4 Nov 2014

Chama cha Republicans kinaelekea kushinda viti vingi katika Bunge la juu la Seneti, na hivyo kuwapa nafasi ya kuwa na 'wabunge' wengi katika mabunge yote mawili, yaani bunge la juu la Seneti na bunge la chini la Kongresi.

Ushindi huo tarajiwa utakuwa wa mara ya kwanza tangu walipomudu kufanya hivyo wakati wa utawala wa Rais George W. Bush. Ni jambo la kawaida kwa chama cha Rais aliye madarakani kupoteza viti katika chaguzi za kati ya muhula (Midterm Elections). Kwa sasa, chama tawala cha Democrats kinaongoza kwa viti 10 katika bunge la Seneti na kilikuwa na matarajio ya ushindi katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.

Kwa bahati mbaya, sababu kadhaa zimejitokeza kuwa vikwazo dhidi ya chama hicho cha Rais Barack Obama, ikiwa ni pamoja na rekodi inayokaribia kuwa ya kihistoria ya kukubalika (approval ratings) kwa Rais Obama, mwenendo usioridhisha wa uchumi wa nchi hiyo, upinzani dhidi ya sera ya afya ijulikanayo kama Obamacare, na matarajio ya kujitkeza wapigakura wachache katika uchaguzi huo.


Mwelekeo wa kushindwa kwa chama cha Democrats unatokana na zaidi ya kuporomoka kwa umaarufu wa Obama ambapo wapigakura asilimia 53 hawaridhishwi na Obama kulinganisha na asilimia 42 wanaoridhishwa) na kawaida ya uchaguzi usiohusisha uchaguzi wa Rais (off-year election).

Democrats pia wanasumbuliwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2012 katika maeneo ambayo wapinzani wao wa Republicans walifanya vema.

Kuna sababu nyingine pia. Moja ni mikakati ya viongozi wa Republicans kuwezesha sheria kali za uchaguzi ambazo zinakwaza wapigakura watarajiwa, hususan katika maeneo yanayoelemea kwa Democrats. Katika miaka 10 iliyopita, takriban sheria 1000 za kitambulisho cha mpigakura zilitambulishwa kutokana na jithada za Republicans. Sheria hizo zinawataka wapigakura kuonyesha kitambulisho chenye picha au kupunguza masaa ya kupiga kura. Katika ya sheria hizo takriban 1000, karibu 100 zimeshapitishwa. Mahakama kuingilia suala hilo kumechangia kukanganya mwenendo wa upigaji kura (jambo linaloweza kuwapa wapigakura kisingizio cha kutopiga kura siku ya uchaguzi).

Bado haijafahamika ushindi wa chama cha Republican katika uchaguzi huo utamaanisha nini kwa siasa za Marekani kwa sababu haijulikani mkakati gani chama hicho kitautumia pindi kitakaposhinda. Hata hivyo, baadhi ya mipango muhimu ya chama cha Democracts, kwa mfano mageuzi kuhusu uhamiaji na hatua za kisheria kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, imeshakumbana na upinzani katika bunge dogo la Kongress linaloongozwa na Republicans. Iwapo Conservatives watafanikiwa kuongoza na Seneti pia, wanaweza kumpa wakati mgumu Rais Obama kwa kupinga uteuzi wa majaji,uteuzi wa mawaziri na teuzi nyinginezo zinazohitaji kuthibitishwa na Seneti.

Uongozi wa Republican kwenye mabunge yote mawili unaweza kumlazimisha Rais Obama kutumia kura yake ya veto kama kimbilio la mwisho.

Rais Obama akipiga kura katika uchaguzi wa kati ya muhula 
Lakini wachambuzi mbalimbali wameonyesha madhara yasiyofichika kwa chama cha Republicans pia. Iwapo chama hicho kitaonekana kumpinga Obama katika kila jambo, watajiweka katika hatari ya kutengwa na umma na hivyo kuhatarisha nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu wa Rais mwaka keshokutwa. Ikumbukwe kuwa chama cha Democrats wana 'mgombea' mwenye uwezo wa kushinda urais mwaka 2016, kwa maana ya Hillary Clinton.Kwa upande wa Conservatives, majina yanayotajwa hadi sasa ni ya wanasiasa wasio na nguvu kubwa.Kwa maana hiyo watahitaji mwonekano bora kwa wapigakura iwapo watataka kushinda katika uchaguzi huo mkuu.

Kingine kinachoweza kuwaathiri Republicans ni kilekile kinachokikabili chama cha upinzani kinachojaribu kuking'oa madarakani chama tawala: kuongoza mabunge yote mawili kutapelekea matarajio kwa wananchi kutoka kwa chama hicho.Republicans wameshatoa ahadi kibao kuhusu kupunguza kodi na miradi ya serikali kuu. Wakishindwa kutekeleza ahadi hizo kutaambatana na gharama ya kisiasa. Kadhalika, sheria kali zitakazotungwa kwa kutumia wingi wao katika Seneti na Kongresi zaweza kuwaathiri wagombea urais watarajiwa wa chama hicho waliopo kwenye Seneti, yaani Rand Paul, Marco Rubio na Ted Cruz, hasa wakiunga mkono maamuzi watakayokuwa na wakati mgumu kuyatetea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Iwapo Republicans watashinda na kuchukua uongozi wa Seneti, jambo moja la wazi ni kupanuka kwa mgawanyiko wa kiitikadi hasa kati ya bunge na serikali.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka gazeti la The Guardian la hapa Uingereza. 



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.