidi amri hiyo, na hatimaye kutolewa rumande na baada ya gazeti alilokuwa akiliandikia kumlipia faini.

Baadaye alihamia kwenye taaluma ya sheria, na kuhitimu kama mwanasheria muda mfupi baada ya Nelson Mandela kutoka kifungoni. Ndani ya miaka 10 tangu muda huo, Masipa aliibuka kuwa Jaji mwanadamizi mwanamke mwenye umri mdogo kuliko wote.

Kuhusu kesi na hatimaye hukumu ya Pistorius, ukweli kwamba Afrika Kusini ni moja na nchi zinazoongoza kwa mauaji duniani uliifanya kesi hiyo na hukumu yake ivute hisia za wengi, ndani na nje ya nchi hiyo. Lakini, kama ilivyobainishwa hapo juu, Jaji Masipa pia ni mhanga wa mauaji, ambapo mmoja wa wanafamilia yake aliuawa kwa kuchomwa kisu. Yawezekana kabisa kuwa wakati anaendesha kesi hiyo, alikuwa akirejewa na kumbukumbu za nduguye huyo aliyekuwa mhanga wa mauaji. 

Na kama ilivyokuwa, baada ya hukumu hiyo dhidi ya 'mzungu' Pistorius, mijadala iliyotawala kwenye mitandao ya kijamii ni pamoja na suala la 'mwanamke mweusi' kutoa hukumu kwa kutumia 'sheria ya mtu mweupe.'

Lakini ukweli unabaki kuwa hukumu aliyotoa Jaji Masipa ilikuwa ya haki, haki haina rangi', wala haibebi vinyongo dhidi ya 'mababu/ mabini makaburu' na kuihamishia kwa 'wajukuu wa makaburu' kama Pisterius. Haki katika hukumu huzingatia ushahidi na uthibitisho iwapo kosa limetendeka au la. Baada ya kuibomoa kesi iliyojengwa na waendesha mashtaka, Jaji huyo alifikia uamuzi kuwa mwanariadha huyo alimuua mpenzi wake bila kukusudia, katika lugha ya kisheria 'culpable murder' au 'manslaughter' kwa hapa Uingereza. 

Ni wazi kwamba baada ya Jaji huyo kuhitimisha kesi kwa kutamka adhabu kwa Pistorius, wengi watamsahau Jaji Masipa. Huenda kesi hiyo ikapelekea kutengenezwa kwa filamu itakayomzungumzia mwanariadha huyo huku kukiwa na uwezekano hafifu wa kuwapo filamu kuhusu kuthibitika kwa umahiri wa Jaji Masipa. 

Hata hivyo, kilicho bayana katika kesi hiyo ni jinsi mwanariadha Oscar Pistorius alivyoweza kuvuka kikwazo cha ulemavu wake na kujitengenezea jina kubwa duniani, na mwanamama mweusi Thokozile Masipa alivyoweza kuvuka vizingiti vya umaskini na mfumo wa kibaguzi na kuibuka msimamizi wa haki katika kesi hiyo ya kihistoria. Kwa hili, ni wazi laiti Mandela angekuwa hai, angejisikia fahari isiyo kifani.

Ni matumaini yangu kuwa historia ya mwanamama huyu-na hata ya Pistorius- itakuwa funzo kubwa kwa wengi wetu ambao katika safari zetu za maisha twakumbana na vikwazo mbalimbali, dhmira thabiti na jitihada zaweza kutufikisha mahala pa kuingiza majina yetu katika historia kama si kubaki katika kumbukumbu kwa jamii zetu.

PENYE NIA PANA NJIA!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube