12 Mar 2015

SIKU chache zilizopita, kikundi hatari cha kigaidi cha Boko Haram cha nchini Nigeria kilitangaza utiifu wake kwa kikundi kingine hatari kabisa cha kigaidi cha ISIS.
Hizi si habari njema hata kidogo kwani ushirikiano wowote kati ya makundi ya kigaidi, hususan, yaliyopo maeneo tofauti, unamaanisha kusambaa kwa vitendo vya kigaidi.
Ujumbe ulitolewa na Boko Haram, ambao hata hivyo bado haujathibitishwa (ni nadra kuthibitisha ujumbe wao ), uliwekwa kwenye akaunti ya kikundi hicho katika mtandao wa kijamii wa twitter, ambayo inaaminika kuwa ya kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.
Kikundi hicho kilianza mashambulizi ya kigaidi mwaka 2009 maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria, lengo kuu likiwa kuanzisha utawala unaoendeshwa kwa sheria za Kiislamu. Tayari kikundi hicho kimeshasababisha mauaji ya raia kadhaa, na hivi karibuni kimekuwa kikijaribu kusambaza unyama wake kwa nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.
Awali, ilifikiriwa kwamba Boko Haram ina mahusiano na kikundi kingine kikubwa na hatari cha Al-Qaeda, ambacho kilikuwa maarufu sana kabla ya kuibuka kwa ISIS.
Kwa upande wake, ISIS kimekuwa kikifanya unyama ambao pengine haujawahi kuonekana katika historia ya vikundi vya kigaidi, licha ya mashambulizi ya kujitoa mhanga, kikundi hicho kimeshawachinja mateka wake kadhaa na kuweka unyama huo hadharani.

Hivi karibuni, ilifahamika kuwa gaidi anayedaiwa kuwa ndiye ‘mchinjaji’ mkuu, anayejulikana kama Jihadi John, aliwahi kufika Tanzania na kuzuiliwa kuingia, kabla ya kuelekea Syria, ambako pamoja na Iraki, ni maeneo yanayosumbuliwa na kikundi hicho.
Lengo kuu la ISIS ni kuanzisha himaya (Caliphate) ya Kiislam, na kiongozi wake, Abu Bakr al-Baghdad, amejitangaza kuwa ndiye mkuu wa himaya hiyo ambayo wanalenga kuisambaza dunia nzima.

Kinachoifanya ISIS kuonekana hatari zaidi, licha ya unyama wake, ni uwezo wake mkubwa wa kifedha, sambamba na ufanisi wa kimuundo kana kwamba ni dola kamili yenye serikali.
Tangazo la Boko Haram kuahidi utiifu kwa ISIS si la kushangaza sana, japo wafuatiliaji wa masuala ya ugaidi walishangazwa kwanini hali hiyo haikutokea mapema zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa mbinu na malengo ya vikundi hivyo yanashabihiana.

Huu ni mtihani mkubwa kwa wana-intelijensia duniani hasa ikizingatiwa kuwa ISIS, kama ilivyokuwa Al-Qaida, si tu imefanikiwa kuwavutia ‘wapiganaji’ kutoka sehemu mbalimbali duniani, bali pia ina dhamira kubwa ya kusambaza unyama wake takriban kila kona ya dunia.
Kwa tafsiri ya haraka, Boko Haram wanaweza kunufaika na ushirikiano wake na ISIS na pengine kufanikiwa kusambaza kampeni yao ya kigaidi katika maeneo mengine ya Afrika.
Lengo la makala hii sio kujadili vikundi hivyo vya kigaidi. Kilichonishawishi kuandika makala hii yenye utangulizi unaohusu vikundi hivyo vya ugaidi ni tamko la hivi karibuni la Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye kuwa kikosi cha ulinzi cha Red Brigade cha Chadema ni kundi la kigaidi.

Lakini Nape si mwanasiasa wa kwanza wa CCM kutoa tamko zito kama hilo. Mwaka juzi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Mwigulu Nchemba, aliandika waraka mrefu katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums kuizungumzia Red Brigade ya Chadema, ambapo pamoja na mambo mengine alidai ina malengo ya “uhaini, ni ugaidi, ni maandalizi ya kupindua nchi au kuvuruga kabisa amani tuliyonayo.”
Kwa upande wake, Nape alidai makundi ya vijana wa ulinzi vya chama hicho (Red Brigade) yameandaliwa kwa ajili ya kuingia msituni kwa shughuli za ugaidi. Alitoa kauli hiyo wilayani Mpwapwa kwenye ziara ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, mkoani Dodoma.
“Chadema wanaandaa vijana kupitia Red Brigade ili kuingia msituni na kuchukua madaraka ya nchi kwa mabavu. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua hawawezi kuchaguliwa kwa njia ya kura wakati wa uchaguzi mkuu,” alidai mwanasiasa huyu muumini wa siasa za uhasama, na kuongeza kuwa, “Taarifa tulinazo ni kwamba Red Brigade ni vikosi vinavyoandaliwa kwa ajili ya vitendo vya ugaidi na shughuli nyingine za ovyo. Taarifa ni kwamba hili ni kundi la kigaidi, wataanzishaje kundi la usalama wakati tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu?”
Huu ni uhuni wa kisiasa. Na baya zaidi, ni mwendelezo wa kasumba ya muda mrefu kwa Nape na Mwigulu kuufanyia mzaha ugaidi kwa kuvihusisha vyama vya upinzani hususan Chadema.
Lakini kabla ya kuwajadili wanasiasa hawa wawili ‘wanaaombea uwepo wa ugaidi nchini mwetu,’ ni vema kutambua kuwa kamwe kauli zao hazijawahi kupingwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete au kiongozi mwingine yeyote yule wa chama hicho tawala. Wakati Julai mwaka, Rais Kikwete alisema si sahihi kwa vyama vya siasa kuanzisha vikundi vya mgambo kwani vitendo hivyo ni viashiria vya uvunjifu wa amani nchini, chama anachokiongoza (CCM) pia kina kikundi cha Green Guard, kama ilivyo Blue Guard kwa CUF.
Kwa maana hiyo, kwa Nape na Mwigulu kukemea Red Brigade ya Chadema ilhali CCM nayo ina Green Guard si tu ni unafiki bali pia wanaweza kuwa wanatumika kama ‘kipaza sauti’ cha Rais Kikwete na CCM kwa ujumla.

Lakini sote tunafahamu siasa zetu za upinzani zilivyo ambapo ‘kurushiana madongo’ ni sehemu ya kawaida. Hata hivyo, jaribio lolote la kuhusisha ugaidi na ‘madongo’ ya kawaida litatugharimu kama taifa. Ugaidi si jambo la kufanyia mzaha hata kidogo.
Moja ya madhara ya kuufanya ugaidi kama jambo la kawaida ni kuwarahisishia magaidi halisi fursa ya kutudhuru. Hivi, kwa mfano, magaidi tulio jirani nao zaidi kuliko Boko Haram, ISIS na Al-Qaeda, yaani Al-Shabaab wa Somalia, wakitaka kufanya ugaidi nchini mwetu (Mungu aepushie) hawawezi kutumia upenyo wa ‘Red Brigade wa Chadema ni magaidi’ kuficha dhamira yao ovu?
Vyombo vyetu vya usalama vinaweza kulazimika kuwekeza nguvu kubwa kuwadhibiti ‘magaidi wa kufikirika’ wa Red Brigade, na hiyo yaweza kutoa fursa kwa magaidi halisi kufanya unyama wao.
Tayari tumeshaona jinsi vyombo vya usalama vinavyotumia nguvu kubwa kulinda maslahi ya CCM, ikiwa ni pamoja na kuwakandamiza wapinzani wake, huku ufisadi, ujangili, biashara ya madawa ya kulevya, na sasa mauaji ya albino vikistawi kana kwamba ni shughuli halali.
Kichekesho, majuzi wakati Rais Kikwete anazindua studio za kituo cha Televisheni cha Azam jijini Dar alitoa karipio kali kwa vyombo vya habari akisema serikali haitavumilia vyombo vya habari visivyosimamia uadilifu, weledi pamoja na kutumika katika kuchochea ghasia. Kwanini ukali huo wa Rais wetu uwe kwa vyombo vya habari tu ilhali wahuni wa kisiasa wakiruhusiwa kufanyia mzaha tishio la ugaidi?

Nimalizie makala hii kwa kuwahamasisha Watanzania wenzangu kuwapuuza wanasiasa mufilisi wanaojaribu si tu kujenga chuki miongoni mwetu bali pia kufanyia mzaha tishio la ugaidi.
Sote ni mashuhuda wa unyama unaofanywa na Boko Haram, ISIS, Al-Qaeda, Al-Shabaab na makundi mengine ya kigaidi, na ninaamini hakuna mtu anayeweza kudiriki kutamani uharamia huo utokee katika nchi yetu. Siasa za chuki za kipuuzi ni hatari sana kwa mustakabali wa Tanzania yetu.
Inahitaji kauli chache tu za kupandikiza mbegu za chuki, lakini ni vigumu mno kung’oa chuki pindi mbegu hizo zikifanikiwa kuotesha chuki.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.