13 Sept 2014


Kwa ajali hizi hakuna aliye salama
KWA mara nyingine Tanzania imekumbwa na ‘msiba’ kwa ajali mbaya iliyotokea mkoani Mara na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 30.

Kama nilivyowahi kuandika hivi karibuni, kwa polepole ajali zinazogharimu maisha ya Watanzania wengi tu zinaanza kuzoeleka. Na hili linakera mno.

Kweli, nchi yetu inafahamika kwa kutoyapa uzito wa kutosha matatizo yanayotukabili, na orodha ya ushuhuda katika hilo ni ndefu, na pengine inahitaji kitabu kizima badala ya makala moja kama hii.
Tunaweza kukumbushana kuhusu matatizo mbalimbali yanayotukabili, na ambayo kwa makusudi tumekubali kuyafanya sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

Angalia, kwa mfano, tatizo la mgao wa umeme. Hili limefanywa ngonjera na wanasiasa wetu mpaka imefika mahali wameamua kukaa kimya tu. Aidha, wamechoka kudanganya, au wameishiwa na uongo wa kudanganyia, au yawezekana wameona hakuna haja ya kuwadanganya watu wasiojali. Hatimaye mgao wa umeme umekuwa sehemu ya kawaida ya maisha ya Mtanzania, na ukiacha lawama na matusi ya hapa na pale dhidi ya Tanesco, wananchi wengi wanaonekana kulikubali tatizo hilo.

Huko nyuma zilipatikana taarifa kuwa kuna baadhi ya Watanzania wenzetu wameiba mabilioni ya shilingi na kuyaficha katika mabenki nchini Uswisi. Zikaanza porojo, mara mwanasiasa huyu adai atalazimika kuyataja majina ya ‘wezi’ hao iwapo serikali haitofanya hivyo, mara tuambiwe kuna kikosi-kazi kimeundwa kufuatilia suala hilo, mara Takukuru nao waje na ‘uzushi’ wao, na porojo nyingine za kukera kama hizo.

Kilicho bayana ni kwamba hivi sasa suala hilo ni kama limekufa kifo cha asili. Hakuna dalili zozote za watu wanaokerwa na wizi huo wala kushinikiza hatua mwafaka za angalau kurejeshwa kwa fedha hizo kama si kudai hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Ukifuatilia kwa karibu kuhusu tuhuma za ufisadi unaweza kuhitimisha kuwa labda tuhuma mpya huibuliwa makusudi ili kuzima tuhuma zilizotangulia.

Katika mazingira ya kawaida tu, kama wahusika wamekataa katakata hadi leo angalau kutaja jina la mmiliki wa kampuni ya Kagoda iliyokwapua fedha nyingi katika ufisadi wa EPA katika Benki yetu Kuu, iliyopo Tanzania, ni wazi kwamba kutakuwa na uwezekano mdogo kwa wananchi kufahamishwa kuhusu fedha zilizofichwa nje ya nchi.

Tukirejea kwenye janga la ajali, Inasikitisha kuona kwamba taifa limezoea ajali hadi imefika mahala hatuoni umuhimu wa kuwa na siku ya maombolezo.

Labda wahusika hawaoni haja ya kuwa na maombolezo kwa vile wanatambua kuwa kuna uwezekano wa matukio ya ajali zaidi huko mbele, na haitawezekana kuwa na siku za maombolezo kwa kila ajali.
Naam, ni ukweli mchungu lakini usiokwepeka kwamba tutaendelea kupoteza maisha ya Watanzania wenzetu kwa ajali kwa sababu hakuna jitihada zozote za kulikabili tatizo hilo.

Walisema ajali haikwepeki lakini sote tunafahamu kuwa ajali zinazosababishwa na binadamu wenyewe zinaweza kuepukika. Ni rahisi kumlaumu Mungu kwa kudai ‘ajali hizo ni mipango ya Mungu, kwa vile siku yako ikifika huwezi kukwepa kifo’ lakini tutakuwa tunamwonea tu Mungu.

Tunaporuhusu askari wetu wa usalama barabarani wahalalishe rushwa kutoka kwa madereva wanaohatarisha maisha yetu au wanaotumia magari yasiyostahili kusafirisha japo takataka, achilia mbali binadamu, hatuwezi kujidanganya kuwa ‘hiyo ni mipango ya Mungu’ pindi kukitokea ajali.
Binafsi ninaamini kuwa kati ya vyanzo vikuu vya ajali huko nyumbani ni rushwa. Rushwa inawezesha vyombo vya usafiri vibovu kuendelea na safari zake na hivyo kuyaweka maisha ya abiria hatarini, rushwa pia inawezesha madereva wasio na sifa za kuendesha vyombo vya usafiri wa abiria kufanya kazi zao kana kwamba sheria za usalama barabarani zipo likizo.

Lakini kama nilivyowahi kueleza huko nyuma, abiria nao wanaweza kubeba lawama kwa kutotumia ‘nguvu ya umma’ pindi wanapokuwa katika chombo cha usafiri kinachoendeshwa kwa mwendo wa ‘kuita ajali.’

Hivi karibuni, rafiki yangu mmoja amekiri bayana kuwa kati ya sababu zinazomfanya kupendelea usafiri wa mabasi ya kampuni fulani inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Dodoma ni ‘mwendo wa kasi wa mabasi hayo.’

Haihitaji kuwa na uelewa mkubwa wa kanuni za fizikia kutambua kwamba mwendo wa kasi unaweza kusababisha ajali kirahisi, na hapo hata tukiweka kando uwezekano wa ajali kutokana na mwendo wa kasi katika basi bovu.

Tuambiane ukweli, wengi wa abiria hupendezwa zaidi na usafiri unaokwenda kasi kuliko wa polepole. Si ajabu kusikia abiria wakilalamika ‘ah dereva huyu anaendesha basi utadhani tumebeba maiti.’ Na dereva akitii kilio cha abiria hao, abiria haohao wanaweza kuishia kuwa maiti!
Kwa vile lawama pekee hazijengi, ni muhimu kwa serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na janga hili linalozidi kushamiri la ajali za barabarani.

Pamoja na kupambana kwa dhati na rushwa ndani ya kitengo cha usalama barabarani katika Jeshi letu la Polisi, serikali ichukue hatua za haraka za kuboresha njia mbadala za usafiri, hususan wa treni.
Kwa hali ilivyo sasa, abiria anaweza kulazimika ‘kuiweka rehani roho yake’ kwa kupanda basi bovu na linalosifika kwa mwendo wa kasi, si kwa kupenda bali kwa vile hakuna njia mbadala ya kufika aendako.

Ni muhimu kuboresha usafiri wa reli ya kati, sambamba na kuangalia uwezekano wa kufufua au kuanzisha njia mpya za treni kufikia maeneo mengi zaidi ya nchi yetu.

Mwisho, wakati tunaomboleza vifo vya wenzetu zaidi ya 30 vilivyosababishwa na ajali mkoani Mara, ninaomba kuwakumbusha Watanzania wenzangu umuhimu wa kuchukua hatua zilizo ndani ya uwezo wao, kwa mfano, kukabiliana na madereva wanaoendesha magari ya abiria kwa mwendo wa kuhatarisha maisha.

Kadhalika, japo ninatambua ugumu uliopo katika kupata ushahidi dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyofanywa na askari trafiki, angalau Watanzania wengi sasa wanamiliki simu zinazoweza kupiga picha au kurekodi video.

Ushahidi wa picha au video pale trafiki anadai au kupokea rushwa kutoka kwa dereva aliyetenda kosa barabarani waweza kuwekwa hadharani kwa mtindo wa ‘name and shame’ au kufikisha ushahidi huo kwa mamlaka husika. Hatua ndogo kama hizo zaweza kuleta mabadiliko makubwa hata kama itachukua muda mrefu.

Tusipojali uhai wetu kwa kupuuzia janga la ajali, tusitarajie miujiza ya kutunusuru

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.